Thursday, 8 December 2016

Futeni na kupiga marufuku NGO za wake wa wakubwa

Image result for photos of salma kikwete and anna mkapa
             Hivi karibuni vyombo vya habari viliripoti kuzuiliwa kwa mzigo wa Taasisi isiyo ya kiserikali ya mke wa rais mstaafu Jakaya Kikwete, Salma baada ya kile kinachosemekana kutaka kupitisha mzigo bila kulipa kodi. Hii ima inatokana na mazoea yaliyojengeka wakati mume wa mwenye taasisi ambazo mimi hupenda kuziita kampuni kupitisha mizigo yake bila kulipia kodi au kutaka kukwepa kodi kwa kawaida kunakoweza kufanywa na mhalifu yeyote.
            Baada ya stori hii kuchapishwa, kwa sisi tuliokuwa tukipiga vita hii aina ya ufisadi unaojificha kwenye mgongo wa rais na matumizi mabaya ya ofisi ya rais, tulianza kuona matunda ya mapambano yetu. Kwani, si mara ya kwanza kwangu kuandika kuhusiana na ubaya wa makampuni haya binafsi yanayotokana na ushawishi na nguvu za kisiasa na yasiyohitajika wala kuwa na la kufanya zaidi ya kuwatumia watanzania kuchumia utajiri.
            Leo nitatoa maangalizo yafuatayo kuunga mkono ni kwanini NGO za wake wa kubwa zifungwe na kupiga marufuku:
            Mosi, kama nilivyoonyesha hapo juu, NGO hizi hazihitajiki na wala kile yanayosema yanataka kufanya kina wenyewe yaani kama ni wanawake na watoto kuna wizara nzima. Hivyo, kama wanataka kusaidia hao wanaosema wanataka kuwasaidia waelekeze misaada waliyo nayo kule.
            Pili, hii ni aina ya ufisadi iliyoanzishwa chini ya tawala fisadi ambazo baba akiwa rais basi mama atatafuta njia ya mkato ya kujitajirisha. Nani mara hii kasahau EOTF mama wa NGO ambayo ilimsababishia mke wa mmilki wa NGO hii kuondoka madarakani akiwa amechafuka na asitamanike wakati aliingia akiwa anaitwa Mr Clean? Kwa ufupi ni kwamba NGO hizi zilianzishwa chini ya tawala zinazosifika kwa ufisadi.
            Tatu, kwa tukio la juzi, ni kwamba kampuni hizi, kwa miaka yote waume wa wenye kuzimilki walipokuwa madarakani,  zilikwepa kodi tokana na kumilkiwa na wake wa viongozi kutokana na kutamalaki kwa ufisadi, ubinafsi, ubabaishaji na jinai nyingine. Kuna kipindi WAMA ilifikia makufuru ya kutumia anwani ya ikulu kwenye rogo yake. Binafsi, baada ya kuliona hili, niliwaandikia barua  wakabadili haraka ingawa walifungia barua yangu pepe. Hili lilinifurahisha kuwa angalau kelele zangu zilikuwa zikisikika.
            Nne, hata kama serikali ingeamua kuzifutia misamaha ya kodi, je wanawake na wasichana wa Tanzania wanahitaji kampuni hizi za mfukoni au wanapaswa kuhudumiwa sawa na watanzania wengine bila kujali jinsia zao? Je huku si kuwatumia kuwaibia wale wale wanaodanganywa kusaidiwa?  Haya ni mambo ya kizamani yanayaposwa kuwa historia kwenye Tanzania mpya. Kinachopaswa kufanyika ni kuzifutilia mbali NGO hizi na kuzifanyia ukaguzi wa kihasibu ili zirejeshe fedha yote zilizokwepa tangu kuanzishwa kwake. Kwanini kuwashughulikia wafanyabiashara wengine wasio na majina wakati na hizi NGO zinafanya biashara tena yenye kutia shaka?
            Tano, tunampongeza rais John Magufuli na mkewe Janet kwa kuona jinai hii na kuiepuka kama alivyofanya baba wa taifa Mwl Julius Nyerere na mkewe Mama Maria. Hata waziri mkuu mstaafu Mizengo Pinda naye ni wa kupongeza. Kwani aliona mbali tofauti na wenzake. Maana, badala ya kumruhusu mkewe kukimbizana na biashara uchwara ya NGO alimshauri kujisomea hadi akajipatia shahada mbili. Hata ukiangalia kwenye bodi ya WAMA, mke wa Pinda, Mama Tunu hayumo. Nadhani mama Pinda aliona faida ya kusoma na kujikomboa badala ya kujilimbikizia mali wakati wengine hata elimu yao ni haba. Kama wangetumia muda wa kuwepo madarakani kujiendeleza, wasingekuwa wanahangaishwa bandarini kwa sasa kwenda kugomboa mizigo ukiachia mbali kuhaha kwenye vyombo vya habari kukanusha mambo yaliyo wazi.  Elimu siku zote ni ukombozi; huwezi kuilinganisha na utajiri tena haramu.
            Sita, ukiangalia malengo namna na wakati zilivyoanzishwa NGO husika, unanusa rushwa tupu na matumizi mabaya ya ofisi ya rais. Equal Opportunity Trust Fund (EOTF) au Fursa Sawa kwa Wote ndiyo iliyofungua pazia la biashara hii ya ajabu itokanayo na ubinafsi na matumizi mabaya ya ofisi za umma.  Kwanini zilianzishwa baada ya waume wa wahusika kupata urais? Je zimekuwa zikifanyiwa ukaguzi wa kimahesabu? Je inakuwaje wamilki–kama siyo mali zao binafsi–wameendelea kuzimilki hata baada ya kuondoka madaraki waume zao? Kuna haja ya NGO hizi kurejeshiwa serikali. Kwani, zilipatikani kwenye mgongo wa rais. Ndiyo. Ukiziangalia NGO hizi kwa sasa, zimedoda. Hakuna anayehamasika kuzipa misaada. Ni kwa sababu kofia haimo tena vichwani mwao. Tunasikia wengine wanamilki hadi mashule na mali. Wanapaswa kutaifishwa na kurejesha mali hizi. Kwani ni za umma.
            Nane, tunapendekeza kufanyike mabadiliko ya katiba ili itamke wazi wazi kuwa ni marufuku wake wa viongozi wanaohudumu kuunda NGO. Hii itasaidia kuzuia wake wa viongozi wajao, sawa na waliopita, kutumia ofisi ya rais kama kijiwe cha kutengenezea utajiri wa haraka kwa kuwatumia akina mama na wasichana ambao tayari wana wizara kamili ya kushughulikia matatizo yao ukiachia mbali kuwa wanapaswa kutendewa sawa na watanzania wengine.
            Kuepuka baadhi ya wajanja kutumia madaraka ya waume zao kuwaibia watanzania, tunashauri tutunge sheria ya kupiga marufuku wake au waume wa viongozi kuanzisha makampuni almaaruf NGO.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.

No comments: