The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 27 May 2026

Twachukia mabeberu, kupenda, na kufanya ubeberu!

Tokana na ufyatu, leo naja kifalsafa kama mwanafalsafa nguli ambaye hajawahi kutokea isipokuwa mimi. Sipigi pembeni wala kuzungusha. Leo nipo na ‘mabeberu’ yanayowabeberu mabebera hadi wanalalamika kama vichanga mbali na kubumburuka tokana na kubumburushwa na mabeberu. Jamaa hawa wanatisha usipime. 
    Mabeberu, hayawani au mafyatu ni viumbe dhalili, hstari, na hovyo.Huchukiana, kushukiana, kuchukuliana, kuibiana, kuogopana, kuogopeshana, na kusingiziana. Huchukua vya wezao wakichukia vyao kuchukuliwa.Kwao, kila fyatu ni mbuzi jike.
Kwanza, kwanini mabeberu yaliitwa mabeberu na siyo madume? 
    Kwa waliowahi kufuga au kuchunga mbuzi, wanajua namna mabeberu yanavyowabumburusha majike lau kuijaza dunia na kutupatia nyama. Kiasili, mabeberu siyo viumbe wabaya. Maana, wasingekuwapo, hata nyama choma isingekuwapo.              Pamoja na nia na uzuri wao, mabeberu huwa yanafanya makeke na kusababisha mikikimikiki na mshike mshike hadi wapate wanachotafuta. Kila beberu akitaka mambo, utamsikia akibembeleza mbuzi jike bee bee beeebeee hadi mswahili anasema hili linabembeleza jike tu. Jamani, huu siyo ustaarabu uliokiuka hasa kwa dunia ya mafyatu wabakaji hadi wanabaka hata kaya? Kwa lugha rahisi, beberu hubembeleza jike tofauti na fahari ambalo hurukia tu na kupata mchezo.
            Tuachane na mabeberu mbuzi. Tuje kwa mafyatu. Kimsingi, kwa mafyatu, mabeberu si wamakonde bali watasha. Tena ni wakwasi usipime. Ukiwapendeza wanakupiga njuluku hadi unaona kuwa kubomu na kukopa ndiyo utaratibu wa maisha hasa kwa zile kaya uchwara zinazokalia mali na kuendekeza kubomu bomu na kukopa kopa. Mabeberu hupenda sana kaya hizi. Uzuri ni kwamba Fyatuland haimo kwenye kundi hili uchwara linalojivua nguo hadharani wakati mali linazo ila linazikalia.
            Japo tunawaponda mabeberu, ni kama tunajisahau kuwa huwa, wao, tofauti na mabeberu ya mbuzi, huwa tunajipeleka kwao wenyewe. Hivyo, sioni kama ni ufyatu badala ya uzwazwa kulalamika pale wanapoacha kutubembeleza. Hata hivyo, kila fyatu hata wadudu wanajua. Badala ya wao watubembeleze kama mabeberu wafanyavyo kwa majike, siye huwa tunawabembeleza pale tunapotaka kuwatoa njuluku. Hapa, jina beberu hubadilika na kuwa mfadhili.                         Waswahili wana msemo kuwa mfadhili mbuzi, fyatu ana maudhi. Alichanacho fyatu, sawa na mabeberu, ni ukosefu na wizi wa fadhila. Ukimpa fyatu njuluku, unaitwa mfadhili, mdau, mshirika na majina mengine matamu. Hepu muulize kazitumiaje. We, utakoma. Utaitwa beberu kana kwamba una akili kidogo kama mbuzi. Huu nao upuuzi tena wa wazi ufanywao na mafyatu chizi wazijue twajua.
            Mafyatu wana mambo. Ukiwa mfadhili ukawanyima njuluku wanakunanga hasa unapostukia rongorongo zao juu ya namna walivyotumia njuluku ulizowafadhii au kuwakopesha. Ukiwastukia, jiandae. Ghafla watageuka na kujifanya hamnazo kama siyo kujitoa ufahamu waanze kukuponda pale walipokuingiza chaka kuwa wanakupenda. 
    Ama kweli, wasohaya wana mji wao. Si unajua sizitaki hizi mbichi? Japo wanajitia kulalamika lau waonewe huruma, mafyatu bumburushwa wana tabia kama ya mafahari aka madume ya ng’ombe. Tokana na ufahari wao, tena uchwara na kupenda ufahari wakati ni mafakiri wa kunuka, hujifaharisha hadi kujisahau na kuwadharau, kuwathumu, hata kuwatukana mabeberu wawapao fahari feki waipendayo na kuifuja.
                Utakuta mifyatu haichapi kazi. Badala yake inachapa majungu na starehe.Mingine inakwapua njuluku za mafyatu kwa mikono miguu na midomo utadhani itaishi milele. Mingine kazi yake ni kujikombokomba kama chawa na inzi. Halafu inataka eti nayo iheshimike au kufanikiwa kama kaya zilizoukata wakati kaya yao ikiendelea kuwa ombaomba na kopakopa! 
    Loo! Mingine inapiga njuluku tena ndefu ya mafyatu wenzao na kuishia ima kuifuja au kuificha ughaibuni. Mingine, inapoteza njuluku kuzurura kama yule habithi wa Kireno Vasco da Gama au yule Mbayuwayu wa zama zile aka Njaa Kaya. Halafu yakiambwe mfanyayo siyo yanagomba, kuzoza, kulalama, na kuwatukana wafadhili kuwa ni mabeberu. 
        Kama ubeberu ni rahisi, ujaribuni muone. Kama mabeberu ni wabaya, mbona mnajipeleka wenyewe? Kama mabeberu ni mabaya, mbona mnapenda nyama choma? Kwani waliofilisi kaya ni hao mabeberu au mabu na mafisi na mafisadi? Huwa nashangaa mafyatu wazima kuogopa mabeberu wakati mbuzi majike, pamoja na uhayawani wao, hawawaogopi. Wakipewa maji, wanatoa wana mbuzi na mafyatu tunakula nyama. Sasa hapa, ubaya wa mabeberu uko wapi?
            Tukiwa wakweli, nani si beberu tena hata wengine majike? Nazoza hivi kwa sababu mabeberu, licha ya kuwa mafahari, hupenda ufahari. Huwa ni shapu yanapotaka vitu. Yanaweza kupata kwa kudandia au kubembeleza beebeeebeeebebe. Kinachofanya nipende mabeberu, kwanza, huwa hayana chawa. 
        Pili, huwa si manafiki. Yakitaka kitu, kila kit uni mambo hadharani. Hamjayaona yanavyowakimbiza na kuwabeberu majike siyo?
Ukiachia mbali ubeberu kuonekana jambo baya hasa wale wanaoitwa mabeberu wanapostuka, hata wale wanaoukandia, ima wanao, kwa kujua au kutojua, au wanautamani na kuuonea gere. Nani asiyependa ubeberu ili awabeberu wenzake? Nenda kawaulize wahanga wa kweli wa ubeberu kama wale Gen Ziro wa kaya ya kufikirika jirani na Fyatuland. Du! Kumbe hii bangi kali!
Chanzo: Mwananchi Jtano iliyopita.

Mafyatu kuandamana kupinga kuhalalishwa upigaji

Juzi, baada ya kuupiga mma na ndumu kisawasawa si nikalikoroga likakorogeka, kunikoroga, na kuwakoroga Mafyatu wangu niliodhani mafala nisijue wananiona vivyo hivo! Kama munene wa Fyatuland, nilimtuma kiherehere wangu atangaze sera mpya. 
            Kwanza, nilitoa matangazo kuwa ningetoa taarifa muhimu utadhani nilikuwa nikiunda tume, sorry, timu ya kuchunguza timu ya kujichunguza na kuwafyatua mafyatu! Mafyatu waliganda runingani wakitegemea madini. Si waliambulia hasira na pumba. Kiherehere huyu aitwaye Aliyejuu             
            Mngojeeechemba,bila hata kufikiri na kuchanganya na zake, alizoza. “Mhesimiwa, Mtakatifu, Mtukufu, Msafi, Mpenda Mafyatu, Profesa Emeritus, Field marshal, Jenero, Mwanafalsafa, Muona Mbali, Mpendwa, Mwenye Udhu, Doktari Fyatu Mfyatuzi kanituma niwaletee habari njema. Kuanzia leo, tutaondoa sharia zinazotipa uwezo kutwaa mali na njuluku zilizopigwa ili kuwapa Mafyatu fursa na motisha kutengeneza njuluku bila kujali namna walivyofanya. Huu ndiyo unaitwa bora utawala bora.”
            Kiherehere wangu alisema mambo mengi. Maskini, hakujua kuwa Mafyatu weshafyatuka. Ukiwafyatua, wanafyatuka na kukufyatua. Hata usipowafyatua, wanajifyatua na kukufyatua. Baada ya kiherehere kufanya kiherehere na kujifanya hamnazo, si nimezinyaka kuwa Mafyatu wanataka kufyatuka na kunifyatua na walaji wenzangu. Wanasema, mara hii, kitaeleweka hata kama hakieleweki. Wanataka kuzuia jinai ambayo niliyotaka kutenda na kuhalalisha.
            Kwa tishio hili, nimeamuru wasiojulikana, lazima kijulikane. Natangaza rasmi. Yeyote asiyejipenda aingie mtaani ajue kilichowanyima ndege meno. Sikubali ufyatu huu kutaka kunifyatua nisifyatue? Sijui kwanini mafyatu wana akil ndogo kama kuku. Mnapewa fursa kupiga njuluku ndefu mnajifyatua ufahamu kama amfahamu dili zima!
            Mifyatu kwa umbea na urongo, sina mfano. Si yapo Mafyatu yenye ntima nyongo na wivu yaliyodai eti sie wanene tumefyatua sana mali na njuluku za Mafyatu. Hivyo, tunajiwekea kinga iwapo siku moja tutafyatuliwa na kujikuta nje ya ulaji tupate pa kuangukia. Nani kawaambia? Yapo mafyatu yaliyokufuru yakidai eti katiba tukufu ya Fyatuland irekebishwe kuondoa kipengele kinachozuia Mafyatu kunifyatua mimi kama kiongozi wao. Hivi, kweli hawa wana akili? Sasa yakiondoa kipengee hiki hayajui kuwa Fyatuland itaingia kwenye machafuko tokana na wapenzi wangu kuchukizwa na kutishiwa na hila hii ya kifyatu? Mnataka wanene tule wapi? Mnataka mali zetu nasi na vitegemezi, na vigegemezi vya vitegemezi na maswahiba zetu vilindwe na nini dhidi ya kufyatuliwa na mafyatu wanaougua ugonjwa wa kufyatufyatuka hovyo?
            Nilishawaonya Mafyatu kuwa Fyatuland ina wenyewe na wenyewe ni sisi. Sijui kwanini hawa Mafyatu hawaelewi inshu nzima! Kweli viumbe hawa wamelaanika sina mfano. Mliona wapi kiongozi wa kaya kama Fyatuland kushitakiwa kikatiba? Pamoja na Mafyatu kujifanya hamnazo, nina mpango mzuri wa kuwalinda Mafyatu wote. Mfano, kama kuna Fyatu atakayejiingiza kwenye ujambazi, uuzaji mihadarati, utakatishaji wa njuluku, na mengine kama haya, lazima mali na njuluku anazoita zake tuzitwae ili akome na kukomaa na kuacha uzwazwa na apigaji wa njuluku za Mafyatu.
            Napanga kutoa elimu ya uraia ambayo itawapa ujuzi Mafyatu wa kutofautisha upigaji wa kalamu na ule wa silaha. Pia, lazima wajue kuwa kuna tofauti kati ya upigaji wa kisiasa na visasi. Hivyo, nikiri kuwa kiherehere wangu alikosea. Niliposema tufute sharia ya kutwaa njuluku zilizopigwa au kupatikana kiharamu, naamaanisha wale wasio wanasiasa. Kwanini Mafyatu hawajui kuwa siasa bila ‘kazi na dawa’, Fyatuland itakosa Mafyatu mahiri wa kuiongoza.
            Inabidi Mafyatu waelimishwe na kuelimika. Wajue kuwa si kila ujambazi ni ujambazi. Upo uliohalalishwa na ule ulioharamishwa. Mbona wachunaji, sorry, wachungaji wanakunywa maziwa na kula nyama toka kwenye kundi la kondoo wao hamzozi? Kuongoza Fyatuland ni kazi kubwa inayompasa mwenye kuibeba kuwa na ukwasi ili asiaibishe kaya pale anapokutana na wanene wenye ukwasi wa kaya nyingine. Mfano, kiongozi wa Fyatuland, hapaswi kuonekana au kuwa kapuku. Akiwa hivyo, wachukuaji, sorry, wawekezaji, hawataweza kumwamini na kuwekeza. Hapa ndipo inapokuja diplomasia ya uchumi. Ili kuwashawishi wawekaji wawekao na kuchukua waa, lazima wanene wawe wananuka na kuonyesha ukwasi wa kufa Fyatu.
            Hii inatokana na ukweli kuwa, ili kuwanasa wawekaji, lazima ufanane nao. Wao, wanakuja na njuluku, wengine mikoba mitupu na kuondoka na njuluku zaidi toka kwenye shamba la bibi, sorry, Fyatuland. Nimesemaje? Namaanisha kaya makini yenye kiongozi makini Fyatu Mfyatuzi mwana wa Mfyatuko mjukuu wa Mfyatuliko.
            Huwezi kuvutia watega uchumi na wawekaji kama unanuka ukapuku. Lazima uwe na kila alama na sura za ukwasi.  Njuluku huleta njuluku. Ukwasi huleta ukwasi. Uongo, sorry, uongofu huleta uongozi. Nani anaweza kumwamini kapuku akawekeza kwake? Si atajiuliza. Kama hawa uchumi wanao lakini wanaukalia, nitajuaje kama hawatakalia njuluku zangu. Lazima kuongoza kwa mfano. Ukitaka kaya yako itajirike, lazima ujitajirishe mwenyewe kwanza ili wengine waone na kuiga. Hii ndiyo sababu ya kutaka kuondoa sharia ya utwaaji njuluku za wanene.
            Du! Hii gongo na mibangi, we acha tu. Badala ya kumwaga pwenti, tazama nimwaga pumba. Dharau kila kilichoandikwa hapa. Nilikuwa naota tu.
Chanzo: Mwananchi Leo Jumatano.

Wanawake wa Kitanga, hakuna libwata

Wengi tunaamini walishasikia mengi kuhusiana na wanawake wa Kitanga. Tunaposema wanawake wa Kitanga, lazima tukiri kuwa Tanga ina makabila mengi tena tofauti. Hivyo, hatuwezi kusema kwa kujiamini kuwa wanawake wote wa Kitanga wana sifa au tabia zinazofanana au kujumlishwa pamoja. Hata hivyo, tutafuata mjumlisho juu ya wanawake wa Kitanga ili tujibu swali jumla litokanalo na mjumlisho huu.
         Leo, tutaongelea wanawake wa kitanga japo si wote. Wasiowajua vizuri na ufundi wao katika mapenzi, hudhani kuwa wanatumia limbwata au dawa ya mapenzi. Hakuna kitu kama hiki. Wanawake wa Kitanga wanasifika kwa uchangamfu, ukarimu, na ufundi wao katika masuala ya mapenzi na ndoa japo si wote.
        Mfano, utasikia watu wakisema kuwa kuingia Tanga ni rahisi na kutoka ni vigumu. Je, ni kwanini? Hatuwezi kutoa jibu moja kwa moja au moja tu. Hatujui chanzo cha imani au msemo huu. Hivyo, ngoja tudurusu na kudadavua kidogo kuhusiana na wanawake hawa wa ambao wanasemekana kuwa wanaweza kumuandalia maji ya kuoga mwanamme na kuyachanganya na malashi ili akishaoga anukie vizuri. Je, hili si jambo zuri? Ni wapi tena hufanyika katika nchi yetu? Nani hawezi kuvutiwa na hili? Hebu jifikirie. Mume ni mvuvi. Anarejea zake nyumbani na shombo. Wewe kama mke utamfanyiani ili awezenukia uzuri? Au mme ni mkulima tena Msukuma au Muha. Anarejea nyumbani baada ya kupiga jembe kwa masaa saba na jasho. Utamsaidiaje?
         Wengine wanakwenda mbali na kudai, japo hatuna ushahidi kuwa wanawake wa Kitanga wanaweza hata kumbeba mume mgongoni kama mtoto! Lahaula lakuata! Nani hawezi kuvutiwa na ukarimu huu?
        Nani anaweza kuchukia kitu hii? Je, hili nalo ni limbwata au usafi? Hamjawahi kusikia kuwa mwanamke ni usafi? Kama ni limbwata, basi kwenye ndoa, linaswihi sana tu. Japo usafi unapaswa kuwa ni suala binafis la wanandoa wote, bado wapo wanandoa wanaosumbuka katika ndoa zao hasa akina mama tokana na kutozingatia suala la usafi wa miili na ndimi zao. Japo usafi ni suala binafsi, kwa wanaotaka kuepuka madhara yake, si chaguo bali wajibu.
        Huwezi, kwa mfano, ukaingia kitandani ukiwa mchafu na unatoa harufu mbaya mambo yakaenda. Japo laweza kuonekana jambo geni, kwani, haya hayapo? Je, ni wangapi wanawaambia wenzao kuwa ni wachafu na hivyo wajisafishe? Msioneane aibu. Ambianeni ukweli. Wapo wasiopenda kukosoana kwa maneno bali mwa matendo. Ni heri kulaumiana kwa kuambiana ukweli iwe kwa maneno au matendo kuliko kukwazana, kuogopana, au kutofautiana hata kufarakana kwa kitu kidogo japo muhimu kama usafi. Hapa, mchague kunyamaziana na kuumizana au kukerana mkilinganisha na kuambiana na mkatatua tatizo pamoja.
        Kuna baadhi ya jamii ambazo huwa hawapigi mswaki wakati wa kwenda kulala. Mtu anashinda anakula. Halafu anaingia kitandani bila kupiga mswaki. Wengine hata hawaogi wala kujitawaza. Jamani, binadamu si mnyama alale na kuamka mchafu. Hata kuku akikaribia kwenda kulala huoga kwa michanga lau alale msafi.
        Tukizingatia hayo juu na kuyahusisha na sifa za wanawake wa Kitanga, huenda tunaweza kupata maana hata bila kuwahoji. Mbali na usafi. Kuna methali moja kuwa njia ya kuingia kwenye moyo wa mwanaume ni kupitia tumboni. Mwake. Hapa, ndipo umuhimu na ustadi wa mapishi unapoingia. Jieulize ni wanawake wangapi wanajua mapishi ya kumfanya hata mtu achukie hoteli.
Anayebishia au kupinga hili ajiulize. Kwanini biashara ya mahoteli ni moja ya biashara kubwa ulimwenguni. Ni kwa sababu binadamu wote hupenda chakula kizuri. Huwezi kupiga michemsho kila siku ukashindana na bingwa wa kuaangiza. Wapo watu matajiri wasiokula vyakula vizuri si kwa sababu hawana uwezo bali wahusika hawana ujuzi wa mapishi. Pia, wapo maskini wanaokula vizuri tu kwa sababu ya ufundi wa jikoni. Kimsingi, hakuna chakula kibaya wala kizuri. Kinachoweza kukifanya kiwe hivyo ua kisiwe ni mapishi tu.
        Mambo ya chumba cha kulala hatugusi. Hata hivyo, kama ilivyo kwenye mambo mengine hapo juu, nako huko kwahitaji juhudi, maandalizi, na ufundi si haba. Leo, tunaishia hapa.
Chanzo: Mwananchi J'pili juzi.

Monday, 18 May 2026

Ndoa ni mwili mmoja wenye vichwa viwili na si kimoja


Mke na mume wote wanapaswa kuwa vichwa vya ndoa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ni vichwa hivi pekee vinavyounda taasisi hii tena kwa haki na usawa. Kwanini tunaseme hivi? Hii ni kutokana na ukweli kuwa bila kichwa kimoja, hakuna ndoa. Ndiyo maana, kwa wale waliosaini vyeti vya ndoa, huwa ni wawili tu wanaobeba jukumu kisheria la kuingia na kuunda ndoa. Wengine wanaoweza kuhusika ni wafungishaji ndoa na mashahidi. Zaidi ya hapo, hakuna mwingine isipokuwa matokeo ya ndoa ambayo ni watoto ambao nao hawana nguvu wala shuruti kwenye uendeshaji wa ndoa kisheria.      
              Hivyo, dhana ya baadhi ya imani na mila kuwa mume ni kichwa cha mkewe ni upoptoshaji na udhalilishaji wa kijinsia. Tutajaribu kudurusu dhana nzima tukiweka wazi msimamo wetu kuwa ndoa ni kiumbe chenye vichwa viwili vinavyolingana vinavyofanya kazi kwa usawa.
                Kimsingi, dini nyingi hasa za kimamboleo zinamchukulia mwanamke kama chombo cha mwanaume kutumia atakavyo. Ndiyo maana, ukienda mbali, utakuta dhana nyingine yenye ukakasi inayodai kuwa mke aliumbwa toka kwenye ubavu wa mumewe. Kiakili, hii si kweli. Mke si ubavu wa mmewe vinginevyo na mume ni ubavu wa mkewe.
                Je, chanzo cha hii dhana ni nini? Kama ilivyodhana ya mume kuwa kichwa cha mkewe iliyozalishwa na Paulo ambaye hakuwahi kuoa, hivyo, kutojua maana ya ndoa, inatokana na imani kuwa Eva aliumbwa atoka kwenye ubavu wa Adamu. Wapo wanaohoji busara na mantiki yake. Je, Mungu aliishiwa udongo kiasi cha kulazimika kutumia ubavu wa kiumbe mwingine? Je, haya ni maneno ya waandishi ambao wengi walikuwa wanaume yaliyolenga kujenga mazingira na mfumo vya kuwanyonya na kuwadhalilisha wanawake kama ilivyotokea baadaye? Hata maandishi yenyewe hayamuiti Eva mke wa Adam bali msaidizi wake sawa na housegirl.
            Tutadurusu kwa ufupi kwanini mke na mume wote ni vichwa vya familia. Katika kufanya hivi, tutajitenga na imani na tamaduni ambazo kwa Waswahili ni za kigeni zikiwemo dini. Tunasema hivi tokana na ndoa kuakisi tamaduni za jamii zinamofungiwa. Tunajua. Imani za kimapokeo karibu zote zimesheheni ngano, uzushi, mila, tamaduni za waliozileta ili kuwatawala na kuwanyonya waliozipokea bila hata kujua walichokuwa wakipokea ikiwamo taasisi ya ndoa.
            Kwanza, tumejitenga na kisa cha Adamu na Eva kwa vile hawakufunga ndoa na hawakuwa mke na mume zaidi ya kuwa mtu na msaidizi wake. Kwa vile safu hii siyo ya uchambuzi wa dini, hili tunaliacha.
            Pili, tunaangazia ubaguzi, unyanyasaji na unyonyaji vya kijinisia ambavyo vimegeuka janga si kwa ndoa tu bali jamii, tuseme dunia nzima kiasi cha mke kugeuzwa kifaa kisichopaswa kuwa na hata utambuliko.
            Tatu, tunaangalia umuhimu wa kichwa katika viumbe vyote hasa binadamu. Kichwa ndicho kinabeba hazina kuu au injini ya kiumbe, yaani ubongo. Kisayansi, ini, mapafu, moyo, na ubongo ndivyo viungo muhimu sana ambavyo visipokuwapo kiumbe hakiwezi kuishi, mara nyingi kiungo kinachotumika sana, kisichopumzika, na ni cha mwisho kufa na hivyo, kiumbe hutangazwa kufa baada ya ubongo kuacha kufanya kazi. Kuna watu au viumbe wanaoishi na kufana katika maisha na shughuli zao wasio na baadhi ya viungo kama vile miguu, mikono, ila bila kichwa, hakuna kiwezacho kuishi.
            Nne, kichwa ndicho pia hujenga utambuliko wa kiumbe. Kwa binadamu ni zaidi kwa vile sura zetu zinabebwa na kichwa mbali na kuwa nyumba ya chombo cha maamuzi na ung’amuzi, yaani ubongo. Ukitaka kujua umuhimu wa kichwa, angalia kitambulisho chako cha utaifa aka NIDA au pasi ya kusafiria, au kadi ya benki. Pale, kuna kichwa chako ambacho ni wewe. Katika utambuliko ambao humtambulisha na kumtofautisha binadamu na wenzake, chenye kutambulika siyo viungo vingine kama kifua, tumbo, kiuno, mikono wala miguu bali kichwa.
            Tano, mbali na hilo la utambuliko, hata kwenye lugha ya kawaida, mtu akikuita kichwa unajisikiaje? Je, akikuita kiuno, pia utajisikiaje? Kati ya viwili, utachagua kipi?
            Tumalizie. Kwa uzoefu wetu, mume na mke wote ni vichwa. Hili linapofanyika, wawili huaminiana na kushirikiana bila wasi wasi wa kudhalilishwa au kunyonywa mbali na kunyanyaswa.
Chanzo: Mwananchi Jpili jana.

Thursday, 14 May 2026

Judge Chande Commission: Congrats President Samia on eye opener


I won’t beat around the bush.  I heard President Samia Suluhu Hassan honestly and succinctly saying that the reports of the Judge Chande Commission she formed to probe the October 29 sacrilege belongs to her. I wholeheartedly congratulate her on this openness shall she accurately, faithfully, and openly address the root causes of the above fatal and shameful event that culminated in 518 deaths, as per the commission’s findings.
         I simply argue that, if the report of the commission belongs to the president, does it mean that even its findings, and recommendations so, too, are? If that’s the case however convoluted it is, whose money did the commission spend and why? Is that what Tanzanians deserved and expected? Is it a solution? Is it the right way to go in our quest to address and thwart the catch-22?
            Let’s start off from here. President Samia recently said “hii ni ripoti ya Rais. Aliyeunda tume ni Rais, kwa hiyo wasitokee watu wengine wakadai umiliki wa ripoti hii, ni ripoti ya Rais. Tume za huko nyuma zilikuwa zinabanwa kimya kimya, mimi nimeamua tuambizane, lakini ripoti ni mali ya Rais.” I don’t want to misconstrue or spoil what the president said. 
        Again, if we honestly and openly face it, whose report is it? Who wanted it and what for, and why in the first place? I strongly intreat the president to let we, the people own the report, its findings and recommendations. It’ll dispel the wrong notion that there’s something fishy the authorities intend to conceal especially when were refer to the words “tume za huko nyuma zilikuwa zinabanwa kimya kimya, mimi nimeamua tuambizane, lakini ripoti ni mali ya Rais. This may be misconstrued or even inferenced as the intention to butcher the report.
            We all know. There are chronic root causes that led to the October 29 mass slaughter as they revolve around injustices mainly the absence of freedom, corruption, inconducive environment for doing business, mismanagement of public funds and resources, poverty, unemployment, and above all, ineptitude. Historically, these problems didn’t commence yesterday under Samia. They’ve been seething for long, precisely since independence and others just recently.
        I don’t seek to blame, convict, or exonerate anybody but put the records straight. The creation of the commission emanated from our quest to heal the injuries we as a nation. It all revolves around how the conflict was handled, or should I say, mishandled. For, soon after the bloodbath, the authorities made many bloopers and convoluted and confusing statements alleging without substantiating that protesters were hired and sponsored by the ‘enemies’ of our country.
        Firstly, the authorities didn’t name names. Nor did it print a picture of how this plot escaped the scrutiny of our intelligence.
        Secondly, the participants were ‘drugged mercenaries.’ For, Tanzanians known for their peaceability, wouldn’t commit such a sacrilege. Where were they from, who, and why? The authorities didn’t even bother to answer these key questions, which would have acted as a hunch of unearthing and thwarting the entire dud that resulted in the miscarriage of justice.
        Thirdly, in law, he/she who alleges must prove or qui dicit, non qui negat. Thus, the authorities bear the burden of proof. That’s so to avoid offering a carte blanche for malicious people to maliciously make allegations to punish or tarnish their enemies.
            Fourthly, if we honestly and seriously underscore the triggers of the conflict and the quest to address it, do truly the Judge Chande Commission report belong to the president really? I humbly beg to honestly agree to disagree with the take of the president. For me, and perhaps for all Tanzanians, though the commission is known as the presidential commission and Judge Chande Commission respectively, belong neither to Chande personally nor the president. They belong to the people as the funders and stakeholders besides being the victims of the bloodbath in question who own everything in their country.
         Essentially, the president didn’t privately fund the commission from her pocket. Even if she did, given that she acts vicariously, namely, on behalf of the people, everything minus the bloodbath belongs to the people, we the people. If this rationale applies, the president must similarly own the massacres of our people.
            Seriously, we must separate between the president as a person and as an institution whose legality and powers come from the constitution, which belongs to the people but not to the president. I honestly beg the president to abandon the position she’s quoted taking. For whoever pays the piper calls the tune.
         Therefore, if indeed, the president owns the commission, its findings, and its report, she does so on our behalf but not on her behalf. Again, I congratulate the president on saying it point blank. For, it’ll help us to decide on the ownership even before interrogating and working on the report of the said commission if we’re satisfied with them.

Wednesday, 13 May 2026

Turidhiane, kuridhika bila kulidhishana?

 Mara nyingi kama siyo mara zote, mafyatu hujifanya wanasiasa na kufanya visasi waviitavyo siasa utadhani nao ni wanasiasa! Uongo huitwa uongozi hata dhuluma ikaitwa haki. Wengine hata uongo huuita uongozi wakati ni uongo tu. Mfano, unapojidanganya ukidhani umewadanya mafyatu wote, ujue ni muongo tu na si kiongozi. Waongo huongoza kwa uongo. Ni mabingwa wa kucheza na kuchezea maneno. Mfano, wanaweza kukushawishi ununue kanuywaji eti mnywe wote kwa faida yenu nyote kumbe ni kwa faida zao. Wanaweza kukuridhisha kuwa mnafanya, maridhiano kutopigana baa kumbe ni maridhishano ambayo mwisho wa siku, watajiridhisha kwa kukuridhisha bila wewe kuridhika wala kuridhishwa mbali na kutopata haki. Mkiwa mnapata kanywaji huongelea amani wakajitenga na haki wakati bila haki hakuna amani na amani isiyo na haki ni amani ya imani.

            Warongo wanaweza kujiridhisha bila kukuridhisha halafu wakesema wote mmeridhika ilhali mmeudhiwa na kunyimwa haki kwa kuongopewa kama hamnazo. Kuna inshu hii ambapo fyatu mmoja alimwaga kanywaji kangu tukiwa baa. Si alisema turidhiane! Turidhiane au tulidhishane kwa kujiridhisha bila kuniridhisha aliyemwagiwa kanywaji? Hili, licha ya kuniudhi, limenichanganya na kunihuzunisha. Hata hivyo, sirithiki hadi nitakapopata maelezo ya kina tena yenye kuingia kichwani. Badala ya kuridhika, nalishughulikia na kumshughulikia anayetaka kuridhiana bila kuridhishana. Mie kulalamikia kanywaji kangu eti fyatu huyu kasema mie ni adui wa amani, mshikamano, na upendo vya wanywaji! Yaani umwage kanywaji kangu halafu uniletee ngonjera za amani? Kwani, alichofanya huyu zwazwa ni haki?
            Kwani, nani anataka kuridhiana na kuridhishana na fyatu asiyeridhisha wala kuridhika mbali na kutoridhishwa na mie ninayetaka haki? Tutaridhikaje wakati ulevi alio nao tena bila kustahiki haumridhishi wala kuridhika nao? Unacheza na kuridhika hasa kwa wale wasiojaliwa mshipa wa kuridhika na vile vinavyoridhisha kwao visiridhishe? Nani atakubali kuridhiana na fyatu tena mlevi asiyeridhika na kanywaji tena ka dezo? Kwani, mie ni zwazwa nisijue vitu rahisi kama hivi ambavyo havihitaji kuridhishana kuvijua? Huwezi kunifanyia undavandava na unyama tena kizwazwa nikakubana ukaja na maridhiano. Nilidhike au kuridhishwa lini au nini wakati uliyeridhia kunifyatua sijaridhia kila kitu na kujiridhisha? Nashauri turidhishane ila siyo kudhalilishana jamanini.
            Leo, nadurusu hii kitu kuridhiana ili kuridhishana kwa kuwa huyu fyatu anayetaka kuniridhisha na kujiridhisha kuwa nimeridhika siridhiki hata punje. Kwanza, turidhike na nani na nini wakati kuridhika kunahitaji kitu kimoja kisichokuwepo kwenye equation yaani haki? Kuridhika hutokana na kuridhika na haki na siyo dhihaka. Kwa hali ilivyo, turidhishane katika dhihaka lakini si haki wala stahiki tena huyu fyatu atakaye kuridhiana na kuniridhisha hatendi  haki wala kustahiki.
            Wapo walevi waliotetea maridhiano wasijue ni marishano si kwa wote bali fyatu mchokozi. Sikuwahi kufikiri kuwa kuna siku fyatu nitaambwa niridhiane kudhulumiwa. Ili iweje yarabi? Nani anamridhisha nani? Nani anamdhihaki nani katika haya maridhishano? Unaridhiana na nani wakati wakati kanywaji kalishamwagwa? Nani anaweza kuridhiana kwa misiba isiyo na sababu bali tamaa na uzwazwa?
            Kuridhiana na kuridhishana siyo mambo mabaya. Ubaya ni kutaka kuridhiana kwa kujiridhisha bila kuwaridhisha wasioridhishwa na maridhishano tena yasiyoridhisha hata wale waliolenga kuridhiana na kuridhishana. Je, tujiridhishe au turidhike kuwa hatuwezi kujiridhisha bila kuwaridhisha wengine? Hapa, ndipo yalipo maridhiano na siyo maridhishano. Hapa, ndipo lilipo jibu la tatizo ambalo fyatu aliyemwaga kanywa kajiridhisha kuwa halipo ilhali lipo.
            Nani awezaye kuzuia muda hata atumie nguvu vipi? Unaweza kuvunja saa zote hata kuua majogoo yote. Muda upo pale pale na hautasimama wala kuharakishwa au kupunguzwa kasi. Ili kufikia maridhiano na marishano, je, yatupaswa kulazimishana au kuridhiana kwanza kuridhiana kabla ya kuridhishana ili sote turidhike? Nani anamridhisha nani na anataka kuridhishwa na kwanini kuridhishwa? Na huyo unayetaka kuridhisha na kuridhishwa tufanye hivyo namna gani? Je, kwa zengwe tulilo nalo, kuna uwezekano wa kuridhisha na kuridhiana na kila mmoja akaridhika?
            Ili kuridhisha na kuridhishana, lazima iwepo haki inayoridhisha na siyo mkosaji kujiridhisha. Je, tuko tayari kuitafuta hiyo haki yenye kuleta ridhiko au kujiridhisha hata bila ya hiyo haki kuwapo? Nani ataridhika pasina haki au haki ya kuridhika? Nani mwenye haki zaidi ya mwingine wakati fyatu anayetaka kuniridhisha ili turidhiane na kulidhishana hataki kutenda haki? Nani aanze na nani amalize? Je, yawezekana kuwapo maridhiano bila maridhiano? Nini kianze na kupatikana kati ya kuridhisha na kujiridhisha kwa kisingizio cha kuniridhisha?
            Tunaweza kujiridhisha kuwa tumeridhiana na kuridhishana. Ila tujue, kuna vitu vingine haviwezi kuridhishwa kwa vile wahusika hawapo mfano, kanywaji kangu.
            Mbali na hayo juu, kuna maswali mengine muhimu. Je, tushirikio maridhiano tunajua na kukubali ni kwanini tunataka kuridhiana? Tunajua. Kila penye maridhiano, kuna kutoridhiana, ndiyo maana yakahitajika maridhiano. Je, nini mzizi wa kutoridhiana au kutoelewana? Je, tunaweza kujibu maswali haya kwa ufasaha kabla ya kuingia kwenye haya maridhiano na maridhishano tena yanayoonyesha kutoridhisha hata kabla ya kuanza maridhiano? Je, kuna hatua, juhudi, nia safi, na hakikisho vyote vya kuridhisha za kufikia kukubali kufanya maridhiano? Kumbe naota!

Wednesday, 6 May 2026

Fyatu aunda timu kujichunguza na kuwachuuza mafyatu

  

Baada ya mafyatu kufyatuka na kunichosha kwa kunisingizia baadhi ya mambo, nina mpango wa kuunda na kutumia timu–––siyo tume–––ya kujichunguza na kuniweka huru. Hii ni kutokana na kuwafyatua mafyatu waliojitia kufyatukakufyatuka wakitaka kunifyatua wasijue ningewafyatulia mbali. Si niliwafyatua tena bila huruma. Baada ya kuwafyatua, si wakatokea mafyatu wakilalamika mie sina huruma wakati mie nasifika kwa kuhurumia wadudu hata wanyama. Hivyo, basi, kuondoa mzizi wa fitina, nimeunda timu ya ‘kutumika’ kunichunguza.

            Kwa vile hii ni timu yangu na inanichunguza, lazima itoe ripoti kwangu. Hii ni ripoti ni mali yangu siyo ya mafyatu. Naweza kuizima au kufanya nitakalo. Ataye fanya fyoko, namfyatua.  Ole wa owaje na mauzauza na rongorongo kuwa niliwafyatua mafyatu. Watakoma. Hata kama kweli niliwafyatua mafyatu waliotaka kunifyatua, walitaka nimfyatue nani? Je, walitaka nifyatuliwe kirahisi hivi bila kufyatuka na kujitetea?

            Katika kuunda timu hii, nimezingatia yafuatayo:

Mosi, nitaiunda mwenyewe bila hata kumshirikisha mshirika wangu wa bedroom. Sitafanya kosa niwahusishe wengine. Nani ajua wanaweza kufyatuka wakanifyatua kama wale waliotaka kunifyatua nikawafyatua kabla hawajanifyatua?

            Pili, nitawalipa wanaounda timu kwa njuluku zangu na si za mafyatu. Maana, nikifanya kosa nikatumia njuluku za mafyatu, mafyatua nao wenye njuluku zao watataka washiriki katika kuunda timu hii ya kunichunguza ili wanifyatue. Nani afanye kosa hili la wazi usawa huu wa kufyatuana kifyatufyatu? Hivyo, mkiona washirika wangu kwenye timu msishangae wala kupoteza muda wenu kufyatuka.

            Tatu, ripoti ya tume, sorry, timu hii itabidi niipitie kwanza kabla haijawekwa wazi. Hapa, nalenga kuondoa makandokando yoyote yanayoweza kusababisha au kuwapa mafyatu fursa au ushahidi wa kunifyatua.

            Nne, nitahakikisha timu hii inanyonga ushahidi wowote unaoweza kusababisha nifyatuliwe. Hapa, lazima wana timu wapewe darasa kabla ya kutoa ripoti ya ujichunguzaji. Nawajua fika mafyatu. Ukizubaa wanakufyatua tena kwa kujifyatulisha. Bila kuwabana, wapo tena maswahiba zako, wanaweza kukugeuzia kibao ukaishia kujikuta umeunda tume ya kujifyatua badala ya kujichunguza na kuwachuuza mafyatu watakao ufyatuliwe.

             Tano, tokana na kuwa na uhuru wa kuunda timu na kutengua, nitahakikisha watakaoleta jambo lolote la kunihusisha na ufyatuaji nilioufanya, nawafyatulia mbali bila huruma. Kama hii italeta shobo, nitapokea ripoti ya timu ya kujichuguza na kuiweka kapuni hadi mafyatu wangoje, wachoke na kusahau. Kwani, nitakuwa wa kwanza kufanya huu ufyatuzi ambao kitaalamu huitwa ufyatuzi wa kuepuka kufyatuliwa. Inshu inakuwa hivi. Unaita kadamnasi ya mafyatu tena kwa mbwembwe. Unakabidhiwa makabrasha na kuyaweka kapuni. Wakizidi kukubana, unawafyatua kwa kuwafunga kamba kuwa una mambo mengine muhimu ya kikaya. Hivyo, unawazuia wasiwe na mbambamba. Wangoje tu. Maana, haraka haraka haina baraka na mvumilivu hula mbivu hata kama wakati mwingine ni mbovu.

            Sita, nitapiga marufuku vyombo vya umbea kupewa nakala ya ripoti ya timu ili visianze kusambaza umbea unaoweza kusababisha nifyatuliwe tena kwa kazi niliyoanzisha mwenyewe. Lisrikal langu litafanya ripoti ya timu kuwa siri. Hivyo, atakayejitia kiherehere na kujifyatua kuijadili, ataozea lupango au nitamtumia wasiojulikane wamjue na kumteka na kumpoteza ili kupoteza kila kitu mbali na kuwatisha na kuwanyamazisha mafyatu ili wagwaye. Unacheza na mimi siyo?

            Saba, nitahakikisha wataalamu wangu wanaandika ripoti na kuipa timu inikabidhi harafu niikalie kifyatu na kinomi ili kufunika kombe wanaharamu wapite.

            Nane, sitatoa hadidu za rejea. Najua. Kufanya hivyo ni sawa na kuwapa vichaa rungu wanifyatulie mbali. Kwa mfano, nitatoa idadi ya mafyatu walionyotolewa roho. Kwa vile sitaki nionekane mie ni nduli kweli, napanga kuiambia timu itoea idadi ya mafyatu watano tu walionyotolewa roho. Tena, timu iseme kuwa walinyotolewa roho wakiwa wanakwapua mali kwenye maduka. Hii ni kutokana na asili na ukweli kuwa ndata wa Fyatuland karibia wote, walitaka kuwa makasisi lakini kale kamjezo kanakofanywa na wenzao wenye majoho ya uroho wa roho mtakakitu, kaliwashinda. 

            Hivyo, hawawezi kuua hata chawa. Abishaye ajikumbushe. Nani haoni chawa wanavyonenepeana Fyatuland? Hii ni kwa sababu ya upendo na kujali viumbe wote. Hivyo, ripoti ya timu itasema kuwa imegundua kuwa hakuna fyatu hata mmoja aliyenyotolewa roho isipokuwa watano waliojitakia kwa kutaka kupora mali za wenyewe ambao waliamua kuwakomesha kwa kuwafyatua.

            Tisa, nitaiamuru timu iseme kuwa waliofanya uzwazwa wa kutaka kuvuruga amani na mshirikiano wa Fyatuland ni mamluki waliokuwa wamelipwa bangi na gongo ili wavuruge tunu hizi kwa sababu ya wivu wa kike tu.

            Kumi, sitataja kiasi cha njuluku ilizopiga timu. Maana, nikifanya hivyo, nitakuwa nawachokoza mafyatu na kuwakumbusha ile kitu. Kutaja kiasi cha njuluku, licha ya kufanya wajue ni kiasi gani nimepiga, itawapa sababu mafyatu kufyatuka tena na kunifyatua. Nani afanye ufyatu huu? Thubutu yako! Timu imekula kiasi gani? Hii, huitwa chiri chirini njomba.

            Kwa vile leo nimeupiga mma vilivyo, sisemi mengi. Hivi, nimesemaje? Fanya kila kitu usomacho hapa siri.

Chanzo: Mwananchi leo Jtano.