Vijana wa kikundi cha Uamsho cha Bara wakimrudi anayetuhumiwa kuwa changudoa
- Viongozi wetu wako wapi kulinda uhuru wetu? Walituahidi maisha bora kwa wote
Taarifa kuwa kundi la Uamsho la Tanzania bara lilivamia mitaa ya Kinondoni usiku na kuwacharaza bakora vyangudoa zimevuma sana. Wengi tumelaani kuchichukulia sheria mkononi na kuumiza watu wasio na hatia. Hawana hatia. Maana kazi ya kumkuta mtu anayetuhumiwa kutenda jinai ni ya mahakama. Kweli vyangudoa na uzinzi ni machukizo kwa wengi. Ila kama tutamia akili vilivyo, umalaya si tatizo kwa taifa kama ilivyo ufisadi, ufisi, ubabaishaji, sanaa, dhuluma na jinai nyingine zinazotendwa na watawala wetu. Kama kweli tunataka kujenga jamii isiyotenda maovu, tungeanza na ufisadi unaoleta umaskini, udhalilishaji na mateso kwa watu wetu. Inashangaza kuona watu wakijichukulia sheria mikononi kupambana na makosa madogo kama vile uchangudoa. Inashangaza kuona watu wanakuwa na roho za kinyama hadi kuwachoma vibaka wanaotuhumiwa kuiba kuku na mikufu huku wakiwaramba miguu mafisadi wakubwa wanaoiba mabilioni! Ningetumia hata kura yangu kuwaondoa wezi na wala rushwa waliojazana bungeni wakipitisha kila aina ya dhuluma kwa taifa letu. Ningetumia kura yangu kuondoa Chama kinachoitwa cha Mafisadi. Ningetumia kura yangu kuhakikisha dhuluma inaondoka. Ningetumia dini yangu kupambana na mafisadi kwanza. Maana wao wanaliangamiza taifa kwa kuliweka rehani kwa mabwana zao waitwao wawekezaji wakati ni wachukuaji na wezi wa kawaida. Je tunafikiri kivivu na kinyumenyume au kichaa? Umalaya ni suala la mtu binafsi wakati ufisadi ni janga la kitaifa. Ingekuwa mimi ningeanza kuwakong'ota mafisadi ndipo nifikiri kuwachapa vyangudoa.
No comments:
Post a Comment