The Chant of Savant

Tuesday 2 March 2021

Wakati Mwingine Waziri Mollel Anaaibisha Serikali kwa Majibu Yake.


 Hii ni mara ya pili naandika makala kwenye gazeti hili juu ya mtu yule yule tokana na na sababu na mazoea yale yale tokana na kile ambacho waingereza kitu fulani kufanyika for all the wrong reasons. Dk Godwin Mollel, Naibu wa waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amekuwa maarufu for all the wrong reasons (sina Kiswahili chake kuepuka kuharibu maana iliyokusudiwa). Mollel amejizolea umaarufu kwa sababu zisizo kutokana na kushindwa kutoa majibu ya maswali anayoulizwa na kujibu maswali ambayo hakuuliza.  Najua. Kwa nafasi yake, ana haki ya kuisemea wizara yake. Lakini hana haki ya kupotosha na kudanganya. Halipwi mshahara wa umma kwa hili hata kidogo. Kitendo cha waziri kushindwa kutoa majibu yanayoingia akilini, kwa msomi wa daraja lake, inatia shaka kuhusiana elimu yake. Mfano, hivi karibuni kulitolewa clips mbili zilizosambaa kwenye mitandao ambapo Mollel aliulizwa juu ya ongezeko la vifo kama vilivyoripotiwa na baadhi ya viongozi wa dini ambao walishiriki mazishi mengi ya wananchi kuliko kawaida. Mollel alijibu “Kikubwa kwanza mimi mimi nawapenda…..inanifanya nikipata likizo… tukauombee ufukizo wa nguvu za roho kwa baadhi ya watumishi wa mungu. Kwa sababu sisi hatuna la kuwasaidia… wanapotaka kutwambia waangalie mazingira kwa kutumia akili zao.” Kimsingi, badala ya kujibu swali, Mollel aliendelea kuelezea namna ambavyo ‘nabii’ mmoja mwenye kutia shaka toka taifa fulani linalosifika kwa utapeli alivyosema kuwa mambo yanayofanyika Tanzania si ya kibinadamu bali ya ki-Mungu. Inakuwaje wanadamu watende mambo ya ki-Mungu wakati wakati wa kufanya miujiza uliisha miaka elfu nyingi zilizopita?

Majibu mabovu ya waziri yanafanya ionekane kuwa kuna kitu taifa linaficha kuhusiana na Covid-19 wakati rais John Pombe Magufuli alishatamka wazi kuwa hana ubishi na uwepo na janga hili. Ambacho wengi wanashindwa kuelewa ni ukweli kuwa rais alisema hataweka taifa kwenye lockdown. Hili ni gumu kwa nchi zisizo na uwezo wa kuwazuia watu ndani na kuwahudumia jambo ambalo kwa nchi maskini linaingia akilini. Kwanini wanamzushia rais na kumwekea maneno mdomoni? Kama Covid-19 haipo na haiuwi, kwanini rais alipendekeza wananchi kuchukua tahadhali na kufunga na kuomba? Wanajitahadhari, kufunga au kuombea nini wakati ugonjwa tajwa haupo? Kama tutakuwa wakweli, rais hakanushi kuwapo kwa Covid-19. Anachokataa ni a) kupangiwa na mataifa ya kigeni juu ya nini afanye, b) anashauri tuwe makini katika kuingiza barakoa na kinga toka nje wakati tunao uwezo wa kupambana kwa njia zetu ukiachia mbali kuweza kuuziwa feki kama ilivyobainika hivi karibuni nchini Marekani ambako mamilioni ya barakoa feki toka China yaligundulika, c) Rais amesikika mara nyingi akiwasihi wananchi kuacha woga na kutulia. Maana, woga unaua pia. Kwani, magonjwa haya ya kupumua yamekuwapo na yatakuwapo tu. Mfano, rais alihoji ni kwanini kila anayekufa tunaambiwa ni Covid-19 wakati magonjwa mengine kama malaria na homa za nyumonia vinaua watu wengi kuliko Covid-19? Kimsingi, swali analouliza rais ni je magonjwa mengine yameacha kuua? Si lazima waziri ajibu maswali haya.

Tukio la pili ni pale waziri alipoulizwa ni kwanini wizara yake haitoi takwimu za walioambukizwa, kupona au kufa. Badala ya kutoa jibu alidai kuwa kutoa takwimu alisema “watu wanasema Tanzania haitoi dataData nataka niwafundishe watu. Data kazi yake si waziri wa Afya kutoka kila siku na kwenda kukaa kwenye TV kusema waliokufa, waliougua, waliozikwa ni ujinga mtupu.” Waziri aliendelea kusema kuwa kazi ya data siyo kutolewa bali kuchakatwa. Kwa mtu yeyote aliyewahi kufanya utafiti, anajua fika kuwa jibu hili si sahihi na haliingii akilini. Takwimu siyo mali ya maabara bali umma. Kwa waliowahi kufanya utafiti, wanachotafuta kwanza ni kujua ukubwa wa tatizo; na pili kuchapisha ili kilichoibuliwa au kazi zao zisaidie wengine. Hatufanyi utafiti kwa kujifurahisha au kuufanya mali binafsi. Utafiti ni mali ya umma na ndiyo maana–––kwa wale wanaofanya utafiti kwenye taasisi za umma kama mashirika, makampuni na hata vyuo vya umma, hugharimiwa na umma kwa sababu data au takwimu zinazopatikana hulenga kuunufaisha umma na si vinginevyo. Hata makampuni binafsi kama vile ya mitandao yanayokusanya data, wakati mwingine yanalazimishwa na baadhi ya sheria za baadhi ya nchi kuhakikisha zinatumika kwa manufaa ya umma.

Kwanini waziri asikubali kuwa hana majibu ya maswali badala ya kupingana na vitu ambavyo viko wazi? Mfano, waziri anaposema kutoa takwimu ni upuuzi kwa sababu kazi ya takwimu ni kuchakatwa na kutafuta majawabu? Kazi ya takwimu kitaalamu si moja. Mojawapo ya kazi ya takwimu kweli ni kuchakatwa na kuonyesha aina na ukubwa au udogo wa tatizo. Pia waziri afahamishwe kuwa kazi ya takwimu ni kuelimisha umma juu ya ukubwa au udogo wa tatizo. Kimsingi, takwimu, hutumika kuelimisha umma kuhusiana na tatizo. Mfano, huwezi kusema kuwa kazi ya sensa ni kusaidia serikali kutoa huduma huku ukipuuzia ukweli kuwa kazi nyingine ni kuujulisha ulimwengu ukubwa wa idadi ya watu.

Kama kweli kutoa takwimu ni upumbavu­­–––kama anavyodai waziri–––kwanini idara mbali mbali za umma hutoa takwimu kwa umma kama vile kuhusiana na mfumko wa bei, ongezeko la uhalifu, mifugo na mambo mengine kama haya? Waziri anamdanganya nani ili kupata nini wakati taaluma siyo kificho? Kwanini kupingana na kuiita vitu ambavyo viko wazi vya kijinga? Kwanini waziri na wizara yake wasiajili wataalamu wa mawasiliano badala ya kuendelea kupotosha na kutia aibu? Na kwanini waziri kamili anamruhusu mdogo wake avurunde kiasi cha kutia aibu wizara na taifa?

Nafasi haitoshi. Muihmu, niiombe wizara na waziri husika waache kujiaibisha na kuliaibisha taifa kwa kutoa majibu yasiyofanyiwa utafiti wala kuingia akilini. Kama mtu hajui, si vibaya kusema sijui au nipe muda nitakupa majibu. Usomi siyo kujua yote bali kujua namna ya kupima hoja na kupambana na matatizo. Kusema sijui ni usomi kuliko kusema najua wakati hujui ambao ndiyo huo ujinga hasa. Pia kutojua si dhambi. Mbona mara nyingi rais amekuwa akiulizwa maswali anapokuwa kwenye ziara zake na kukiri kuwa hajui na badala ya kutoa majibu yasiyoingia akilini, huwataka wataalamu wajibu. Kuna haja ya wizara kuajiri msemaji mwenye taaluma yake ili kuondosha hii aibu. Ni ushauri tu.

Chanzo: Raia Mwema Kesho.

No comments: