The Chant of Savant

Wednesday 7 May 2008

Leo mafisadi tunawapa ‘live’

BAADA ya kuwa mbali na Kijiwe kwa muda mrefu tukiwasaka mafisadi, tumerejea na kukutana kutoa shinikizo: watuhumiwa wote wa ufisadi na ugaidi wa kiuchumi wawajibike, huku sirikali ikitakiwa kuwawajibisha wanaogoma kujiwajibisha. Hii kaya ni yetu si yao wala mama zao.

Mzee mzima nilitafuta appointment na Tunituni Mkahapa na kunyimwa kiasi cha kumtwanga note wiki iliyopita.

Mgosi kama kawaida analianzisha.

"Mzee Mpayukaji hebu kwanza tipe stoi ya safai yako ya Kanada uikofuatiia nyendo na nyayo za Kadamage."

Najikakamua na kuanza: "Wazee, safari yangu ya Calagary kule Ukanada haikuwa mbaya. Nilikula mikuku na kunywa sana. Kuna baridi si mchezo. Nilifika kwenye Hoteli ya New Calgary aliyokaa Kadamage kupokea mshiko wa Richmond."

Natulia kidogo na kumeza kahawa na kuendelea: "Kwanza nilipitia London. Niliposhuka Heathrow nilitimka zangu Cardiff kwa rafiki yangu. Pia nilishangaa kidogo mitaa ya Trafalgar Square bila kusahau St. James Park na baadaye nilikwenda makao makuu ya SFO kupitia mafaili ya bilionea wa vijisenti.

"Niliyoona ni makubwa na hapa kutokana na sababu za usalama sitayasema. Kifupi ni kwamba Kaya inagugunwa, acha kuliwa."

Kabla ya kuendelea Makengeza anaamsha kibendera: "Mzee lengo la kukutana ni kutoa shinikizo kwa mafisadi wanaong’ang’ania ofisi zetu."

Anakohoa na kugida kahawa. Anajikakamua baada ya kashata kumkwama.

Anasema: "Yaelekea mafisadi wanataka kunipiga juju."

Kicheko kwa sana.

Anaendelea: "Wazee, tuseme bila kumung’unya. Hivi Eduwad Hosheya, Grei Mgonjwa, Johansen Mwananyika, Olewake Naikome na wengine wanangoja nini kwenye ofisi zetu? Nasikia na mama wa Ghasia ni nduguye Bi Mkubwa wa Mkuu!"

Kabla ya swali kujibiwa, Mchunguliaji anafoka kwa jazba: "Kwanza kabla ya kuwabana hawa waondoke, tutamke wazi mkuu asikie. Tunataka mgodi wa makaa wa Kiwila na njuluku alizokwapua baba lao Makapu na nkewe, kitegemezi na nke wake na Kivyele na Jona wa kutisha tisha virejeshwe haraka ndipo tuelewane.

Lazima tutoe uvivu na kusema laivu na kavu: tunataka mali zetu kinga baadaye. Maana hawa hawana kinga wala Kiwila."

Mpemba anaongeza chachandu. "Yakhe mwajua? Kama siyo mafisadi kuiba pesa yetu kaya yetu ina uwezo wa kuwa na watu wanokula yai, keki na pilau kila siku katika nlo wao. Tazameni Unguja watu wazalisha karafuu peke yao duniani lakini wao wa mwisho kwa umaskini."

"Ami usemayo kweli tupu. Hebu nenda kule Mwanza, Kahama, Buzwagi, Geita na Tarime. Wanazalisha dhahabu kwa fujo. Kadhalika wanaongoza kwa umaskini nchini huku mijitu kama Chenga lasema bilioni moja ni vijisenti!" Anaunga mkono Kapende.

Mara Mbwa mwitu anaingilia kwa ghadhabu. "Kapende hujakosea. Hii mijitu haiibii umaskini bali roho mbaya, ulafu na ushamba wa maisha. Tazama inavyoanza kuumbuliwa huko ilikodhania ni salama wakati si salama."

Kabla ya kuendelea, mzee Maneno ankwanyua mic. "Mie hamjui. Hata huyu Chinga mwenzetu ipo siku yake na nkewe yatafichuka iwe ni Sauzi, Uswisi au Amerikani."

"Du! Mzee Maneno kwa pwenti sikuwezi! Ila hadi wakoloni waseme. Maana hata hawa mafisadi wa sasa wamefichuliwa na wakoloni si wetu wapendao kuvuna wasipo panda." Anashangaa Kapende.

Msomi mkata tamaa anaingilia. "Wazee michango yenu ni makini sana. Haya majitu kama alivyosema Kapende pale yanaibia roho mbaya. Kinachotia kinyaa ni ile hali kuwa ni mbweha na fisi hawa hawa wanaokesha Ulaya eti wakiomba misaada kwa ajili ya Kaya kumbe wako kwenye kuficha pesa yetu!

Zitazameni shule, barabara, hospitali zetu hata wanakaya wetu. Hoi kabisa. Kinachokera ni ujuha na upofu wa fisi watu wetu. Mbona Mchonga amekufa mtu maskini na anaheshimika kuliko mabilionea wa vijisenti kama Chenga na Mobutu?"

"Msomi hujakosea. Hii mifisi ni minafiki sina mfano. Unakumbuka Daniel arap Mwai alivyokuwa hakauki kanisani kila Jumapili hadi tukadhani mlokole? Lakini angalia alivyoichezea kaya yake na kuwaua wapinzani wake utadhani Attila the Hun!"

Msomi anaendelea: "Ndugu yangu ulokole kwani dili siku hizi? Hujawaona madaktari tena waheshimiwa waliokimbilia polisi kutafuta kuhalalisha usanii wao?

Mwana wa Maria alisema si wote wasemao Bwana Bwana ni wake. Sasa usishangae siku ya siku kumkuta ambaye hukumdhania na usimkute uliyemdhania.

Nani alidhani Tunituni hata Chekacheka wangegeuka mifisi? Nani alitegemea Ewassa awe fisadi wakati kila siku alijitia kuhimiza maendeleo wakati yeye ndiye kikwazo chake? Wanafiki hawa. Hujamsikia Hosehena akisema eti atawabana mafisadi wakati yeye ndiye kiranja wao!"

Anakatua kashata na kupiga funda kama tatu za kahawa na kuendelea. "Nani kwa mfano alitegemea Jongwe Robert Mugabe kugeuka mbwa tena kusiri au Tunituni kibaka?

Nani alitegemea Yoshwa M7 kugeuka dikteta mchana?

Hivi nyoka angepewa miguu angedhuru wangapi? Hivi na jongoo angepewa macho angechimbua wangapi?"

Falsafa yake si saizi ya Kijiwe. Kila mtu amebung’aa akitafakuri.

Msomi anaendelea: "Dalili za mfumo mchovu na mbovu ni kung’ang’ania mabaki ya watu wenye mawazo machovu na mabovu kiasi cha kuwa na utawala mbovu na mchovu uzalishao wananchi maskini na watawala vibaka na majambazi. Ndege hatununui tunakodisha mikweche! Pesa tunaficha nje, vitambulisho, paspoti, upelelezi wa mafisadi wetu vyote nje! Mawazo nje! Hata Mpayukaji, nje! Nje nje utadhani bendi ya Pwagu na Pwaguzi!"

Anakohoa na kuendelea: "Je, na kuondoa mipaka na mimbweha kwenye taasisi zetu tunangoja amri kutoka nje? Kufikiri hadi wafadhiri! Nani kasahau ya Ballalii? Sijui naye kaishia wapi?

Yaani Kaya imekosa hata mtu mmoja mwadilifu na mwenye akili akamkamata fisadi huyu?

Tumeshindwa tunaokula nao kila siku tutamuweza Ballalii wa majuu?"

Anakohoa huku Mbwa mwitu akiguna. "Du! Mzee hatukuwezi. Wewe ndiye ulifaa kuwa mkuu."

Msomi anatabasamu akifurahia ujiko na kuendelea: "Kinacho kera zaidi ni majambazi yanayouibia umma, kushitaki vyombo vya habari eti yamechafuliwa majina wakati wao ndio wanaichafua jamii. Utaliona jitu lina gari, nyumba, ofisi, hata sura nzuri. Lakini jizi linalolilia uheshimiwa wakati halina heshima!

Kwani hawapo hawa miongoni mwetu? Hawa wanaong’ang’ania taasisi za kaya ilhali waliishajichafua, ni nini? Hawa wanaowalinda nao si majambazi na makapi wenzao?"

Anabwia kahawa na kuendelea: "Ni upuuzi watu wazima kufanya mambo ya kitoto halafu wakataka watendewe kiutu uzima badala ya kitoto. Mtoto huosha tumbo lake akadhani kaosha mwili mzima. Huyu ni mtoto. Hivi jitu zima linapofanya upuuzi wa kitoto kuficha pesa nje halafu eti likadai si kibaka, hivyo liheshimiwe wakati umma unajua, ni nini kama si utoto?

Jitu linatumia madaraka makubwa kujipatia utajiri utokanao na ujambazi halafu linataka liheshimiwe!

Jitu linawajaza marafiki na vibaka kwenye taasisi za kaya wanafanya madudu halafu eti linataka liheshimiwe na kuaminiwa!

Jitu linaua miiko ya uongozi halafu eti linataka liitwe kiongozi badala ya jisanii na tapeli!

Jitu linaishi kwa kubabaisha na kuuhadaa umma halafu linataka eti lipewe nafasi nyingine huko tuendako! Jitu …"

Kabla ya kuendelea mara mzee maneno aliyekuwa akishangaa falsafa anaangusha kikombe.

Kinalipuka kama bomu dogo. Tunaruka kila mmoja kunusuru roho yake. Tulidhani magaidi wa tindikali wamevamia kijiwe!

Source: Tanzania Daima, Mei 7, 2008.

No comments: