Friday, 9 December 2016

Heri ulevi wa kanywaji kuliko madaraka

 
            Wiki iliyopita ilitoa somo moja kubwa dunia kuwa kweli cheo ni dhamana. Nikiwa natoka kupiga kanywaji si nikamkuta bi nkubwa ameganda kwenye runinga yetu ya inchi 60! Naona yule anatikisa kichwa akidhani najipa ujiko. Unadhani natania? Kwa taarifa yenu, nina bonge la Hi Def. Ila hii ni siri. Maana, majambazi wakiinasa, watakuja kunivunjia hekalu na kuiiba wakauze chapchap hasa usawa huu ambapo njuluku za deal zimekaushwa.  Turejee kwa bi Nkubwa Nesaa bin Shemtwashua. Kwanza, si kawaida yake kuganda kwenye runinga saa za mchana. Badala ya kuwa jikoni akiniandalia kalaji si nilikuta ameganda tu. Kuuliza kuna mchezo gani mpya umetoka hadi ukambabaisha na kumgandisha vile; si alijibu. “Kweli cheo ni dhamana na kila chenye mwanza shurti kiwa na mwisho.”
            Kiasi fulani aliniudhi ikabidi nisonye na kutaka kurejea kwenye kanywaji. Nilimjibu kuwa kama amenona nyodo ndizo zana za kumkabisha mume mwema kama mimi, basi narudi zangu kwa mama Kote kupata kalaji  na kanywaji kule. Kusikia hivyo nyodo zote zilimtoka akiogopa nisichunwe buzi kule.
            Nikiwa najiandaa si ndiyo akanitonya kuwa yule rais kigeugeu na ng’ang’anizi wa Gambia mwenye kujipachika vyeo kuliko hata Idi Amin, Yahya Jammeh alikuwa ameshindwa uchaguzi!
Mwenzenu, hamu na kiherehere vya kurejea kwenye kanywaji viliniisha; ikabidi mimi na bi mkubwa tugandiane pale kabla ya kwenda kupata kalaji.
            Japo kudondoka kwa Jammeh si stori tena, kuna masomo kibao. Kwanza–hebu fikiria jamaa aliyewahi kusema kuwa alikuwa akiwasiliana moja kwa moja na kuongoza kwa amri ya Allah asingeondoka kwa uchaguzi utadhani Allah ndiye aliyepindua–kuondoka kwa njia aliyoichukia.
            Pili, somo jingine ni kwamba cheo ni dhamana. Ukifika wakati wa wenye dhamana kuirejesha, hata uwe mjanja, na nguvu, au unapendwa au kujipendekeza kiasi gani, utaondoka tu. Cheo ni kama koti mabegani. Si la kulewa wala kukufanya ujifanye u bora kuliko wengine.
            Tatu, fikiria jamaa kama hili lililokuwa limepindua na kukaa kwenye ulaji kwa miaka zaidi ya 22 kudondoka kirahisi hivi.  Itakuwaje kwa wale wa kuteuliwa tena kwenye vijinafasi uchwara wanavyotumia kutukogea na kutudhalilishia walevi wakati wanapwaya kulhali?
            Nne, niligundua kuwa heri kulewa kanywaji kuliko madaraka.  Maana, Jammeh alikuwa na uwezo wa kuwapiga makofi raia waliokuwa wakimbana wakati wakitaka kumsalimia ukiachia mbali kuwafunga hata kuwaua wapinzani. Jammeh hakujua kuwa kuna mwisho. Hata hivyo, ana bahati ya mtende. Kwani ,hakuondolewa kigadafigadafi ingawa ni mapema kusema nini utakuwa mwisho wake; hasa ikizingatiwa kuwa alichafua ofisi ya rais vilivyo. Nadhani hii, ima ni kutokana na ulevi wa madaraka, au ujinga tu utokanao na kiwango kidogo cha uelewa alichokuwa nacho Jammeh na wapambe na washauri zake.
            Tano, nimejifunza kuwa sisi wavutaji wa bangi tuna nafuu. Kwani, huwa tunajivutia bangi na kubanguliwa nayo lakini si ukubwa. Heri kuvuta bangi kuliko kuvuta ukubwa tena ukubwa wenyewe uchwara.
            Baada ya kudurusu namna Jammeh alivyojisahau kwa ulevi wa madaraka na kubanguliwa na ukubwa, hebu turejee kwenye kaya ya walevi. Kwanza, tunao akina Jammeh wangapi hata kama si marais? Hapa naongelea vijijamemeh vidogo vidogo vinavyonyevuanyevua ndiyo viishi. Vipo vilivyolalamikiwa hata kuwatukana watendaji wenzao kama alivyolalamika dingi wa haki za walevi hivi karibuni akilaani ulevi huu wa madaraka. Nani angeamini kuwa mlevi anayetumwa angemtukana mwenzie anayetumwa kama yeye? Juzi si nilisikia chizi mmoja wa madaraka akimtukana mwenzie eti ni chizi wakati ukiangalia wawili hawa chizi yuko dhahiri. Wakati mwingine kiherehere, kujikomba na tongotongo ni matatizo. Majuto ni mjukuu. Tumewaona wangapi tena wanaojaa kwenye kiganja wakaondoka kama wezi? Wapo waliosema tulikuwa wavivu wa kufikiri wakaishia kuwa mabingwa wa kutofikiri.  Japo siasa ni usanii, mwingine unatia kinyaa. Huwezi kufanya madaraka kuwa maonyesho ukafanikiwa. Na ukifanikiwa ni kwa muda tu. Madaraka, hata kama ni ya kutawala walevi, ni kufuata sheria na kanuni badala ya kujikombakomba na kufanya usanii. Kwanini hawakujifunza toka kwa mzee Nchonga jamani? Huwezi kuwa wewe peke yako ndiyo mwema wakati wote waliokuzunguka ni wabaya. Nyani huandamana na nyani. Huwezi kuwa malaika katikati ya mashetani. Hata hivyo, binadamu ni nini hadi ajione bora kuliko wenzake wakati ni mazabe matupu?
            Tumalizie kwa kuwakumbusha kuwa tulichojifunza kwa Jammeh ni kwamba ulevi wa madaraka ni mbaya kuliko wa kanywaji. Na ubanguaji wa madaraka, kadhalika una madhara kuliko wa bangi yenyewe. Nadhani akina Jammeh wetu wasioona mbele wala nyuma wamenipata. Tieni akilini. Hakuna marefu yasiyo na ncha jamanini.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: