The Chant of Savant

Tuesday 3 January 2023

Rais Samia Jifunze kwa Raila Odinga

 

Alipotangaza nia ya kugombea Urais nchini Kenya na baadae kugombea, Kiongozi wa upinzani nchini humo, Raila Odinga alipewa kila aina ya sifa kiasi cha kulewa, kujisahau, na kuishia kushindwa kwenye uchaguzi tata wa mwezi Septemba 2022. Wengi hawakuamini kama Odinga angebwagwa na mwanagezi wake wa siasa aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma lukuki za ufisadi, unyakuzi ardhi, na nyingine nyingi mbali na kuzungukwa na watu wasio na udhu kama mgombea mwenza ambaye sasa ni naibu wa Rais.
            Hivi karibuni, kwenye vikao vilivyopita vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) vilivyokumbwa na tuhuma nyingi za rushwa, wasaka ngawira wengi walimmwagia sifa kedekede Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Japo rushwa haimo ndani ya CCM bali nchi nzima, kwa chama tawala, hii ni aibu na ushahidi kuwa kinahitaji kufanya marekebisho makubwa hasa kwa upande wa maadili. Leo safu hii itagusia namna makada wengi wa CCM wanavyohanikiza kuwa Mheshimiwa Rais Samia anatosha kuwa mgombea wake wa 2025. Si vibaya kumpenda Mwenyekiti wao na Rais wa nchi. Hata hivyo, mbona wanaanza siasa za uchaguzi ujao wakati haujafika kisheria? Mbona wanakinzana na msimamo wa Mwenyekiti kuwa sasa ni wakati wa kufanya kazi na si siasa hasa ikizingatiwa kuwa uchaguzi uliisha mwaka juzi?
            Katika kuwasikiliza makada wengi wa CCM, wengi wao wakiwa ni wastaafu, hawajengi hoja zenye mashiko wala kuelezea ni kwanini Samia pekee. Kwanini hawajui kuwa, kumpitisha––––hata kama anapendwa sana, jambo ambalo halina ubishi–––bila kufanya uchaguzi wa ndani ya chama si sahihi na ni kinyume na demokrasia ambayo, kimsingi, inapaswa kuanzia ndani ya chama? Kimsingi, wanaomshauri na kumpotosha Mheshimiwa Samia kugombea Urais kwa kuwazuia wanachama wengine hawamsaidii. Kwa anavyokubalika, sioni kama anahitaji kufanya au kufanyiwa hivyo.
            Si vibaya kusema wazi: wengi wa makada wakongwe wanaomshauri awe dikteta ndani ya chama wanamtakia mema. Kinachowasukuma ni matumbo yao zaidi ya mapenzi ya chama, kwa Samia, na hata taifa. Wanaonyesha kuwa hawakujifunza tokana na utawala wa chama kimoja ambao uliondolewa na wakubwa zetu baada ya kuwa chaka la uimla na ufisadi.
            Tukirejea kwa Odinga, licha ya kuwa mwanasiasa mkongwe, mkomavu, mwenye mbinu na anayependwa, aliungwa mkono na utawala uliopita wa Uhuru Kenyatta bila mafanikio. Kimsingi, Odinga alihadaika na sifa za kinafiki na kigeugeu cha waliokuwa wakimwimbia mapambio maarufu akiwa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi cha Kenya (COTU), Francis Atwoli aliyesikika kabla na wakati wa kampeni akisema kuwa William Ruto asingechaguliwa wala kushinda. Atwoli alikaririwa mara nyingi akimsifia Odinga kuwa hapakuwa na mwanasiasa nchini Kenya ambaye angeweza kumshinda.
            Kuonyesha unafiki wa waimba mapambio, Odinga alipoangushwa kwenye uchaguzi uliogubikwa na shutuma za wizi wa kura, Atwoli sasa anamwimbia Ruto mapambio akimkosoa vibaya Odinga. Hadi tunaandika, wapo vigogo wengi waliokuwa wakimwamisha Odinga kinafiki kuwa angeshinda kirahisi waliokwishamgeuka na kumkimbia. Kundi hili linahusisha aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Daktari Francis Matiang’i, Gavana wa zamani wa Meru Kiraitu Murungi, na wengine wengi wakiwamo waliogombea ubunge kwa tiketi ya Chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM). Hawa ni makahaba wa kisiasa au political prostitutes waliojazana duniani.
            Uzoefu toka Kenya umeonyesha kuwa wapo wanasiasa wengi wachumia tumbo na wasasi wa ngawira wanaojifanya kumpenda kiongozi fulani wakitegemea ashinde. Anaposhindwa, humgeuka na kumkimbia wengine tena wakigeuka maadui zake wakubwa. Hata Tanzania tunao wachumia tumbo kama hawa waliowahi kumzunguka Hayati John Magufuli na kuishia kumgeuka hata wengine kumsimanga. Bahati mbaya, baadhi yao wamerudishwa ima  chamani au serikalini bila kuchelea tabia yao ya kuunga mkono yeyote ilimradi wafanikishe miradi yao ya kusaka ulaji au kulinda biashara zao. 
            Japo Rais Samia hana mpinzani wa kuweza kumshinda sasa tokana na upinzani nchini kuwa goigoi na uliosambaratika, kuna haja ya kuangalia waliomzunguka. Wanaweza wasimkimbie tokana na mfumo mzima wa Tanzania kuwa wa kikale uliowezesha CCM kushinda chaguzi zote. Bado wachumia tumbo hawa wenye sifa ya kujikomba na kujipendekeza, wanaweza kumchafulia jina lake kwa kujiingiza kwenye biashara haramu kama vile ya usafirishaji nyara za taifa, ufisadi, mihadarati, mengine kama hayo, Umma hausemi japo unawajua tena kwa majina.
            Hivi karibuni kumefumka kashfa ya bonde la Ihefu inayohusisha familia 12 za vigogo waliochefusha maji na kuathiri mazingira vibaya sana. Je Rais atawachukulia hatua gani? Je atakubali watajwe na kushughulikiwa sawa na wahujumu uchumi wengine? Kadhia hii inaweza kuonyesha ni kwanini baadhi ya makada wa sasa na wastaafu wanajitahidi kuhanikiza kumpigia debe Samia hata kabla ya uchaguzi. Si kwamba wanaipenda CCM au Tanzania. Hasha. Wanachopenda ni matumbo yao. Na hakuna kingine.
            Tumalizie kwa kumtaka Rais Samia na wanandani wake wa karibu kupiga darubini na kuwabaini vyura wengi wanaopiga makelele ya kumpigia kampeni kabla ya wakati mbali na kumsifia kwa kila jambo bila kumkosoa utadhani yeye ni malaika asiyekosea. Tumeyaona haya wakati wa Hayati Magufuli na kwenye kadhia ya kushindwa kwa Odinga. Ni suala la kujifunza tu tokana na uzoefu wa wengine na pengine.
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: