Kudos to President Magufuli

Sunday, 31 December 2017

Taathmini fupi ya mwaka uliopita

                 
              Mwaka uliopita, sawa na miaka mingine, ulikuwa na changamoto zake na mazuri yake. Blog hii iliupokea na kuuishi mwaka uliopita kwa namna mbili kibinafsi na kijamii. Kwa mfano, kwa upande wa mambo mazuri, madikteta watatu walidondoka yaani Eduardo Dos Santos wa Angola aliyeamua kuachia ngazi , Yahya Jammeh aliyepigwa mweleka kwenye uchaguzi aliouandaa mwenyewe kabla ya kugoma kuondoka na kulazimishwa kufunga virago na kukimbilia uhamishoni huku Robert Mugabe akipinduliwa kiulaini na kulazimika kujiuzulu. Kadhalika, taifa lenye nguvu kuliko yote duniani, Marekani, lilipata rais mbaguzi na mnyanyasaji asiyejua kitu kuhusiana na sera na siasa za kigeni Donald John Trump. Nchini Uganda, imla wa miaka mingi Yoweri Museveni alibadilisha katiba kuendelea kuwa madarakani sawa na wenzake wa Rwanda na Burundi bila kusahau Sudan ya Kusini zote zikiwa mwanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki.
           Tanzania ilipiga vichwa vya habari kwa sababu nzuri na mbaya tokana namna ya uongozi wa rais John Pombe Magufuli huku akipendwa na wanyonge wengi na kuchukiwa na watu wa kipato cha kati baada ya kuminya vyuma kiasi cha kukaza. Jambo baya lililotekea Tanzania ni kupigwa risasa kwa mwanasiasa machachari Tundu Lissu ambaye anaendelea vizuri hospitalini nchini Kenya akingojea kupelekwa Ulaya kwa matibabu zaidi. Nchini Kenya uchaguzi uligeuka vita kiasi cha watu wasio na hatia kuuawa ukiachia mbali mafahari wawili Raila Odinga na Uhuru Kenyatta kuendelea kuigawanya nchi kikabila na kisiasa hadi sasa.
     Habari funga mwaka ni kuripotiwa kuuzwa kwa waafrika utumwani nchini Libya huku dunia ikinyamazia unyama huu kana kwamba waafrika hawana thamani na kama wanayo hawana tofauti na kuku, mbuzi hata punda wa kuuzwa bila kustusha. Sambamba na hili lilotokea tukio la rais Trump kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel; jambo ambalo lilipata msisimko dunia nzima huku nchi nyingi zikiandamana na kupinga na kulaani lakini zikakaa kimya dhidi ya kadhia ya kuuzwa waafrika. Ajabu ya maajabu, na baadhi ya waswahili chini ya mwamvuli wa Uislam waliingia kwenye bandwagon huku wakishindwa kulaani kuuzwa kwa ndugu zao.
         Kwa ufupi mwaka huu ulikuwa na ugumu wake. Binafsi, kitinda mimba wetu Nkwazi Mhango Jr alianza vidudu huku kaka yake Nkuzi akiingia darasa la pili.
Kwa ujumla ndivyo tulivyouona na kuuishi mwaka uliopita. Je msomaji nini tathmini yako fupi ya mwaka ulioisha?1 comment:

Yasinta Ngonyani said...

Tathmini yangu ya mwak uliopita ni kwamba ulikuwa mwaka wa changamoto sana lakini twamshukuru Mungu tumeuona mwaka mpya 2018