Sunday, 13 April 2008

Butiama na CCM mpya ya kale

WENGI tulitarajia kufanyika kwa mikutano ya siku mbili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kijiji cha Mwitongo, Butiama, mkoani Mara, mahali alikozikwa Mwalimu Julius Nyerere, mwanzilishi wa taifa hili, kungeleta changamoto na nafuu kwa siasa za nchi yetu. Kumbe tulikosea sana.

Haikuwa na haitakuwa kwa CCM hii na utawala huu. Hii ni fursa ilipotea na kama ni tumaini, basi limekufa na halitafufuka.

Tulitarajia angalau, CCM, kama nyoka wa kuchusha na kutisha, ingejitoa ngozi yake ya zamani na kuja na mpya ili kuanza upya kuipelekea mbele nchi yetu. Kadhalika tulikosea!

Hapa kuna tatizo tena kubwa tu.

Sasa mikutano ya CCM kule Butiama imekwisha. Hakuna cha mno wala cha maana kilichofanyika!

Ni hasara kiasi gani? Je, kwa nini imekuwa hivyo? Je, ni kutokana na ile tabia mbaya na sugu ya watawala kuichukulia nchi kama shamba lao au mali binafsi?

Je, ni kukosekana kwa visheni na uongozi wenye kuona mbali? Je, ni kichwa ngumu tu au bahati mbaya?

Sijapata jibu kwa nini CCM imeshindwa kujitenga na ufisadi kiasi cha kuupamba badala ya kupambana nao. Bado nalisaka na kulitaka jibu tena lenye kuingia akilini, si ‘gereshabwege’ tuliyozoea. Je, wahusika wako tayari kutoa jibu au kukubali kushindwa na kuwajibika?

Hatuelewi ni kwa nini CCM imeshindwa hata kutoa karipio dhidi ya mafisadi wanaojulikana, acha kufukuzana kwenye chama kama tulivyodhania.

Je, mafisadi wameshinda? Wameiteka na kuikalia nchi yetu?

Je, kwa mara nyingine, CCM imejibainisha kuwa ni ya kina nani? Je, ni kwa nini ilikwenda Butiama alikozaliwa gwiji wa siasa za ukombozi wa kweli wa Mtanzania na Mwafrika kufanya mambo iliyofanya?

Kwa nini kwenda kule kufanya kinyume naye au ndiyo kumdhihaki kwa vile hatafufuka? Je, madhara ya hili ni yapi kama wananchi wataamua kuyatumia vilivyo hasa kwenye uchaguzi ujao?

Uko wapi mwafaka na serikali ya mseto tuliyopigiwa upatu? Tunaambiwa Karume na kundi lake wameupiga teke na kukataa katakata! Je, Karume, CCM na Kikwete nani zaidi?

Wataalamu wa uhai wana kanuni kuwa kitu chochote kikikaribia kufa hujenga chembe chembe za kukiua ndani mwake. Wazungu husema, ‘arrogance creates the source of destruction within itself so as to die.’

Hatuna tafsiri ya moja kwa moja ila ni kwamba: ujanja ujanja huwa na tabia ya kujenga kiini cha kujiua wenyewe. Je, CCM nayo inatii kanuni hii ya maumbile?

Je, ni kwa nini CCM inaamua kujimaliza yenyewe kirahisi hivi? Je, imepitwa na wakati kama wanavyosema baadhi ya wachambuzi wa mambo? Maswali ni mengi na tata kuliko majibu.

Kama kuna aliyepata pigo kipindi hiki kwenye mkutano wa Butiama si mwingine bali Mwenyekiti wa chama na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete.

Maana, umma ulidhani kwa kutumia ushawishi wa Mwalimu angeweza kubadili sura ya hali ya mambo nchini. Hii ilikuwa ‘second chance’ iliyopotea bila sababu za msingi.

Lakini bahati mbaya hakufanya hivyo. Je, ni kwa nini?

Je, amezidiwa na wahafidhina waliomzunguka au ameshindwa kuliona hili? Amekubali kutumiwa na mafisadi kiasi cha kuhatarisha madaraka yake? Na hatima ya hili ni nini ndani ya chama chenyewe kinachoonekana kuanza kumeguka makundi kutokana na mitandao yenye maslahi na vinara tofauti?

Je, Watanzania bado wataendelea kuwa na imani na chama kisichokidhi matarajio yao? Wataendelea kukipenda?

Kukiamini na kukichagua huku kikionekana kulalia kwenye maslahi ya wachache kikiwatelekeza wengi? Je, ni wakati wa upinzani kujiandaa kuziba ombwe hili?

Tulitarajia litolewe tamko dhidi ya ufisadi. Halikutolewa! Tulitarajia mafisadi washughulikiwe huku mbinu na mikakati mipya ikitangazwa ya kufanya hivyo.

Haikuwa! Je, tumuulize nani? Nani atapambana na ufisadi iwapo tuliotarajia kufanya hivyo wametugeuka?

Je, huu si ushahidi tosha kuwa Kikwete ameishiwa na hatatufikisha popote zaidi ya kuturudisha nyuma? Hili ni swali kwa Mwenyekiti CCM na Rais wa Tanzania, Kikwete.

Je, umma nao utakubali uendelee kuteseka ilhali mali na rasilimali zao zikitumiwa vibaya na kikundi kidogo cha watu?

Hapa ndipo wapinzani wanapopaswa kujifunza. lazima jibu lipatikane vinginevyo tuendako ni kubaya zaidi.

Sasa vikao vya Butiama vimekwisha bila mafanikio yoyote kwa umma. Je, huu ndiyo mwisho? Hili swali linakwenda kwa Watanzania wote na wapinzani hasa wasioshiriki vitendo vya ufisadi na usaliti kwa taifa.

Je, tuendelee kulialia au tuchukue hatua ambazo kimsingi ni kutangaza mgogoro wa umma dhidi ya watawala.

Hivi tukiamua kuitisha migomo isiyo na ukomo kitaifa, hawa wanaotuchuuza na kutugawana watapa nafasi ya kuendelea kutanua kama wanavyofanya?

Kwa nini tuendelee kushuhudia maangamizi ya kutengenezwa na wanadamu kama yaliyojiri Mererani? Natuma rambirambi na kuwataka wananchi wajifunze kutatua matatizo kwa njia muafaka badala ya kubabaisha.

Hakuna haja ya kuhilikiwa mashimoni kama muhanga ilhali watu wachache wanafaidi matunda ya uhuru wetu. Hii ni dhambi kubwa na ya mwisho kutendwa na binadamu wenye akili, tena taifa.

Haya ni machukizo ya machukizo kufanywa na binadamu kwenye karne ya 21.

Tusimung’unye maneno. Adui yetu mkuu sasa ni CCM na watawala ambao wameshindwa kutafuta suluhu ya matatizo yetu. Walituahidi wangefanya hivyo.

Tuliwaona wakiapa kufanya hivyo. Kwanini leo watugeuke tena bila sababu isipokuwa uchoyo na upogo na upofu? Je sisi ni wa ovyo kiasi cha kufanyiwa haya na kuridhika?

Tumekuwa wanafiki na wapumbavu. Kwa nini tuweze kutatua migogoro ya Kenya tushindwe yetu?

Kwa nini tuwe na uwezo wa kupeleka jeshi Comoro tushindwe kuleta suluhu kwetu wenyewe?

Yanayowasumbua Wakenya na Wakomoro hadi wakafikia walipofikia ni sawa kabisa na yanayotuhangaisha sisi.

Je, kwa nini hatuelekei huko ili haki itendeke? Maana wahenga walisema haki ni haki daima huvunja hata milima. Na amani haiji ila kwa ncha ya upanga.

Je, tuanze kuutafuta upanga? Na kwa nini wahusika watufikishe hapo? Je, nani atanusurika kama tutaamua kutumia nguvu kupata haki yetu?

Je, haki yetu inawezekana kuletwa kwenye sahani ya dhahabu au kupitia sulubu ya baadhi yetu?

Hapa ndipo tunaporejea kisa cha Ansbert Ngurumo cha kuoza na kuota ili kuzaliwa upya tena kwa mamilioni.

Hivyo ifahamike kuwa hatutetei vurugu. Vile vile hatuungi mkono wala kutetea amani ya ukondoo.

Ni amani gani inayoweza kushamiri bila kutenda haki? Ni haki gani inaweza kuwa na maana bila kutendwa na kutendeka wote wakaona?

Mficha uchi hazai.

Na mtaka cha uvunguni sharti ainame. Je, umefika wakati wa kuinama ili tukipate cha uvunguni au kuendelea kujidanganya tukisimama na kutegemea cha uvunguni?

Wakati baadhi yetu wakijipiga vifua na kushabikia upuuzi wa kutatua migogoro ya Comoro na Kenya, wenzetu wanatucheka na kutuona kama majuha au hata manyani.

Nani kasahau kisa cha mtoto wa nyani aliyechekea kuungua kwa msitu asijue atalala wapi?

Ni kwa nini tunahamanika kutatua ya wenzetu wakati sisi kwa sisi tukiumizana. Hivi kuna amani pale Pemba? Hivi wananchi wetu vijijini wana amani?

Mererani, Buzwagi, Geita, Kahama, Kiwira na kwingineko wana amani?

Kwa nini wenzetu waweze sisi tusiweze? Wapi kuna tatizo kati ya watu wetu na watawala wao?

Je, na watawala wetu wanatuchukuliaje?

Je, sisi tunawachukuliaje? Kikwete, CCM na Watanzania wote tutafute majibu sahihi ya hali na maswali haya tena haraka bila kuchelewa wala kuzungushana.
Source: Tanzania Daima Machi 13, 2008

1 comment:

SIMON KITURURU said...

Kwa mwendo huu, cha moto tutakiona!Ila kwa mwendo huu muda wa CCM kuwa untouchable , unahesabika.