Wednesday, 25 July 2012

Vigogo wanapanda midege, sisi twapanda mimeli mibovu


NIKIWA nimeandamana na bi mkubwa wangu Mama Kidume, kwa majonzi na hasira na uchungu mkubwa, Mzee Mzima Alhaj, Dokta, Profesa, Kanali, Field Marshal, Shehe, Padre, Mtukufu Mpayukaji Msemahovyo nilijikusuru siku ya Alhamisi kwenda kuwafariji wafiwa kule Zenj.
Hii ni baada ya kuona wahusika wa misiba hii wakijifanya hamnazo wakijipeleka hata bila kuogopa kukong’otwa na walevi wanaowaua kwa uzembe na ufisi wao. Hawa walipaswa kupokewa kama si kupelekwa Segerea wakanyee debe kwanza. Hakuna kosa kubwa katika kaya kama kusababisha vifo vya wanakaya.
Mpayukaji alikumbuka jinsi alivyotua Mwanza mwaka 1995 na kukuta rais keshafika na bi mkubwa wake huku wakija mikono mitupu badala ya kutoa mdege wao kusafirisha waokoaji.
Ajabu wao waliwahi kufika hata kabla ya waokoaji wakati nao walipaswa kuokolewa kutoka kwenye ulimbukeni, roho mbaya na kupenda makuu. Huu ni uongozi au uongo tena zii.
Viongoziii kwa uongoziiii wao hawana maana wakati mwingine. Lisirikali lako linafanya uzembe hadi walevi wanavyotoka roho wewe unajifanya unawajali badala ya kujali hatua za usalama wa maisha yao.
Ningekuwa mimi nisingejipeleka kutia aibu. Badala yake ningeshughulikia upuuzi na uzembe vinavyoua walevi wetu. Ningejishughulisha na kuweka mfumo wa kuhakikisha vyombo vya usalama na huduma vinakuwa salama na vya haki badala ya huu upuuzi unaoendelea ambapo kila mwenye vijisenti vyake hujifanyia atakavyo kiasi cha kuangamiza walevi bila hatia.
Ungewaona wasanii hawa walivyokuwa wamekunja nyuso utadhani walikuwa na huzuni. Utadhani hawakujua kuwa maafa haya yangetokea. Hivi unategemea nini unapoacha kijiwe au kaya kila mtu ajifanyie atakavyo ilmradi apata mradi wake?
Unategemea nini unapokuwa bize kwenye uzururaji usishughulikie kile kilichokufanya usimikwe na kuwekwa ofisini? Hata hivyo, tusishangae. Ukimuona mamba anaulilia mzoga wa aliyemuua usidhani anasikitika zaidi ya kuwa machozi ya furaha.
Tukubaliane. Hata hawa simanzi zao zilikuwa si simanzi bali usanii na kujiaminisha kuwa wamefanikiwa kuwafunga kamba walevi kwa kujifanya wanajali wakati hawajali kitu zaidi ya matumbo yao. Ila waelewe.
Kuna siku isiyo na jina mambo yatabadilika na walevi watajitambua na kuamua kufanya kweli ili kujikomboa. Mamba watu ni viumbe wa hatari kuliko hata mamba wa kweli. Maana hayawani akitenda uhayawani ni saizi yake kuliko mja kutenda uhayawani bado akajiona mjanja kama hawa mamba watu. Pambaffu na kumbaff zenu sana na mshindwe na kulegea kama siyo kuteketea kama Mwamali Gadafififi.
Naona yule anatikisa kichwa kwa kusoma usongo huu. Ndiyo. Naandika kwa hasira leo. Maana hawa wanaotelewa kafara na uongozi ulioshindwa ni ndugu na jamaa zangu. Ni wenzangu. Ni walevi wenzagu sawa nawe. Hawa si jamaa wala ndugu wa rahisi na genge lake.
Wao wanapanda midege kwenda hata chooni wakati walevi wanapanda mikangafu ya magari na meli tena kwa kulanguliwa. Baada ya walevi kupoteza maisha eti lisirikali linakuja na sanaa kuwa litanunua meli! Kama siyo kamba kwanini hamkununua meli baada ya kutokea ajali mbili za mwanzo?
Kutokana na kuzidi mauaji yatokanayo na uzembe, kijiwe kina mpango wa kukaa na kupitisha hoja ambayo tutaipeleka Umoja wa Mataifa (UN) ima kudai uhuru upya ua kuundwa Mahakama ya kushughukia watawala wazembe wanaosababisha mauaji ya halaiki kama haya ya Zaainzibaa.
Mauaji ya namna hii hayana tofauti na mauaji ya kimbari ikizingatiwa kuwa wanaouawa ni watu wa mbari ya visiwani. Pia hata wanaouawa barabarani kutokana na matrafiki kupiga mabao wanapaswa kuwa chanzo cha kufungua kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Kuzuia Uzembe (MKKU) au International Tribunal on Irresponsible Governments and other Institutions (ITIGI).
Jamaa zangu wa Itigi msianze kujisifu kuwa mahakama hii kwa vile ina jina kama eneo lenu basi itakuwa na makao yake makuu Itigi. Mmenoa sana. Nani alete mahakama kama hii kwenye kaya ambapo mabalaa inayopaswa kuyashughulikia yanafanyika kuliko yoyote nyingine kwenye anga zake Wadudi?
Turejee kwenye mauaji ya halaiki ya Zaainziba. Mzee mzima nilikwenda kule nikiwa na mabirika kibao ya kahawa na magunia ya kashata ili kuwafariji wafiwa. Tofauti nami, wanasihasa wa hovyo si walikwenda na mikono yao na wake zao utadhani wale waathirika hawakuhitaji kitu cha kuwachangamsha!
Ajabu wanasiahasa hao hao waliamrisha hata mandata kuwapiga mibomu wana Uangusho ambao hawana tofauti na wao. Yaani mnaleta siasa kwenye misiba! Eti hawa nao wanajiita watu wa dini wakati ni watu wa shaitwan! Mnawezaje kuutumia msiba tena wa kaya kufanya siasa zenu za chuki za hatuutaki Muunganiko wakati wake na vitegemezi vyenu wamejazana huko bara mnakochukia.
Hivi mnamdanganya nani nyie? Ni upuuzi usio mpaka mtu kuwadanganya wengine naye akajidanganya. Bila Muunganiko hawa wanaoanza kudengua na kukufuru kwa sababu ya shibe watanywea. Mara hatutaki Muunganiko mara hivi. Bila Muunganiko wengine si mngekuwa msharejeshwa kwenu India na Arabuni? Kwani hatujui? Leo utasikia jitu likisema hapa wabara hawatakiwi wakati mababu zake waliotoka huko huko tena wengine waliletwa wakiwa na kamba shingoni kutoka Kongo, Malawi, Zambia na hata Angola.
Kweli nyani haoni kundulile! Hata hivyo niliwashangaa walevi walivyopigwa changa la macho kwa lisirikali uaji kuwafunga kamba kuwa litagharimia maziko na kutoa siku tatu za maombolezo kikaya.
Huu ni upuuzi. Badala ya kuahidi kuhakikisha waliosababisha maafa haya wanashughulikiwa mnacheza makidamakida siyo? Hata hivyo, nani angethubutu kuongelea haki na kuwakamata wahusika wakati wahusika na watuhumiwa wa mauaji haya ni wale wale waliokuwa wakijipiga vifua na kuapa kuwa wameguswa na msiba huu wa kujitakia?
Kwa vile nina uchungu na hasira sana, kama siyo kujihadhari naweza kuishia kufanya vitu vya ajabu nikaitwa na kuonekana gaidi bure. Maana siku hizi magaidi wanafanyiana ugaidi tofauti ni kwamba magaidi wanaochukiwa ni wale wasio na madaraka kwani hata huu msiba ni ugaidi wa kawaida.
Acha niende kupata gongo kidogo lau nitulize hasira. Baibai kutoka Bububu na ububu.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 25, 2012.

No comments: