Sunday, 4 December 2016

Tunahitaji mfumo wa utawala si makondism


             Baada ya rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani, staili yake ya uongozi imeanza kuleta hisia mchanganyiko. Wapo wanaopenda staili yake. Na wapo wanaoiponda kutokana namna baadhi ya mambo yanavyofanywa na baadhi ya watendaji wake. Mmoja wa watendaji wake aliyevutia wengi kwa sababu tofauti si mwingine bali mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda anayesifika kwa ufundi wake wa kuchongea wenzake kwa bosi wake. Pia Makonda amevutia wengi kutokana na kusifiwa sana na rais Magufuli zaidi ya mara moja jambo ambalo wengi wanaona kama ni kumpa kichwa kiasi cha msifiwa naye kukoleza mambo.
            Hivi karibuni, vyombo vya habari viliripoti kuwa rais alimpigia simu kumpongeza na kumueleza kuwa yuko nyuma yake katika kutatua matatizo ya wananchi. Kupiga simu si jambo baya ingawa rais. Ila kwa nafasi yake, angeweza kuwasiliana na Makonda kupitia njia za kiofisi bila umma kujua. Wakosoaji wanaona; Magufuli alifanya hivyo kutaka sifa rahisi, cheap popularity ambayo inaweza kuchukuliwa kama mpango wa wawili kufikia malengo yao. Hatusemi hivi kwa kubuni. Ushahidi ni kwamba maongezi ya Magufuli na Makonda umerekodiwa na kuwekwa kwenye mitandao; ukiachia mbali kurushwa moja kwa moja kwa wananchi aliokuwa akiwahutubia Makonda.
            Tunaweza kusema kuwa Magufuli alipiga simu ili kuwaonyesha wananchi anavyokerwa na namna wanavyozungushwa na kukwamishwa. Kwani lazima rais ahangaike kumpigia simu mkuu wa mkoa wakati wana uwezo wa kuwasiliana au ni kutaka umma ujue kuwa anayosema Makonda anatumwa na bosi wake? Nadhani wananchi wanachotaka si kusikia namna Magufuli anavyomkubali Makonda bali wanataka utatuzi wa matatizo yao. Na hili likifanyika rais na wasaidizi wake wanatimiza wajibu wao. Hivyo, hawahitaji sifa wala kuwajulisha wananchi kuwa wanaunga mkono vitu kama hivyo. Tunajua kuwa kwa kumteua Makonda, rais anamuunga mkono sawa na wakuu wa wateule wengine. Rais ana mambo mengi ya kufanya.
            Magufuli hakuishia kupiga simu. Aliwataka wakuu wengine wa mikoa kumuiga Makonda. Je hii ni sahihi wakati kila mkuu amepewa madaraka kamili na kujiwekea malengo na namna ya kuyafikia? Waige nini? Mkuu wa mkoa kwenda kukamata machangudoa wakati mgambo wa jiji wangeweza kuamriwa kulifanya hili? Hiki ndicho naweza kuita cheap populism au tuiite makondism. Hii maana yake ni kwamba, wakuu wa mikoa wengine watapaswa kufanya mambo kwa hofu ya rais; na si kwa namna walivyojipangia. Wakuu wa mikoa hawawezi kutimiza majukumu yao kwa kumuiga mtu bali kufuata sheria na kanuni kulingana na mipango kwa madaraka yao.  Na hili si kwa wakuu wa mikoa tu. Hata mawaziri wetu wengi wanafanya kazi si kwa ujuzi na mipango yao bali kutaka kumridhisha bwana mkubwa. Hapa kunaonyesha ombwe la kukosa mfumo wa kuendeshea nchi; ambao, hata hivyo, Magufuli anaonekana kutopenda na kuwa tayari kuuanzisha tokana kuuhofia unaweza kumbana. Mfano rahisi ni kitendo cha Magufuli kukwepa mjadala wa kurejesha mchakato wa Katiba Mpya iliyouawa na mafisadi walioogopa kuwaumbua na kuwashuhgulikia.
            Tokana na Magufuli kuonekana kumshabikia Makonda, saa nyingine kuliko hata wasaidizi wake wengine kama vile Makamu wa rais na Waziri Mkuu, unaweza kujenga hisia kuwa anamuandalia mambo makubwa huko tuendako. Je atafanikiwa?  Uzoefu unaonyesha kuwa ivumayo haidumu. Kwa wanaokumbuka Augustine Mrema chini ya utawala wa mzee Ali Hassan Mwinyi na alivyojionyesha bora kuliko wenzake, ni rahisi kutabiri nini mwisho wa hali hii. Hakuna ndoa ya maisha kwenye siasa.
            Na Makonda naye kutaka kumfurahisha bosi wake, amelikoleza kweli kweli. Maana, anaamini kuwa asemacho lazima kitakubaliwa na bosi wake. Rejea alivyomchomea aliyekuwa Mkurugenzi wa Jiji marehemu Wilson Kabwe, Kamishina wa kipolisi wa mkoa wa Dar Es Salaam Simon Sirro na RPC wa Kinondoni, Susan Kaganda hivi karibuni. Je tokana na makondism, Magufuli atawatumbua wahusika kama ilivyotokea kwa Kabwe? Kama haitoshi, hivi karibuni, Makonda alikaririwa na vyombo vya habari akiwaita wafanyakazi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mizigo isipokuwa watatu tu ambao hakuwataja bila kusahau alivyodai wafanyakazi wengi wa mkoa wake ni wapiga majungu na washirikina. Wengi waliona tabia hii kama udhalilishaji wa wafanyakazi wasio wateule wa rais ambao wengi wameishaanza kuulalamikia sehemu mbali mbali nchini.
            Makonda amepata umaarufu ghafla tokana na kujua kucheza ngoma ya Magufuli ukiachia mbali kumsifia kupita kiasi. Kwa mfano, Makonda anaonekana kama kiongozi anayetaka kuleta maendeleo jambo ambalo ni kweli japo kwa kutumia njia za shaka. Huwezi kuleta maendeleo kwa kuwakashfu wenzako. Sijui kama Makonda anajua kuwa akiendelea na tabia hii, wa chini yake ima wanaweza kumtenga au kumkomoa akaishia ambako hakutarajia. Hueanda ni kutokana na kutokuwa na uzoefu au ukomavu kisiasa ukiachia mbali kusifiwa sana.
            Magufuli kweli amedhamiria kuleta maendeleo. Hili halina shaka.  Shaka ni ile hali ya kutumia kisingizio cha kuleta maendeleo kwa kupiga marufuku vyama vya upinzani kufanya siasa.Tunataka maendeleo; lakini si kwa sababu Magufuli anayataka bali tunayataka kama watanzania; na lazima yasitumike kuua demokrasia na kusimika uimla kwa mlango wa nyuma. 
            Je staili ya Makonda ya kufanya mambo ya kiofisi kienyeji itamsaidia Magufuli kupata anachotaka au kuzidi kuwastua wananchi?
            Tumalizie kwa kusema kuwa, kama taifa tunahitaji mfumo unaoleweka wa utawala badala ya kutegemea jazba za watu binafsi kiasi cha kushauriana kuigana na kuigizana.
Chanzo : Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: