Saturday, 12 September 2009

Mpayukaji awa mgeni wa Gadaffi


WIKI mbili zliyopita sikuonekana mitaa ya Posta, Magogoni na Kariakoo. Nilikuwa nchini Libya nikijichana mikuku kwenye sherehe ya miaka 40 ya kuadhimisha kusimikwa kwa demokrasia ya kijeshi nchini Libya.

Najua wambea wengi watapinga na kuniona mzushi. Hawa siwajibu. Picha zangu kwenye mitandao ya kijiwe zitawaonyesha nani muongo na nani mkweli.

Tuliongea mengi na mheshimiwa mwana mapinduzi ambayo mengi ni siri kwa ajili ya usalama wa kijiwe.

Ingawa yote ni siri, nitawamegea moja. Kwanza , jamaa pamoja na wakosoaji kumuita imla amejenga nchi yake. Wakati sisi tuna watu wasio na kazi zaidi ya nusu ya idadi ya wana kaya wetu, yeye ana aslimia 13 tu. Wakati sisi tunajenga uhujumaa na kujimegea, mwenzetu anajenga himaya yake vilivyo. Maana anamuandaa mwanae Sayf al-Islam kuchukua ukanda sawa na Ala Mubarak atakavyofanya huko Misri.

Kitu kimoja kilinistaajabisha. Kumbe jamaa huyu ana asili ya Bongo tena Ushoto kwa akina mgosi Machungi wa Sengaa! Maana wao wanamuita Kadhafi. Je hii ina tofauti gani na Kashafi wa Lushoto? Hiyo mtajaza wenyewe.

Jamaa anaongea bwana. Wakati mwingine anavuka mipaka. Unajua alituchamba kuwa tunapaswa kuzitumia vizuri raslimali zetu badala ya kuwa ombaomba kwa wazungu ambao ingawa siku hizi amekubali yaishe, hawapendi. Pia alisema hakuna haja ya kuwa na uchaguzi kama mtawala aliyepo ni kipenzi cha watu na chaguo la Mungu kama mimi. Jamaa ananata anapoelezea mafanikio ya utawala wake ambao, kimsingi, ulituvutia kiasi cha kutaka tuwe karibu naye lau atumegee galoni kadhaa za mafuta.

Najua wabaya wangu watasema nilikwenda kule kuzurura na kutafuta sifa. Nimesikia wengine wakihoji ni kwanini sikumkaripia Hugo Chavez aliyetoa mwaliko kwa jamaa yetu wa Sudan , Omar Bashir anayesakwa na mahakama ya kimataifa kwa kuwadedisha wadafuri. Hawajui kijiwe chetu kinamuunga mkono mia kwa mia na kwa geresha bwege tumetuma jamaa zetu waende kumsaidia!

Mie siwezi kumlaani Chavez wakati ana wese ambalo tunalihitaji kwa udi na uvumba. Upo hapo? Pili sisi AU tunamuunga mkono Bashir kwani ni mwenzetu na anafanya vitu vyake kama sisi. Tofauti ni kwamba yeye anataka kuibinafsisha Sudan kwa waarabu. Sisi tunagawa kwa wawekezaji na wachukuaji.

Kabla ya kuanza maroroso ngoja niwamegee msafara wangu wa juzi kule Tree-pori nilikokaribishwa na kiongozi wa watu mpendwa kwa sifa na kujisikia Kanali Kadhafi alipokuwa akisherehekea mapinduzi yake matukutu.

Ingawa wachambuzi wengi wanatukandia kuwa ombaomba tulijipeleka na kujipendekeza kwa imla huyu huku nchi za wafadhili zikimpiga kibuti, si haba tulitanua. Kwanza kulikuwa na vimwana wa kimanga usisikie. Mie na Mswati tulitaka kuondoka na kimoja kila mmoja lakini si unajua wamanga wasivyoruhusiwa kuolewa na waswahili ambao huwaita watumwa?

Noma nyingine ni kwamba bi mkubwa alikuwapo kiasi cha kunichunga utadhani mbwa kaingia jikoni.

Mambo ya vidosho tuyaache. Wakati wanakijiwe kwa uvivu wa kufikiri kama alivyosema mjasiriamali Che Tunituni wa Makapu, wanasota kwenye nyumba za kupanga na kuishia kubakana, nchini Libya serikali hutoa nyumba na mahari kwa wanaotafuta majiko tena majiko kweli kweli siyo haya yetu ya chuma ulete.

Tulikuwa tukishutumiwa kuwa tunatumia vijisenti vya walipa kodi kusherehekea upuuzi. Jamaa alimwaga bonge ya pati kwa wiki nzima huku akiupamba mji wa Tree-Pori kama bibi harusi. Una habari jamaa kalipa pauni za Uingereza 30,000,000 kwa watumbuizaji tu? Wapo wanaosema kuwa jukwaa tulilokuwamo lilojengwa na kampuni ya kiingereza liligharimu pesa nyingi zaidi ya watumbuizaji. Bado hujaweka makando kando mengine kama zawadi wa watawala wachovu na omba omba. Hizi zikitolewa kwa kijiwe chetu angalau watoto wote wa wanakijiwe na kaya kwa ujumla wanaweza kusoma hadi chuo kikuu huku wakiendesha migari ya bei mbaya kama yetu na wengine kusafiria midege kwenda kufanya mitahani.

Kitu kingine, wapo waliosema eti wamanga wa Kiswahili wa Libya ni wabaguzi. Si kweli. Kama ni wabaguzi basi ni kichini chini. Hata kama wanabaguliwa kuna mtu aliwaita? Mbona niliona waswahili wengi wanaotaka kuzamia zao majuu wamejazana pale Tree-Pori. Mswahili bwana hana dogo. Wakati napita kwenye mitaa ya Sawan bin Adam kuelekea Awlad bin Ahamad kabla ya kwenda kuhudhuria maonyesho ya ngoma za kiasili kwenye mitaa ya Suq al Jum’ah na mingine mingi yaliyotukaribisha kwa kupamba mitaa tukitoka Tripoli International Airport niliona maajabu. Nikiwa nafaidi maraha yangu si nilisikia mzamiaji mmoja akipayuka kwa Kiswahili: “Mzee sisi huku tunasota tupigie debe lau tupate gamba tujichome zetu majuu.” Mie nilikausha. Naye hakunikawiza. Nilisikia akisema Ibn Muthnake huyo hana lolote bali kuzurura na kujilisha pepo.” Jamaa inaonekana anatokea kwenye mitaa ya Saigon na Sinza Sinza kwa washikaji zangu au Makongo na UDSM kwa vidosho. Maana nilivyomuona si mgeni kwangu. Nilipoulizia maana yake nilitaka kupasuka. Tuyaache haya ya waswahili na misoto yao .

Nyakati za usiku tulikwenda kujimwaga kwenye mitaa ya Umar al Mushtar na An Nasir na Jamhuriyah kutaja kwa uchache.

Makazi yangu yalikuwa kwenye hoteli ya kifahari ya Bab al Bahr. Nilipenda sana heshima ya Walibya. Kila anayekuja kukuhudumia utasikia akikuita Basha. Msidhani nawatukana waswahili, Basha kwa ndugu zetu wa Libya na Misri ni bosi na si matusi ya nguoni kama kwenu uswekeni. Hivyo nilikuwa bonge ya Basha yaani Bosi.

Ujumbe wangu ulipelekwa bichi kwenye maeneo ya Bu Sittah ambapo kila mmoja alijimwaga kivyake. Vijana watawasimulia makamuzi na matanuzi ya siku hii. Mshirika wetu Chavez alikipiga kwenye hotel ya Zumit kwa ajili ya usalama wake huku ujumbe wake ukikipiga kwenye hotel za Funduq al Bahar na Funduq an Naher. Si unajua tena anavyowindwa na mabeberu. Hayo tuyaache.

Kuna kitu nimejifunza. Tuache utani. Kumbe ukipambana na ufisadi na ukausikiliza umma hata uwe dikteta, ukiwapa watu riziki zao na maendeleo wanatulia! Kumbe demokrasia kwenye umaskini ni uongo. Maana demokrasia siyo maneno bali matendo. Ingawa jamaa anasifika, kuna tatizo. Sifa zake zote zinatoka upande mmoja yaani serikali yake.

Hakuna upinzani kule. Nani apinge? Hajitaki? Watamzomea.

Loh! Kumbe muda umekwisha!

1 comment:

Anonymous said...

Very Interesting!
Thank You!