Kuna wanawake wapumbavu, wenye roho mbaya na wachoyo wanaokamia kuolewa huku wakipania kwenda eti ‘kuwakomesha’ ndugu wa mume! Mara nyingi, wanawake wa namna hii wanaokwenda kuolewa ili kufarakanisha wana familia ya waume zao ni mijitu isiyo na huruma wala maadili. Wanasumbuliwa na ujinga na uchoyo. Yupo mmoja alikamia kwenda kuwakomesha ndugu za mtarajiwa wake akidhani alikuwa anawapa fedha nyingi. Ajabu ya ajabu, huyu mama alimhusisha hata mama mkwe asijue hicho chema kakizaa, kukilea na kukisomesha tena akiwa single mother baada ya kufiwa na mumewe tena kwa kuuza vitumbua na kufanya kazi ndogondogo.
Binti huyu kipofu kiakili, aliamua kupania jambo ambalo ima hakulijua vizuri wala kulifanyia utafiti. Pamoja, na kujiridhisha–––na waharibifu wengi wa namna hii hufanya hivyo–––mhusika hakufanya wala utafiti wala kuweka juhudi kulijua alilokuwa akipania kufanya. Kwanza, hakujua kuwa ukipanda ubaya, unavuna ubaya na isitoshe, maovu hayalipi ukiachia mbali ukweli kuwa tamaa mbele mauti nyuma. Alipofunga ndoa, alianza haraka kutekeleza malengo yake mabovu. Alianza kuwachukia ndugu za mumewe wazi wazi. Alianza kumdharau mama mkwe hata kumsingizia kuwa mchawa, kama wengi wafanyavyo wasijue wanaweza kuzaa watoto wa kiume wakalipwa na wakazawana wao au hata kabla.
Pili, hakujua ukubwa wa tatizo alilotaka kulitengeneza hata aina ya adui aliyetaka kumtengeneza na kumteketeza. Hakujua kuwa kumbe mumewe alikuwa mdogo wa kwa kaka yake mwingine aliyekuwa akiishi kwenye nchi mojawapo ya Ulaya. Na katika mambo yaliyomvutia kuolewa na huyu jamaa ambaye hakumpenda vilivyo, ilikuwa ni kuambiwa mpango wake wa kuhamia Ulaya. Hata hivyo, mpango huu ulitegemea kaka mtu yaani shemeji yake ambaye alikuwa kipenzi cha familia na aliyekuwa na ushawishi mkubwa kufikia kuwa kama baba wa familia ambaye asingefanya uamuzi wowote bila kuhakikisha anapata na kuutumia ushauri wa mama yao. Hivyo, kuanza kupambana na mama mkwe, huyu mama alianza, bila kujua, kuvuruga ima mpango mzima wa kwenda Ulaya au kuendelea kuolewa. Kufupisha kisa, mama alikosa vyote kwani aliachika hata bila kwenda huko Ulaya alikokamia au kuwakomesha ndugu wa mumewe. Mume au mke haoti kwenye mti. Anatokana na ana watu waliomtegeneza na waliomzunguka.
Hili liwe somo kwa wenye mawazo kama hayo. Kama wapo waliofanikiwa kuchonganisha na kukomesha familia walimoolewa, ni wachache. Nao pia, hawajui kama Mungu akiwapo uhai, wakazawana wao watawalipa vipi. Wahenga walituhusia kuwa malipo ni hapahapa duniani.
Kuna kisa kingine. Kupo mmoja aliyewahi kujuta kwanini hakuolewa na mume ambaye wazazi wake walikuwa wameisha kufa. Hii ilitokana naye kutoelewana na mama mkwe wake. Huyu mkazana mwana, alikuwa mjinga na mshirikina hakuna mfano. Kuna siku alikwenda kuomba ushauri kwa mjomba wake ambaye alimkemea na kumuonya juu ya hisia na tabia hizo. Alimwambia ‘omba Mungu mama mkwe wako asifariki. Anaweza kufariki mambo yako yote yakaharibika.” Na kweli, tokana na kumtia presha za hapa na pale, mama mkwe hatimaye alikufa ghafla kiasi cha kuzua wasiwasi kuwa alikuwa ima amelishwa sumu au kuzidiwa na mawazo tokana na mkazamwana alivyokuwa akimtenza.
Baada ya mazishi tu, mume wa yule mama alianza ufuska hadi kuzaa watoto kadhaa nje ya ndoa. Raha aliyokuwa akitegemea kuipata baada ya kufariki kwa mama mkwe ilitoweka na akaja kujutia kuwa kumbe kuwepo kwa mama mkwe kulikuwa na neema zake.
Je ni wangapi wamefanya au wanajua au kuwajua waliofanya visa kama hivi viwili kati ya vingi katika ndoa kuhusiana na ndugu japo nao siyo malaika? Je vinawasaidia nini wao na wenzi wao na wale wanaotaka kuwaumiza tokana na ujinga na upumbavu wao? Ni wangapi wanaolewa na kupendelea ndugu zao huku wakiwatenga na kuwachukia ndugu za waume zao? Licha ya kuwa unyama na upumbavu, tabia kama hizi zinaonyesha roho mbaya, ujinga, uroho, uchoyo, ukale, ushamba, na mengine kama haya. Kwa wale wanaoolewa kwenda kula au kuchuma mali, walewe. Mara nyingi, huwa wanaishia kujuta. Kama wewe unawachukia ndugu wa mumeo hivyo, kama una kaka, unajisikiaje mkewe anapoanza kuwachukia nyinyi na wazazi wenu? Mkuki kwa nguruwe.
Chanzo: Mwananchi Jpili.
No comments:
Post a Comment