The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Monday, 18 May 2026

Ndoa ni mwili mmoja wenye vichwa viwili na si kimoja


Mke na mume wote wanapaswa kuwa vichwa vya ndoa. Hii ni kutokana na ukweli kuwa ni vichwa hivi pekee vinavyounda taasisi hii tena kwa haki na usawa. Kwanini tunaseme hivi? Hii ni kutokana na ukweli kuwa bila kichwa kimoja, hakuna ndoa. Ndiyo maana, kwa wale waliosaini vyeti vya ndoa, huwa ni wawili tu wanaobeba jukumu kisheria la kuingia na kuunda ndoa. Wengine wanaoweza kuhusika ni wafungishaji ndoa na mashahidi. Zaidi ya hapo, hakuna mwingine isipokuwa matokeo ya ndoa ambayo ni watoto ambao nao hawana nguvu wala shuruti kwenye uendeshaji wa ndoa kisheria.      
              Hivyo, dhana ya baadhi ya imani na mila kuwa mume ni kichwa cha mkewe ni upoptoshaji na udhalilishaji wa kijinsia. Tutajaribu kudurusu dhana nzima tukiweka wazi msimamo wetu kuwa ndoa ni kiumbe chenye vichwa viwili vinavyolingana vinavyofanya kazi kwa usawa.
                Kimsingi, dini nyingi hasa za kimamboleo zinamchukulia mwanamke kama chombo cha mwanaume kutumia atakavyo. Ndiyo maana, ukienda mbali, utakuta dhana nyingine yenye ukakasi inayodai kuwa mke aliumbwa toka kwenye ubavu wa mumewe. Kiakili, hii si kweli. Mke si ubavu wa mmewe vinginevyo na mume ni ubavu wa mkewe.
                Je, chanzo cha hii dhana ni nini? Kama ilivyodhana ya mume kuwa kichwa cha mkewe iliyozalishwa na Paulo ambaye hakuwahi kuoa, hivyo, kutojua maana ya ndoa, inatokana na imani kuwa Eva aliumbwa atoka kwenye ubavu wa Adamu. Wapo wanaohoji busara na mantiki yake. Je, Mungu aliishiwa udongo kiasi cha kulazimika kutumia ubavu wa kiumbe mwingine? Je, haya ni maneno ya waandishi ambao wengi walikuwa wanaume yaliyolenga kujenga mazingira na mfumo vya kuwanyonya na kuwadhalilisha wanawake kama ilivyotokea baadaye? Hata maandishi yenyewe hayamuiti Eva mke wa Adam bali msaidizi wake sawa na housegirl.
            Tutadurusu kwa ufupi kwanini mke na mume wote ni vichwa vya familia. Katika kufanya hivi, tutajitenga na imani na tamaduni ambazo kwa Waswahili ni za kigeni zikiwemo dini. Tunasema hivi tokana na ndoa kuakisi tamaduni za jamii zinamofungiwa. Tunajua. Imani za kimapokeo karibu zote zimesheheni ngano, uzushi, mila, tamaduni za waliozileta ili kuwatawala na kuwanyonya waliozipokea bila hata kujua walichokuwa wakipokea ikiwamo taasisi ya ndoa.
            Kwanza, tumejitenga na kisa cha Adamu na Eva kwa vile hawakufunga ndoa na hawakuwa mke na mume zaidi ya kuwa mtu na msaidizi wake. Kwa vile safu hii siyo ya uchambuzi wa dini, hili tunaliacha.
            Pili, tunaangazia ubaguzi, unyanyasaji na unyonyaji vya kijinisia ambavyo vimegeuka janga si kwa ndoa tu bali jamii, tuseme dunia nzima kiasi cha mke kugeuzwa kifaa kisichopaswa kuwa na hata utambuliko.
            Tatu, tunaangalia umuhimu wa kichwa katika viumbe vyote hasa binadamu. Kichwa ndicho kinabeba hazina kuu au injini ya kiumbe, yaani ubongo. Kisayansi, ini, mapafu, moyo, na ubongo ndivyo viungo muhimu sana ambavyo visipokuwapo kiumbe hakiwezi kuishi, mara nyingi kiungo kinachotumika sana, kisichopumzika, na ni cha mwisho kufa na hivyo, kiumbe hutangazwa kufa baada ya ubongo kuacha kufanya kazi. Kuna watu au viumbe wanaoishi na kufana katika maisha na shughuli zao wasio na baadhi ya viungo kama vile miguu, mikono, ila bila kichwa, hakuna kiwezacho kuishi.
            Nne, kichwa ndicho pia hujenga utambuliko wa kiumbe. Kwa binadamu ni zaidi kwa vile sura zetu zinabebwa na kichwa mbali na kuwa nyumba ya chombo cha maamuzi na ung’amuzi, yaani ubongo. Ukitaka kujua umuhimu wa kichwa, angalia kitambulisho chako cha utaifa aka NIDA au pasi ya kusafiria, au kadi ya benki. Pale, kuna kichwa chako ambacho ni wewe. Katika utambuliko ambao humtambulisha na kumtofautisha binadamu na wenzake, chenye kutambulika siyo viungo vingine kama kifua, tumbo, kiuno, mikono wala miguu bali kichwa.
            Tano, mbali na hilo la utambuliko, hata kwenye lugha ya kawaida, mtu akikuita kichwa unajisikiaje? Je, akikuita kiuno, pia utajisikiaje? Kati ya viwili, utachagua kipi?
            Tumalizie. Kwa uzoefu wetu, mume na mke wote ni vichwa. Hili linapofanyika, wawili huaminiana na kushirikiana bila wasi wasi wa kudhalilishwa au kunyonywa mbali na kunyanyaswa.
Chanzo: Mwananchi Jpili jana.

No comments: