The Chant of Savant

Monday 4 July 2022

Dini inapogeuka janga jipya Afrika (III)

Kama tulivyoahidi kwenye makala ya pili, leo tunarejea kwenye mada hii juu. Makala ya kwanza na ya pili zililidurusu namna ambavyo waswahili tumehujumiwa na kudhulumiwa kwa kisingizio cha dini. Mbali na hayo, waswahili tumekamuliwa utajiri wetu kwa kisingizio cha dini aidha na dini zenyewe au matapeli wa ndani na nje wanaowaibia watu wetu wajinga na waliokata tamaa au wasiojua kutumia njia mujarabu kutatua matatizo yao.  Hivyo huamua kuamini katika mambo ya ajabu ajabu kama vile miujiza na upuuzi mwingine vya hovyo kama vile ni mataahira. Ni kuku pekee apewaye nafaka akaamini anapendwa asijue ananenepeshwa ili alipie kwa kuliwa.

        Kimsingi, makala mbili za awali ziliangalia janga la dini kwa waafrika kijamii. Katika makala hii kwenda mbele, tutaangalia janga hili kiuchumi. Je waafrika, tunapoteza mabilioni ya fedha tukitoa fungu la kumi kwa wajanja fulani wale wakati Mungu wanayesema wanamwakilisha hana haja ya fedha zenu za madafu? Kama ni watu wa dini kweli, kwanini hawasemi ukweli kuwa wanamtumia Mungu kupiga fedha kwa sababu Mungu ahitaji chochote ikiwemo fedha? Je kusema uongo si dhambi? Je hii ina tofauti gani na kosa la jinai la kujipatia fedha kwa kujifananisha na mwingine?  Mungu si maskini hadi awakamue maskini anaopaswa kuwatajirisha tokana na utajiri wake usiomithalishwa na chochote. Kinachofanyika, licha ya wahusika kujitafutia fedha ya kula na kujikimu, wanawatwisha waumini wao zigo la kuendesha ajenda na miradi ambayo hawakupanga.
        Mbali na fungu la kumi hata sadaka na matozo mengine kwa kisingizo cha dini, tunapoteza fedha nyingi kwenda kuhiji sehemu mbali mbali tulizoaminishwa kuwa ni takatifu kwa wenzetu badala ya kwenye makaburi ya mababu zetu kama vile Olduvai, Engaruka na kwingineko. Je tulishwahi kujiuliza au kujipa fursa ya kuuliza vigezo vilivyotumika kubaini na kutangaza kuwa sehemu fulani ni takatifu na nyingine siyo? Kwa waliosoma astrophysics, astronomy, geology wanajua kuwa uhai katika sayari nyingi umo hapa duniani pekee. Hivyo, dunia imebarikiwa yote na siyo sehemu zake kama tunavyoaminishwa. Na kama tutalinganisha sifa za sehemu tofauti, ni kwenye Ikweta ambapo kuna uzuri kuliko sehemu nyingine duniani kama zile zenye majangwa au baridi na theluji.  Hakuna sifa wala kigezo chochote kinachoingia akili kwa sehemu ziitwazo takatifu kuwa takatifu zaidi ya utumwa wa kimila na uongo wa kawaida. Kama ni utakatifu, basi dunia yote ni takatifu ikilinganishwa na sayari nyingine zisizo na uhai.
        Hatuhoji maana ya hija kuwa ni kwenda kuzuru makaburi. Je sisi hatuna makaburi hadi twende Israel nchi ya dhuluma tupu au Makka kama siyo Roma sehemu yenye makufuru ya kutisha? Nani anajiuliza kuwa Roma inayozunguka Vatican ina sanamu kibao tena za aibu zilizopambwa na masanamu ya utupu?  Nani anahoji hata historia ya ima Jerusalem, Makka au Roma ajue kuwa hii miji ndiyo chimbuko la ushirikina? Nani analinganisha dini zake asilia ambazo zinaabudiwa kwenye mapango na dini za kisasa ambazo nazo asili zake ni kwenye mapango. Je mtume Muhamad hakupata ujumbe akiwa pangoni au Yesu kuzikwa pangoni ukiachia mbali kuwaacha wanafunzi wake na kwenda kule kuomba? Tofauti ni nini na dini zetu zenye kuamini kwenye vinyamkera waishio mapangoni? Je Yesu hakutoa sadaka ya damu kama ambavyo mababu zetu walifanya au Muhamad kufanya hivyo kwa kuchinja wakati wa hija sawa na dini zetu asilia? Kama dini zote hutegemea damu na kafala, kwanini tunashindwa kutofautisha hadi tunaingizwa mkenge kirahisi hivi?
        Je ni wangapi wanajua kuwa Saudia hutengeneza mabilioni mengi ya dola kwa kununua mbuzi na kondoo Afrika na kuwauzia mahujaji tena kwa kuwalangua? Je Saudia au Israel na Italia wanaingiza mabilioni kiasi gani kwa kuuza viza kwa mahujaji wengi wakiwa waswahili? Je ni wangapi wanajua kuwa kinachoitwa utakatifu wa sehemu tajwa si lolote bali janja ya kuvutia watu kufanya utalii na kuingizia nchi husika fedha za kigeni bila hata kupoteza muda kutangaza utalii huu? Je huu si ubaguzi wa kijiografia na kisiasa?
        Huu mbona ni ubaguzi wa wazi. Hao wanaotuaminisha kuwa kwao ni ardhi takatifu, wanatubagua kwa rangi hata vyakula vyetu. Je wabaguzi hawamfanyi Mungu aliyetuumba kwa rangi na mazingira yetu? Wangekuwa wajanja mbona hawabugui ardhi na vyakula vyetu. Utaambiwa dini na mila zetu ni haramu. Inakuwaje kuku, maziwa, mihogo na vyakula vyetu siyo haramu? Inakuwaje mabinti na wake zetu siyo haramu? Inakuwaje haramu sisi kuwaolea wao au kuingia kwenye nchi zao kama wanavyowazuia wakimbizi toka Afrika kwenda hata huko Jerusalem, Makka na Roma wakati wao wamejihalalishia kutuolea na kuingia kwenye bara letu kama shamba la bibi? Mbona ushahidi na viashiria viko wazi? Wakati wa uchaguzi wa papa Roma, kwa mfano, ukitokea moshi mweusi ni habari mbaya ya kutopatikana papa. Ila ukitokea moshi mweupe ni habari njema ya kupatikana papa! Je huyu papa anayepatikana kwa moshi mweupe atashidwa kuwa mbaguzi dhidi ya weusi?  Je nani aliwahi kuhoji ni kwanini hivi karibuni hajachaguliwa papa mweusi au kuwapo swahaba mweusi wa mtume ukiachia mbali Bilali ambaye naye kazi yake ya kuadhini haina thamani ikilinganishwa na mashehe wala maswahaba?
        Tumalizie kwa kuwataka wasomaji wetu wazidi kutafakari janga hili ili wachukue hatua kwa pamoja au binafsi ili kukomesha unyonyaji huu wa wazi ambao hauna mwisho kwa vile dini zipo hadi siku ya mwisho kama zinavyotuaminisha ambayo nayo hatujui ni lini.
Chanzo: Nkwazi Mhango, Manitoba Kanada, Raia Mwema juzi.

No comments: