Saturday, 3 December 2016

Mlevi atathmini mwaka mmoja wa Makufuli


            Japo wengi wameishatoa tathmini yao ya utawala wa awamu ya tano, haitakuwa vyema kwa walevi kutofanya hivyo. Hata kama ni mlevi, nina haki ya kutoa tathmini yangu ya kilevi hasa ikizingatiwa kuwa na walevi ni watu kama wengine tena wana kaya orijinali. Isitoshe mabadiliko  yote  yanayotokea kayani yanawakumba. Nilingoja wengi waronge na kumaliza ili nimalizie; na kuwashinda pwenti.
Hivyo, ifuatayo ni tathmini yangu ya utawala wa rahis Joni Kanywaji Makufuli.  Baada ya kufanya mahojiano yasiyo rasmi na walevi na marafiki zangu wa karibu nimegundua yafuatayo:
Mosi, walevi–japo wanalalamika kupigika–wameanza kunyooka. Yapo mambo wanayojivunia yaliyosababishwa na utawala huu. Kwa mfano, ndoa zao nyingi zimeimarika. Hii ni baada ya warume kukosa njuluku za kunywea na hata kuhongea. Hivyo, wengi hurejea majumambani mwao mapema na kuwasaidia washirika zao wa bedroom ukiachia mbali vitegemezi vyao kuwaona kwa mara ya kwanza wakiwa sober.
Pili, matajiri uchwara na wajivuni siku hizi wana adabu.  Wengi wa matajiri tuliokuwa tukiwagwaya kumbe walikuwa wamekopa njuluku toka kwenye mabenki bila kulipa! Huwezi kuamini namna kiama kilivvyowakumba huku wengi wakipoteza mali walizodhani ni zao wasijue za mabenki. Taratibu, tunaanza kuheshimiana na kuthaminiana tofauti na ilivyokuwa chini ya utawala wa mauzauza na holelahola. Migogoro ya ndoa, kama vile ugomvi, nyumba ndogo na unyanyasaji vinaanza kupungua.
Tatu, kazi na uwajibikaji vimeanza kuthaminiwa baada ya mirija yote na misheni town kufyekwa. Bila kuchapa kazi huli. Hata wale waliozoea kuchapa kazi kwa kutumia vyeti vya kughushi au kugeuza ofisi kuwa maduka na vijiwe kwa sasa wanalia na kusaga meno huku walevi tukiwazomea. Huwa nawambia kuwa wameishaisoma namba; na mikogo na maringo yao kwishenei. Walie tu. Lazima tunyooshe kaya hata kama ni ya walevi walioiruhusu ikageuzwa shamba la chizi.
Nne, katika mahojiano nimegundua kuwa matapeli kama vile waganga wa kienyeji na wachunaji wanasherehekea biashara zao kuchanua tokana na kihoro na ujinga vya walevi. Hebu fikiria kwa mfano, eti jitu zima lenye kuitwa msomi linakwenda kwa mganga njaa tapeli au mchunaji kutafuta eti namna ya kuzuia benki isikamate mjengo au biashara zake. Inasikitisha kiasi cha kuhoji maana ya elimu pale unapoona baba au mama zima likilala kwa waganga eti kulinda cheo chake. Yupo mlevi mmoja kigagula aitwaye Wajingandiyowaliwao alinitonya kuwa huwa haamini macho yake kuona walevi wanaofurika kwake eti kutafuta dawa ya bahati wakati mwenyewe maisha yake ni bahati mbaya tupu. Kama haitoshi, utasikia jitu linakwambia kuwa kigagula fulani ni bingwa wa kuzindika kesi. Hivi kweli unaweza kuizindika kesi au ni ujinga wa kutojua namna zinavyofanya kazi?
Naona yule anasonya wakati waraka huu umelenga kumsaidia asiendelee kuliwa na kugeuzwa bwege kwa ujinga na kutojiamini kwake. Unakuta jitu zima ambalo lilijenga uadui na kanisa au nsikiti likikimbilia kwa wachunaji eti liombewe utadhani limeishanyatuka roho. Unaombewa kwani wewe maiti? Si ujiombee tena kwa lugha na namna unavyoyaona matatizo yako. Hata hivyo, kuomba ni suluhu au kujirekebisha na kukubali kufanya hivyo tokana na kubadili kwa mambo?
Tano, siku hizi hata kelele za mabaa ya kukesha zimepungua. Walevi wanatononoa usingizi kama hawana akili nzuri. Hata hivyo, kuna tatizo moja. Kuna uwezekano wa kutengeneza vitegemezi vingi kiasi cha kaya kushindwa kuvihudumia tokana na mkwamo huu.  Maana jamaa wengine walikuwa wakilewa hadi kushindwa kazi ya chumbani. Unadhani nazusha? We ngoja uone vitegemezi vitakavyoongezeka hasa usawa huu ambapo huduma za afya zinaanza kuimarika.
Mwisho, inapotokea mlevi akakupiga ofa ya kanywaji au mapupu unamshukuru na kufakamia kana kwamba ni mara yako ya kwanza na mwisho kupata zana hizi.
Tuonane wiki ijayo jamani.
Chanzo: Nipashe Jumamaosi leo.

No comments: