How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Thursday, 5 December 2024

Changieni Maisha na Si Harusi


Japo ndoa ni ya wawili, inagusa jamii pana na ni muhimu lakini maisha ya ndoa ni muhimu zaidi. Utaliona hili pale inapofana au kutofana. Leo tutaongelea utamaduni mbaya uliojaa ubinafsi. Tutaanza na kisa kinachotuhusu kwa karibu kwa sababu kinamgusa mwenzetu. Mwaka 2000, tulialikwa kuchangia harusi ya mwenzetu huyu. Wakati ule, kijana huyu alikuwa bado anaishi nyumbani kwao. Alibahatika kupata kibarua chenye kipato na kupanga chumba siyo nyumba alipokaribia kuoa. Hata hivyo, kibarua hiki kilichotoweka baada ya kufunga ndoa. Hivyo, alirejea kwenye umaskini.
            Kutokana na ukaribu wetu, tulichaguliwa kwenye kamati ya maandalizi ya harusi. Tulihudhuria kikao cha kwanza kuweka mikakati ya namna harusi itakavyokuwa. Kila mmoja alitaka harusi ‘ifane.’ Sisi, tokana na upendo na uzoefu wetu, tulitaka fursa hii itumike kuonyesha tunavyoweza kujenga ndoa ya wahusika kwa kuwarahisishia maisha. Kitu ambacho hatukujua, wakati sisi tukifikiria namna ya kumsaidia kijana huyu aliyekuwa ndiyo ameanza maisha, wenzetu walifikiria juu ya namna ya kuwa na harusi kubwa na gharama bila kujali kuwa yule kijana alikuwa bado maskini wa viwango vya kawaida! Hili lilituudhi na kutustua.
            Baada ya kikao kumalizika, tulijikuta na azimio la kufanya harusi ya kukata na shoka. Hata hivyo, harusi ya namna hii haiji kirahisi. Huja na gharama. Katika mipango ya kamati, wengi walitaka harusi iwe ya milioni kadhaa. Pesa kubwa kuliko hata ya kununua ubavu wa mbwa au kiwanja maeneo ya karibu na jiji la Dar es Salaam tulipokuwa. Wakati wenzetu wakiangalia na kukamia kuangusha harusi ya kukata na shoka, sisi tulishauriana na kukubaliana tuwashauri kuwa, katika zawadi ambayo kamati ingempatia kijana huyu, iwe kiwanja ili ahagaike na kuweka japo vyumba viwili. Hili lilikuwa tofauti kabisa na wenzetu.
            Hivyo, wakati kamati ikikaribia kumaliza kikao, Nkwazi alitoa wazo kwenye kipengele cha zawadi kuwa tununue kiwanja na kuwapa maharusi kama mtaji na zawadi katika maisha yao mapya. We! Miguno na manung’uniko yaliyosikika, yalitushangaza. Mbali na Nesaa, hakuna aliyeunga mkono pendekezo na wazo hili. Nkwazi alijaribu kulitetea bila mafanikio. Kamati ilishikilia msimamo wake ‘kunogesha’ harusi. Katika vuta na nikuvute nguo kuchanika, alisimama baba mdogo wa bwana harusi na kumwangalia Nkwazi usoni na kusema ‘usituletee Ujamaa wako hapa. Hata Ujamaa una Kujitegemea ndani yake.” Baada ya kutoa kombora hili tena toka kwa baba mdogo, wawili tulitazamana na kuamua kutosema chochote hadi kikao kilipokwisha. Kimsingi, wazo la kuwazawadia maharusi kiwanja liliuawa hapo kwenye kikao cha kwanza siku ya kwanza.
            Kwa kujua uhovyo wa watu maskini kuchangia pesa nyingi kwenye mambo yasiyo muhimu sana na kuacha yaliyo muhimu, tuliahidi kutoa mchango kidogo huku nyingi tukiziweka ili tuwape maharusi baada ya harusi hii ya kukata na shoka.
            Kufupisha kisa kirefu, michango ilikusanywa na milioni kadhaa zikapatikana. Ulipangwa ukumbi wa bei mbaya ambao hata sisi hatukuwazia. Bajeti na makulaji na manywaji ndo usiseme. Kimsingi, pesa yote iliishia kwenye kula na kunywa na kujifurahisha huku harusi ikiisha na kuwaacha maharusi kwenye chumba cha kupanga. Je hapa tunajifunza nini? Mosi, si wote wanaochangia harusi wanawachangia maharusi. Kwa uzoefu wetu, wengi wanajichangia ili kujiburudisha na kujifurahisha kupitia mgongo wa harusi. Pili, kuna kasumba na tabia mbaya. Tunapenda kuchangia vitu visivyo lazima na muhimu na kuacha vilivyo vya lazima na muhimu. Ukitaka kujua hili, angalia mtu anapougua au kuuguliwa. Watu hawaendi hata kumjulia hali achilia mbali kumsaidia kifedha. Lakini anapokufa, wanafurika kumuaga tena wakiwa wamemvisha nguo za thamani mbali na jeneza la bei mbaya. Huu tuuite nini? Maana ukisema ni ubinafsi, umepitiliza.
            Watu wako tayari kutoa fedha kwa matapeli wa kiroho lakini hawako tayari kumchangia yatima anayeshindwa kuendelea na shule. Wako tayari kuchangia shughuli kama ubarikio na mambo mengine yasiyo muhimu lakini si matibabu. Wanaweza kuchangia nyumba za ibada tena nyingi feki kuliko kuchangia ujenzi wa shule au zahanati. Jamani, changieni maisha kwanza na si harusi. Maisha ni ya kudumu na harusi ni ya muda tu.
Chanzo: Mwananchi Jpili. iliyopita.

No comments: