The Chant of Savant

Tuesday 3 March 2009

Tunaanza na filamu ya Kagoda

Tunaanza na filamu ya Kagoda bin Fisadi

Wasomaji wapendwa,

Kwanza , kwa ukarimu wa aina yake niwakaribisheni kwenye gazeti lenu jipya la MAWIO. Pia niwakaribishe kwenye safu hii. Kabla ya kuzama kwenye fikra nzito, ningependa niwahakikishieni kuwa jiandaeni kubwaga nyoyo zenu zitakazokongwa kwa hoja nzito na makini tutakayowaleteeni tukilenga kuibua mijadala mikali.


Katika toleo hili kifungua mimba, safu hii licha ya kuwakaribisha na kuwahakikishia uhondo, ingewataka mjongee tufikiri pamoja ili kutafuta jibu ya matatizo yetu sugu kuu likiwa ni ufisadi uandamanao na wizi wa pesa ya umma. Kwanza tunasema. Tusiwe na subira na ufisadi na uoza. Tusijali nani anautenda au kuushabikia ukiachia mbali kufaidika nao.

Leo tutaanza na filamu maarufu kama Ufisadi. Sinema hii inahusu gendaeka wakubwa walioaminiwa madaraka na umma wakayatumia kuutesa na kuudhulumu umma.


Hapana shaka mmeona sinema nyingi zenye kuchukiza. Kama jamii, tumewahi kushuhudia sinema nyingi. Zilikuja na kupita. Lakini tatizo halijapita wala kupungua zaidi ya kukua.


Tutadurusu sinema maarufu ya Kagoda. Ina kila aina ya uchafu na ngoa. Ilitungwa na Njaa Kaya Kikwekwe na Denjamani Makapi. Ila hawataki iendelee kuonyeshwa. Wanazuia isionekane kwa kutunga nyingine. Kwa sababu inawaumbua na kuwaacha uchi. Inaonyesha uovyo na uovu wa jamii ya mafisi waitwao mafisadi. Ni watu kama wewe na mimi kwa juu. Lakini kwa ndani ni wanyama sawa na mazimwi hata nunda mla watu. Wanang’aa kwa juu kama makaburi ilhali ndani ni uoza mtupu!

Viumbe hawa ukiwaona huwezi kuwatofautisha na waja wa kawaida. Kwa sura hawana tofauti nasi. Kwa tabia na hulka tu mbali mithili ya kifo na uhai. Wao hufikiri kwa matumbo badala ya ubongo. Kama mashimo, humeza kila kilichoko mbele yao bila kujali ni chao au cha wengine.


Ni genge la hatari lililojificha nyuma ya utukufu. Husifika kwa ulafu na usaliti. Wako tayari kuwauza hata mama zao tena kwa malipo ya upuuzi uitwao ten percent. Rejea rada na ndege ya rais.


Pia wako tayari kuwatoa watu roho ilmradi uchafu wao uendelee kuwa siri tena kubwa. Laiti marehemu Daud Ballali angefufuka, si haba, angesema mengi. Angefufuka na kuhiari kusema ukweli, ungeshangaa kuwakuta ambao hukuwategemea. Ungeshangaa na kutikisa kichwa kuwa kumbe ulikuwa ukiwaamini na kuwaheshimu nguruwe ukidhani ni binadamu.

Hatutamung’unya maneno. Kama kuna mtihani unaikabili serikali ya awamu ya nne iliyoingia kwa kauli mbiu ya ari mpya, kasi mpya na nguvu mpya iliyogeuka kuwa utata, si mwingine bali kumfichua mnyama aitwaye Kagoda. Hili ni kampuni lililoiba zaidi ya shilingi 40,000,000,000 toka kwenye fuko la malipo ya madeni ya nje.


Wizi huu uliogeuka kuwa donda ndugu unahusisha wakubwa wengi. Ushahidi wa hili uko wazi. Jiulize. Kwanini kila tunapofikia kuwafichua akina Kagoda hutungwa sinema nyingine kama vile ya matumizi mabaya ya madaraka, wizi katika ujenzi wa minara pacha ya aibu pale Benki kuu?


Kwanini tunapokaribia kumnasa Kagoda hutoka kauli zinazopingana. Juzi juzi ilitoka kauli kuwa faili la Kagoda liliondolewa kwenye ofisi ya msajiri wa makampuni na tume ya rais ya kuchunguza kashfa hii. Haraka haraka ikulu ilikanusha kuhusika na faili hili. Baada ya hapo, hakuna ambaye yuko tayari kusema lilipo faili la Kagoda!


Alipobanwa msajili wa makampuni kuhusiana na Kagoda ni nani, alitaja majina ya vidagaa wawili ambao kimsingi ni bangusilo au mbuzi wa shughuli. Taratibu, Kagoda imegeuka serikali ndani ya serikali ukiachia mbali kuwa ugonjwa wa moyo kwa mamlaka zetu. Pamoja na mbinu hizi na zile za kutaka tusahau ya Kagoda, bado umma una hamu kubwa ya kutaka kujua Kagoda ni nani na kwanini hafikishwi mahakamani na kurejesha pesa yetu ukiachia mbali kutupwa gerezani.


Kagoda imegeuza watu wazima majuha kiasi cha kutapatapa wakidhani umma utalewa kwa sanaa na sinema mbali mbali unaopewa uzimeze ili kusahau ya Kagoda. Je ya Kagoda yatasahaulika na kusameheka? Thubutu. Hakuna kufuru na dhambi itakayolingana na dhambi ya kusamehe na kusahau ujambazi na ufisadi wa Kagoda.


Je lipi lifanyike? Kuepuka utoto na kupoteza muda, wahusika waikamate Kagoda na kuifikisha mahakamani haraka sana iwezekanavyo. Bila kufanya hivi, umma utatoa hukumu mwakani kwenye uchaguzi mkuu. Maana umma utauliza: je tulipowaamini madaraka yetu mliyatumiaje na kutufanyia nini? Hapa ndipo Kagoda na mzimu wake vitafufuka na kuwatafuna waliotutafuna nyuma ya pazia.


Sambamba na sinema ya Kagoda, kuna nyingine maarufu kama Richmond . Tofauti na Kagoda, wahusika walikwishatajwa na kuchukuliwa hatua za kisiasa. Je kwanini inakuwa vigumu kuwachukulia hatua za kisheria tena kwa dola linalojinakidi linaongozwa kwa utawala bora na wa sheria?


Kuongeza viungo na vionjo katika sinema yetu ya mawio ya leo, tunaambiwa wahusika bado wanalipwa marupurupu manono ya kustaafu baada ya kuuibia umma! Allah Akbar! Hebu fikiria. Jitu linaiba na kuthibitika limefanya hivyo, halafu linaendelea kulipwa pesa ya wale wale lililowaibia! Juzi bwana mmoja aitwaye Hassy Kitine alishangaa kuona watu wanawajibishwa kwa kufanya ufisadi lakini bado wanaendelea eti kuwa wabunge! Je hawa zaidi ya kuwakilisha maslahi yao machafu wanaweza kumwakilisha nani katika nini zaidi ya matumbo yao ?

Je jamii iwafumbiao macho wahalifu ni ya kihalifu. Je ni kwanini tunakubali kuwa kundi moja na wahalifu? Je woga na upogo huu utatufikisha wapi zaidi ya kuzimu?

Tukirejea kwa sinema yetu, wapo wahusika wakuu wengine licha ya Kagoda. Ni Deep Green Finance, Meremeta, Mwananchi Gold na magenge mengine ya kijambazi tena yenye majina makubwa chini ya mwamvuli tutakaouita Chukua Chako Mapema (CCM).


Kuna wanaosema: sinema yetu ina uhusiano na sinema nyingi inayolindwa na kufichwa sawa nayo iitwayo Kiwira Coal Mine ambapo wahusika wakuu ni akina ANBEN, Tanpower, Fosnik na Devconsult Ltd zote zikiwa ni kampuni zinazomilkiwa na watu wazito waliowahi kuwa serikalini. Kinachochanganya umma ni kwanini serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha wahusika hawatajwi wala kuchukuliwa hatua za kisheria? Waziri wa Nishati na madini Willliam Ngeleja ameishaahidi vikao vya bunge mara tatu angewataja wamilki wa Kiwira bila kufanya hivyo. Alianza kwenye kikao cha 12 cha bunge,akafuatia cha 13 na juzi juzi cha 14 kimeisha kwa sinema ile ile-nitataja. Lakini asitaje!


Wakati umma ukitafuta majibu ya maswali haya muhimu unaahidiwa kuwa unaweza kuletewa maisha bora kwa kila mtu! Ebo! Tuache utani. Maisha bora yatapatikana wapi iwapo pesa ambayo ingeyawezesha ndiyo hiyo inayoibiwa na wezi wachache wenye mitandao yao ya kiutawala?


Maisha bora yatapatikanaje wakati wahusika hawajawahi kutimiza ahadi hata moja waliyotoa wakati wa uchaguzi? Au maisha bora kwa wote maana yake ni wao wote? Tuambizane tujue.

Busara ya leo: Si kila ving’aavyo ni dhahabu.

Sinema yetu ni ndefu mno. Leo tunaikatishia hapa.
Chanzo: Gazeti jipya la Mawio Feb. 3, 2009.

No comments: