The Chant of Savant

Tuesday 31 July 2012

Tumepata kamanda mwingine


Mnamo tarehe 30 Julai hii, familia ya  Mpayukaji ilijaliwa kupata kamanda mwingine Nkwazi Mhango Jr aka Mpayukaji Jr. aliyezaliwa kwenye hospitali ya Boundary Trail MB. Tunachukua fursa hii kuwafahamisheni wasomaji wetu ambao licha ya kuwa marafiki mmekuwa ndugu zetu. Mtoto, mama na baba wanaendelea salama. Tunawakaribisheni kujumuika nasi wakati huu wa furaha ya pekee kwa kumpata kamanda wetu wa pili.

'Kufuturisha' ni aina mpya udini au ufisadi?

Rais Jakaya Kikwete akiongea na wananchi wakati alipowafuturisha huko mkoani Lindi alikokwenda kwa ajili ya mazishi ya shemeji yake.


Wabunge 'wakifuturu' pamoja  mjini Dodoma akiwamo 'shehe'Samuel Sitta.

Miaka ya karibuni baada ya madaraka kuwekwa maji na kuchakachuliwa, umezuka mtindo wa viongozi wa serikali walio waislam na wasio waislam,makampuni ya biashara na wenye nazo kufuturisha ima wananchi hata viongozi wao. Kfuuturisha huku ni kwa ajabu kidogo. Maana hakujali dini. Kidini, wanaopaswa kufuturu ni waislam tena waliofunga. Lakini siku hizi utasikia rais akifuturisha mawaziri bila kujali kama wamefunga ni waislam au la. Utasikia shirika fulani au kampuni hasa ya biashara yakifuturisha wananchi. Je huu ni udini au aina mpya ya ufisadi au tuseme ufisadi wa kiimani? Je watanzania wanahitaji futari au haki zao na huduma stahiki yao? Je watanzania wana njaa kiasi cha kuonekana kama wenye kuhitaji futari tu na si haki zao?Je wale ambao si waislam wanafuturu nini na kwa dini gani iwapo hawafungi wala kuamini katika imani husika? Je nani hapa anamdanganya au kumtumia nani? Je pesa inayotumika kununua na kuandaa futari hasa zile zinazotelewa na viongozi kama wa rais zinatoka mifukoni mwao au kwenye kodi ya watanzania ambao nchi yao haina dini ingawa wao wana dini?

Monday 30 July 2012

Hongera Sipho 'Hotstix' Mabuse kumaliza fomu six

South African musician Sipho Mabuse performs during the Joy of Jazz festival in Johannesburg on August 2010. Photo/FILE
Kwa wale wapenzi wa zilipendwa wanamkumbuka gwiji la muziki toka Afrika Kusini Sipho 'Hotstix' Mabuse (Pichani). Gwiji huyu alitoroka umande katika miaka ya 60 kuendeleza kipaji chake cha muziki. Pamoja na mafanikio yake kimuziki, hakuridhika kuwa kihiyo au kughushi shahada au vyeti wa usomi. Alijipinda na kurejea shule ambako hivi karibuni alihitimu elimu ya kidato cha sita akiwa na umri wa miaka 60. Kwa wale wanaodhani wamechelewa au kughushi kuna somo kubwa hapa. Kwa habari zaidi BONYEZA hapa.

Sunday 29 July 2012

Hivi mzazi wa namna hii ni mzima na tumfanyeje?



Mtoto achanjwa viwembe mwilini na mamaye kwa kula maharage



Mwanafunzi wa darasa la pili jijini Dar es Salaam amefanyiwa unyama wa kutisha na mama yake mzazi kwa kuchanjwa na viwembe mwili mzima na kumsababishia kushindwa kwenda shuleni kutokana na kupata maumivu makali.
NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kufika katika eneo la tukio huko Mbezi Temboni mtaa wa Gape na kuzungumza na mwanafunzi huyo wa kiume mwenye umri wa miaka nane aliyesema kuwa mama yake, Jane Maparuwe alimchanja na viwembe maeneo ya mgongoni na kwenye paja juzi majira ya saa 5:00 usiku.
Akisimulia mkasa huo mtoto huyo alisema kuwa alikula maharage baada ya kusikia njaa kwa muda mrefu na mama yake aliporudi nyumbani na kuanza kuulizia yaliyopo maharage hayo, alimwambia kuwa amekula ndipo alipomkamata na kuanza kumpiga na kumchanja na kiwembe.
Alisema mbali na kuchanjwa pia alipigwa kwa kutumia mkanda huku akimkwaruza na kucha zake usoni na kumwachia alama.
Alisema kutokana na kipigigo hicho alishindwe kwenda shuleni kwa kuwa alikuwa na maumivu makali ya mguu na mgongo. Alisema mpaka sasa hapati huduma ya hospitali na kwamba mama yake mdogo alinunua plasta na kumbandika katika kidonda cha mguuni.
Alisema katika kipindi chote amekuwa akiishi na mama yake na kwamba baba yake Nassor Hassan anaishi eneo la Mwananyamala.
Hata hivyo, mtoto huyo amekuwa akiishi maisha ya tabu kwani mama yake huwa anaondoka na kwenda katika biashara zake za kuchoma mihogo na kurudi usiku, huku mtoto huyo akisubiri huruma ya majirani kumpa chakula. "Huwa ninashinda peke yangu mama anakwenda katika biashara zake anarudi saa 3 usiku huwa nakula kwa majirani wakati mwingine ananipa hela ya kununua juisi na skonzi," alisema.
NIPASHE Jumapili ilifanikiwa kuzungumza na Mjumbe wa shina namba nane katika mtaa huo wa Gape, Pendaeli Kahaya, ambaye alisema majira ya saa 6 :15 mchana akiwa katika shughuli zake alipigiwa simu na majirani zake na kumjulisha tukio la mtoto kuchanjwa na viwembe na kisha kufungiwa ndani.
Alisema fundi ujenzi mmoja ambaye huwa anafanya ujenzi katika nyumba hiyo alitaka maji ya kunywa, alipoingia ndani alishangaa kukuta damu zikiwa zimetapakaa na ndipo alipomuuliza mpangaji mwenzake.
"Fundi huyo alijibiwa kuwa kuna mtu alikuwa anakula mali yake alipomuuliza ni kwanini amchanje chanje na kumfungia ndani mpangaji huyo alimjibu hawezi kuelewa ndipo fundi huyo alipokwenda kumuangalia," alisema Kahaya.
Kahaya alisema kabla ya mama huyo kumchanja kwa viwembe alichukua kisu na kumtaka kumchinja mtoto huyo lakini mdogo wake aliingilia kati na kumueleza kuwa ataondoka kama atathubutu kufanya kitendo hicho.
Alisema mdogo wake aliondoka na ndipo mama wa mtoto huyo alipoamua kumuagiza mtoto wa jirani kwenda kununua viwembe na kuamua kumchanja na kumfungia ndani kwa siku mzima.
Hata hivyo, alisema wakati mtoto huyo akifanyiwa tukio hilo jirani yake aliamka na kumuuliza ni kwanini anampiga mtoto huyo kwa muda mrefu lakini mama huyo alimtukana jirani huyo na kumtaka afuatilie mambo yake na sio ya kwake.
Alisema tukio hilo lilimsikitisha na kuamua kwenda kumjulisha diwani wa kata ya Msigani, Rogati Mbowe, na kumwambia aende kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa serikali za mtaa.
Aidha, alisema aliwasiliana na uongozi wa serikali za mtaa ambao ulichukua hatua juu ya suala hilo na askari walifika katika eneo hilo na kufanikiwa kumkamata mama huyo.
Alisema wameshangazwa kuona mtoto huyo mpaka sasa hajapelekwa hospitali na pia mama huyo ameshaachiwa na polisi jambo ambalo limewashtua wakazi wa eneo hilo.
"Sijaelewa sababu ambayo polisi imepelekea mama huyo kuachiliwa tunataka kuona sheria inachukua mkondo wake maana nilijiuliza maswali mengi hivi ni mtoto wake aliyemzaa kwa kumbebea mimba ya miezi tisa na kuamua kumchanja na viwembe," alisema. NIPASHE ilifanikiwa kuzungumza na diwani Mbowe ambapo alisema kuwa ni kweli tukio hilo limetokea na kwamba kesho atalifuatilia kwa ukaribu kwani alikuwa amepata majukumu mengine.
NIPASHE ilimtafuta mama mzazi wa mtoto huyo katika sehemu yake ya biashara eneo la Kimara Temboni lakini wafanyabishara wenzake walidai kuwa alikuwa ameshaondoka katika biashara zake na kuelekea nyumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela, alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo hakuweza kupatikana.
Hata hivyo, habari za ndani ambazo limelifikia gazeti hilo ni kwamba polisi wameagizwa kumkamata mama huyo ambaye aliachiwa.
Chanzo: Nipashe Julai 29, 2012.

Hapa nani alimtapeli mwingine?


  1. Kuna vitu vitu vingine ni vigumu kuvielezea. Ukiangalia picha hiyo hapo juu na mandhari yake unabaki kushangaa. Unajiuliza swali moja kuu kuwa kati ya mwenye picha yake anayetabasamu na wale walioweka nani anamtapeli mwenzake? Ukiona picha ile utadhani mwenye kibanda anampenda aliyepo katika picha. Anaweza akawa na anampenda kwa ujinga wake. Ila akijitambua atamchukia bila shaka. Maana alimuahidi maisha bora.

Ingekuwa mimi ningepiga mafisadi


Vijana wa kikundi cha Uamsho cha Bara wakimrudi anayetuhumiwa kuwa changudoa


Taarifa kuwa kundi la Uamsho la Tanzania bara lilivamia mitaa ya Kinondoni usiku na kuwacharaza bakora vyangudoa zimevuma sana. Wengi tumelaani kuchichukulia sheria mkononi na kuumiza watu wasio na hatia. Hawana hatia. Maana kazi ya kumkuta mtu anayetuhumiwa kutenda jinai ni ya mahakama. Kweli vyangudoa na uzinzi ni machukizo kwa wengi. Ila kama tutamia akili vilivyo, umalaya si tatizo kwa taifa kama ilivyo ufisadi, ufisi, ubabaishaji, sanaa, dhuluma na jinai nyingine zinazotendwa na watawala wetu. Kama kweli tunataka kujenga jamii isiyotenda maovu, tungeanza na ufisadi unaoleta umaskini, udhalilishaji na mateso kwa watu wetu. Inashangaza kuona watu wakijichukulia sheria mikononi kupambana na makosa madogo kama vile uchangudoa. Inashangaza kuona watu wanakuwa na roho za kinyama hadi kuwachoma vibaka wanaotuhumiwa kuiba kuku na mikufu huku wakiwaramba miguu mafisadi wakubwa wanaoiba mabilioni! Ningetumia hata kura yangu kuwaondoa wezi na wala rushwa waliojazana bungeni wakipitisha kila aina ya dhuluma kwa taifa letu. Ningetumia kura yangu kuondoa Chama kinachoitwa cha Mafisadi. Ningetumia kura yangu kuhakikisha dhuluma inaondoka. Ningetumia dini yangu kupambana na mafisadi kwanza. Maana wao wanaliangamiza taifa kwa kuliweka rehani kwa mabwana zao waitwao wawekezaji wakati ni wachukuaji na wezi wa kawaida. Je tunafikiri kivivu na kinyumenyume au kichaa? Umalaya ni suala la mtu binafsi wakati ufisadi ni janga la kitaifa. Ingekuwa mimi ningeanza kuwakong'ota mafisadi ndipo nifikiri kuwachapa vyangudoa.

Saturday 28 July 2012

Kuna nini kwenye Mahama na umakamu wa rais Ghana?

Pia jina John nalo linatawala kwenye urais wa Ghana
John Kuffor, John Atta Mills na sasa John Mahama!


John Dramani Mahama rais mpya wa Ghana


Aliu Mahama makamu wa rais wa zamani wa rais wa Ghana

John Dramani Mahama rais mpya wa Ghana aliyechukua urais baada ya kifo cha rais John Atta Mills alikuwa makamu wa rais kuanzia mwaka 2009 hadi alipochukua nafasi ya bosi wake. Kuna jambo la kufurahisha. Ni kwamba mtangulizi wake kwenye nafasi ya umakamu wa rais naye aliitwa Mahama yaani Aliu Mahama amabaye alikuwa makamu wa rais kuanzia Januari 7, 2001 hadi  Januari 7, 2009.  Tofauti ni kwamba Mahama John ameweza kuwa rais wakati Mahama Aliu hakuwahi kuwa. Nani anajua huko tuendako?

Dawa za mgeuza mwanaume kuwa mwanamke

William McKee, now Mandi McKee, claims a baldness drug turned him into a woman. (Facebook)
William McKee (38) alijikuta kwenye wakati mgumu kutokana na uamuzi wake wa kutumia dawa ya kupambana na upara. Dawa hiyo aina ya Propecia imemgeuza McKee kuwa mwanamke jambo ambalo limemfanya aachane na mkewe waliyeishi kwa miaka 10. Ghafla alijistukia akiota matiti huku mapaja yake yakitanuka na kuwa na alama zote za mwanamke. Kwa sasa McKee amefadhaika na maisha yake yameanza kupoteza maana. Kwa habari zaidi BONYEZA hapa.

First lady alipobembezwa kama mtoto!


 Huyo si Hilary Clinton bali mwana mieleka wa Marekani  Helena Pirozhkova akimbeba Michelle Obama wakati wa shamra shamra za michezo ya Olimpiki inayofanyika jijini London Uingereza. Wenzetu wanajua kuchanganyikana na watu wakijua fika madaraka yao ni koti la kuazima. Hawajioni kama miungu-watu wetu wanaoogopa wale wale ambao kodi zao zinawalisha na kuwavisha wao familia zao na hata marafiki na washirika wao.

Friday 27 July 2012

Viongozi wa namna hii sijui kama wana akili sawa sawa?



Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein kaja na mpya. Eti ametoa amri kwa mamlaka ya Zanzibar kuhakikisha pesa ya kununulia meli kubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 1,000 na tani 100 za mizigo ndani ya wiki moja. Je hii maana yake ni kwamba serikali inafanya kazi kwa nguvu ya soda au inakurupuka? Je huu siyo mwanya wa kwenda kupata mikopo yenye masharti ya kinyonyaji ukiachia mbali wajanja wachache kutumia mwanya huu kujinufaisha? Je huku ni kutatua tatizo au ni kuwa sehemu ya tatizo? Viongozi wa namna hii wana akili sawa sawa au ni miradi yao ya sirini?

Usalama Wa Taifa Wakanusha Kumtesa DR.Ulimboka


Kama kweli huu ndiyo uwezo wa kufikiri wa chombo kinachoitwa Usalama wa Taifa basi tumekwisha. Ukisoma kanusho lao hapa chini, unagundua kuwa ima walioandika ni wahuni wa kawaida wasio na elimu ya kutosha ya chochote au wajinga wa kawaida wasiojua wanachosema. Hatutaki kuchambua tamko lote la 'Usalama wa Taifa' ila kilicho wazi kama kweli hili ndilo tamko tena jepesi na la hovyo kuhusiana na suala nyeti basi hawa si Usalama wa Taifa bali Balaa la Taifa au tuseme Uhasama wa Taifa. Msomaji soma mwenyewe uone hoja iliyotolewa isivyotoa majibu kwa swali lolote zaidi ya kuwa upuuzi wa kawaida unaolenga kuwafanya wananchi waonekane wapuuzi wa kuuamini upuuzi.


IDARA YA USALAMA WA TAIFA YAKANUSHA KUMTESA DR ULIMBOKA STEVEN

Katika siku za hivi karibuni, kumejitokeza taarifa zenye tuhuma kadhaa dhidi ya Idara ya Usalama wa Taifa. Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha Idara hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa wananchi.

Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dr. STEPHEN ULIMBOKA, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa mipango ya kuwadhuru baadhi ya Viongozi wa Vyama vya Upinzani. Gazeti moja la kila wiki limekuwa likurudia tuhuma hizo mara kwa mara kwa madai kwamba ni
habari za uchunguzi na kuihusisha Idara.

Idara inataka kuwahakikishia wananchi kwamba taarifa hizo ni za UZUSHI NA UONGO ambazo zina nia ya kuharibu jina na sifa ya Idara. Taarifa hizo zimekuwa zikiunganishaunganisha vipande vya taarifa mbalimbali
ili kukidhi malengo yaliyokusudiwa na wanaolitumiagazeti hilo. Idara haikuhusika wala haihusiki na matukio yoyote yaliyotajwa katika tuhuma hizo. Hivyo tunawaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo.

Matukio yaliyotajwa katika tuhuma hizo yanachunguzwa na Jeshi la Polisi ambacho ndicho Chombo Chenye Dhamana, na kwa Maslahi ya Taifa si vizuri kuachia upotoshaji huo uendelee.

Aidha, tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa uzushi na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Idara hazitatuvunja moyo bali zitatuunganisha na hivyo kutuimarisha katika azima yetu ya kuhakikisha nchi yetu inaendelea kubaki salama kwa kushirikiana na wanachi na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama.

Imetolewa na Idara ya Usalama wa Taifa,
Makao Makuu,
DAR ES SALAAM
26 Julai, 2012.

Thursday 26 July 2012

Mwanzo wa mwisho wa Bashar?



Kwa mujibu wa shirika la habari la Al Jazeera ni kwamba rais wa Syiria Bashar Asaad na kundi lake wanaweza kukabidhi madaraka wakati wowote. Al Jazeera lilimnukuu waziri mkuu wa Uturuki Recep  Teyyip Erdogan akisema kuwa ni suala la muda kwa Bashar na genge lake kukabidhi madaraka kwa umma. Erdogan alisema kuwa utawala mpya unaweza kuchukua hatamu wakati wowete. Hata Umoja wa Mataifa umeachana na juhudi zilizokuwapo za kujadiliana na wapinzani. Je mwanzo wa mwisho wa imla mwingine Bashar Asaad ndiyo umewadia? Nani atafuatia? Afrika Kusini mwa Sahara watakengeuka na kuzinduka toka usingizini? Time will surely tell.

Wednesday 25 July 2012

Vigogo wanapanda midege, sisi twapanda mimeli mibovu


NIKIWA nimeandamana na bi mkubwa wangu Mama Kidume, kwa majonzi na hasira na uchungu mkubwa, Mzee Mzima Alhaj, Dokta, Profesa, Kanali, Field Marshal, Shehe, Padre, Mtukufu Mpayukaji Msemahovyo nilijikusuru siku ya Alhamisi kwenda kuwafariji wafiwa kule Zenj.
Hii ni baada ya kuona wahusika wa misiba hii wakijifanya hamnazo wakijipeleka hata bila kuogopa kukong’otwa na walevi wanaowaua kwa uzembe na ufisi wao. Hawa walipaswa kupokewa kama si kupelekwa Segerea wakanyee debe kwanza. Hakuna kosa kubwa katika kaya kama kusababisha vifo vya wanakaya.
Mpayukaji alikumbuka jinsi alivyotua Mwanza mwaka 1995 na kukuta rais keshafika na bi mkubwa wake huku wakija mikono mitupu badala ya kutoa mdege wao kusafirisha waokoaji.
Ajabu wao waliwahi kufika hata kabla ya waokoaji wakati nao walipaswa kuokolewa kutoka kwenye ulimbukeni, roho mbaya na kupenda makuu. Huu ni uongozi au uongo tena zii.
Viongoziii kwa uongoziiii wao hawana maana wakati mwingine. Lisirikali lako linafanya uzembe hadi walevi wanavyotoka roho wewe unajifanya unawajali badala ya kujali hatua za usalama wa maisha yao.
Ningekuwa mimi nisingejipeleka kutia aibu. Badala yake ningeshughulikia upuuzi na uzembe vinavyoua walevi wetu. Ningejishughulisha na kuweka mfumo wa kuhakikisha vyombo vya usalama na huduma vinakuwa salama na vya haki badala ya huu upuuzi unaoendelea ambapo kila mwenye vijisenti vyake hujifanyia atakavyo kiasi cha kuangamiza walevi bila hatia.
Ungewaona wasanii hawa walivyokuwa wamekunja nyuso utadhani walikuwa na huzuni. Utadhani hawakujua kuwa maafa haya yangetokea. Hivi unategemea nini unapoacha kijiwe au kaya kila mtu ajifanyie atakavyo ilmradi apata mradi wake?
Unategemea nini unapokuwa bize kwenye uzururaji usishughulikie kile kilichokufanya usimikwe na kuwekwa ofisini? Hata hivyo, tusishangae. Ukimuona mamba anaulilia mzoga wa aliyemuua usidhani anasikitika zaidi ya kuwa machozi ya furaha.
Tukubaliane. Hata hawa simanzi zao zilikuwa si simanzi bali usanii na kujiaminisha kuwa wamefanikiwa kuwafunga kamba walevi kwa kujifanya wanajali wakati hawajali kitu zaidi ya matumbo yao. Ila waelewe.
Kuna siku isiyo na jina mambo yatabadilika na walevi watajitambua na kuamua kufanya kweli ili kujikomboa. Mamba watu ni viumbe wa hatari kuliko hata mamba wa kweli. Maana hayawani akitenda uhayawani ni saizi yake kuliko mja kutenda uhayawani bado akajiona mjanja kama hawa mamba watu. Pambaffu na kumbaff zenu sana na mshindwe na kulegea kama siyo kuteketea kama Mwamali Gadafififi.
Naona yule anatikisa kichwa kwa kusoma usongo huu. Ndiyo. Naandika kwa hasira leo. Maana hawa wanaotelewa kafara na uongozi ulioshindwa ni ndugu na jamaa zangu. Ni wenzangu. Ni walevi wenzagu sawa nawe. Hawa si jamaa wala ndugu wa rahisi na genge lake.
Wao wanapanda midege kwenda hata chooni wakati walevi wanapanda mikangafu ya magari na meli tena kwa kulanguliwa. Baada ya walevi kupoteza maisha eti lisirikali linakuja na sanaa kuwa litanunua meli! Kama siyo kamba kwanini hamkununua meli baada ya kutokea ajali mbili za mwanzo?
Kutokana na kuzidi mauaji yatokanayo na uzembe, kijiwe kina mpango wa kukaa na kupitisha hoja ambayo tutaipeleka Umoja wa Mataifa (UN) ima kudai uhuru upya ua kuundwa Mahakama ya kushughukia watawala wazembe wanaosababisha mauaji ya halaiki kama haya ya Zaainzibaa.
Mauaji ya namna hii hayana tofauti na mauaji ya kimbari ikizingatiwa kuwa wanaouawa ni watu wa mbari ya visiwani. Pia hata wanaouawa barabarani kutokana na matrafiki kupiga mabao wanapaswa kuwa chanzo cha kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Kuzuia Uzembe (MKKU) au International Tribunal on Irresponsible Governments and other Institutions (ITIGI).
Jamaa zangu wa Itigi msianze kujisifu kuwa mahakama hii kwa vile ina jina kama eneo lenu basi itakuwa na makao yake makuu Itigi. Mmenoa sana. Nani alete mahakama kama hii kwenye kaya ambapo mabalaa inayopaswa kuyashughulikia yanafanyika kuliko yoyote nyingine kwenye anga zake Wadudi?
Turejee kwenye mauaji ya halaiki ya Zaainziba. Mzee mzima nilikwenda kule nikiwa na mabirika kibao ya kahawa na magunia ya kashata ili kuwafariji wafiwa. Tofauti nami, wanasihasa wa hovyo si walikwenda na mikono yao na wake zao utadhani wale waathirika hawakuhitaji kitu cha kuwachangamsha!
Ajabu wanasiahasa hao hao waliamrisha hata mandata kuwapiga mibomu wana Uangusho ambao hawana tofauti na wao. Yaani mnaleta siasa kwenye misiba! Eti hawa nao wanajiita watu wa dini wakati ni watu wa shaitwan! Mnawezaje kuutumia msiba tena wa kaya kufanya siasa zenu za chuki za hatuutaki Muunganiko wakati wake na vitegemezi vyenu wamejazana huko bara mnakochukia.
Hivi mnamdanganya nani nyie? Ni upuuzi usio mpaka mtu kuwadanganya wengine naye akajidanganya. Bila Muunganiko hawa wanaoanza kudengua na kukufuru kwa sababu ya shibe watanywea. Mara hatutaki Muunganiko mara hivi. Bila Muunganiko wengine si mngekuwa msharejeshwa kwenu India na Arabuni? Kwani hatujui? Leo utasikia jitu likisema hapa wabara hawatakiwi wakati mababu zake waliotoka huko huko tena wengine waliletwa wakiwa na kamba shingoni kutoka Kongo, Malawi, Zambia na hata Angola.
Kweli nyani haoni kundulile! Hata hivyo niliwashangaa walevi walivyopigwa changa la macho kwa lisirikali uaji kuwafunga kamba kuwa litagharimia maziko na kutoa siku tatu za maombolezo kikaya.
Huu ni upuuzi. Badala ya kuahidi kuhakikisha waliosababisha maafa haya wanashughulikiwa mnacheza makidamakida siyo? Hata hivyo, nani angethubutu kuongelea haki na kuwakamata wahusika wakati wahusika na watuhumiwa wa mauaji haya ni wale wale waliokuwa wakijipiga vifua na kuapa kuwa wameguswa na msiba huu wa kujitakia?
Kwa vile nina uchungu na hasira sana, kama siyo kujihadhari naweza kuishia kufanya vitu vya ajabu nikaitwa na kuonekana gaidi bure. Maana siku hizi magaidi wanafanyiana ugaidi tofauti ni kwamba magaidi wanaochukiwa ni wale wasio na madaraka kwani hata huu msiba ni ugaidi wa kawaida.
Acha niende kupata gongo kidogo lau nitulize hasira. Baibai kutoka Bububu na ububu.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 25, 2012.

Huyu naye mtasemaje?


Mapishi, sanaa au matusi?


Tuesday 24 July 2012

Monsinyori afungwa kwa kuzaidia mapadre kunajisi


Monsignor William Lynn in March 2012
Ingawa miaka mingi imepita tangu kashfa ya uzinzi na unajisi kwenye kanisa la Katoliki ifumke, wengi wa waliotuhumiwa waliweza kupotea kimya kimya bila kufungwa. Monsinyori William Lynn wa Marekani amefungwa kwa miaka kuanzia mitatu hadi sita kwa kusaidia na kuficha visa vya uzinzi vya mapadre waliokuwa chini yake. Akiwa msimamizi wa mamia ya mapadre kwenye jimbo la Philadelphia alikokuwa katibu wa Dayosisi, Lynn anakuwa kiongozi wa kwanza wa juu kufungwa kwa kosa hili. Kwa habari zaidi BONYEZA hapa.

Je hiki ni kitu gani?


Breaking News rais Mills wa Ghana hatunaye







Kwa mujibu wa shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, rais wa Ghana John Atta Mills (68) (Pichani) amefariki dunia baada ya kuugua ghafla. Msemaji wake hakutoa maelezo zaidi kutokana na mstuko na pigo kwa taifa hili linaloelezeka kuwa miongoni mwa  nchi mfano mzuri kidemokrasia. Kwa habari zaidi BONYEZA hapa.