The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 13 May 2026

Turidhiane, kuridhika bila kulidhishana?

 Mara nyingi kama siyo mara zote, mafyatu hujifanya wanasiasa na kufanya visasi waviitavyo siasa utadhani nao ni wanasiasa! Uongo huitwa uongozi hata dhuluma ikaitwa haki. Wengine hata uongo huuita uongozi wakati ni uongo tu. Mfano, unapojidanganya ukidhani umewadanya mafyatu wote, ujue ni muongo tu na si kiongozi. Waongo huongoza kwa uongo. Ni mabingwa wa kucheza na kuchezea maneno. Mfano, wanaweza kukushawishi ununue kanuywaji eti mnywe wote kwa faida yenu nyote kumbe ni kwa faida zao. Wanaweza kukuridhisha kuwa mnafanya, maridhiano kutopigana baa kumbe ni maridhishano ambayo mwisho wa siku, watajiridhisha kwa kukuridhisha bila wewe kuridhika wala kuridhishwa mbali na kutopata haki. Mkiwa mnapata kanywaji huongelea amani wakajitenga na haki wakati bila haki hakuna amani na amani isiyo na haki ni amani ya imani.

            Warongo wanaweza kujiridhisha bila kukuridhisha halafu wakesema wote mmeridhika ilhali mmeudhiwa na kunyimwa haki kwa kuongopewa kama hamnazo. Kuna inshu hii ambapo fyatu mmoja alimwaga kanywaji kangu tukiwa baa. Si alisema turidhiane! Turidhiane au tulidhishane kwa kujiridhisha bila kuniridhisha aliyemwagiwa kanywaji? Hili, licha ya kuniudhi, limenichanganya na kunihuzunisha. Hata hivyo, sirithiki hadi nitakapopata maelezo ya kina tena yenye kuingia kichwani. Badala ya kuridhika, nalishughulikia na kumshughulikia anayetaka kuridhiana bila kuridhishana. Mie kulalamikia kanywaji kangu eti fyatu huyu kasema mie ni adui wa amani, mshikamano, na upendo vya wanywaji! Yaani umwage kanywaji kangu halafu uniletee ngonjera za amani? Kwani, alichofanya huyu zwazwa ni haki?
            Kwani, nani anataka kuridhiana na kuridhishana na fyatu asiyeridhisha wala kuridhika mbali na kutoridhishwa na mie ninayetaka haki? Tutaridhikaje wakati ulevi alio nao tena bila kustahiki haumridhishi wala kuridhika nao? Unacheza na kuridhika hasa kwa wale wasiojaliwa mshipa wa kuridhika na vile vinavyoridhisha kwao visiridhishe? Nani atakubali kuridhiana na fyatu tena mlevi asiyeridhika na kanywaji tena ka dezo? Kwani, mie ni zwazwa nisijue vitu rahisi kama hivi ambavyo havihitaji kuridhishana kuvijua? Huwezi kunifanyia undavandava na unyama tena kizwazwa nikakubana ukaja na maridhiano. Nilidhike au kuridhishwa lini au nini wakati uliyeridhia kunifyatua sijaridhia kila kitu na kujiridhisha? Nashauri turidhishane ila siyo kudhalilishana jamanini.
            Leo, nadurusu hii kitu kuridhiana ili kuridhishana kwa kuwa huyu fyatu anayetaka kuniridhisha na kujiridhisha kuwa nimeridhika siridhiki hata punje. Kwanza, turidhike na nani na nini wakati kuridhika kunahitaji kitu kimoja kisichokuwepo kwenye equation yaani haki? Kuridhika hutokana na kuridhika na haki na siyo dhihaka. Kwa hali ilivyo, turidhishane katika dhihaka lakini si haki wala stahiki tena huyu fyatu atakaye kuridhiana na kuniridhisha hatendi  haki wala kustahiki.
            Wapo walevi waliotetea maridhiano wasijue ni marishano si kwa wote bali fyatu mchokozi. Sikuwahi kufikiri kuwa kuna siku fyatu nitaambwa niridhiane kudhulumiwa. Ili iweje yarabi? Nani anamridhisha nani? Nani anamdhihaki nani katika haya maridhishano? Unaridhiana na nani wakati wakati kanywaji kalishamwagwa? Nani anaweza kuridhiana kwa misiba isiyo na sababu bali tamaa na uzwazwa?
            Kuridhiana na kuridhishana siyo mambo mabaya. Ubaya ni kutaka kuridhiana kwa kujiridhisha bila kuwaridhisha wasioridhishwa na maridhishano tena yasiyoridhisha hata wale waliolenga kuridhiana na kuridhishana. Je, tujiridhishe au turidhike kuwa hatuwezi kujiridhisha bila kuwaridhisha wengine? Hapa, ndipo yalipo maridhiano na siyo maridhishano. Hapa, ndipo lilipo jibu la tatizo ambalo fyatu aliyemwaga kanywa kajiridhisha kuwa halipo ilhali lipo.
            Nani awezaye kuzuia muda hata atumie nguvu vipi? Unaweza kuvunja saa zote hata kuua majogoo yote. Muda upo pale pale na hautasimama wala kuharakishwa au kupunguzwa kasi. Ili kufikia maridhiano na marishano, je, yatupaswa kulazimishana au kuridhiana kwanza kuridhiana kabla ya kuridhishana ili sote turidhike? Nani anamridhisha nani na anataka kuridhishwa na kwanini kuridhishwa? Na huyo unayetaka kuridhisha na kuridhishwa tufanye hivyo namna gani? Je, kwa zengwe tulilo nalo, kuna uwezekano wa kuridhisha na kuridhiana na kila mmoja akaridhika?
            Ili kuridhisha na kuridhishana, lazima iwepo haki inayoridhisha na siyo mkosaji kujiridhisha. Je, tuko tayari kuitafuta hiyo haki yenye kuleta ridhiko au kujiridhisha hata bila ya hiyo haki kuwapo? Nani ataridhika pasina haki au haki ya kuridhika? Nani mwenye haki zaidi ya mwingine wakati fyatu anayetaka kuniridhisha ili turidhiane na kulidhishana hataki kutenda haki? Nani aanze na nani amalize? Je, yawezekana kuwapo maridhiano bila maridhiano? Nini kianze na kupatikana kati ya kuridhisha na kujiridhisha kwa kisingizio cha kuniridhisha?
            Tunaweza kujiridhisha kuwa tumeridhiana na kuridhishana. Ila tujue, kuna vitu vingine haviwezi kuridhishwa kwa vile wahusika hawapo mfano, kanywaji kangu.
            Mbali na hayo juu, kuna maswali mengine muhimu. Je, tushirikio maridhiano tunajua na kukubali ni kwanini tunataka kuridhiana? Tunajua. Kila penye maridhiano, kuna kutoridhiana, ndiyo maana yakahitajika maridhiano. Je, nini mzizi wa kutoridhiana au kutoelewana? Je, tunaweza kujibu maswali haya kwa ufasaha kabla ya kuingia kwenye haya maridhiano na maridhishano tena yanayoonyesha kutoridhisha hata kabla ya kuanza maridhiano? Je, kuna hatua, juhudi, nia safi, na hakikisho vyote vya kuridhisha za kufikia kukubali kufanya maridhiano? Kumbe naota!

No comments: