Kudos to President Magufuli

Wednesday, 7 March 2018

Kijiwe chaipongeza BASATA kupiga marufuku nyimbo chafu

            Baada ya wanene kuzinduka kwenye lepe zito la usingizi ambapo waliachia kila kitu kijiendee chini ya tawala uchwara zilizopita zikisifika kuridhia ufisadi na wizi wa fedha na mali za umma, kijiwe kimekaa kama kamati kupongeza hatua za makusudi zilizopelekea kupigwa chini miziki na nyimbo chafu kayani.
Leo Kapende ndiye anaanzisha mada. Anakunywa kahawa yake na kuzoza “jana mliona namna wanene walivyoamua kutolea uvivu mila chafu kwa kupiga marufuku baadhi ya nyimbo na miziki michafu? Japo wamechelewa kulienga hili, hapa kusema ukweli wamenikuna; na nawapongeza japo sitaki walemae tokana na pongezi hizi. Pia, napendekeza wote waniocheza na kuchezea mambo machafu kama vile kigodoro wanyongwe huku wale wote wanioshabikia wafungwe maisha.”
Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea “unasema wanene wamekukuna; wamekukuna vipi na wapi? Hebu ongea tukuelewe na ueleweke.”
Kabla ya kujibu, Mipawa anakula mic “tuache utani. Hali ilikuwa imefikia pabaya kiasi cha kushindwa kutofautisha kama kaya yetu ni  ya vyangu au wanyama. Maana chini ya utaahira wa kuigiza majuu, ilifikia mahali wachovu wakaanza kutembea uchi kama vile wale wanaovaa milegezo wakionyesha michupi yao michafu. Natamani kila mwanakijiwe atembee na bakora ili tuwavue hiyo milegezo na kuwanasa bakora kama siyo kuwafanyia kitu mbaya au vipi?”
Mzee Maneno anampoka Mipawa mic na kudema “kama ulipopiga na kugusa ndiyo penyewe mzee mwenzangu. Ni kweli kaya yetu imejiruhusu kudhalilishwa na mataahira wachache wanaosumbuliwa na ujinga na ulimbukeni kwa kisingizio cha usanii na kutafuta njuluku. Mie napendekeza hawa watembea uchi nao wafungwe maisha ili wakaozee lupango. Maana nao wanachochea ubakaji na udhalilishaji wa akina mama hasa wale wasiotaka kujidhalilisha na kudhalilishwa.”
 Mijjinga aliyekuwa akimaliza kuvuta kipisi cha sigara kali anaamua kutia guu “napedekeza wasanii wa kigeni waliojazana kayani wakieneza uchafu kama wale waliosamehewa kwa makosa ya ubakaji watimliwe kayani haraka. Maana wanachafua maadili yetu huku majuha wengi wakichekelea na kuhadaiwa kuwa hii ni burdani. Burdani gani ya kudhalilishana?”
Kabla ya kuendelea Kanji anakula mic “veve sema jambo kuba sana. Kama hii geni nakuja cheja ngoma itaendelea na chafu yao kaya yetu navezapoteza hishma. Kama iko vachowu nataka burdan ya uchi kama nyama basi iende fungia kwa nyumbani yao ifanye chafu yao. Kama nataka faidi basi iende funga kwenye bedrooms zao na kuenjoy hii laana zao.”
Kabla ya Kanji kuendelea, da Gau Ngumi Nungaembe anakula mic “jamani hali inatisha na kukatisha tamaa. Sijui nani aliyeroga kaya hii? Kwanini kuwaonyesha vichanga mambo ya kiutu uzima. Wakifyatuka na kuanza kuushobokea mnawalaumu wakati mliruhusu nyie wenyewe kwa ujuha wenu.”
Msomi Mkatatamaa anaamkua kutia guu “naungana na wasemaji wote waliotangulia kuwa kuna tatizo tena la kimfumo si kuhusiana na maadili tu bali mambo yote. Tumegeuka shamba la bibi kwa kila kitu. Tumegeuka tegemezi kiasi cha kutia kinyaa. Yaani tunaruhusu wachafuzi wa maadili toka kaya jirani kana kwamba sisi hatuna muziki wetu kama kaya? Nakubaliana na wanaohoji aliyeturoga. Nadhani baada ya Mzee Mchonga kutuonya tukashinda kumeuelewa, sasa tunalipia kwa bei mbaya zaidi. Hebu tuwe wakweli. Unaposamehe wabakaji zaidi ya kuwapa motisha wabakaji wengine ambao hawajapatikana unafanya nini? Hivi kweli hili nalo linahitaji uwe mwanasheria ndiyo uelewe?”
Mpemba aliyekuwa akiteta jambo na mgoshi Machungi Shekiango anakula mic “yakhe hata mie hili lantisha. Sijui kama hawa watoto walobakwa wangekuwa wa wanene kama wangefikiri, achia mbali kusamehe hawa wahalifu ambao sasa wametumia fursa hii kuwa masupastaaa. Watu wazima na akili zao watembea uchi kama wanyama huku wengine wakitanatana nguo eti wadai hii fasheni wakati ni ulimbukeni, umajinun na ulimpyoto. Mboni hao watasha wanioigizwa hawaigizi fasheni zetu?”
Kabla ya kuendelea Mchunguliaji anadakia “Ami umeniacha hoi na hilo neno kutanatana lamaanishani?”
Mpemba anajibu “kutana huku bara mwaita kuchana sie twasema kutana. Hata njia huita ndia wakati nyie huku mwasema njia.”
Mgoshi anaamua kula mic “kama hawa waiosamehewa ubakaji wangekuwa Ushoto bia shaka tingewatwanga zongo angaau waewe tisivyocheza na utu wetu. Kwa kwei inaniuma sana kuona watoto wetu wanahaiibiwa haafu wae waiofanya hivyo wanaachiwa kiahisi. Huu ni udhaiishaji wa akina dada na mama. This is unfair kusema ue ukwei.”
“nyie mnaongelea miziki michafu. Nani anaongelea lugha chafu kwenye madaladala? Nani anaongelea lugha chafu kwenye magazeti ya uchafu? Nani anaongelea lugha chafu maofisini ambako dada zetu wanadhalilishwa kila uchao? Nani anaongelea uchagudoa kila kona hadi kwenye makaburi na mitaani kwetu? Sofia Lion aka Kanungaembe analalamika huku akikatua kasha yake.

Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita binti mmoja alonjaza huku miguu kama chelewa akiwa amevalia kijisuruali kilichochanwa chanwa na kubana manonihino yake utadhani yatapasuka. Acha tumtoe mkuku tukimzomea kabla ya kukimbilia kwenye kijiduka jirani hadi ndata walipotutawanya tusimfanyie kitu mbaya!
Chanzo: Tanzania Daima, Machi 7, 2018.

No comments: