The Chant of Savant

Wednesday 7 December 2016

Kijiwe toka Gambia kwenye sherehe ya mweleka wa Jammeh

 
            Baada ya kuweka vitu vyangu kumsaidia sister Hill Clint na kupigwa na Don Drumpfy yule mfanyabiashara wa kutia shaka na mbaguzi wa kunuka, niliamua kula kuku kidogo kule wachovu hupenda kuita majuu kwa Joji Kichaka mwenyewe. Niliuguza maumivu ya kupigwa na msanii wa kawaida baada ya Wamerekani kuchagua kwa hasira za kibaguzi. Baada ya kuondoka zangu kwa Joji Kichaka, nilialikwa na upingaji kule Gambia kwa Shehe, Profesa, alhaji, Daktari, Ulamaa, Ustaadh Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh Naasiru Deen Babili Mansa na madude mengine aliyepigwa mweleka baada ya kuupa tafu upingaji ukiongozwa na mshrika wangu tuliyekutana kule kwa mama kwenye katikati mwa 2000 Adama Barrow. Yaani hata sasa ninavyoandika, niko nyumbani kwake tukipata ti au chai na gahawa au café na kusherehekea ushindi huu ambao wengi wameuona kama muujiza wasijue hakuna kisichowezekana wachovu wakiamua kuwafungisha virago watawala wao. Nilishangaa kugundua kuwa kumbe kuna uhusiano baina ya kabila la Wolof la nchini humo na wamasai wa Bongo. Huwezi kuamini kuwa salam zao hazina tofauti na za kimasai. Wao husalimiana Naka Subasi asubuhi sawa na Subayi ya akina Morani. Mchana husema Naka Bichek bi na usiku, Naka Ngon Si. Nao wamandika ambao ndilo kabila kubwa husema Esama asubuhi na Etinyang mchana na usiku Suto Yediya. Hayo ni baadhi ya maneno niliyochukua toka Gambia bila kusahau sangara au naan yaani kinywaji au kwa ki-Wolof au dolo au mingo kwa Ki-mandinka. Hayo tuyaache.
            Hebu tuangalie ukweli.  Nani alidhani Blaise Compaore angetimka kama mbwa koko ukiachia mbali akina Mobutu Sese Seko Kuku Mwizi wa Zabanga? Nasikia rafiki yangu M7 na Jongwe Bob walipopata matokeo walipigwa na butwaa kiasi cha kushindwa kumpongeza Barrow wakati walikuwa wa kwanza kumpongeza Drumpfy alipompiga sister Hill Clint. Nao zao zinahesabika. Nawashauri wafanye maamuzi magumu kama Jammeh.
            Tunaandika hili tukio la kihistoria kule Gambia, kaya ndogo yenye watu wasiofikia hata milioni moja na nusu ambayo kimsingi ni kipande cha ardhi kwenye mto Gambia ikiwa imezungukwa pande zote na Senegal. Kama siyo wakoloni kugawana bara letu kijambazi, kihuni na kishenzi, kuna viinchi havikupaswa wala kuwepo. Hayo tuyaache. Tunaweza kuviudhi viichi vidogo kama Gambia. Ukiachia hilo, kilichonisukuma kuandika waraka huu ni ile hali ya bara letu kuwa na ving’ang’annizi wa madaraka wanaobadili katiba kuendelea kuula kinyume cha sheria.
            Kitu cha pili ni ile namna Jammeh alivyoamua kirahisi kukubali kushindwa japo baada ya muda kufanya hivyo, zilikuja taarifa kuwa kimsingi hakuwa na mpango wa kukubali matokeo. Ila alivyobanwa na kuhakikishiwa usalama wake tokana na madhambi aliyotenda kwa miaka 22 aliyokaa madarakani, alikubali kuwa kitumbua kimeishaingia mchanga.
            Kwa wanaomjua Jammeh, hakuwa na tofauti na kichaa wa kaiwada. Tofauti ni kwamba alikuwa ikulu tu. Maana, aliwahi kutangazia dunia kuwa ana uwezo wa kutumia Korani kutibu ukimwi jambo ambalo ni wendawazimu mtupu. Kama haitoshi, aliongeza mkogo kwa kusema kuwa ana uwezo wa kuwasiliana na Allah moja kwa moja.
            Nakumbuka, baada ya kushuhudia Jammeh akikiri, niliwapigia simu washirika zangu akina Mgoshi Machungi na Mipawa waliokuwa wametoka kuongea nami. Kwanza, walidhani nilikuwa nawatania. Nilipowaambia wafungulie mtambo wa Al Jazeera na kuangalia nyuzi, si ndipo walipokubali kuwa nilichokuwa nimewaeleza kilikuwa kweli tena kweli tupu.
            Kimsingi, kuanguka kwa Jammeh kumekuwa gumzo duniani tokana na kutoa somo na motisha kwa wale wote walioko chini ya utawala wa kiimla, kutokata tamaa. Wanachopaswa kufanya, ni kwa upinzani kuunganisha nguvu na kutowasahau vijana hasa wakati huu wanapotumia mitandao kama hawana akili nzuri. Jammeh alijimilkisha vyombo vya habari akasahau miandao. Hivyo, kijiwe sasa kinaanza kuandaa kuwa na wavuti wake ili ikiwezekana kuwahusisha vijana kwenye kupata gahawa mara moja moja.
            Ubazazi aliotenda Jammeh ni ima kuwafunga au kuwanyotoa roho wapinzani wake huku wengi wao wakikimbilia uhamishoni kunusuru maisha yao. Wagambia wengi wanataka apelekwe kwa pilato na kusulubiwa. Wengine wanadhani kidhabi huyu atakimbia kaya kwenda kuishi ughaibuni na kula njuluku zake alizowachapa. Mpaka sasa Barrow hajaonyesha makucha yake hasa ikizingatiwa kuwa hajakabidhiwa mikoba kuongoza Gambia. Hata hivyo, ameahidi kurejesha uhuru wa vyombo vya umbea, kufungulia wafungwa na kuirejesha Gambia kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC).
            Tukiachana na kudondoka kwa Jammeh, Mgoshi alinitonya kuwa bi mkubwa wa dingi aliyepita Njaa Kaya Kitwitwi juzi alilizwa na mamlaka ya kukusanya njuluku alipoingiza kago yake bandarini na kubanwa. Naona hata Bongo mambo yanaanza kubadilika kiasi cha waliojiona wako juu ya sheria kuanza kubanwa mbavu. Napendekeza haya makampuni ya washirika wa bedroom wa madingi waliopita yataifishwe na kulazimishwa kulipa njuluku yote waliyokwepa wakiwa kwenye ulaji. Wakishindwa watupwe lupango bila kuangalia nyani usoni. Au siyo.
            Naona kuna mlinzi wa Barrow anaingia. Huenda kuna jipya ambapo naweza kutoa ushauri.
Tuonane wiki ijayo nikirejea Bongo. Acha niwaage kwa kimandika, Foo watido.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: