Thursday, 19 July 2012

Walevi tukigoma, mtakwenda mahakamani?

WALIPOGOMA matabibu lisirikali baada ya kuwatisha bila mafanikio, lilimteka, kumtesa na kujaribu kumuua kinara wao Dk. Steve Walimboka anayeendelea na matibabu kwa mzee Madiba kule Sauzi.
Kama haitoshi, lisirikali lilizidi kuthibitisha ujuha wake kwa kukimbilia kutumia mapilato wake ambao Tundu Jissu alisema waliteuliwa kishikaji na kifadhila. Na hili ni kweli maana wahusika hawajakanusha. Wakanushe nini wakati ni ukweli mtupu?
Muhimu walelewe; sisi walevi hatuogopi lisirikali wala mapilato maana kama ni kupigika tulishapigika sana. Hivi hawa hawaoni gharama za maisha zinavyoongezeka kila uchao huku wao wakijiongezea mishiko na safari za matanuzi nje? Hivi hawa hawaoni tunavyosota huku wakizidi kutufanya majuha kwa kusema eti bado wanatekeleza ahadi ya maisha bora kwa walevi wakati maisha bora yenyewe ni kwa walevi wenye maulaji na madaraka?
Hivi hawa hawaoni vitegemezi vyetu vikizidi kujazwa ujinga kwenye misekondari ya kata wakati wao wanapeleka vyao nje na kwenye international academies zilizoota kama uyoga? Hivi hawaoni wanavyotupotezea muda kwa kushabikia na kuruhusu promotions za kipuuzi kama kuwa mjinga na Tapelitell wakati ni utapeli mtupu? Hivi kweli hawa jamaa wana macho? Kama wanayo basi wana roho mbaya na uchu wa fisi kusema ukweli.
Nani amesahau kuwa walipotishia kugoma wapiga chaki hatua ikawa hiyo hiyo-kukimbilia kwa mapilato wao wa kutengezwa. Je, tutakapogoma walevi mtakwenda kutushitaki wapi au mtawaambia ndata wenu watubambikie kesi? Sisi ni ngangari na si kama jamaa yenu toka kaya ya Nyayo kwa akina Nyang’au na Moi Kibaka mliyembambikia kesi kuokoa nyuso zenu.
Sisi ni ngangari kweli kweli. siyo kama ngangari madevu aliyewekwa ndani kule Zaainzibaa akanywea na kutoa kafala damu ya wahanga wa vurugu alizozianzisha katika kusaka ulaji binafsi. Adui yake kweli muombee njaa. Maana jamaa alivyogeuka mtoto mzuri ghafla sina mfano.
Ukimuona akitabasamu kwenye runinga huku roho ikimsuta kwa uzandiki na usaliti wake unamuonea huruma. Wenzake wenye akili kama akina Jadwong Madwong Laila Odingadi na Morgan Twangilai walikomaa wakagawana sawa kwa sawa yeye anapewa kipande cha kiti anaridhika! Kweli wabongo hawana bongo na kama wanayo basi ni bongolala.
Tunajua kila kitu hata kama sisi ni walevi. Najua mnatugwaya kama ukoma. Maana mkiamua kutuulimboka hamtuwezi tuko wengi. Nani atakwenda kwa pilato kutafuta kutuzuia kugoma wakati sisi ndiyo mahakama yenyewe na tena isiyo tishwa wala kufanyiwa uhuni ikiamua?
Sisi ni Vox populi Vox Dei asiyejua hili aelewe. Acha niwatafunie maneno haya ya kilatini. Yana maana kuwa sauti ya wengi ni sauti ya Mungu. Anayebishia hili ajaribu kutufanyia uhuni kama mliomfanyia Walimboka. Hatulimbokiki wala kutusokoine.
Sisi ni watoto wa njini bwana. Anayebisha aende Masri na Libya atajua ninachoamaanisha kuhusu mahakama hii ya walevi. I am serious mark my words. Hii ni mahakama kweli msidhani naongelea ile mahakama ya mbuzi au ya ndizi. No I mean vox populi vox Dei kwa wale wanaokumbuka ile lugha mfu ya Kilatini. Mkiamua kutunamalamkopi tutajaza mahakama zenu na mtaaibika bure.
Mwenye akili asikie na asithubutu kutuletea uhuni wa kizamani katika karne hii. Isitoshe, hata wale wauaji wa uhasama wa taifa hawatuwezi. Tutawanywesha migongo walewe au tuwagonge na michupa yetu ya gongo. Sijui kwanini matibabu hawakuwachoma na misindano yao wakakoma kutumiwa kama mijibwa koko!
Kwa wanaoujua walevi tunavyowabeba wezi kila aina chini ya dhana mbali mbali kuanzia wakuu wa wilaya na mikoa wa vijiwe hadi waheshimiwa wa kuteuliwa kula pesa yetu na kujaza mitumbo yao, watakubaliana nami kuwa walevi tumechoka. Tumepigika lakini hatuko tayari kuliwa. Najua mgosi Machungi angenisikia hili angelalamika. Maana anaogopa kuliwa usipime.
Kinachokera ni matapeli wa kisiasa kutuaminisha kuwa tunatawala kaya yetu kidemokrasia wakati ukweli ni kwamba tunatawaliwa kidemonghasia.
Demokrasia gani ambapo watu hawaruhusiwi hata kugoma kupinga upuuzi na unyonyaji visivyo na lazima wala kichwa na miguu? Leo tunaambiwa hakuna pesa ya kuwalipa matabibu lakini genge la walaji linasema lina ubavu wa kuleta wengine toka nje. Hii pesa inapatikana wapi?
Kama pesa haipo mbona mkuu kila siku yu kiguu na njia kuhudhuria minuso ya ajabu ajabu kama wa juzi wa kupanga uzazi wakati ana vitegemezi vingi kama nyenyere au kusalimiana na makocha wa kimataifa wa mpira wa miguu? Nani anataka makocha wa kimataifa wakati ligi ya Uropa inatosha kuwafanya majuha na walevi majuha zaidi na kushindwa kuwashughulikia wezi wao?
Unadhani wanasihasa hawajui kuwa upuuzi huu unawasaidia kuendelea kuwaibia walevi? Kwani hatujui?
Turudi kwenye kupanga uzazi. Nani hajui kuwa wanaojipeleka kwa kimbelembele chao kwenye mikutano ya kupanga uzazi wao hawapangi uzazi. Mkuu Jake Zuma hili alijua fika. Hata Jake wetu hapa kijiweni naye analijua hili.
Anayebisha amuulize aseme ana vitegemezi vingapi. Ajabu mkuu wetu hapa kijiweni eti ndiye anakwenda kuhudhuria vikao vya kuupanga! Naona alipaswa kuhudhuria vikao vya kupangua na kuvuruga uzazi na si kuupanga. Maana ushahidi wanao mikononi kuwa walishindwa kwenye somo hili la kupanga uzazi. Hapa lazima tuambizane ukweli.
Huwezi kuwa na wake lukuki ukapanga uzazi. Hapa hatujaongelea nyumba ndogo kibao ambazo wengi huwa nazo na kuzificha tena kwa gharama ya kaya. Nimekumbuka stori ya dada mmoja, sijui ameishiwa wapi siku hizi baada ya wanoko kumfichua na kumshupalia? Hayo tuyaache turejee kwa wapanguaji uzazi.
Jamaa anaendelea kutotoa pamoja na uzee ule kutokana na kuficha mvi zake kwa kupaka piko, hivyo, aendelee kuonekana kijana wakati ni babu. Hata hivyo, hayuko peke yake. Najua akina wengine kule mjengoni Dodoma nao wana vifaranga kama hawana akili nzuri. Ajabu wanamcheka daktari Silaha eti anazaa uzeeni wakati wao wanazaa ubabuni! Kweli nyani haoni kundile!
Naona yule kunguru aliyeachika anazidi kutotoa vifaranga. Acha nikampe somo la kupanga uzazi na akikataa nakwenda kwa pilato.
Chanzo: Tanzania Daima Julai 18, 2012.

No comments: