Thursday, 22 December 2016

Mgoshi kukomba appointment na rahis

           Leo Mgoshi Machungi ana hasira ya kufa na mtu. Si juzi dada yake Zuhura alikwenda ku-renew hati yake ya kusafiria akaambiwa alete cheti cha kuzaliwa chake na mama yake wakati wote walizaliwa wakati wa ujima. Zuhura alitaka kupasuka alipoambiwa alete cheti cha kuzaliwa cha Mamihiyo aliyezaliwa wakati wa Mkoloni mjerumani.
            Mgoshi anaanzisha mada “wagoshi siku hizi tina watu hawana akii kabisa. Mtu anakwenda kushughuikia jambo dogo wanamzungusha utazani alikuwa akishughuikia kujua nani na nini kiimua fau John! Hivi tiache utani. Hivi kwei zie pembe aizopeekewa waziii mkuu kwei ni za Fau John au ni za kuchongwa?”
            “Kwani ulikuwa hujui kuwa hatuwezi wote kuwa na akili timamu! Mbona hili liko wazi kuwa kuna vichaa wengi tena wengine huwezi hata kuwadhania kuwa ni vichaa. Wangenitakisha mimi saini ya bi mkubwa Mahiza basi ningewapelekea picha ya kaburi lake ili wakome ushenzi na ujuha. Mwambie Zuhura akirejea kushughulikia pasi yake aandae kisimu chake awarekodi akupe uniletee niwape jamaa zangu wa Usalama wa Kaya au vipi?” anamkatiza Mbwamwitu bingwa wa kuchomekea.
            Tunaangaliana kuona huu mkwara anaochimba Mbwamwitu kuwa ana watu wake wa Usalama wa Kaya wakati kaya yenyewe si salama. Wangekuwapo na wanajua wanachopaswa kufanywa wangehangaika na wenye mitandao wakati kaya yetu ikigeuzwa shamba la bibi?
            Mgoshi anaendelea “hata kama kwei kuna vichaa kia mahai sikutegemea kuwa wengi tingekuwa nao kwenye ofisi za seikai. Maana aichofanyiwa dada yangu Zuhua aipokwenda kushuhukia pasipoti yake si kitendo cha watu wenye akii.”
            Kabla ya kuendelea Kapende anamuuliza swali “je walitaka kumtoa upepo au walimfanyia mtima nyongo kama ada ya walio wengi hasa mtu anapoonyesha dalili za kwenda nje ya kaya hata kama ni kaya jirani tena zenye shida kuliko kaya yetu?”
            Mgosi anajibu “waa wakati huu hakuwa akienda nje bali kutaka pasipoti mpya. Au ni kwa vie aiwahi kwenda Ujeumani! Si waimwambia eti apeeke cheti cha kuzaiwa cha mama yetu Mamihiyo aiezaiwa wakati wa mkooni Mjeumani!”
            “Hao nadhani ni wapiga dili wachache waliobakia kwenye ofisi za umma wakidhani wao ni wajanja hasa usawa huu wa hapa kazi tu. Laiti angerekodi maongezi yao na kuyatua kwa wanaohusika, hawa waliotaka mambo ya kipuuzi wangetumbuliwa,’ anajibu Mipawa huku akifyonza gahawa yake.
            Kanji anakamata mic “veve zani vatu baya nakwisa. Kama Kufuli nakua kali lakini bado iko vatu naua faru John iko dhani itaacha chezo yao valiozoea? Kama napata chance ya kuongea na Kufuli iko taka yeye nabadili katiba ili ifunge ile yote nasumbua vatu kama hii nasumbua dada ya Gosi.”
            Mpemba anakwanyua mic “wallahi msinkumbushe kifo cha faru John. Wallahi mie sikudhani kama wangengusa hasa ikizingatiwa kuwa alikuwa kaletwa kuzalisha faru wengi ili nasi tuendelee kujivunia urithi wetu. Yaani watu wachache wanafanya vitu kana kwamba hamnazo!”
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia guu “hili suala la kusumbuliwa dada yako dogo sana Mgoshi. Hukumsikia mkuu wa bandari akilalamika kuwa kuna wanasiasa wanaomzonga wakitaka awaache waendelee kupiga dili kama walivyozoea? Kwa vile huyu bwana kaamua kuweka mambo hadharani, napanga kwenda kumuona na kumtaka aweke majina ya hao wanasiasa wanaomsumbua ili watumbuliwe haraka. Kilasiku nalalamika kuwa hapa tunachopaswa kufanya ni kufumua mfumo huu wa mbovu wa wa mazoea na kuufuma upya. Hata hivyo, inaonekana wahusika hawapati somo hasa wanapong’ang’ania kuendelea kuongoza kwa katiba viraka ya kifisadi. Sijui wanaogopa kuwakamata na kuwatumbua washitili wao au marafiki zao? Sijui kwanini wanashikwa kigugumizi huku wakituaminisha kuwa wanataka kuibadili na kuinyosha kaya yetu ya mafwisadi.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua naye kutia buti “tuwe wakweli. Kama alivyosema kaka Msomi ni kwamba bila kuufumua huu mfumo, tutaendelea kutwanga maji kwenye kinu tukitegemea kupata unga. Nadhani tukubali. Bila kuwabana wakubwa wakatueleza ni kwanini hawataki kurejesha mchakato wa katiba mpya watawezaje kufanikisha hiki wanachotaka kufanikisha.”
            Mheshimiwa Bwege anamnyang’anya mic Sofi na kudema “nadhani hawa tunaowalalamikia wanadhani sisi tu mabwege wa kugeuzwa kama samaki. Kwanini tusifanye mpango tukaandamana kudai katiba mpya hasa usawa huu baada ya UKAWI kutukawiza kwa kukumbatia yale waliyokuwa wakipinga kama alama ya kuramba matapishi yao? Hakuna ubwege kama kukalia kulalamika wakati tunajua kuwa nguvu ya wanyonge ni umoja wao? Kama hatuwezi kulianzisha kikaeleweka basi tunyamaze kuliko kuendelea na wendawazimu na ubwege wa kulalamika. Nataka hapa niseme wazi. Wakati huu tusitegemee UKAWI wanaoramba matapishi yao, kutukawiza na kuingizwa mkenge kirahisi kama ilivyotokea kwenye uchakachuaji. Hivi kweli tuna sababu ya kuendelea kuamini kuwa kuna UKAWI wakati madai yao ya katiba yaliwekwa kitanzini?”
            Mgoshi anarejea na kusema “kaka hapa umenipa desa. Ngoja tifanye mipango ya kuomba kupata appointment na dokta Kanywaji ii timpe inshu hii ii aweze kutumbua haaka sana. Haiwezekani tiendee kugeuzwa shamba la bibi tena wakati huu ambapo tina seikai inayosema inataka kutiondoa kwenye ujima wa kuchuuzana. Mnaonaje wagoshi jamani? Kwanini tisipange kufanyia kijiwe ikuu kama aivosema dokta Kanywaji kuwa kia mmoja anaweza kufanyia mikutano yake pae kwa vie ie ni nyumba ya umma?”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita jamaa mmoja wa uhamiaji. Acha tumtoe mkuku!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano jana.

No comments: