The Chant of Savant

Saturday 31 December 2016

We Wish You a Very Spiffy New Year 2017

Image result for happy new year

Mlevi kuanzisha kanisa la Upasho na Vitisho na Mipayuko

            Baada ya kuona walevi wenzangu tena vihiyo na wasio na ujanja hata nusu yangu wakianzisha madhehebu yao na kuukata, nami nimeamua nianzishe kitu hii lau niweze kuendesha michuma ya “zawadi’ nitakapowakuna kwa vituko na ulevi wangu kama jamaa yangu Lusekelela. Nani asiyetaka kuukata hata kama ni kitapeli? Kuukata ni kuukata bila kujali umepata namna gani.
            Baada ya kuanzisha dhehebu langu likalaoitwa Upasho, nitajipachia cheo cha Mtume ili kuvutia wateja wa biashara yangu hii mpya. Kama haitoshi, nitatangaza kuwa natenda miujiza kupitia maombi. Mimi ni specialist wa kuombea wagumba, maskini na wanaougua miwaya.
            Baada ya kuwa nimepata njuluku ambazo zitamwagika kama mana kwa wana wa Israel mwenda usiku, lazima nichape kanywaji kama sina akili nzuri. Niatakuwa na uwezo wa kukata bia na whisky na siyo mataputapu niliyozoea pale Kwa Mfuga Dog na Uwanja wa Hyena.
            Najua kuna wanoko wengi wanaoitwa waandishi wa habari. baada ya kuwa nimepiga mma, hata kama nitaangusha gari na kufanyiwa kitu mbaya wao inawahusu nini?
 Nitoe onyo. Watakaoniandika vibaya nawapiga mkwara kuwa watakufa ndani ya miezi mitatu. Ili kuhakikisha wananyotoka roho lazima niwakodishe wanyotoaji roho wawanyotoe roho halafu nitangaze kuwa nilitabiri vifo vyao ambavyo vitatokana na kunishfu mimi mlevi wa God.
            Tokana na kaya yetu kutoa misamaha kwa madhehebu ya kidini, nitaanza kuwasaka wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi ili watumie dhehebu langu kuingizia biashara zao ambazo nitazitangaza kama misaada kwa dhehebu langu. Kwa vile hakuna cha bure duniani, mie nitawatoza kodi kidogo na kuukatata. Bila shaka hapa nitapata midola na kununua migari ya bei mbaya halafu nawahadaa walevi kuwa nimepewa zawadi na watoaji ambao hawapendi kutangazwa majina yao.
            Ili kuputa njuluku lazima mbali na kutegemea kupitishia wafanyabiashara mizigo yao, lazima niuze bwimbwi kama sina akili nzuri. Nikichanganya na njuluku nitakazowatoa wasaka miujiza, bila shaka nitaukata haraka iwezekanavyo. 
            Kuna kipindi nilipanga nilipanga kuingia kwenye siasa na kuanzisha chama cha familia yangu ambapo mimi nitakuwa mwenyekiti wa maisha na ndugu na jamaa zangu vigogo wa chama. Lakini tokana na kuwa kule kuna kukaguana namna mlevi alivyochuma, siendi.   Baada ya kuingia kwa dokta Kanywaji, naona kama siasa hazilipi kama mwanzo. Sitashangaa kusikia siku moja akiweka masharti juu ya namna ya kutumia ruzuku vipatavyo vyama vya kisiasa. Hivyo, nimeonelea kuanzisha dhehebu badala ya chama.
            Kwanza, kuendesha chama ni ugonjwa wa moyo hasa unapokuwa king’ang’anizi kama mimi. Kule wanataka demokrasia wakati kwenye neno la Bwana unakuwa wewe ndiyo kila kitu.
            Pili, kwenye vyama kuna fitina kibao. Wanaingia na kutoka tokana na kila mmoja kuwa na misheni yake kwenye siasa. Kwenye dini ukishajipachika cheo chako bab kubwa, hakuna mpinzani wala wa kukubughudhi. Unakusanya kodi mwenywe, unatumia mwenyewe; na hakuna wahasibu wa lisirikali kuja kuumbua ulaji wako. Hata ukinunua mchuma wa bei mbaya na kujipa kama zawadi halafu ukatangaza kuwa umepewa zawadi, hakuna sheria ya maadili itakayokubana kama wanasiasa. Huku ni madili matupu. Wakati kweney siasa ni maadili matupu. Kwenye dini unabukanya kama utakavyo huku ukizidi kuwahimiza waumini kutoa sana ili Mungu ‘awazidishie” hata kama si kweli. Who cares?  Afadhali nianzeshe dhehebu langu la upasho na vitisho na mipayuko huku nikiendelea kupiga kanywaji kama sina akili nzuri.
            Kwa vile nimemaliza na kuanza mwaka mpya, haya ndiyo maazimio yangu ya mwaka mpya. Huu ni mwaka wa upasho, kupiga kanywaji na kuendesha michuma ya bei mbaya nitakayonunua na kudanganya nimepewa zawadi. Tuonane wiki ijayo kwa mipango mingine babu kubwa.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

Thursday 29 December 2016

Akina Lusekelo wachunguzwe na “zawadi” zao

Image result for photos of anthony lusekelo
         Image result for photos of anthony lusekelo
Baada ya kukumbwa na kashfa ya kile kilichoripotiwa na vyombo vya habari kama ulevi na kuonyesha tabia mbaya, mchungaji Anthony Lusekelo ametoa mpya mbili za kufungia mwaka. Moja ni kuwaombea waandishi wa habari walioandika habari za kashfa yake wafe. Amesema kama hawatakufa ataacha kuhubiri akauze gongo. Sijui kwanini amechagua gongo na si nyanya au hata kuuza vitabu vya neno. Lusekelo ametoa hadi mwezi wa tatu mwakani jambo ambalo limeshangaza wengi. Kwani mtu wa kweli wa Mungu tena anayehubiri neno la Mungu asingekuwa mtu vitisho, kushabikia kifo wala kulipiza visasi kwa makosa aliyotenda kutokana na kutokuwa makini. Hivi Yesu anayehubiriwa na wachungaji aina ya Lusekelo angekuwa kama wao kweli kungekuwa na kanisa hata moja? Je Lusekelo tutamtofautishaje na wale manabii wa uongo aliotahadharisha Yesu kama mambo yake ni hivi? Je Lusekelo alitoa tishio hili ili kuwafanya waandishi wa habari wagwaye kuripoti uoza wake kama kiongozi wa kiroho anayepaswa kuwa kioo cha jamii? Kwa wale waliotishiwa maisha, wanapaswa kuripoti polisi ili lolote likiwatokea Lusekelo awajibishwe kisheria. Maana, hakuna anayejua atakavyowaua hasa katika dunia hii yenye watu rangi mbili. Isije mkatumiwa wauaji au kupewa hata sumu au kugongwa akaishia kujisifu kuwa alitabiri wakati kuna mkono wa mtu.  Nani alijua kuwa baadhi ya wachungaji wangesafirisha mihadarati au taasisi zao kukwepa kulipa kodi, kulipia umeme hata kutoa utabiri wa uongo na kufanya mambo ya kishirikina na kitapeli? Wangapi wako kwa pilato wakishitakiwa na waumini wao waliowatapeli au kuwanyonya na kuwaibia?
             Sasa kama anadhani wote wanaogopa kifo kana kwamba yeye ataishi milele, basi mie naandika tena kwa uchambuzi wa kina na afanye atakavyo. Sidhani kama Mungu ni wa hovyo kiasi hiki kiasi cha kila anayetaka kumtumia anamtumia utadhani ni bunduki yake. Mungu, tena wa kikristo, ni mwenye rehema na si Mungu wa visasi vinginevyo Lusekelo angetafuta mahali pengine pa kufanyia biashara zake. Mungu si mjinga kiasi cha kumlipizia kisasi mkosefu aliyejichafua akasingizia wenzake wanamchafua.
            Pili vyombo vya habari viliripoti kuwa Lusekelo, baada ya kukumbwa na kashfa ya ulevi, eti alipewa zawadi ya magari mawili mojawapo likiwa Toyota Land Cruiser yenye thamani ya shilingi za kitanzania milioni 200. Sijui kama kweli hawa wanaokuja na sanaa kama hizi wanajua ukubwa wa fedha wanayotaja. Je ni nani hao ambao Lusekelo hawataji waliompa zawadi kubwa hivyo? Je wana utajiri kiasi gani na wameupataje? Mbona maaskofu tena wa kweli kama mhashamu Polycarp Pengo au Shehe Mkuu hatusikii wakipewa zawadi kama hizo? Je serikali itaacha watu watengeneze fedha kiharamu na kuzitakatisha kwa njia rahisi kama hii? Je hawa watoaji wanafanya biashara gani na wanalipa kodi kiasi gani?
            Kuondoa utata, Lusekelo anapaswa kutaja majina ya waliompa magari husika vinginevyo yakamatwe hadi afanye hivyo ili kuchunguza kama ni halali au ni hila mojawapo ya kuhalalisha utajiri haramu na wa kificho. Haiwezekani usawa huu ambapo watu wengi wanalalamikia ukosefu wa fedha tokana na serikali kuziba mianya ya rushwa na wizi watokee watu tena wasiotajwa majina watoe zawadi kubwa kiasi hiki. Kwa lipi kama siyo sanaa? Je ni wangapi wa aina hii wanaogeuza nchi yetu hamnazo kiasi cha kufanya michezo ya ajabu kama hii? Nimeandika wiki chache zilizopita kuwa hata viongozi wa dini wachunguzwe kwa vile ni watanzania na viongozi wa umma. Napendekeza itungwe sheria ya kushughulikia zawadi kama hizi za akina Lusekelo sawa na inavyowabana viongozi wa serikali. Hii ni kwa sababu zawadi zile zinatokana na madaraka ya umma aliyo nayo mhusika. Hivyo, zawadi zozote anazopewa hazipaswa kuwa mali binafsi kama kweli tutataka kujenga taifa la wawajibikaji na lisiloruhusu wachache kutumia nafasi zao za uma kujineemesha. Kama sheria kama hii itatungwa, inaweza kuzuia au kuondoa motisha wa baadhi ya matapeli kuunda madhehebu ya kidini kwa nia ya kuyatumia kujitajirisha.
            Tumalizie kwa kumtaka Lusekelo aache vitisho na awataje hao wafadhili wake wenye fedha za kumwaga kiasi hicho. Pia namshauri asome Biblia, Mathayo 18:22 pale Yesu anapoulizwa kama alisema kuwa tunapaswa kusamehe mara saba na akajibu tusamehe mara sabini na saba. Pia asome Mathayo 6: 15-15 isemayo, usiposamehe hutasamehewa. Zipo aya nyingi tu ambazo zinaweza kumpa mwanga  Lusekelo akaondoka na aibu na dhambi hizi anazotenda za kujifanya Mungu. Haiwezekani kiumbe dhaifu na mchafu kama mwanadamu akamuamuru Mungu kufanya uovu wala kuruhusu mhusika afanye uovu. Wakati huu si wa kutishana bali kujadiliana.  Ama kweli Yesu alisema, watakuja manabii wengi wa uongo na watadanganya wengi; na pia miti mizuri hutoa matundo mazuri na miti mibaya kadhalika na utaijua kwa matunda yake, Mathayo 7: 16-20. Hapa busara ya Yesu inasema mengi kuhusiana na Lusekelo, vitisho, na vitendo vyake bila kusahau na hizo tabia na “zawadi” zake.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.

Kakoko wataje wanasiasa wanaotaka kukukwamisha bandarini

            Hivi karibuni, vyombo vya habari vilipoti kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari (TPA) Deusdedit Kakoko akisema “wapo wanasiasa wakubwa wakiwamo wabunge wananiambia kwamba vita ya flow mita kamwe sitaiweza, nawaambia sitaki kuingiliwa na mwanasiasa yoyote nitafanya kazi zangu kulingana na maagizo ya Rais John Magufuli, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi na Mawasiliano (Profesa Makame Mbarawa).” Je haya ni ya kweli; na kama ni ya kweli, kulalamika kunatosha?
            Ukiangalia nafasi ya Kakoko, madai yake na aliwaowatuhumu utagundua kuwa haya ni madai mazito yanayohusu mambo mazito na watu wazito. Hivyo, hayawezi kuchukuliwa kirahisi na kuacha yapite bila kudurusiwa. Kwanza, tunadhani Kakoko hakukurupuka wala kutaka sifa hasa ikizingatiwa kuwa, kwa nafasi yake, hana sababu ya kufanya hivyo.
            Pili, tunadhani mtoa madai, kisheria, ana wajibu wa kuthibitisha madai yake kwa kutoa ushahidi. Je hao wanaomtishia Kakoko kuhusiana na kutaka kulinda ufisadi kwenye mita za kupimia mafuta ni akina nani? Kakoko anapawa kuwataja ili watanzania wawajue wanaotaka kuwakwamisha ukiachia mbali rais kuwajua na kuwatumbua haraka iwezekanavyo?
            Tatu, tunamtaka na kumshauri Kakoko awataje haraka ili kuondoa mazoea ya baadhi ya wakubwa wanaotumia dhamana ya umma kutoa madai mazito juu ya mambo nyeti bila kutoa ushahidi wa kile wanachodai. Haya yameanza kuwa mazoea ya ajabu. Bila kutoa maelezo na ushahidi Kakoko anarejea kile kilichotokea hivi karibuni kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda aliyedai kutaka kuhongwa milioni 50 kwa mwezi ili aruhusu shisha liuzwe ukiachia. Hadi tunaandika, Makonda ima kwa hiari au kulazimishwa na vyombo husika hajatoa ushahidi kuhusiana na madai yake makubwa hivyo tena yanayowahusu wakubwa. 
            Mbali na Makonda, Waziri wa Ardhi, William Lukuvi naye aliyewahi kutoa madai kama haya bila kutoa ushahidi kuwa kuna walanguzi wa ardhi walitaka kumhonga mabilioni ya shilingi bila ya wahusika kuwataja waliotaka kufanya hivyo. Kama Makonda, vyombo husika havijambana mhusika kutoa ushahidi ili kuwashughulikia wahusika.  Ni ajabu kuwa hata vyombo vinavyoshughulikia jinai kama hizi vimekaa kimya bila kutoa maelezo ni nini kimefuatia na ni nani walitaka kutenda makosa haya. Je hawa wakubwa wanaotoa madai bila kutoa ushahidi si washirika wa wale wanaowatuhumu hasa ikizingatiwa kuwa wameamua kuficha majina yao kwa faida wajuazo? Je umma utaendelea kugeuzwa mabwege wa kupokea kila uongo unaolenga kuwajenga wahusika na kuwaonyesha kama wachapakazi waaminifu wakati ukweli wa mambo unaweza kusema tofauti?
            Kakoko kama mtendaji mkuu wa TPA anapaswa ataje majina ya hawa wanasiasa ili washughulikiwe. Sijui wananchi waliomchangua na kumtuma mbunge awawakilishe akaishia kujiwakilisha na kuhujumu taifa lao watajisikiaje watakapogundua kuwa yule waliyedhani ni mbunge wao si wao bali mbunge wa tumbo lake? Hapa ndipo ulazima wa kuwataja watuhumiwa unakuwa muhimu zaidi. Kwani, utawasaidia wananchi wanaowakilishwa na wabunge kama hawa matapeli kujua la kufanya ili kupata mtu safi wa kuwawakilisha bungeni.
            Je baada ya hao wanasiasa wakubwa kutaka kumkatisha tamaa, Kakoko amechukua hatua gani? je aliwahi kuwambia bosi wake ili awatumbue? Je kimya chake kuhusiana na kutochukua hatua mujarabu zinaashiria nini na kujenga dhana gani? Je Kakoko aliogopa nini kuwataja wahusika au kuwaripoti kwa bosi wake kama hakuna namna? Je Kakoko alipotoa madai yake kwa vyombo vya habari alijua namna umma utakavyoyatafakari na kuyafanyia kazi? Ni ajabu.kama mtumishi na kiongozi wa umma wa nafasi na hadhi kama ya Kakoko sawa na Lukuvi na Makonda hajui taratibu za kisheria katika hali kama hii? Je hawa wanangoja nini kwenye ofisi za umma wakati wanaonyesha wazi wasivyofaa?
            Madai ya Kakoko, sawa na ya Lukuvi na Makonda yanaweza kuonekana kama poroja za kisiasa za kutafuta umaarufu kama wataendelea kukalia taarifa nyeti kama hizi zinazoweza kutusaidia katika kupana na ufisadi. Sijui kama rais au wasaidizi wake walisoma habari hii. Je kama waliisoma, wanangoja nini kuchukua hatua au ni yale yale ya kulindana? Sitaki niamini hivyo. Hata hivyo, tokana na unyeti wa safu hii, naamini wahusika wote watapata taarifa juu ya namna umma tunavyofanyia kazi madai yao. Haiingii akilini kwa watendaji wanaojua wazi kuwa wanachoambiwa kufanya ni jinai wakae kimya bila kuwa na maslahi binafsi au mapungufu kiutendaji. Hata kama wahusika ni vipenzi na jamaa za waliowateua, wanapaswa kufahamu kuwa wanashughulikia umma wenye watu wenye akili na wengine hata taaluma kuliko wao. Wanapaswa kujua umma wa wa-Tanzania si mazuzu wa kuweza kupokea machukizo kama habari za furaha kama ilivyo kwenye kadhia hii tunayoongelea leo.
            Tumalizie kwa kumtaka Kakoko achague moja. Ima awataje wahusika huku akiomba msamaha kwa kutochukua hatua mujarabu au aachie ngozi ili kuendelea kuwalinda hao wenzake. Pia tunamshauri rais awe mwepesi wa kuwatumbua watendaji wanaotoa habari za hovyo zinazoonyesha uzembe wao kama hawa watatu tajwa kwenye makala hii bila kujali ukaribu wake nao. Tunadhani Kakoko amepata ushauri wa kutosha. Hivyo, tunangoja utekelezaji. Tunaomba kutoa hoja.
Chanzo: Tanzania Daima jana Jumatano.

Kijiwe chashanga kaya kubinafsishwa kwa magabacholi

Mpemba anaonakena ana ishu inayomkera. Ameingia akiwa na gazeti mkononi huku akisonya nakutikisa kichwa. Kwa waliomzoea, wanajua kuna jambo linamkera.
Mbwamwitu anamuuliza “Mgoshi mbona unaonekana kukereka kunani tukusaidie?”
            “Yakhe we niache. Kwani hukusikia eti magabacholi wawili wamedai wilaya na Nkuranga ni mali yao? Kama hujasoma basi chukua gazeti usome.” Anampasia Mbwamwitu gazeti la Danganyika Daima.
Kichwa cha habari gazeti kimeandika “Magabacholi Wawili Wadai Wana Hati Milki ya Wilaya ya Nkuranga.”
            Habari inayofuata inasema “Magabacholi wawili Mahanji na Kahanji wametoa notisi kwa wakazi wa Wilaya na Nkuranga kuhama mara moja ili kuondoka kwenye ardhi wanayosema wamekuwa wakiimilki tangu walipogawiwa na Nkoloni.”
            Kapende anaamua kutia guu na kusema “mimi nilidhani kaya yetu ilikuwa huru tangu mwaka 61 kumbe nilikosea! Sasa inakuwaje magabacholi wawili, tena bila aibu, wanaweza kudai kuwa wilaya nzima ni mali yao? Hapa lazima kuna tatizo tena kubwa.”
            Msomi Mkatatamaa naye hangoji. Anakula mic “usemayo kaka yana mashiko. Lazima kutakuwa na tatizo tena kubwa tu. Nadhani nichukue fursa hapa kumtaka rais Joni Kanywaji awatumbue hawa jamaa ili waende kwao India na kudai ardhi kule. Ni ajabu. Hawa inaona hawaheshimu uhuru wetu tulioupata toka kwa manyang’au waliotuletea balaa hili la mijitu mibaguzi inayodhani sisi ni manyani wasio na akili hata kujua kuwa hii kaya ni mali yetu tuliyopewa na Muumba mwenyewe. Hapa bila shaka kutakuwa na wapiga dili waliowapa hizo hati feki. Je kwanini tusiwatokee na kuwatimua kama lisirikali linawagwaya kama ambavyo limekuwa likifanya siku zote?”
            Mipawa anakula mic “wala mie sishangai. Tumejiruhusu kuchezewa na kudhalilishwa kama vile tu hamnazo. Inakuwaje wanahizaya hawa wanaweza kudiriki kututia midole machoni bila woga wala aibu? Lazima kuna namna. Haiwezekani magabacholi wadiriki hata kuwafukuza viongozi wetu wastaafu wasiwe na kinachowapa hiki kiburi cha ajabu. Sasa kama wanaweza kudai wilaya nzima ni mali yao, watashindwaje kusema hata ikulu ni mali yao?”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu na kuronga “habari hii imenitia kichefuchefu na kuharibu siku yangu. Hapa lazima wanene wetu watueleze: kunani kama si ubwege na kutojiamini? Hamkumsikia yule gabacholi Maanji anayejidai kuwa bilionea alivyopeleka mikataba feki kwa pilato. Hii ni dharau kiasi gani wajameni? Hapa lazima wanene watueleze haraka kabla hatujachenchiana pakachimbika bila jembe.”
            Mgoshi Machungi anakatua mic “hapa azima tiangaie nani anawapa kibui hawa wanahizaya ii naye timshughuikie kikamiifu ii iwe somo kwa engine wanaodhani kaya yetu ni shamba la bibi. Mimi napendekeza kwa wazii Ukuvi afute hii hati miiki inayowapa kiburi haafu achunguze na kuwakamata hawa magabachoi ii wafie upango.”
            Mzee Maneno anakwanyua mic “Tulishawaambia kuwa tumeuzwa japo tunajidai kuwa tunaimilki kaya ambayo tunaiita yetu wakati ina wenyewe. Kama siyo siasa za kuendekezana, hawa jamaa walipaswa kufia lupango. Wallahi leo hii imenifanya nimkumbuke jamaa yetu marehemu Chris Mtikisa aliyewatikisa na kuwatia aibu. Hata hivyo, niseme wazi. Dokta Kanywaji hatawaacha watende haya makufuru. Lazima watakwenda na mtu hawa.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic na kusema “kumbe wakati mwingine unaweza kudhani unaota wakati si kweli! Hata kama ni jeuri ya njuluku, jamani hii imezidi. Bila kujitambua na kuwatambua na kuwatumbua wabaya wetu, kuna siku tutaambiwa tufunge virago na kutafuta pa kwenda baada ya kuambiwa hii kaya si yetu.” Anamaliza huku akimkazia jicho Kanji ambaye naye anamtazama kwa mshangao.
            Kanji naye anaamua kula mic “hii iko sangaza mimi sasa dugu zangu. Kama dugu bili nasema namilki wilaya, hiyo vatu nazaliwa pale takwenda wapi?”
            Kabla ya kujibu, Mchunguliaji anajibu kiuchokozi “India.”
            Kanji anajibu “veve iko jua India au natania. Kule iko mtu mingi sana dugu yangu. Kama veve nakwenda India hapana kaa hata siku moja takimbia kama napata kurutu veve.”
            Mpemba anakatua mic “yupo jamaa yangu alokuwa akienda kule kununua bidhaa. Alintonya kuwa kule watu wababana hadi kujisaidia kwenye madebe tokana na ukosefu wa sehemu ya kuchimba vyoo. Yule jamaa aliongeza kuwa hata hii hali ya kuchoma  maiti wafarikipo yatokana na ukosefu wa ardhi ati.”
            Kapende anajibu “usemayo Ami ni kweli japo hawa magabacholi wa hapa kaya wanajifanya kutojua ugumu wa maisha unaoendelea kule Ugabacholini. Huoni wakiwa hapa wananenepeana wakati kwao wakondeana?”
            Msomi anarejea “nadhani walidhani tutaendelea kutojua kinachoendelea kwao. Kwenye kizazi hiki cha mitandao wataficha nini.” anachomoa kisimu chake na kuanza kutafuta video kuonyesha ugumu wa maisha huko India. Mara video inaanza kucheza ikionyesha magabacholi maskini wanavyosoteshwa na ukapa kule.
            Msomi anaendelea “kama wanene wetu wangejua kuwa tunajua kila kitu, wala wasingeendekeza kunguru yoyote zaidi ya kutupa lupango. Napendekeza twende zetu Nkuranga na kuungana na wachovu wa huko ili tuwahamasishe wadai magabacholi wote warejeshwe kwao au kwa Kwini aliyewaleta hapa kutengeneza reli na si kudai umilki wa kaya na ardhi yetu.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shumbwengu la gabacholi mmoja. Acha tulitoe mkuku ili kumtia adabu!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.
 

Saturday 24 December 2016

Yaani hata machangu mnaimpoti toka Ugabacholini!

 
            Niliposoma kuwa ndata walidaka vyangudoa toka Nepali na India nilicheka sana. Kwanza nilijiuliza; Hawa jamaa walivyo wabaguzi, vyangu wa kibongo wakienda kule watapata soko kweli? Je inakuwaje tunaruhusu kila uchafu toka ugabacholini kiasi cha kuamua hata kutuletea migonjwa ya ajabu ajabu? Je huu nao ni uwekezaji auuteketezaaji?  Kama siyo hivyo, inakuwaje hawa jamaa wanaleta vyangu toka ugabacholini wakati tunao wa kumwaga hadi wanageuka kero kwenye mitaa yetu?  Hapa kuutakuwa na namna ima kwenye mfumo au kwa wale magabacholi wanaowaleta vyangu hawa. Je sisi tunaweza kuwapelekea vyangu wetu kule wasirudi kwenye majeneza baada ya  wa kule kuwanyotoa roho kwa kuingilia ulaji wao? Je wanakuja kuhudumia waswahili wakati wanawabagua au ni ile caste system ya kumbagua mswahili kiasi cha magabacholi kuamua hata kuleta vyangu wao ili kuepuka kuchanganyikana na waswahili?  Mbona nilipokuwa nasoma kule niliwahi kuona vyangu wengi wakijigonga kwa waswahili kiasi cha kuamsha chuki hadi wajalaana kutoana roho? Hawa jamaa licha ya kuwa wabaguzi wana roho mbaya sina mfano. Pamoja na kuletwa kujenga reli na kung’ang’ania wamekaa miaka yote wakiendeleza ubaguzi dhidi ya wale wanaowategemea kwa kila kitu. Hivi walevi wakiamua kuacha kununua bidhaa zao na kununua kwa walevi wenzao wanaweza kuwa matajiri? Hata hivyo, walevi nao wamelaaniwa. Pamoja na kubaguliwa kwa miaka nenda rudi, bado wengi wanajigonga kwa wabaguzi hawa wa kunuka. Sijui nani aliwaroga hawa wajalaana wanaobaguliwa lakini bado wakajigonga na kuwazimia watesi wao? Huoni walivyoamua kuachia kila kitu hadi majumba ya Asajile Mwaijumba kwa magabacholi wakati wenyewe wakibanwa mbavu kwenye mbavu za mbwa Uswekeni? Tutaendelea kulea ubaguzi huu wa wazi utokanao na udhalili wa hiari hadi lini? Yaani tumeridhika na umachinga wakati wenzetu wanaendelea kukalia kila kitu kiuchumi?
            Pamoja na kwamba ukisema unaonekana mbaguzi kuliko wanaotenda wazi wazi, bila kubadili mfumo na kuwaadabisha hawa jamaa, kuna siku watatia kaya kibiriti na kujiondokea. Kama sisi tunaonekana kinyaa kiasi cha kubaguliwa hivi, kwanini wasilete na nyanya, unga, mchele na hata maji yao kuepuka kutumia vitu vya Kiswahili? Kwanini hata huo uchuuzi wakafanyie kwao kwani kuna aliyewaita au shida zao? Mbona waswahili wanaojipeka kule kusoma wanabaguliwa hadi wengine kuuawa wakati huku miswahili ikiangalia bila kuchukua hatua mujarabu kuhakikisha kuwa tabia hii ya kidhalimu inakomeshwa ima kisheria au vinginevyo? Mnakumbuka yule binti wa kibongo aliyedhalilishwa na kupigwa baada ya Msudani kumgonga gabacholi? Kuonyesha tulivyo wa hovyo, uliza nini kilifanyika? Lisirikali lenyewe lilikaa kimya huku wanene wakiwapongeza magabacholi kuwa wana uwezo wa kupiga kura huku na kule wakati sisi tunazuiliwa uraia wa kaya mbili.
            Kwa vile wenye madaraka wameamua kula pini kuogopa kuwaudhi wateule, mimi kiongozi mkuu wa walevi lazima nisema kuwa ubaguzi wa namna hii utakuja kuwa bomu huko tuendako. Haiwezekani wajalaana watubague hadi wanaleta vyangudoa wao kana kwamba sisi hatuna vyangudoa. Wakati mwingine walevi wanapaswa kujilaumu. Wanabaguliwa nao wanajigonga. Wamenikumbusha mfumo wa kibaguzi ambao tunaanza kuuzoea. Siku moja si nikaupiga na kumtokea mtoto wa kimanga. Kimwana alionekana kunizimia. Lakini wazazi wake walipoipata si wakamkimbizia umangani na kumuozesha kule haraka ili nisimuwowe mie. Ajabu hawa nao wanapenda kuoa vibinti vyetu chuma na kuwakimbizia wao umangani ambako nasikia wanabaguliwa na kuitwa waswahili.  Wabaguzi hawa wako tayari hata kuoa dada zao ilmradi walevi wa Kiswahili wasiwapate. Huwa namkumbuka marehemu Abeid Karumekenge aliyewalazimisha kuchanganyikana kwa kuwowana kiasi cha kuleta usawa na kuheshimiana. Laiti na mzee Nchonga angechukua msimamo wa kuigiwa mfano kama huu tuliponyaka uhuru, nadhani tusingekuwa tunadhalilishana hadi kuleteana vyangudoa toka Ugabacholini ili kuepuka magabacholi kuwatumia vyangu wetu.
            Nasikia kama tumbo linauma. Acha niende kwa mama Kote lau nipate mapupu na kutuliza hii njaa.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

Thursday 22 December 2016

Makonda aeleze anavyopata pesa anayotoa

Hivi karibuni vyombo vya habari vilipoti kuwa mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda alitimiza ahadi yake ya kutoa fedha taslimu za mitaji na vifaa vyenye thamani ya shilingi 164 272, 000 kwa baadhi ya wakazi wa Dar Es Salaam aliowahaahidi kufanya hivyo. Sijui mshahara wa Makonda. Ila kwa nijuavyo uchumi na kiwango cha mshahara wa Tanzania, hii fedha si kichele hata kidogo.
Je Makonda anatoa mfukoni mwake? Na kama anatoa mfukoni mwake ametengenezaje utajiri huu kwa muda mfupi aliokuwa madarakani? Je anachangiwa; na kama anachangiwa, ni akina nani hao wanaofanya hivyo? Pamoja na nia njema, uzoefu umeonyesha kuwa hata wahalifu wengi hupenda kutakasa fedha zao na kuwa karibu na wakubwa kwa kutoa michango itokanayo na fedha chafu. Rejea namna baadhi ya wafanyabiashara waovu walivyokuwa wakichangamkia kununua leso au hata soksi za rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi lakini wakaacha kufanya hivyo alipoachia madaraka. Rejea hata namna ya wafanyabiashara wenye kutia kila aina ya shaka walivyokuwa wakichangia NGOs za marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete lakini sasa wasifanye hivyo. Hivyo, kama serikali imeamua kuchunguza namna watu walivyopata utajiri wao lazima na Makonda aeleze hata kuchunguzwa namna anavyotengeneza fedha yake bila kujali yuko karibu mbali au karibu na rais.
            Hapa tunaongelea milioni mia na ushei. Vunja rekodi ni pale Makonda alipoahidi kulijengea Baraza Kuu la Waislam  Tanzania (BAKWATA) makao makuu yenye thamani ya shilingi bilioni tano na ushei. Na tunapoandika, vyombo vya habari vimeisharipoti maendeleo makubwa ya mradi huu. Huyu si mtu wa kawaida. Lazima awe na namna anavyotengeneza fedha. Tungependa aiweke wazi ili iwasaidie viongozi wengine  waweze kuwakwamua watu wao. Muhimu ningependa kujua siri ya Makonda ili amsaidie rais John Pombe Magufuli naye afanye mambo makubwa kama anayoyafanya.
            Sitaki kuonekana kama natia chumvi. Huyu bwana kwa sasa anaonekana kuwa Bwana Mapesa aka moneybag ambaye akisema lazima liwe. Hapa lazima kuwa na namna iwayo yoyote ile iwe halali au haramu. Pia nichukue fursa hii kuwaomba wale mashabiki wa Makonda kutoniona kama namuonea wivu au kuvuruga ulaji wao. Hasha. Wakati huu wa uwajibikaji lazima kila kitu kiwe wazi hasa ikizingatiwa kuwa sote ni binadamu tunaoshughulika na masuala ya umma. Ninachojaribu kutetea hapa ni utaratibu na mfumo wazi wa kisheria usio na kujuana wala kupendeleana.
            Kwanza, siamini katika utegemezi wa misaada. Wachina wana msemo kuwa ukitaka kumsaida mtu mfundishe kuvua na si kumpa samaki.nasi kadhalika, badala ya kutegemea viongozi kutuchungishia vijifedha vyenye kutia shaka, wajenge mazingira ya kutengeneza utajiri wa kujitegemea.
                        Pili, kama nilivyosema hapo juu, Makonda ni binadamu tena maskini sawa na wengine. Je tutajuaje kuwa hapo alipopata hiyo fedha ni hizo tu zilizopatikana? Je kuna chombo gani cha umma kinachosimamia huo upatikanaji wa fedha kama anachangiwa? Nijuavyo, ukiachia fedha za michango ya harusi, sheria ya Tanzania hairuhusu mtu kuwachangisha wenzake kwa sababu yoyote bila kusimamiwa na serikali. Nasema. Makonda ni mtu binafsi anayetumia nafasi yake kujijenga kisiasa hata kama anayofanya yana wengi wanaoyashabikia. Tunasema hivi kwa vile yeye ni mkuu wa mkoa. Asingekuwa na mamlaka aliyo nayo, hiyo fedha wala asingepata hata moja ya kumi yake.
            Tatu, najua kuwa tokana na umaskini na utegemezi wa wengi wetu, wengi wanafurahia hii misaada isiyojulikana inakotoka. Kiuwazi, uwajibikaji na utawala bora, lazima mhusika aeleze anavyopata hiyo fedha.ni bahati mbaya hata vyombo vya habari vilivyoripoti neema hii, vilishindwa kumuuliza Makonda ilikotoka fedha hii na vigezo gani alitumia kuwateua hao aliowapa hiyo fedha na vifaa. Tusisitize kuwa hatuhoji misaada hii kwa nia mbaya. Uzoefu wetu unaonyesha kuwa kuna wakati mwingine misaada inaweza kuonekana mizuri lakini ikawa na matukio mabaya. Mfano wa karibuni ule wa rais wa zamani wa Kenya Daniel arap Moi. Huyu bwana alipenda kumpa kila aliyemtembelea mabulungutu ya fedha. Baada ya kung’oka aligundulika kuwa alikuwa amefanya ufisadi mkubwa ili kujijengea sifa ya kuwa mkarimu kiasi cha kupendwa wakati nyuma ya pazia alikuwa mwizi na fisadi wa kawaida. Moi anasifika kwa kutumiwa na wafanyabiashara wa kihindi kufikikia karibu kuifilisi kenya chini ya kashfa maarufu ya Goldenberg.
            Mfano wa pili ni ile hali ya rais Magufuli kusema wazi kuwa hakuruhusu wafanyabiashara wamchangie wala kumdhamini wakati akitafuta urais. Hii imempa jeuri ya kutekeleza mipango yake kwa umma bila kusumbuliwa na wafadhili. Sijui kama Makonda analikumbuka hili.
            Tumalize kwa kusema yafuatayo:
            Mosi, wananchi wanataka mazingira ya kujijengea uwezo wa kujiletea maendeleo na taifa na si ufadhili ambao uzoefu wetu umeonyesha kuwa ni udhalilishaji na wenye nia ya kurejesha fedha zake kwa faida.
            Pili, Makonda aeleze kinagaubaga anavyopata hiyo fedha; na vigezo anavyotumia kuwateua wa kuwapa hiyo fedha. Je ana kibali cha kufanya hivyo? Je fedha husika inaratibiwa na taasisi gani ya umma kulingana na sheria? Je hiyo fedha inalipiwa kodi? Je yuko tayari kuwataja wanaomchangia?
            Mwisho, tunamshauri Makonda aige mfano wa rais Magufuli ambaye fedha yote aliyotumia kufanya mambo ambayo wengi hawakutegemea kama kuondoa posho bungeni na kuelekeza kwenye barabara na hospitali amezitolea maelezo hata kabla ya kuombwa kufanya hivyo.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.

Mgoshi kukomba appointment na rahis

           Leo Mgoshi Machungi ana hasira ya kufa na mtu. Si juzi dada yake Zuhura alikwenda ku-renew hati yake ya kusafiria akaambiwa alete cheti cha kuzaliwa chake na mama yake wakati wote walizaliwa wakati wa ujima. Zuhura alitaka kupasuka alipoambiwa alete cheti cha kuzaliwa cha Mamihiyo aliyezaliwa wakati wa Mkoloni mjerumani.
            Mgoshi anaanzisha mada “wagoshi siku hizi tina watu hawana akii kabisa. Mtu anakwenda kushughuikia jambo dogo wanamzungusha utazani alikuwa akishughuikia kujua nani na nini kiimua fau John! Hivi tiache utani. Hivi kwei zie pembe aizopeekewa waziii mkuu kwei ni za Fau John au ni za kuchongwa?”
            “Kwani ulikuwa hujui kuwa hatuwezi wote kuwa na akili timamu! Mbona hili liko wazi kuwa kuna vichaa wengi tena wengine huwezi hata kuwadhania kuwa ni vichaa. Wangenitakisha mimi saini ya bi mkubwa Mahiza basi ningewapelekea picha ya kaburi lake ili wakome ushenzi na ujuha. Mwambie Zuhura akirejea kushughulikia pasi yake aandae kisimu chake awarekodi akupe uniletee niwape jamaa zangu wa Usalama wa Kaya au vipi?” anamkatiza Mbwamwitu bingwa wa kuchomekea.
            Tunaangaliana kuona huu mkwara anaochimba Mbwamwitu kuwa ana watu wake wa Usalama wa Kaya wakati kaya yenyewe si salama. Wangekuwapo na wanajua wanachopaswa kufanywa wangehangaika na wenye mitandao wakati kaya yetu ikigeuzwa shamba la bibi?
            Mgoshi anaendelea “hata kama kwei kuna vichaa kia mahai sikutegemea kuwa wengi tingekuwa nao kwenye ofisi za seikai. Maana aichofanyiwa dada yangu Zuhua aipokwenda kushuhukia pasipoti yake si kitendo cha watu wenye akii.”
            Kabla ya kuendelea Kapende anamuuliza swali “je walitaka kumtoa upepo au walimfanyia mtima nyongo kama ada ya walio wengi hasa mtu anapoonyesha dalili za kwenda nje ya kaya hata kama ni kaya jirani tena zenye shida kuliko kaya yetu?”
            Mgosi anajibu “waa wakati huu hakuwa akienda nje bali kutaka pasipoti mpya. Au ni kwa vie aiwahi kwenda Ujeumani! Si waimwambia eti apeeke cheti cha kuzaiwa cha mama yetu Mamihiyo aiezaiwa wakati wa mkooni Mjeumani!”
            “Hao nadhani ni wapiga dili wachache waliobakia kwenye ofisi za umma wakidhani wao ni wajanja hasa usawa huu wa hapa kazi tu. Laiti angerekodi maongezi yao na kuyatua kwa wanaohusika, hawa waliotaka mambo ya kipuuzi wangetumbuliwa,’ anajibu Mipawa huku akifyonza gahawa yake.
            Kanji anakamata mic “veve zani vatu baya nakwisa. Kama Kufuli nakua kali lakini bado iko vatu naua faru John iko dhani itaacha chezo yao valiozoea? Kama napata chance ya kuongea na Kufuli iko taka yeye nabadili katiba ili ifunge ile yote nasumbua vatu kama hii nasumbua dada ya Gosi.”
            Mpemba anakwanyua mic “wallahi msinkumbushe kifo cha faru John. Wallahi mie sikudhani kama wangengusa hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa kaletwa kuzalisha faru wengi ili nasi tuendelee kujivunia urithi wetu. Yaani watu wachache wanafanya vitu kana kwamba hamnazo!”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu “hili suala la kusumbuliwa dada yako dogo sana Mgoshi. Hukumsikia mkuu wa bandari akilalamika kuwa kuna wanasiasa wanaomzonga wakitaka awaache waendelee kupiga dili kama walivyozoea? Kwa vile huyu bwana kaamua kuweka mambo hadharani, napanga kwenda kumuona na kumtaka aweke majina ya hao wanasiasa wanaomsumbua ili watumbuliwe haraka. Kilasiku nalalamika kuwa hapa tunachopaswa kufanya ni kufumua mfumo huu wa mbovu wa wa mazoea na kuufuma upya. Hata hivyo, inaonekana wahusika hawapati somo hasa wanapong’ang’ania kuendelea kuongoza kwa katiba viraka ya kifisadi. Sijui wanaogopa kuwakamata na kuwatumbua washitili wao au marafiki zao? Sijui kwanini wanashikwa kigugumizi huku wakituaminisha kuwa wanataka kuibadili na kuinyosha kaya yetu ya mafwisadi.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua naye kutia buti “tuwe wakweli. Kama alivyosema kaka Msomi ni kwamba bila kuufumua huu mfumo, tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu tukitegemea kupata unga. Nadhani tukubali. Bila kuwabana wakubwa wakatueleza ni kwanini hawataki kurejesha mchakato wa katiba mpya watawezaje kufanikisha hiki wanachotaka kufanikisha.”
            Mheshimiwa Bwege anamnyang’anya mic Sofi na kudema “nadhani hawa tunaowalalamikia wanadhani sisi tu mabwege wa kugeuzwa kama samaki. Kwanini tusifanye mpango tukaandamana kudai katiba mpya hasa usawa huu baada ya UKAWI kutukawiza kwa kukumbatia yale waliyokuwa wakipinga kama alama ya kuramba matapishi yao? Hakuna ubwege kama kukalia kulalamika wakati tunajua kuwa nguvu ya wanyonge ni umoja wao? Kama hatuwezi kulianzisha kikaeleweka basi tunyamaze kuliko kuendelea na wendawazimu na ubwege wa kulalamika. Nataka hapa niseme wazi. Wakati huu tusitegemee UKAWI wanaoramba matapishi yao, kutukawiza na kuingizwa mkenge kirahisi kama ilivyotokea kwenye uchakachuaji. Hivi kweli tuna sababu ya kuendelea kuamini kuwa kuna UKAWI wakati madai yao ya katiba yaliwekwa kitanzini?”
            Mgoshi anarejea na kusema “kaka hapa umenipa desa. Ngoja tifanye mipango ya kuomba kupata appointment na dokta Kanywaji ii timpe inshu hii ii aweze kutumbua haaka sana. Haiwezekani tiendee kugeuzwa shamba la bibi tena wakati huu ambapo tina seikai inayosema inataka kutiondoa kwenye ujima wa kuchuuzana. Mnaonaje wagoshi jamani? Kwanini tisipange kufanyia kijiwe ikuu kama aivosema dokta Kanywaji kuwa kia mmoja anaweza kufanyia mikutano yake pae kwa vie ie ni nyumba ya umma?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita jamaa mmoja wa uhamiaji. Acha tumtoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.

Saturday 17 December 2016

Hakikini mali za walevi wote na si wanene tu

            Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa sirikali ina mpango wa kuhakiki mali za wanene na wazito ili kubaini wangapi walipiga wakaficha kwa majina bandia au ambao ni wa kweli kama Dk Kanywaji na mimi. Tokana na hili, japo kwa ulevi, nina maangalizo kiduchu.
             Kwanza, naipongeza sirikali kwani kwa kuchunguza mimali hii ya kukwapua itatenda haki kwa walevi hata wapigaji waliotajirika haraka kwa njia za mkato. Sirikali inafanya hivyo ili kubaini kama kuna wanaotumika kuficha mali za wanene waliozipata kinyume cha sheria. Hili ni wazo zuri na mwanzo mzuri wa uwajibikaji na urejeshaji maadili kitaifa.  Hili ni jambo zuri la kupigiwa mfano kuwa sasa kaya yetu inaanza kujiondoa kwenye makucha ya ufisadi, uroho, ubinafsi na ufisi vilivyokuwa vimetamalaki kwa muda mrefu.  Hivyo, nashauri zoezi hili liwe endelevu ili kuepuka kuondoa wezi wa sasa na kuruhusu wezi wa baadaye kuendelea kuliibia kaya yetu huku walevi wetu walio wengi wakiteseka kwa umaskini wakati kaya yao imejaliwa utajiri wa kila aina.
            Pili, ifahamike kuwa si wanene peke yao walioibia na kufilisi walevi na kaya yao. Hata baadhi ya walevi wa kawaida ima walishirikiana na wanene au walishiriki kutokana na fursa za kufanya hivyo zilizojitokeza tokana na ubovu wa mfumo. Kwa mfano, wale wote walioruhusu bandari zetu kuwa mashamba binafsi wasakwe na kushughulikiwa. Pia, wale waliofunga mita ya kupimia wese bandarini kwa miaka mitano na kuacha kaya iingize wese bila kulipiwa ushuru wala kuhakikiwa viwango vyake vya ubora lazima wasakwe na kukamatwa ili haki itendeke.
            Tatu, ikumbuke; mfumo mzima ulikuwa wa kiwiziwizi na hovyo sana kiasi cha kuruhusu kila tapeli ajihomolee kiasi cha kufanya wanaopaswa kuchunguzwa kuwa wengi kuliko wanene na watumishi wa lisirikali.
            Nne, kushughulikia wanene au watumikaji wa umma na wanaodhaniwa kuwa washirika wao ni ubaguzi na mwanya wa kuwaacha wengine waendelee kufaidi mali za wizi bila stahiki yao.
            Tano, uhakiki wa mali uwe ni wa kaya nzima kuanzia walevi wa kawaida hata wanene wa dini ,taasisi binafsi, na kila mmoja ili haki itendeke sawa kwa wana kaya wote. Mfano ulio wazi ni ile hali ya kuibuka wanene wa majoho wengi matajiri wakati kazi ya kuhuburi wanayofanya haina malipo wala utajiri. Je hawa wanaramba sadaka au kutumia misamaha ya kodi kujitajirisha? Kama siyo hivyo, waeleze wanavyoweza kupata ukwasi wa ghafla bin vu hivi kwenye kaya maskini wakati hawafanyi kazi zaidi ya kupiga kelele. Tena ngoja niweke msisitizo kuwa mahubiri ima yafanyike siku zisizo za kazi au baada ya kazi. Nani anaweza kula au kunywa mahubiri? Akikutwa mlevi anahubiri saa za kazi akamatwe kama mzuraraji wa kawaida. Maana “Hapa ni Kupiga Mzito Tu.” Kimsingi, jamaa zangu wa majoho hasa wale wa kujipachika wanapaswa kuchunguzwa sana hasa ikizingatiwa kuwa Yesu au Mtume Mohamad walikuwa maskini wa kawaida waliotumia kila walichopata kula na si kuwala waumini wao. Jamaa zangu wa majoho wanapaswa kuiga mfano wa hawa viongozi waasisi wanaowahubiri. Tujikumbushe wosia wa Yesu kuwa ni heri ngamia kupita kwenye tundu la sindano kuliko tajiri kwenda mbinguni.
            Sita, hata wafanyabiashara ambao shughuli yao ni ya kuleta utajiri tuwachunguze ili kuona kama biashara na utajiri wao ni halali. Kama wanalipa kodi na kufanya biashara halali. Maana, tunao wafanyabiashara matajiri hadi wengine kuwekwa kwenye kundi la mabilionea wakati utajiri wao umetokana na kuuibia umma. Rejea mfano tajiri mmoja ambaye kampuni yake ya Kagoda ilishiriki wizi wa fedha za umma kwenye kashfa iliyotikisa nchi ya EPA.
            Saba, wale watakaopatikan na mali haramu wataifishwe na kufikishwa mahakamani ili watakaopatikana na hatia waadhibiwe ndiyo haki itendeke kwao na kwa taifa.
            Kumbe sijapata kanywaji! Ngoja nikitoe kwenda kuongeza mafuta. Message sent and received. Kama niliyosema yamekuudhi au kukukwaza ujue unapaswa kuchunguzwa. Kama umeyafurahia basi ujue wewe ni mlevi hata kama hunywi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

Wednesday 14 December 2016

Akina baba tusiwe kama baba Kamakl

Huu muziki ni wa kikuyu. Umetungwa na John Njagi na kuimbwa na binti ambaye jina lake halikutajwa. Muziki huu una somo kubwa kwa wanaume -tena watu wazima -wanaopenda kuharibu watoto wa wenzao.
Binti ameamua kumshitaki mzee mwenzie kwa baba yake ambaye ni rafiki yake. Anamwambia baba yake aende akamuonye mzee mwenzake kuacha kutaka kumharibu binti wa mwenzie.
Anamwambia baba yake
Baba Kamaki ni rafiki yako
Nilikutanaye juzi pale Kanunga
Nilikuwa nikitokea kanisani
Aliniita na kuomba namba yangu ya simu
Niliuliza ya nini wakati anaiona
Alijibu ana jambo moja anataka kuniambia.

Aliniita kwenye baa na kutaka tupendane
Alisema akiniona hujihisi vyema
Nilishangaa sana

Mbona mke wa baba Kamaki ni mama mwema?
Mbona rafiki yake mama toka shuleni?
Baba Kamaki ni baba choyo
Kichwa kimejaa mvi
Lakini anataka kuhangaika na vitoto

Baba nenda kamuonye
Kwani si rafiki yake
Nilikutana naye akiendesha gari nzuri ya toto
Aliahidi angeninunulia moja
Hata anunue meli hanipta
Ashindwe kabisa.

Siwezi kutafisri wimbo mzima. Hiyo ndiyo faida niliyoipata kuishi Kenya kwa miaka mitatu ambako nilitia bidii na kuondoka na lugha ya Kikuyu.

Hata kama hujui lugha, unaweza kusikiliza na kuburudika angalau baada ya kukupa kwa ufupi ujumbe mkuu na mahsusi wa wimbo husika.

Kugomea uraia pacha ni kujikwamisha

Image result for bendera ya india

            Hivi karibuni, baada ya kubainika kuwa watanzania wanaochukua uraia wa kigeni hupotgeza haki muhimu ya kumilki ardhi, kumekuwapo mjadala kwenye mitandao ya kijamii. Tokana na unyeti wa suala zima, napenda kutoa maangalizo yafuatayo kama mwana diaspora:
            Kwanza, nilishangaa kuona kuwa bado tunaendelea kuwa na mawazo ya kijima ya wakati wa vita baridi ambapo nchi za magharibi na mashariki zilitutengeneza kuwa kama maroboti yenye kushikiana na kuchukiana bila hata kujua ni kwanini. Zama zile tuliogopa na kukata uraia pacha kwa hofu ya kuweza kuingiza wapelelezi na mawakala wa maadui zetu kutuchunguza na kuhatarisha usalama wetu. Je kwa sasa tunahofia nini zaidi ya kutumia mabaki ya ukoloni (colonial carryovers)? Ajabu, wakati sisi tunabaniana uraia pacha, wale waliotutawala na kutujengea shaka na uadui wanaruhusu! Ukiachia hili, sisi tuna nini cha kuhofia wakati ni nchi tegemezi zilizoharibiwa kiasi cha wananchi wake kuzikimbia kutafuta riziki kwingine?
            Pili, inapaswa kufahamika kuwa wakati sisi tukisuasua na kubaniana uraia pacha, nchi tajiri hazizuii wageni waliochukua uraia wao kubaki na uraia wao wa kuzaliwa. Kama ni kuogopa kuhujumiwa basi hizi ndizo zingeogopa hili kwani zina mali na fedha nyingi za kupoteza. Nchi nyingi za kiafrika zinategemea fedha inayotumwa na wana diaspora. Kwa mfano gazeti la Mail and Guardian (2 Juni, 2015) linaripoti kuwa nchi za Eritrea zinategemea pesa toka kwa diaspora kwa kiasi cha  38%, Cape Verde, 34%, Liberia , 26%, na Burundi 23% ikilinganishwa na pato la taifa. Hii si pesa kidogo na rahisi kwa nchi kuipata. Japo sina takwimu za Tanzania inaingiza kiasi gani, kutokana na uzoefu binafsi, najua inaingiza fedha zinazoweza kuelezwa kuwa zinakwenda kwa watu binafsi. Huu ni ushahidi kuwa wana diaspora wana mchango mkubwa kwa nchi zao jambo ambalo linapaswa kuwa kama njia mbili yaani nipe nikupe (twoway traffic).
            Tatu, kuonyesha kuwa bado tunaendelea na mawazo ya kijima, kuna taarifa nyingi toka Tanzania ambapo wageni wanaopewa uraia wa Tanzania huwa hawabanwi kama watanzania wanaochukua uraia wa kigeni. Wengi wa wageni hawa hubaki na uraia wao kiasi cha kutumia status hii kuifilisi na kuiibia Tanzania wakati ikuzuia wazawa wake kuwa na uraia pacha. Mifano ya wahalifu walioibia Tanzania mabilioni ya fedha kama vile Chavda Group ambaye mwaka 1993 aliyetumia mashamba ya mkonge kukopa fedha na kuyatelekeza na Saileth Vithlania wa kashfa ya rada inaweza kukueleza hali ikoje ukiachia mwingine wa hivi karibuni Hermant Patel aliyejitwalia ardhi ya Tanzania ipatayo hekari 35,000 na kwenda ulaya kwenye mabenki kuiweka kwenye poni. Je tunamkomoa nani; na ili iweje au ni kwa vile matapeli na wahalifu wa kimataifa wanashirikiana na maafisa wa juu wa serikali kama ilivyokuwa kwenye kesi mbili hapo juu?
            Nne, sheria ya ardhi ni kimeo. Inawazuia watanzania waliochukua uraia nje kumilki ardhi wakati ikishindwa kuwadhibiti waliochukua uraia wa Tanzania kuutumia kuiibia kama tulivyoonyesha hapo juu. Je mhusika akiwa na makaburi ya wazazi wake nayo serikali itayachukua? Je kwa zuio hili, ni busara kwa diaspora wenye uraia wa kigeni kuwekeza Tanzania wakati hawakubaliki? Mbona nchi nyingine za kiafrika kama Rwanda zimeruhusu uraia pacha? Nadhani Tanzania bado tuna mawazo ya kizamani ya enzi za vita baridi.
            Nini kifanyike?
            Kwanza, kushawishi serikali ya Tanzania kuruhusu uraia pacha au kuzi-lobby nchi zilizoendelea zilizotoa uraia kwa watanzania kuhakikisha watu wao wanapodhulumiwa ardhi nazo zisitishe misaada na ushirikiano hata ikiwezekana kuingilia kati.
             Pili, kuna haja ya kujiuliza: Kwanini watanzania wanachukua uraia wan je? Wanafanya hivyo ili wapate fursa ambazo hazipo nyumbani. Serikali ambayo inapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kuweka mazingira mazuri kwa watanzania kupata fursa kama hizi haipaswi kupewa mamlaka ya kuamua nani awe na uraia pacha au la. Kwani, kimsingi, serikali ndiyo chanzo cha haya yote. Watu wanataka elimu bora, maisha safi, kuaminika wanapotaka kusafiri nje na mengine mengi tu. Wekeni mazingira bora kwanza ndiyo mkataze watu kuwa na uraia pacha. Mbona nchi tajiri zenye kila huduma bora zinawaruhusu watu wenu kuchukua uraia wao, kufaidi huduma zao na hata kutuma fedha huko wanakonyimwa uraia pacha?
            Tatu, kwa mjibu wa mtandao wa dualcitizenshipmalawi.blogspot.ca nchi zipatazo 23 za kiafrika zinaruhusu uraia pacha. Hivyo, Tanzania inapaswa kujifunza toka kwa nchi kama hizo tena jirani kama vile Kenya na Rwanda zinazoruhusu uraia pacha na namna zinavyofaidika nao ikilinganishwa na kuupiga marufuku. Bila kubadilika, Tanzania itajikuta inaruhusu raia wa nchi jirani ambao watatumia fursa ya kujipatia ardhi Tanzania na kubaki na uraia wao huku watanzania wa kuzaliwa wakinyimwa ardhi. Rejea kilichotokea baada ya RPF kuchukua madaraka nchini Rwanda, wanyarwamnda wengi waliokuwa wamepewa uraia wa Tanzania waliutelekeza na kurejea kwao bila kizuizi cha kuhitaji kuomba upya kama ilivyo kwa Tanzania ambayo ilikula hasara kwa kuwasomesha na kuwatunza tangu wengine wazaliwe hadi walipoondoka.
           Nne, Tanzania iache kupoteza muda kuwazuia wananchi wake wa kuzaliwa uraia wa pacha wakati ukiugawa kama njugu kwa matapeli wa kimataifa wanaoutumia kuhijumu tofauti na wana dispora wanainufaisha kwa kutuma fedha kwa watu wake. Pia ifahamu kuwa Afrika kwa mtu yeyote mweusi ni mama ambayo hakuna namna yoyote ya kuitenganisha na watoto wake kwa sababu za kijima na wakati mwingine hata ujinga na roho mbaya. Kwanini wakenya na wanyarwanda, kama si roho ya korosho waweze Tanzania ishindwe? Nadhani uraia pacha ni haki na si suala la nani watake au kutoa kama ofa. Wote tunahitajiana. Rekebisheni kinachowasukuma watu wenu kukimbilia nje uone kama kuna atakayelalamika.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

Kijiwe chasheherekea na kutathmini uhuru

      Image result for sherehe za uhuru

      Wakati wapo waliosherehekea kumbukumbu za miaka 55 za uhuru kwa kununa tokana na kutokuwapo makulaji na posho, kijiwe kilisherehekea kwa tafakuri na tathmini nzito.  Wakati wengi walikuwa kwenye uwanja wa taifa wakishuhudia gwaride, kijiwe kilichegama sehemu ambayo ni siri kubwa ili kutathmini uhuru husika na ikiwezekana kuwasuta baadhi ya wenzetu.
            Baada ya kukusanyika tukiwa kwenye mood ya kuwa huru, Mpemba ndiye anayelianzisha.
            Anakula mic “hongereni ndugu zangu wa bara kwa kusherehekea miaka 55 ta uhuru wenu.” Kabla ya kumaliza Kapende anampoka mic “tunashehekea uhuru au udhuru? Nadhani wanaosherehekea ni wala nchi lakini si waliwao kama sisi. Je kama uhuru huu ni wa bara siew a pwani wetu ni lini? Maana naona wasema wabara kana kwamba kila ntu ni mbara. Sie Ntwara, Lindi, Dar na Tanga si wabara kama unavyosema.”
            Mpemba anajibu haraka “nilimaanisha msio wa visiwani kama siye. Sie kwetu kila aniotokea mahali pasiyo kisiwa humwita mbara bila kujali yua aishi bara pwani au bara ndani.”
            Kapende anakula mic tena “sasa nimekuelewa. Je kwenu visiwani haliwi kama hapa hasa wale wasiokuwa kwenye ulaji? Maana usipokula hapa shurti uliwe vinginevyo uwe mpiga dili, muuba bwimbwi, mfanya biashara au mfanya ujambazi.”
            Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungu anachokea kwa kuonya “Kapende angaia hiyo ugha. Wewe ni wa kutwambia eti tunaiwa! Kama kuiwa dii basi iwa wewe.”
            Msomi Mkatatamaa aliyekuwa akisikiliza huku akisoma jarida kubwa la kimataifa ambalo jina lake nimelisahau, anaamua kuingilia ili kuikoa mjadala.  Anakohoa kidogo na kusema “jamani tuweni makini na tunavyotafsiri mambo. Sioni kama kuna sababu ya kutumia uoni mmoja kutafsiri kila jambo. Nadhani, kimsingi, Kapende na Mgoshi mnongelea kitu kimoja sema kwa uoni tofauti. Nadhani kuliwa hapa anamaanisha wanaonyonywa.”
            Anakohoa tena na kumtazama da Sofia Lion aka Kanungaembea na kuendelea “najua kwa tafsiri mbaya hata kunyonywa laweza kugeuzwa tusi. Hata hivyo, huko nisingetaka niende.”
            “Kaka Msomi wala huna haja ya kujitetea. Kwani kuna mtu ambaye hakunyonya? Wasingenyonya wangekuwapo hapa?”
            “Nashukuru sana. Dada hapa nimekupata na nadhani kila mmoja amepata ujumbe. Ngoja nijikite kwenye mada baada ya kuondoa utata wa tafsiri na uoni. Nadhani tunachopaswa kufanya leo ni kuangalia mambo yafuatayo. Mosi, je kweli sis tuko huru au walio huru ni baadhi yetu wenye nazo? Pili, je tangu tupate uhuru, tumefanikiwa kufika kule tulikotaka na kutarajia kufika kwa wakati na kasi inayotakiwa? Tatu, je uhuru maana yake ni nini? ni nyimbo, gwaride na hotuba au maisha kwa ujumla? Yapo mengi ya kuangazia na kutoa tathmini ya haki na kisayansi kwa kuangalia uzoefu wetu kama wana kaya.”
            “Profesa Msomi nikushukuru sana kwa lecture yako fupi lakini yenye kusheheni nondo. Ndiyo, lazima tujiulize: je ni wanakaya wangapi hawajahi kutumia umeme kiasi cha kuwa chanzo kizuri cha uharibifu wa mazingira na afya zao ukiachia mbali kuwachelewesha kimaendeleo kibinafsi na kitaifa? Tusiishie hapo. Twende mbele na kuhoji. Je ni wanakaya wanagapi hawajawahi hata kukanyaga barabara ya lami achilia mbali kuzifaidi? Je hawa nao wanasherehekea miaka 55 ya uhuru au udhuru?” anauliza Mipawa huku akiinua kombe lake na kubwia kahawa.
            Mgoshi naye anaamua kupoka mic na kuronga “ninakuabaina ya maangaizo yako profesa Mipawa. Nataka nikuchomekee kidogo tu kwa kuongeza kuwa tihoji ni wangapi wamesoma vilivyo ukiachia hawa wanaoghushi na vihiyo wengine wa kuchapia chapia kama kiswangiish? Je timejiandaaje kwa ajiii ya kesho? Je sisi tiko huu kwei kwei au tinajidanganya hasa ikizingatiwa kuwa baa letu bado ni tegemezi?”
            Kanji anaamua kula mic “vengi nasema kweli kwelikweli. Mimi ona kama tangu napata huru iko endeleo kuba sana. Naona Swahili mingi endesa gari na kujenga jumbani kubakuba. Zamani gari na jumba kubakuba ilikuwa ya hindi tu. Sasa naona ikobadili sana. Witu wingi nachenji. Kila mtu sasa naveza waa wivalo paka napendeza sana. Naona jumba nyingi Kariakoo . Hata kama sisi hapana endelea kama Europe, iko piga hatua sana.”
            Mpemba anaamua kurejea. Anakatua mic na kuronga “tusemapo twahitaji wote kuwa huru, twamaanisha maendeleo. Pia niseme wazi, haya maendeleo tuniotaka si njini tu bali kaya nzima. Kama yawezekana kuwapelekeni Pemba muone tulivopigwa, nadhani wengine wasingesema waniyosema japo haki yao. Naungana na Nsomi kusema wazi kuwa twapaswa kuhoji maana ya uhuru wetu ili kujua kama uhuru kweli au udhuru. Haiwezekani maendeleo yakapimiwa njini na kusahau mashambani ambako waishi watu wetu wengi na ambao shughuli zao zaendesha kaya hii. Hivi nkulima akiacha kazi nani aweza kaa hapa njini?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si linakuja shangingi la muuza bwimbwi maarufu mtaani akipiga honi kushangilia miaka 55 ya uhuru! Mara anashuka na kutumwagia mabulungutu ya njuluku. Tukiwa tunashangaa jamaa anadandia mchuma wake na kuondoka. Ndipo Kapende anasema “hawa kweli ndiyo wako huru ingawa zao zinahesabika.” Je wewe ni huru kwa maana ya uhuru au kwa maana ya kisiasa? Soma na kutia akilini na kutafakari ili kujiletea uhuru wa kweli wewe na kaya yako na vizazi vyako.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.