How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 5 December 2024

Somo Uchaguzi Mkuu Botswana


Hivi karibuni Botswana inayosifika kwa ufanisi kiuchumi na ubora na ugwiji katika demokrasia na utawala bora, kwa mara ya Kwanza tangu lipate uhuru miaka 58 limelibwaga chama kilicholeta uhuru na kuchagua upingaji baada ya kukichoka kilicholewa maulaji hadi kikajisahau kisijue kinaweza kusahaulika kama wenzake kule Kenya, Malawi, na Zambia.

Pili, nikiri. Nilitamani nasi tujifunze kitu hapa. Akihojiwa na radio moja ya kwa mzee Madiba, Kiboko mwana wa Duma mnene mpya wa Botswana aliniacha hoi hadi nikamtwangia simu ingawa hakupokea. Alikuwa bize japo baadaye tulichonga mambo makubwa ambayo ni siri kuba. Huyu dogo nilimfundisha sharia pale chuo cha university of Harvard zama zile nikifundisha kwa Joji Kichaka kabla ya kuingia Tarampu na taarabu zake za shari nikaamua kutimua nisifanyie kitu mbaya nikafungwa bure. Tuyaache.

Pili, chama twawala kililiwa na wapiga kura kiasi cha kudondoka kifo cha mende au kunguni kama si chawa kisiamini. Uzuri wa siasa za kiTswana, katika uchaguzi, hakuna kuchakachua, kutishana, kukamata wapingaji wala kuwateka au kuwapoteza. Hakuna uhuni wa aina yoyote. Ukibwagwa, kama kwa Joji Kichaka, unamtwangia mpinzani wako na kumpongeza bila mikiki wala kasheshe kama kule kwingine ambako vyata tawala, ima vinabakia ulajini kwa kuchakachua, kunyamazisha au kuwanunua baadhi ya wapingaji, kuongopea wapika kura ya kula, kutangaza matokeo ya urongo na upuuzi mwingine. Mfano mzuri ni kule kwa akina Njomba. Felihumo kimeminywa kiasi cha kujikuta kikikumbana na maandamano ambayo hadi leo hatujui yataicha hiyo kaya kwenye hali gani. Hivyo, Botswana imepata rais wa kwanza aliyezaliwa baada ya uhuru.

Sasa tuangalia tunajifunza ni kutoka Botswana.

Mosi, upingaji unaweza kuongoza kaya. Rais wa Botswana anasema waziwazi kuwa yeye ni fyatu anayetenda makosa anayetaka kaya iwe na upingaji wa kutosha ili kumkosoa akifanya makosa akiwa mtumishi wa mafyatu na si mtumikishaji wa. Mafyatu.

Pili, alitaka kuunda baraza la mawaziri kumi wataalamu wakamkatalia akaamua kuunda la mawaziri 18.

Tatu, Boko ni fyatu anayesema wazi kuwa sirkal yake lazima iongope mafyatu na siyo mafyatu kuiogopa kwani, sirkal yoyote inayoogopwa au kuogopesha mafyatu yake lazima iwaibie na kuwaonea. Pia, aliongeza kuwa kama sirkal ikiwaogopa wanene wake hawawezi kuwaibia njuluku kama kwenye kaya ambapo mafyatu wanaogopa sirkal.

Nne, rais Boko anasema waziwazi kuwa sirkal yake lazima ishirikishe mafyatu na siyo kuwatenga huku ikiwakamua na kukusanya njuluku na kuanza kuzitapanya itakavyo kwa wanene wachache kuteuana na kula kila kitu huku mafyatu wakiendelea kusota.

Tano, huyu dogo rais Kiboko mwana wa Duma anasema wazi kuwa anataka kurejesha madaraka kwa mafyatu kwenye kile anachosema ni kuondoa uungu au to demystify power kwa kinyakyusa. Anasema yeye ni fyatu na si muungu wala hana akili wala nguvu yoyote kuliko yoyote bali ni mtumishi wa mafyatu. Nilipomuuliza kama anaweza kuwa mbeba maono, alicheka sana na kusema niache utani. Yeye alisema maono ya kaya yako kwenye katiba na mipango ya kaya na siyo kwenye kichwa wala moyo wa rahis.

Sita, alionya kuwa kuna uwezekano wa kupunguza marupurupu na mishahara ya wanene na matumizi mabovu ya kichoyo, roho mbaya, na uroho. Kama hayati Magu, anataka kupiga marufuku utanuaji na uzururaji wa wanene kupenda kwenda majuu bila sababu. Anasema wazi kuwa kama Watswana watahisi kuna sehemu amekosea, wasichelewe wala kuomba ruhusa kuingia mitaani. Anasema kuwa kiongozi bora na anayejiamini, haogopi maadamano wala kukosolewa. Ahitaji kusifiwa wala kuabudiwa zaidi ya kuambiwa ukweli tena mchungu ili, kama fyatu yeyote, ajirekebishe kabla ya kuadhibiwa na mafyatu waliompa ulaji. Ameonya kuwa atakayemsifia atampuuza na kumuona kama adui anayetaka kumtia majaribuni ili baadaye wapika kura ya kula wambwage kama chata tawala.

Saba, dogo Boko ameahidi kupambana na ufisi na ufisadi kulhali. Kwani, anasema lazima sheria impambane na mafisadi na wala rushwa, wezi, mijambazi na wengine kwenye sirkal iwe yake au ile aliyoibanjua bila huruma au kumtafuta mchawi bali kutenda haki.

Nane, aliniacha hoi aliposema kuwa atajenga uhusiano wenye siha na wapinzani wake ili kujiona kuwa kuondoka maulajini si tishio kwa yeyote. Aliongeza kuwa naye alikuwa mpingaji ambaye sasa ni munene wa kayana ndiyo maana aliwaalika wapingaji wengi toka barani ili kuonyesha kuwa nao wanaweza kuingia kwenye maulaji. Pia, alitaka kuonyesha kuwa upingaji siyo kinyume cha sheria bali takwa la kikatiba ambalo hakuna anayepaswa kulivunja au kulifanya kuwa hisani.

Tisa, kwenye kuapishwa kwake alikaribisha na wapingaji ili kutoa somo kuwa hakuna haja ya kuumizana kwa vile hata wapingaji wanaweza kutwaa ulaji hasa. Ikizingatiwa kuwa uongozi wa mafyatu si ufalme wala mali ya família kama kwa akina M7 pale na kwingineko.

Kumi na mwisho alipendekeza wanene wa Afrika wawe wanakosoana badala ya kuongoja kukaripiwa na watasha kama vichanga. Kumbe niko Botswana!

Chanzo: Mwananchi jana.


Changieni Maisha na Si Harusi


Japo ndoa ni ya wawili, inagusa jamii pana na ni muhimu lakini maisha ya ndoa ni muhimu zaidi. Utaliona hili pale inapofana au kutofana. Leo tutaongelea utamaduni mbaya uliojaa ubinafsi. Tutaanza na kisa kinachotuhusu kwa karibu kwa sababu kinamgusa mwenzetu. Mwaka 2000, tulialikwa kuchangia harusi ya mwenzetu huyu. Wakati ule, kijana huyu alikuwa bado anaishi nyumbani kwao. Alibahatika kupata kibarua chenye kipato na kupanga chumba siyo nyumba alipokaribia kuoa. Hata hivyo, kibarua hiki kilichotoweka baada ya kufunga ndoa. Hivyo, alirejea kwenye umaskini.
            Kutokana na ukaribu wetu, tulichaguliwa kwenye kamati ya maandalizi ya harusi. Tulihudhuria kikao cha kwanza kuweka mikakati ya namna harusi itakavyokuwa. Kila mmoja alitaka harusi ‘ifane.’ Sisi, tokana na upendo na uzoefu wetu, tulitaka fursa hii itumike kuonyesha tunavyoweza kujenga ndoa ya wahusika kwa kuwarahisishia maisha. Kitu ambacho hatukujua, wakati sisi tukifikiria namna ya kumsaidia kijana huyu aliyekuwa ndiyo ameanza maisha, wenzetu walifikiria juu ya namna ya kuwa na harusi kubwa na gharama bila kujali kuwa yule kijana alikuwa bado maskini wa viwango vya kawaida! Hili lilituudhi na kutustua.
            Baada ya kikao kumalizika, tulijikuta na azimio la kufanya harusi ya kukata na shoka. Hata hivyo, harusi ya namna hii haiji kirahisi. Huja na gharama. Katika mipango ya kamati, wengi walitaka harusi iwe ya milioni kadhaa. Pesa kubwa kuliko hata ya kununua ubavu wa mbwa au kiwanja maeneo ya karibu na jiji la Dar es Salaam tulipokuwa. Wakati wenzetu wakiangalia na kukamia kuangusha harusi ya kukata na shoka, sisi tulishauriana na kukubaliana tuwashauri kuwa, katika zawadi ambayo kamati ingempatia kijana huyu, iwe kiwanja ili ahagaike na kuweka japo vyumba viwili. Hili lilikuwa tofauti kabisa na wenzetu.
            Hivyo, wakati kamati ikikaribia kumaliza kikao, Nkwazi alitoa wazo kwenye kipengele cha zawadi kuwa tununue kiwanja na kuwapa maharusi kama mtaji na zawadi katika maisha yao mapya. We! Miguno na manung’uniko yaliyosikika, yalitushangaza. Mbali na Nesaa, hakuna aliyeunga mkono pendekezo na wazo hili. Nkwazi alijaribu kulitetea bila mafanikio. Kamati ilishikilia msimamo wake ‘kunogesha’ harusi. Katika vuta na nikuvute nguo kuchanika, alisimama baba mdogo wa bwana harusi na kumwangalia Nkwazi usoni na kusema ‘usituletee Ujamaa wako hapa. Hata Ujamaa una Kujitegemea ndani yake.” Baada ya kutoa kombora hili tena toka kwa baba mdogo, wawili tulitazamana na kuamua kutosema chochote hadi kikao kilipokwisha. Kimsingi, wazo la kuwazawadia maharusi kiwanja liliuawa hapo kwenye kikao cha kwanza siku ya kwanza.
            Kwa kujua uhovyo wa watu maskini kuchangia pesa nyingi kwenye mambo yasiyo muhimu sana na kuacha yaliyo muhimu, tuliahidi kutoa mchango kidogo huku nyingi tukiziweka ili tuwape maharusi baada ya harusi hii ya kukata na shoka.
            Kufupisha kisa kirefu, michango ilikusanywa na milioni kadhaa zikapatikana. Ulipangwa ukumbi wa bei mbaya ambao hata sisi hatukuwazia. Bajeti na makulaji na manywaji ndo usiseme. Kimsingi, pesa yote iliishia kwenye kula na kunywa na kujifurahisha huku harusi ikiisha na kuwaacha maharusi kwenye chumba cha kupanga. Je hapa tunajifunza nini? Mosi, si wote wanaochangia harusi wanawachangia maharusi. Kwa uzoefu wetu, wengi wanajichangia ili kujiburudisha na kujifurahisha kupitia mgongo wa harusi. Pili, kuna kasumba na tabia mbaya. Tunapenda kuchangia vitu visivyo lazima na muhimu na kuacha vilivyo vya lazima na muhimu. Ukitaka kujua hili, angalia mtu anapougua au kuuguliwa. Watu hawaendi hata kumjulia hali achilia mbali kumsaidia kifedha. Lakini anapokufa, wanafurika kumuaga tena wakiwa wamemvisha nguo za thamani mbali na jeneza la bei mbaya. Huu tuuite nini? Maana ukisema ni ubinafsi, umepitiliza.
            Watu wako tayari kutoa fedha kwa matapeli wa kiroho lakini hawako tayari kumchangia yatima anayeshindwa kuendelea na shule. Wako tayari kuchangia shughuli kama ubarikio na mambo mengine yasiyo muhimu lakini si matibabu. Wanaweza kuchangia nyumba za ibada tena nyingi feki kuliko kuchangia ujenzi wa shule au zahanati. Jamani, changieni maisha kwanza na si harusi. Maisha ni ya kudumu na harusi ni ya muda tu.
Chanzo: Mwananchi Jpili. iliyopita.