The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Wednesday, 24 September 2025

Walichagua mbung’o wakidhani mbunge

Mbung’o, chafuo, au ndorobo au tsetse fly kwa kimasai ni mdudu asababishaye ugonjwa hatari wa malale kwa wanadamu na nagana kwa wanyama. Kama inzi wengine, mbung’o si hatari tu bali mchafu na mwenye kueneza maradhi mbali na kuchafua vyakula. Je, wajua mja aweza kuwa mbung’o?
    Kuna kisa kilitokea kwenye kaya ya Fyatuko. Katika kisa hiki, mafyatu waliokataa kufyatuka na kuwafyatua wanaowafyatua, walichagua mbung’o wakidhani mbunge kuwawakilisha kumbe waishie kulala na kufyatuliwa kiasi cha kushindwa kufyatuka wakafyatua. Kila kitu kililala.
    Afya ililazwa kiasi cha akina mama kujifungulia majiani. Hospitali na zahanati zilikosa vitendea kazi kama vile madawa na ambulansi ilhali ndata wa Fyatuko wakijinoma na mindinga mipya na bei mbaya hata ambayo hawakuihitaji. Maendeleo yalilala. Elimu ililala. Kila kitu na mafyatu walilazwa kulhali.   
            Kama vile haitoshi, mbung’o waliyemchagua, hakuishia kuwa mbung’o tu katika maendeleo na afya zao, alisifika kwa kulala mjengoni. Alilala kiasi cha kushindwa hata kuuliza swali au kuchangia au kuibua hoja. Hoja yake kubwa zilikuwa mbili, kuupiga usingizi na kushobokea mshiko aka posho ya makalio bila kuvitolea jasho lolote wala kustahiki.
        Hakuna haja ya kuwacheka mafyatu ukajikuta unajicheka mwenyewe bila kujua. Mafyatu wangewezaje kuacha kushangaza wakati walilala baada ya kuambukizwa ugonjwa wa malale hadi wakaliwa wanajiona? Unapopata ugonjwa wa malale, huwezi kuwaza, kuhoji, kushuku, kukataa, hata kuchukia. Unatenzwa kwa kadri mtesi wako atakavyo, nawe unaona ni sawa. Ukijitahidi, badala ya kulalamika wazi wazi, unaishia kung’unika wakati unajua tatizo na suluhu yake. Ama kweli, mbung’o na malale ni balaa ambalo hata adui yako huwezi kumtakia!
        Pamoja na kisa hiki kuwa cha kufikirika, kuudhi, na kuhuzuisha, kinafikirisha na kufundisha. Je, ni mafyatu wangapi waliochagua mbung’o wakidhani mbunge? Inakuwaje unamchagua fyatu asiyejua hata kile anachokwenda kufanya huko mjengoni wakati anaonyesha wazi kuwa si hajui tu bali hajijui wala kufaa?
        Hebu tudurusu zaidi. Linakujia bambataa na mikelele yake na kukusumbua kwa kukuchafulia mazingira kwa njia ya sauti unalipa kura yako usijue kura ni kula? Juzi, nililisikia moja likisema eti watoi watasoma skuli kuanzia la saba hadi la kumi halafu wakimaliza wasome darasa la kwanza hadi la saba! Jimbung’o hili la kileo lilikuwa limefungulia miziki ya kipedejee lisilojua hata maana ya ujumbe wake huku likimwaga manonihinoo kama chizi lenye kiherehere lililojitoa ufahamu.
        Du! Wakati najiotea na mbung’o naye ananinyemelea aninyonye damu, kunichafua, na kuniambukiza malale!Silali tena nimekustukia mbung’o na wengine kama wewe. Nyambaff kabisa.
        Kilichoongeza vilio kwa mafyatu wa Fyatuko ni ile hali ya mbung’o sorry mbunge mbung’o wao kuwa kihiyo wa kutupwa ambaye hakuna alilojua zaidi ya kueneza ugonjwa wa malale. Siku moja, alihojiwa na kuulizwa nini maana ya mswada. Bila aibu na tokana na ugonjwa wa malale, alijibu kuwa mswaada si chochote wala lolote wala hoja ya kuhagaishwa nayo kuijua. Kwake, si kitu cha maana japo kazi yake aliyochaguliwa kwayo ilipaswa iwe kutunga sharia ambazo huletwa njengoni kama miswada.
        Hivyo, alishauri mwandishi wa umbea aachane nayo kwa vile haikuwa na maana kwake! Je hili halikuhitaji msaada lau lifunzwe maana ya mswada na umuhimu wake kwa kazi yake na mafyatu lililowafyatua wakalipa ulaji?
    Mbung’o huishi kwa kuwachafua waja, kuwasababishia magojwa, na kunyonya damu ya watu na wanyama. Bila uchafu, uwe wa kijamii au kimfumo na damu iwe ya fyatu au hayawani, hakuna mbung’o. Hivyo, licha ya mbung’o kuwanyonya mafyatu na kuwasambazia magonjwa, alisifika kwa kuwaaibisha mbele ya jamii tokana na uzwazwa wake.      
      Ajabu ya maajabu, hata chata kilichompitisha mbung’o kugombea ubunge ilhali alikuwa bingwa wa kula udohoudoho tena mwenye ubuge usio kifani, kiliwashangaza mafyatu ambao walishindwa kujishangaa wenyewe. Pamoja na mafyatu kushangaa, kadhalika dunia ya wenye akili iliwashangaa ikiwaza ilikuwaje wakachagua mbung’o bila kuchelea madhara yake wakati kulikuwa na mafyatu waofaa kufyatuka.
        Hapa, ukiliwa na kuambukizwa migonjwa, unashangaa wakati umeamua uliwe? Kama si hivyo, kwanini usimfyatue mbung’o kabla ya kukusababishia magonjwa, hasara, hata vifo? Ni wangapi wamekumbana na kadhia hii tokana na kushindwa kufyatuka na kufyatua? Je,tunao wangapi wafananao na kufanya kama huyu mbong’o kwenye rubaa za kisiasa za kisasa ambazo zimejaa visa, visasi, na mikasa?
        Ajabu, hata mafyatu walikwenda kulisikiliza badala ya kulizomea hata kulitimua! Badala ya kuja na sera, jimbung’o hili, lilikuja na ngebe na ngega na kuwapotezea muda mafyatu. Ajabu jingine, eti na timu ya uchafuzi ililipa mshiko likaeneze malale. Wakati mbung’o kama huyu na wengine kama yeye wakipewa njuluku za kueneza malale, mafyatu waliokuwa wengi, walikuwa wakilia kwa umaskini wa kujitakia!
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

Sunday, 21 September 2025

EAC, what a hypocritical and hypothetical pipedream!

The just ended CAF African Nations Championship (CHAN, 2024) tournaments unearthed some  cagey and duplicitous incongruities of the East African Community (EAC). For those who bothered to honestly dissect it, it left the EAC with egg on its face and some good lessons, which we can’t push under the rag. Up to now, I don’t know why Kenya, Tanzania, and Uganda jointly hosted the games.
How were they awarded this honour as if they’re the only East Africa countries? What does this say about the EAC, especially the countries, which joined after the three founding countries? Was there any consensus among all East African Countries? Did the conveners consider the first EACs?  If so, why? If not, why only three countries? Again, are the three the only official countries of East Africa if we legally refer to the EAC?
        What are the adverse ramifications hither for the others? Why were the ‘rests’ of EAC not part of this honour, which served many interests economically and politically? Were they consulted? If yes, what did they say, and what were the reasons of their decisions? If not, why? How was the decision to appoint the three countries above reached? There are many more questions than answers.
            Local Organiser Committee chair, Nicholas Musonye was quoted by the Daily Nation (August 19, 2025 ) as saying that due to the rivalry, selfishness, and short-sightedness of the three countries, there was an absence of key emblematic elements, namely the mascot, theme song, and local organising committee. This is not because these countries didn’t know the significance even symbolism of these missing elements. One of the reasons revolves around greed, selfishness, and myopia.
            The three countries have their different national symbols. It wasn’t possible to display all three symbols. Therefore, the EAC symbol, if it ever exists, would have footed the bills. Regarding them song, the same applies. The three, if were true on the same boat, would have composed the song. If they consulted me, I’d have advised them to settle on Sina Makosa of Les Wanyika to signify that they have no rivalries.
Major bottleneck
Who would believe that the citizens and fans of one country would throw a party after one of the team of the host country was forced out of the games? Who? Again, it happened. Much of rivalries was between Kenyans and Tanzanians, which can trace their roots to colonial times when British who colonised Kenya and later got Tanzania as protectorate treated Kenyans more preferentially than Tanzanians.
            As for Uganda, despite being a British colony alongside with Kenya, the British didn’t like it simply because it had organised and powerful empires, which were at par with theirs. Therefore, when the three countries got their independence, colonial masters left coloniality abaft, and it’s gone on haunting and hunting our countries and our people. Due to such coloniality, greed, myopia, and to refuse to learn, the EAC union has never been actualised.
A major bottleneck is the fact that there is a deficit of democracy almost in all EAC countries. If there were true democracy, the people of EAC would easily unify their countries. However, the obstacle has always been their rulers who cling to their statehouses and the emoluments that come with them.
        A lack of democracy has created corrupt dictatorial and parasitic regimes, which also attract opportunists from within and without to plunder their resources. This causes a lot of miseries, which provoke conflicts in some countries that equally attract foreign enemies who, in the end, disturb peace and engage themselves in corruption and illegal supply of weapons.
Coloniality and historicity
When the EAC countries were colonized, they found themselves allying with different colonial masters. Kenyans were allied to Britain as its blue-eyed boy while Tanzania and partly Uganda after independence allied with the East in their quests of becoming socialist countries. This created a chasm that’s prevailed up until.                     Being a Tanzania who once lived in Kenya and oft travelled to Uganda, among others, I know how the citizens of the two countries despise and distrust each other. Jomo Kenyatta used to say that Tanzania was an ‘eat-nothing society’ while Julius Nyerere used to say that Kenya was a ‘man-eat-man society’. Have candour, coloniality, and rancour between the two ceased or changed?
          As for Ugandans, after Tanzania defeated and overthrew Idi Amin and liberating Uganda, and Tanzanians or wakombozi literary liberators became good buddies who get along easily and well. I remember the many Ugandan refugees with who I taught in Tanzania. Thanks to this. I’ve already contributed 28 pieces to the DM compared to only six to the DN. Also, Tanzania cloned Museveni who has performed wonderfully by staying in power for close 40 years apart Muhoozi Keinerugaba who’s born in Dar.
            In sum, what’s been ongoing among the EAC countries isn’t sibling rivalry but coloniality, greed, and myopia.
Source: Daily Monitor Sunday today.

Msiwatelekeze watoto wa nje ya ndoa


 Visa vya matajiri wakubwa watatu duniani na marais wawili wa Marekani vinasisimua, kufikirisha, na vinafundisha kwa wenye akili na busara. Marehemu Steve Jobs muanzilishi wa wa kampuni kubwa la Apple, Jeff Bizos wa Amazon, na Larry Elison wa Oracle wanaweza kutufundisha kitu juu ya nani anapaswa au anaadhibiwa kati ya wazazi na watoto waliozaliwa nje ya ndoa. 
        Hawa wote watatu wana sifa zinazofanana. Mosi, wote ni wanaume. Pili, ni wazungu. Tatu, ni wamarekani. Nne, wote walitelekezwa na baba zao. Na tano, wote ni mabilionea. Sita, wote wamethibitisha kuwa jiwe kuu la pembeni lililokataliwa na waashi. Maana, baba zao waliowatelekeza walikuja kujigonga kwao baada ya kufanikiwa. Ni wangapi uwajuawao kama hawa hata kama siyo mabilionea? Mfano, mwingine ni wa marais wawili wa Marekani Bill Clinton na Barack Obama waliotelekezwa na baba zao wakatokea kuwa watu mashuhuri sana duniani.
     Wakati mkifikiria kuwakubali au kuwatelekeza watoto wa nje ya ndoa, jiulize yafuatayo: mjue. Si makosa yao bali yenu.  Kama ni makosa, basi ni yenu. Sasa wanaadhibiwa kwa lipi? Hivi, huwa wazazi kama hawa wanajisikiaje? Je, huwa wanajiuliza wangekuwa ni wao wangetaka watenzwe vipi? Mkuki kwa nguruwe na udhaniaye ndiye, kumbe siye. Tia maanani.
Wengi, ambao ni wanaume, huwakataa na kuwatelekeza watoto wao kwa kuogopa kuvunja ndoa zao. Unapomtelekeza mtoto, unaharibu maisha yake. Ila matokeo, yanaonyesha kuwa unaharibu hata maisha yako mwenyewe tokana na ubinafsi usio na kichwa wala miguu.                                 Kinachosikitisha, watoto hao hao wanapofanikiwa, wahusika hawa hawa waliowatelekeza huwa hawaogopi kuvunja ndoa zao. Na badala yake, hujifanya hamnazo kiasi cha kutaka misaada au heshima toka kwa watu waliowaumiza maishani.  Huu ni nini kama siyo unyonyaji na unyama?
            Kimsingi, kutokana na uzoefu na visa hivyo hapo juu, unaweza kukataa almas ukidhani ni jiwe, na baadaye ukajikuta ukijutia kufanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa watoto ni malaika na Mungu hamtupi mja wake. Kwa wale waliotelekezwa, ni vizuri kuwasamehe hawa wazazi waliowatelekeza. Ila msiwape huduma yoyote kwa vile nao waliwanyima haki na huduma. Ni wezi wa kawaida wanaopwakia na kushabikia kuvuna wasipopanda na kupanda wasipovuna. Jifunzeni.
            Tuseme wazi. Hatuhimizi watu wazae nje ya ndoa au kuzaa bila mpangilio. Je, ikiishatokea tufanye nini? Hili ndilo swali na somo la leo kwa wanandoa na hata wazazi wote. Kama umemtelekeza mwanao, hata akifanikiwa, endelea kumtelekeza na si kumlaumu au kumsumbua na kumtuhumu kuwa hakujali wakati humkujali. Kimsingi, hapa, unavuna ulichopanda. Ukipanda shubiri, usitegemee kurina asali. Ulimfanyia dhuluma, ukatili, na unyama. Akishafanikiwa, unataka kumnyonya na kumsumbua bure. Kama ambavyo hakukusumbua, usimsumbue. Kama ulivyomsahau, asikukumbuke. Na kama ulivyomkana, si kosa akikukana. Kama ambavyo hukumjali, si vibaya asipokujali. Mechi au ngoma droo.
            Japo mila nyingi za Kiafrika hata dini zinafundisha kusamehe, nani awezaye kumsamehe nyoka aliyemng’ata ili amng’ate mara ya pili na kumuachia sumu iletayo kifo? Nani awezaye kutukuza upanga uliomkata akanusurika kimiujiza? Waingereza wana msemo usemao fool me once, shame on you. Fool me twice, shame on me, yaani, ni upumbavu kung’atwa na nyoka kwenye shimo moja mara mbili.
            Wapo wengi waliolala njaa, kubagazwa na kubaguliwa kwa sababu ya kutelekezwa. Pia, wapo waliokosa fursa kama vile afya, malezi, elimu, na mengine mengi kama hayo. Hata hivyo, tokana na kudura za Mwenyezi Mungu walijitahidi hadi wakafanikiwa. Japo tunaweza kuwachukulia kirahisi hasa pale wanapokataa kuwasamehe waliowatelekeza, tujue. Wana mengi tusiyojua kwa sababu si rahisi kuvaa viatu vyao na kuhisi wanavyohisi hasa hasara walizopata maishani kutokana na kutelekezwa.
            Je hao hapo juu wanatufundisha nini? Hili ni funzo kwa wote waliotekelekezwa. Badala ya kupoteza muda kulaumu waliowatelekeza, wahanga, wachukie na kugeuza hasara hii kuwa faida katika maisha yao. Mfano,  Jobs, aliyekutana na baba yake mzazi kwa bahati mbaya alipoulizwa kuhusiana na baba yake alisema “nilijifunza mambo kidogo juu yake na sikupenda nilichojifunza.” Nani anayetaka mwanae asimjue au kutofurahishwa na kutomjua?
        Tumalize. Hadi anafariki dunia, Jobs, hakuwahi kupoteza muda kukutana na baba yake anayeitwa Abdulfattah Jandali ambaye bado yu hai na anasema alichobaki nacho ni huzuni usio kifani kwa makosa yake.
Chanzo: Mwananchi J'pili leo.

Sunday, 14 September 2025

Wakati gani bora wenza ‘kubwagana?’

Uliwahi kuhusishwa kwenye mgogoro wa ndoa na kuombwa ushauri? Tunadhani ni wengi wamewahi kufanya hivyo iwe kwa kutaka au vinginevyo. Hakuna jambo gumu na hatarishi kama kuombwa ushauri hasa kwenye ndoa ambayo hairekebishiki. Sisi tumewahi kuombwa ushauri. Katika kutoa ushauri, kuna jambo moja wanandoa wengi huliogopa au kuliepuka, yaani kumwambia mwenye kutaka ushauri aachane na mwenzake. Wengi huogopa kushiriki dhambi ya kuachanisha wawili walioungana kwa hiari yao. Pia, huchelea madhara yatakayowapata wahusika, watoto, na familia zao.

            Hata hivyo, ingawa kushauri wawili waachane kuna ukakasi, kuna kipindi kuachana ni bora kuliko kumalizana. Tumewahi kuongelea mauaji ya wanandoa wengi wao wakiwa akina mama, na siku hizi, hata watoto kwa upande wa Afrika. Kwa upande wa Amerika, madhara ni kwa yeyote. Mfano, wapo wanandoa wanaoudhiana ambapo mmoja wao, wengi wakiwa wanaume, huchukua bunduki na kwenda kuua watu wasio na hatia. Mfano, kwa mujibu wa jarida la Bloomberg (2022), nchini Marekani, kati ya mwaka 2014 na 2019, asilimia 60 ya waliotekeleza mauaji ya watu wengi walikuwa ni waathirika wa unyanyasaji wa majumbani, na wengi walikuwa ni wanaume wakati waathirika wakiwa wanawake na watoto. Kuna visa vingi sehemu mbalimbali duniani.

            Kama binadamu angekuwa na uwezo wa kuyajua ya kesho, ungeombwa ushauri na watu kama hao hapo juu wanaoua wenzao tokana na ugomvi wao, ungewashauri nini zaidi ya kuachana?

            Kipi bora? Kuogopa kuwatenganisha na watoto nao kuathirika wakati watatengana milele baada ya kusababisha mauaji ya wenzao na wengine wasiohusika au kuwashauri waachane tena kwa amani ili waendelee kuishi wao na wengine ambao matendo na hasira zao vingewaathiri tena vibaya?

            Kama mmekutana na kukubali kufunga ndoa kwa hiari, ni kwanini wengi hawapendi au kushindwa kuachana kwa hiari? Tunaishi mara moja. Hivyo, kuna haja ya kuyaangalia mambo kama yalivyo vila kuchelea lawama. Hivi, utajisikiaje utakapogundua kuwa wale waliokuja kukuomba ushauri ukawashauri waendelee ‘kuvumilia’tu wamemalizana? Je, hautakuwa umechangia kwenye msiba huu unaoweza kuepukwa kama tutakubali kuupokea uhalisia wa mambo kuwa kuua siyo jibu?

            Je, ni kwanini wengi wanaua wenzao tena wasiohusika wala kuwa na hatia? Jibu ni kwamba mafarakano na ugomvi katika ndoa ni chanzo kizuri cha changamoto ya afya ya akili. Hivyo, mabingwa wa vurugu na udhalilishaji kwenye ndoa wajue kuwa wanajiletea au kuwaletea wenzao tatizo hili ambalo matokeo yake ni mabaya sana.

            Tafiti nyingi zimeonyesha kuwa udhalilishaji wa majumbani huchangia pakubwa katika changamoto ya afya ya akili, urahibu, kujiua, msongo wa mawazo, na mengine mengi. Je, kama tunaoombwa ushauri na kuogopa kushauri wahusika waachane kwa usalama wao na wengine, tungejua ukubwa wa tatizo, tungeendelea kuona kuwa ni dhambi kuwashauri wanandoa waendelee kuvumiliana katika udhalilishaji?

            Wengi wa wadhalilishaji na wahanga, wote wana changamoto ya afya ya akili. Japo tunaweza kuwaona ni watu wa kawaida, ndani, wanatukuta na kuficha mengi. Ni kama volkano iliyolala ikingoja kulipuka. Siku inapolipuka, si rahisi kujua ukubwa wa madhara yake. Hivyo, tunapaswa kuachana na imani za kizamani za kuogopa kuwasaidia wanaotuijia wakitaka msaada wa mawazo. Muhimu, ni kupima kiwango cha uharibifu kilichokwishatokea kwenye ndoa, ndipo iwe rahisi na sahihi kutoa ushauri sahihi.

            Japo wanandoa wanaweza kutaka ushauri kwa marafiki, ndugu hasa wazazi, mara nyingi, ndiyo wanaokimbiliwa. Wapo wazazi kwa sababu mbali mbali, huwashauri watoto wao wavumilie. Hivi, unajisikiaje kuwa binti yenu mliyemshauri aendelee kuvumilia udhalilishaji wa mumewe mliyeagana naye jana kauawa na mumewe? Hivi, kuna dhambi kubwa kama hii? Wapo wanaowashauri mabinti zao kuendelea kuishi kwenye ndoa hatarishi kwa kuogopa kudaiwa mahari. Hivi mahari ina thamani kuliko uhai wa mtu tena asiye na hatia zaidi ya kupenda? Wengine ni kutokana na kuwashauri kabla ya kuoana wakapuuza ushauri wao nk.

            Tumalize kwa kushauri kuwa unapogundua kuwa mahusiano ya ndugu au rafiki aliyekuja kukuomba ushauri ni hatarishi, usiogope ‘kumpa’ ukweli kuwa kuna wakati kuachana ni bora kuliko kuendelea kuishi kwenye ndoa hatarishi ambayo matokeo yake yanaweza kuwa vifo vyake na wengine wasiohusika.

Chanzo: Jpili leo.


Wednesday, 10 September 2025

Fyatu kususia uchafuzi, uchakachuaji, sorry, uchaguzi

 Sambamba na nchi zote zitakazokuwa na uchaguzi mwaka huu, hata Mafyatu, nchi ya ndotoni, itakuwa na uchuguzi karibuni. Kama mjuavyo, Fyatu niliahidi ningeshiriki na kushinda kwa kishindo tena bila kuchakachua au kuchakachuliwa kama uchaguzi ungekuwapo na si uchafuzi na uchakachuaji unaokuja soon. Naona wale wanashangaa. Hamjui fyatu anaweza kufyatuka wakati wowote? Now, why? Nafyatua kimombo msidhani nina PhD ya kununua. Kama akina msukusi na gwajimmy. Juzi, njemba zangu wa vyombo vya ‘uhasama’ walinitonya kuwa mpango wa kunfiyatua aka kunienguakwa kuniibia kura. Hivyo, baada ya kugundua kuwa uchakachuaji, sorry, uchaguzi ujao waweza kuishia kuwa uchafuzi baada ya baadhi ya mafyatu kupanga kunipangua, natangaza rasmi sitagombea. Wale walionichangia njuluku ili kuwakomboa, nawataarifu. Njuluku hizi sasa ni zangu. Nitazitumia vizuri kujiuguza baada ya wajumbe kunifyatua mfukoni.

            Pia, nitamnunulia Bi Mkubwa ndinga kali kama ile ya Abidulii aache kutishia kunifyatua akidai kujitoa kumemnyina u-first lady ambapo angeanzisha kampuni yake ya ulaji wa dezo, yaani NGO na kutajirika na kutesa kama hana akili nzuri hivyo kuninyima uhouse. Nilijitoa ufahamu nikamshauri agombee niwe first lad na kujificha nyuma yake, maana mafyatu hawajazoea first lads isipokuwa first ladies. Kagwaya kupigwa mpina, sorry mpini. Najua mmetastuka na kujiuliza: kwanini nimefyatuka nikaamua kuachana na urahis au tiketi ya kufyatua na kutanua kirahisi.
            Msisituke. Sababu zifuatazo zilinifyatua nikafyatuka nikaacha ndoto za urahisi nikichelea kufyatuliwa.
            Mosi, nani ashiriki ufyatuaji ambao si chochote bali kiini mato, matusi ya nguoni, na ufyatuaji njuluku za mafyatu waliogoma kufyatuka wakafyatua hadi wanafyatuliwa kila upande? Fyatu si mwanasesere wa kuchezewa na kuchezeshwa na majambazi kama Joyce Wowowo. Si msanii nishiriki mazingaombwe ambapo Timu yenye Uhuru wa Uchakachuaji (Illegally Notorious and enabling Committee (INeC), ilishapitisha fyatu wake ‘ashinde au kushindishwa’ hata kabla ya uchafuzi wenyewe. Kama humjui mshindi mpaka sasa, nenda kwa matapeli wa kiroho na wapiga ramli wakuibie. Au mnataka nitabiri? Mshindishwa ajaye atakuwa ni mademoiselle na siyo monsieur kwa Kimasai. Hayo, tuyaache.
            Pili, kama mgombea tena Fyatu, nataka Tume siyo Timu Huru iliyo uhuru kupiga mipini wagombea tishio kama mimi na kudhulumu na kudhalilisha demokrasia. Mie siyo Mpino. Hayo, tunawaachia wale waliokubali tokana na kuogopa au kugoma kufyatuka na kufyatua hadi wanafyatuliwa kila mwaka.
            Tatu, natangaza. Hakutakuwa na uchaguzi bali uchafuzi wa demokrasia. Uchaguzi ni kuchagua kilicho bora toka kwenye vingine ili kupata kinachofaa zaidi. Kwa hujuma nilizogundua, hakutakuwa na uchaguzi bali ushindishaji wa wale ambao ningewashinda tena saa moja asubuhi. Huwezi kuibua kitu kibaya baada ya kukataa kilicho bora kama fyatu, ukasema kuna uchaguzi. Uchaguzi, kwa tafsiri yake sahihi, ni ule unaohusisha wapiga kura, wa wazi, haki (kama alivyosema Masaji Jajiii mkubwa), na wenye ithibati ambapo kura za kupika kula uheshimika na si wale waliowekwa kutangaza dhuluma, uchakachuaji, viini mato, na vurugu.
            Nne, nimepata taarifa kuwa hata majini na maruhani yatapiga kura. Sijui itakuwaje wadudu nao watakapoamua kupiga kura hasa ikizingatiwa kuwa ni viumbe wachafu na wengi. Kwa vile sina mahusiano na viumbe hawa habithi, sitegemei kupata kura zao ukiachia mbali kuwa hawa mashetani si raia wa kaya yetu ya Fyatuland. Nasikia wengi ni raia wa kaya ya kufikirika iitwayo Bongolaland ambayo iliangamizwa na huu mchezo mchafu miaka zaidi ya milioni nyingi zilizopita.
            Tano, naogopa kushiriki dhambi ya ujambazi, uhujumu, na wizi wa njuluku za mafyatu. Kwanini kuunguza mabilioni kwenye kiini mato na kituko ambacho matokeo yake yameishajulikana hata kwa kunguru wa India kabla ya uchaguzi, sorry, uchafuzi wenyewe? Mfano, Timu ya Uchafuzi imetangaza kutoa ndinga kwa kila mgombea! Unawezaje kuwa na uchaguzi bila uwazi na ukweli? Hawa, wanapewa ndinga wakati mteule anapeta kwa njuluku na pipa vyote vya mafyatu akimwaga hongo, sorry, misaada! Haki iko wapi hapa? Unawezaje bila kuwa na tume huru ila timu huru ya kuzuia uhuru wa wengine? Unawazaje kuwa na uchaguzi ambapo refa ni mchezaji, mshika kibendera, na kamisaa? Unawezaje kushiriki uchaguzi ambapo mteule anapewa nyundo awatwange washindani wake tena waliofungwa mikono nyuma?
                Sita, naogopa kushiriki israfu ya mali za mafyatu mfano, kutoa ndinga kwa ‘wagombea’, wengi si wagombea bali wambea, wasindikizaji, na vikaragosi wa chata twawala, waliowekwa na mteule ili kuwazuga mafyatu na kutufanya wagombea tishio tupigwe mipini wahalalishe haramu yao. Jiulize. Inakuwaje ninapatikana ndinga za kuwahonga wanasiasa lakini za wagonjwa hazitoshi? Kwanini zisipigwe mnada na kuwanunulia mafyatu matrekta na kuwapa kwa mkopo ili tuongeze uzalishaji badala ya kuongeza udhalilishaji na ulaji?
             Kwa vile nina mikakati mipya, sitasema mengi bali kujiandaa kuleta mapinduzi ambayo yatawafyatua mafyatu waache kugoma kufyatuka na kuendelea kufyatuliwa na wale viherehere waliojitoa ufahamu. Hivi nimesemaje?
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.

Tuesday, 9 September 2025

Ruksa mwenzi wako kukuchunguza

 

 
Tufuatane katika kisa cha kufikirisha na kusisimua hata kuogopesha japo kinafundisha kitokanacho na upendo wa kweli. Kawaida, wanandoa, hulala pamoja. Hili haliepukiki wala kujadilika katika maisha ya ndoa. Siku moja, baba alikosa usingizi lakini akakaa kimya kuchelea kumuamsha mwenzie. Alistuka. Akiwa hana hili wala hili, mkewe aligutuka usingizini. Alianza kumnusa vidole. Baba aliamua kukaa kimya akajifanya yuko fofofo ili kuona nini kitafanyika. Kwa vile hakujua lengo la mwenzie, alitaka kujua mwisho na sababu zake. Mwanzoni, alidhani mkewe alikuwa mwanga au alikuwa akiota akiwa macho. Mama alimnusa vidoge hata masikio akatabasamu na kulala.
Jambo hili, licha ya kumstua mume, lilimchanganya na kumwachia fikra nyingi asijue aambue au kufanya nini. Je, tukio hili au kitendo hiki, kama ungekuwa wewe, ungechukuliaje? Ungechukia? Ungefurahia? Ungechanganyikiwa au? Je, linakufundisha nini?
 Kimsingi, binadamu anapolala, licha ya kuota, anaweza kuwa macho kwa kiwango fulani kwa vile ubongo wake huwa haulali. Hivyo, kuna mambo mhusika anaweza kuwa akifikiria yakamrejea na akayafanya ima akiwa nusu usingizini au macho alivyofanya mwanandoa huyu.
            Japo, hatuwezi kujua sababu za mama kumnusa vidole na masikio mumewe, tunajifunza mambo yafuatayo:
            Mosi, mwenzi wako anafuatilia karibu kila jambo unalofanya, liwe kubwa au dogo, la maana, hata lisilo la maana. Licha ya kuwa haki yake, ni ishara kuwa anakujali na kukupenda vilivyo. Pia, inaonyesha kuwa yuko tayari kukukosoa, kukurekebisha, hata kukuboresha inapobidi. Hivyo, usimuewe vibaya wala kuhamanika. Kwani, hakuna aliye mkamilifu hasa katika masuala yahusuyo miili yetu.
Pili, anaweza kuwa kanusa kitu. Hivyo, anatafuta kukielewa na kukirekebisha. Muhimu, anafanya hivyo si kwa nia mbaya bali kukujua vizuri hata wakati mwingine kutokujua vizuri, kukushuku, kuhisi, au kujifurahisha.
            Tatu, hata kama hakwambii, kuna uwezekano mkubwa kuwa si kila anachokufanyia anakijua sawa nawe unavyomfanyia. Hivyo, baadhi ya vitendo, ima ni mrejesho au mwitikio wa matukio na matendo yako au hata yake.
            Nne, anakufuatilia wakati mwingine kuliko unavyomfuatilia. Katika hili, akina mama wako mbali kuliko akina baba. Kimsingi, mkeo anakutunza kama vile ajitunzavyo au atunzavyo watoto wenu. Wakati mwingine, anafanya mambo kama haya bila kuhiari au kupanga. Hivyo, ujue. Mkeo si mnoko wala mwanga.
 Ni wanandoa wangapi limewahi kuwatokea hili au jingine lifananalo na hili? Mbali na hili, je, ni wangapi wanaangalia simu za wenzao kujua namna wenzao wanavyozitumia? Uzoefu unaonyesha kuwa akina mama ndiyo mabingwa wa kufuatilia matumizi ya simu za wenza wao japo, pia, wapo akina baba wanaofanya hivyo.Tuliwahi kujadili namna ndoa zinavyoharibu ndoa na namna ya kuzuia balaa hili. Hivyo, wahusika wajue wajibu huu na kuukubali hata kama unaweza kuwa na ukakasi fulani hasa kwa wale wenye “mambo yao.”
Wangapi wanawaruhusu au kutowaruhusu wenzao wasiguse, achia mbali kuziangalia hata kuzipekuwa simu za wenzao? Wangapi wanawaficha wenzao simu zao? Japo unaweza kuona kama uchimvi, mwenzio angependa kujua wote unaowasiliana nao na anaweza kutaka hata nywila za baruapepe na simu zako. Je, ni busara, salama, au hatari kumpa mwenzio nywila za baruapepe na simu yako?
Japo unaweza kuona kama uchimvi, mwenzio ana lengo zuri la kukulinda wewe na ndoa yenu. Hivyo, usijisikie vibaya akitaka kukujua kama ilivyo kwenye kisa tulichoanza nacho. Anakuwa na nia nzuri ya kutaka kuhakikisha usalama wenu wote. Kama tulivyobainisha pale juu, anakulinda kama kichanga japo wewe si kichanga.
Kama hujui, japo si wote, mwenzio anakuchunguza kila sekunde, saa, na siku. Yote ni kwa nia nzuri. Kwa wanandoa wanaopendana na kuaminiana vilivyo, wewe ni mali yake naye ni mali yako. Tusisitize. Hafanyi hivyo kwa nia mbaya au kutokuamini ingawa wengine ni tofauti. Wakati mwingine, hata hajui kama anafanya haya.
Tusikutishe. Tumalizie kwa kusema kuwa unachopaswa kujua  na kuzingatia ni ukweli mchungu kuwa saa zote uko kwenye mawazo yake na ukochini ya uangalizi na uchunguzi muda wote katika maisha yako. Kama huna “mambo yako” usiogope mwenzio kupitia mitandao au simu yako. Kuepuka au kuogopa, hata kama huna, kunajenga shaka kuwa una “mambo yako” ujue.
Chanzo: Mwananchi Jpili juzi.

Wednesday, 3 September 2025

Fyatu kuzoea viti vyote chatani na kayani

 

Kama Mafyatu na wasomaji wangu wote wajuavyo, hiki ni kipindi cha uchakachuaji, sorry, uchafuzi, sorry, uchaguzi. Mbali ya kuwa msimu wa kufyatuana na kufyatuliwa, ni msimu wa kutumia akili vilivyo. Ni msimu wa kusukuti namna ya kufyatuana mkenge. Wakati mwingine inabidi ujitoe ufahamu ili kuwanasa mafyatu ambao unaweza kuwashitaki kwa kujitoa ufahamu kutaka kufahamu mambo yako. Juzi hamkumsikia fyatu fulani wa hovyo akijitoa ufahamu na kuwashutumu mafyatu waliomstukia kujitoa ufahamu waliompa vidonge vyake ili kuzuga mafyatu wasijue hujuma anayoifanyia kaya. Kumbe ndiyo maana mzee Nchonga alimshiti! Kufanikisha dili hili, lazima ukengeuke kama kenge na kuwaacha mafyatu wamchekao kenge kukimbilia mtoni mvua inyeshapo wasijue anajua sayansi kuiko wao. Maskini, mafyatu, pamoja na wengine kuwa na PhD ziwe feki, kweli, au heshima, hawajui kuwa maji ya mto ni ya uvuguvugu kuliko ya mvua nyakati za asubuhi na mvua zikiwa zinanyesha! Ajabu, kenge hajasomea shahada wala kupewa lakini anayajua haya. Pamoja na kufundishana sayansi, mafyatu bado hawalijui hili hadi wanamcheka kenge wakati makenge ni wao wa kuchekwa kwa ujinga na ulimbukeni wao kujicheka bila kujua. Kwa sababu kenge ni mjanja na mjuzi, huwa hapotezi muda kuwacheka wala kufanya uzwazwa wao wa kujitoa ufahamu kama wao.
                    Juzi, baada ya kumaliza kuchangisha michongo, sorry, michango kwa ajili ya uchaguzi, sasa lazima nitafute namna nyingine ya kufyatua viti vyote tena kwa kishindo hata iwe ni kwa goli la mkono. Kwa ufupi, huu ni msimu wa kutia nia, kuonyesha nia za ufyatuaji. Hivyo, mimi niakuja na mkakati kamambe mwingine wa kuhakikisha nashinda viti vyote. Nina sera ya KUBIKU, yaani Kupita Bila Kupingwa.
                    Kwa kutumia kanuni na sera ya KUBIKU, nitahakikisha kuwa nashinda kwa kishindo hata kama nitashindwa ili wanaojaribu kunishinda niwashinde kwa kishindo. Baada ya kujihakikisha ushindi, nahakikisha na Bi Nkubwa wangu, vitegemezi, maswahiba, hata waramba manonihino yangu lazima wanapitishwa bila kupingwa. Atakayejitia kiherehere cha kunipinga au kuhoji lolote kuhusiana nami nilivyowaburuza mafyatu na kujiteua kugombea unene, ajiandae kupigwa chini bila kumuangalia usoni. Ukitaka kumfyatua nyani, waambwa, usimuangalie usoni. Mie huwa namuangalia makalioni na kuwachoma mkuki. Tuendelee.
                    Huu ndiyo mpango mzima ambao umefanyiwa utafiti katika kaya nyingi zilizocheza na kutumia kamchezo haka. Kwanza, nitahakikisha hata bata, kuku, mbwa, na paka wanapita bila kupingwa chini ya sera ya KUBIKU. Hii inaitwa demoncracy ambapo maruhani, mapepo wachafu, hata wadudu hushirika. Hii huwa na maana ikizingatiwa kuwa kuna mafyatu wanaonichukia wanaosema eti namna mafyatu wanaovyonichukia, hata nikigombea na chawa waliojaa kitandani mwangu, nitashindwa. Hashindwi fyatu hapa. Kawaulize wale waliojitia kujiondoa kwenye chata chetu na kuanza kunitupia matope. Wameshindwa. Na punde, wataregea na kutoweka. Mifyatu mingine, nadhani inahitaji kukutana na wale wasiojulikana wanaojulikana kwa uanimo wao. Wangejua ninao mtandao mkali wenye historia ndefu katika kaya hii, wasingejaribu hata kunung’unika achia mbali kupayuka na kuzoza. Kama ni wajanja, si wafyatuke niwafyatue kama ninavyowafyatua mafyatu waliogoma kufyatua na kutufyatua hadi tukawafyatua kila baada ya miaka mitano tutakavyo. Nina hasira na namna wajumbe walivyotufyatua wasijue nasi tutawafyatua tena kwa miaka mitano fresh.
                    Pili, nilifanya uchaguzi wa ndani ya chama cha Mafyatu (ccM). Guess what? Mafyatu wote walioonyesha kutishia ulaji wangu na washikaji zangu walipigwa chini na kuanguka kama mende. Sina simile na yeyote anayejitiatia. Lazima nifyeke wote wanaotishia ulaji wetu hata wawe binadamu, chawa, au mafyatu. Nilihakikisha wanakatwa kinoma ili wasituletee noma kinomi. Wanaotaka kuendelea na ukumbaff huu wa kuhoji nitakavyojipitisha kuwa mgombea wa chata letu bila kufuata katiba na utaratibu, wajiandae kwa kiama kitakachowakumbwa soon.
                    Tatu, lazima niongee na washikaji wangu walioko kwenye NGOs za kusimamia uchakachauaji kuwapiga chini viherehere wanaotaka kushindana nami. Hao, wajiandae. Nao kiama chao kinakuja. Nitahakikisha wanapigwa chini hata kwa kupinda sheria.
                    Nne, nitahakikisha vibaraka wangu na vyata vyao vya mfukoni ambavyo vinaishi kwa kutegemea hisani yangu wanaingia kwenye kinyang’anyiro kama boya la kunipinga wakati lao moja.
                    Kwa vile muda hautoshi, naachia hapa. Nakwenda kuandaa mikakati ya kushinda kwa kishindo hata kama itahitaji kujitoa ufahamu na kuchakachua kura za mafyatu walikataa kufyatuka na kulinda kura zao. Sijui ni kwa sababu hawajui kuwa kura ni mali. Nadhani hawajui kuwa kura ni zana ya kula tena dezo na kutanua bila kufyatuliwa na yeyote kwa vile inakuweka juu ya sharia. Sijui ni kwanini mafyatu hawajui kuwa ukitumia vibaya kura yako unafyatuliwa hata kuliwa! Nadhani tatizo ima ni kujitoa ufahamu au ukenge makengeza wa kutojua thamani ya kura. Jamani, kura ni kula ila kula si kura. Mbona rahisi hivi? KUBIKU hoyeee!! Du! Kumbe bangi imenitoa ufahamu!!!!!!
Chanzo: Mwananchi J'tano leo.