TAARIFA zilizotolewa na Benki ya Taifa ya Uswisi (SNB) kuwa wakubwa wachache wezi wa Tanzania wameficha zaidi ya shilingi 300,000,000,000 nchini humo ni za kusikitisha achia mbali kuhuzunisha hasa kwa nchi maskini na ombaomba kama Tanzania.
Kwa mujibu wa taaifa hizo ni kwamba kiasi tajwa cha pesa kilichofichwa nchini Uswisi ni malipo ya rushwa kwa watawala toka kwenye makampuni ya mafuta na madini.
Hii maana yake ni kwamba wakati umma unalalamikia mirahaba kidogo, pesa nyingi inaingia kwenye mifuko ya mafisi wachache. Hiyo pesa ni kubwa kwa viwango vyovyote. Na isitoshe si Uswisi tu wanakoficha pesa yetu.
Je ni kiasi gani kipo London, Paris, New York, Mumbhai na kwingineko? Je, ni kiasi gani kimefujwa humu nchini kwenye miradi ya kipuuzi kama kujenga mahekalu ya aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii Ezekiel Maige, kununua magari ya bei mbaya na upuuzi mwingine kama huo? Huu ni ushahidi tosha kuwa nchi yetu si maskini bali maskini ni utawala wetu uliokubali kulala kitanda kimoja na ufisadi huu wa kunuka.
Ajabu wakati pesa kubwa kama hii inaozea nje, nchi yetu haina hata pesa ya kulipa stahiki za madaktari. Wanagoma hadi kusababisha misiba kwa watu wetu ukiachia mbali wahusika kukwepa kutumia akili na badala yake kutumia uhuni kama kuwateka na kujaribu kuwaua ili kuwanyamazisha madaktari.
Kwa wanaojua ubovu wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) walisikitika na kushangaa kusikia kinara wake Dk. Edward Hosea akisema kuwa TAKUKURU itahakikisha hiyo pesa iliyofichwa nje inarejeshwa nchini.
Kwa kujitafutia umaarufu, Hosea alikaririwa akisema kuwa TAKUKURU inawasiliana na mamlaka nchini Uswisi. Huu ni uongo na njia nyingine ya kujitafutia rushwa zaidi. Kwani wakati hiyo pesa ikifichwa huko nje TAKUKURU ilikuwa wapi zaidi ya kuwaonea vidagaa huku ikiwagwaya mapapa?
Waulize TAKUKURU walifanya nini kwenye sakata la ufisadi wa Richmond zaidi ya kuwasafisha wahusika kabla ya Bunge kushituka na kuunda Kamati Teule iliyomuondoa madarakani aliyekuwa Waziri Mkuu Edward Lowassa? Kama TAKUKURU wanataka kutuaminisha kuwa wanaweza kupambana na mtandao huu wa kifisadi ni kwanini hawakumfungulia mashitaka Lowassa baada ya kukiri kwa njia ya kujiuzulu?
Kwanini TAKUKURU haihoji uhalali wa Lowassa kuendelea kulipwa pesa ya umma kama stahiki ya kustaafu wakati hakustaafu zaidi ya kuwajibishwa kisheria? TAKUKURU wameshughulikia vipi suala na “vijisenti” vya rada ambapo vigogo wawili yaani Mbunge wa Bariadi Mashariki na Waziri wa zamani na Mwanasheria Mkuu Andrew Chenge na Gavana wa zamani wa Benki kuu, Dk. Idris Rashid walitajwa moja kwa moja?
Kwanini TAKUKURU haikuwafungulia mashitaka wala kujaribu kufanya hivyo kama kweli inapaswa kuaminika? Waulize TAKUKURU walifanya nini kuhusiana na wizi wa EPA hasa kampuni la Kagoda linalohusishwa na aliyekuwa Mbunge wa Igunga Rostam Aziz aliyejiuzulu ubunge baada ya kutuhumiwa gamba kabla ya rais Jakaya Kikwete hajagwaya kuyashughulikia magamba mengine yaani Chenge, Rashidi na Lowassa?
Waulize TAKUKURU kwanini vitendo vya rushwa vinazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka nchini wakati yenyewe ikiwa bize kwenye kutafuta rushwa hiyo hiyo kwa masilahi ya watumishi wake? kama Watanzania wataendelea kufanya makosa kuiamini TAKUKURU basi huu utakuwa ni kupoteza wakati. Kama tunataka kupambana na rushwa na sio kuipamba, lazima tuiondoe TAKUKURU isiwe chini ya ofisi ya rais.
Hiyo ni kutokana na ukweli kuwa Rais anaweza kuitumia apendavyo hasa pale yeye au watu wake wa karibu wanapotuhumiwa. Na hili si dhana tu. Limeishatokea. Kwa kumbukumbu ni kwamba mwanasheria Michael Bhindika Sanze aliyeshuhudia na kuratibu mpango mzima wa wizi wa EPA aliwataja wazi wazi Rais Kikwete, Rais Mstaafu, Peter Noni, Mwanaidi Majaar na wengine wengi. Kutokana na kuguswa rais na wazito wenzake, TAKUKURU iligwaya kuwashughulikia.
Nani anaweza kuukata mkono unaomlisha? Nani mara hii kasahau kukiri kwa Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Hosea, kipindi fulani kwa mwanadiplomasia wa nchi moja ya kigeni kuwa rais alikuwa akiikwamisha taasisi yake ingawa baadaye alikana baada ya kashfa hii kufichuliwa na wikileak?
Hatuongelei umbea wala uzushi. Jiulize watajwa kwenye kashfa ya EPA waliotajwa hapo juu wako wapi? Noni ni mkurugenzi wa Benki ya Raslimali, Majaar ni balozi Marekani na Mkapa pamoja na kashfa yake ya Kiwira kuendelea kujitokeza tuliambiwa tumwache apumzike na mkewe na wakwe na marafiki zake walioshirikiana kwenye ufisadi huu.
Mfano mwingine ni kutuhumiwa kwa aliyekuwa katibu mkuu wa wizara Maliasili na Utalii wa zamani alishutumiwa kwa kutoa vibali vya kusafirisha wanyama nje. Kabla ya hata kuundwa tume ya kuchunguza, rais alimpa nafasi ya kuwa balozi wa Uganda.
Je, TAKUKURU haiyajui au kuyaona haya? je imefanya nini kuhakikisha haki inatendeka? Je, rushwa ni ile pesa inayotolewa kwa watu wadogo hata mazingira ya ulaji wowote ni rushwa inayoweza kuchunguzwa?
Kama TAKUKURU ingekuwa na meno au kuwa pale kupambana na rushwa, bila shaka ingeingilia kati kuzuia uteuzi wa Komba kuwa balozi wakati akikabiliwa na shutuma. Turejee kwenye ufisadi wa wazi.
Waulize TAKUKURU wameshughulikia vipi tuhuma za Maige alinunua nyumba kwa pesa dola 700, 000. TAKUKURU imeishachukua hatua gani? ‘God knows’. Je, TAKUKURU kuhusiana na ufisadi wa kuficha pesa Uswisi inataka kumdanganya nani wakati nayo ni mshirika au mwezeshaji kutokana na mifano hai tuliyotoa hapo juu?
Hebu tumalizie na maneno ya Hosea mwenyewe uone ni upogo kiasi gani kuiamini TAKUKURU. “Tutakapogundua fedha hizo zimetoka wapi, tutafuata taratibu zinazohusika kuhakikisha zinarudi nchini. Tutatumia sheria zilizopo katika nchi hizi.” Taarifa zilizotolewa tena za uhakika zinasema kuna pesa imefichwa Uswisi. Yeye anasema kama watagundua kana kwamba taarifa husika ni za uongo au uzushi! Hii ni ajabu kabisa.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 11, 2012.
No comments:
Post a Comment