The Chant of Savant

Wednesday 4 March 2009

Ufunuo Kwa Watu Wote



TAZAMA malaika wa Mungu ananiletea ujumbe maalumu kwa watu wote.

Wengi watahoji, mbona mitume walikwishapita, huyu katoka wapi?

Kumbuka, Mungu habadiliki, hata mkitaka kumbadili hatabadilika. Ukitaka kujua hivyo jaribu kuyasema niyasemayo.

Naambiwa nena. Nami nanena. Uongozi usio na miiko na maadili si uongozi bali ujambazi, maana bila kanuni kutakuwa na mvurugano na mparaganyiko. Je, ni nani awezaye kufundisha usafi ilhali yeye ni mchafu? Uchafu wa roho ni zaidi ya ule wa nguo.

Kuongoza siyo kuwa juu ya watu, bali kuwaonyesha njia ukitangulia katika kila jema. Je macho yangekuwa kichogoni tungeona mbele? Unapoongoza ukikaa nyuma ujue umma utarudi nyuma hata kukusaga wewe uliyeko nyuma. Ukiwa mbele, utakufuata kwa hatua maridadi na mwendo salama.

Jaribu hili uone utakavyopumua badala ya kujifungia nyuma ya walinzi wenye bunduki. Je, nani anaweza kuukimbia umma milele? Huyu hakika ni mpumbavu sawa na mtoto akimbiaye kivuli chake asikiache. Je, ni bora kwa mtu mzima kufanya utoto? Mtoto hufanya utoto akitegemea kukua; je, mtu mzima asiyekua si hovyo kuliko hata mtoto anayekuwa?

Viongozi wa kweli waliandika vitabu na kueleza mawazo na mipango yao, yeyote ajiitaye kiongozi asieleze mawazo yake, si kiongozi bali mzigo na mbabaishaji. Maana kukaa hata kukatiza usingizi kuonyesha mawazo ya kiongozi ni ishara kuwa ana mipango katika uongozi wake. Kwa nini upatikane muda wa kuhudhuria hafla hata kufanya ziara lakini ukosekane wa kuonyesha dira?

Kwa kueleza mipango na mawazo yako ya uongozi ni kutoa fursa pana kwa unaowaongoza kukutathmini, kukulaumu hata kukukosoa. Kiongozi asiye na sifa hizi ni imla hata kama havai magwanda. Hata rubani ama nahodha huwa na ramani ya safari yake, maana bila ramani licha ya kupotea atagongesha chombo na kuua abiria wake ambao uhai wao uko mikononi mwake.

Ni daktari gani anafanya kazi bila rejea? Kwa nini kiongozi ale kwanza kabla ya anaowangoza ambao kimsingi yeye ni mtumishi wao na siyo mtumikishaji? Ni mzazi gani anakula kwanza kabla ya watoto hasa vichanga?

Kuna watawala wapendao kujiita viongozi. Viongozi wa baadhi ya mataifa hawalipi kodi; wanawahimiza walipa kodi maskini walipe ili wao waziibe na kuzitumia vibaya, wanaishi kwa kutegemea kodi za maskini! Huu ni uchu na siyo lazima kila chui awe na madoa au kucha. Kuna kucha nyingine huwa ndani zikifichama. Ni wenye busara wanaoweza kuyaona ila wapumbavu huwa hawawezi.

Kaburi hung’ara kwa juu lakini ndani hujaa uoza na harufu mbaya. Kaburini kumejaa uharibifu usio wa kawaida, nani haogopi ukaburi? Je hawa wanaozini kwenye makaburi siyo mashetani hata kama wana sura na viwiliwili vya binadamu? Hawa siyo makasha matupu yasiyo na mioyo? Je, wawaibiao maskini siyo makaburi? Maana kaburi likishameza huwa halitapiki.

Kipi bora kufanya kazi ya kusafisha kikombe ndani na nje? Je, nani mpumbavu anaweza kupamba mzoga?

Dunia ya sasa imeharibika, imelaaniwa si haba, imejaa silaha za maangamizi kila aina. Zipo za sumu na moto, za kielektroniki, za kibaolojia na nyingine nyingi zitagunduliwa katika mashindano haya ya ukichaa wa kuiangamiza dunia.

Kazi ya silaha ni kuua siyo kuponya ingawa tunazitumia kujilinda. Je silaha bora ni zipi? Leo binadamu wanaogopana kuliko hata simba! Lugha ya sasa ni ya vita tupu. Mhalifu anamhukumu mhalifu saa nyingine mwenye nafuu kuliko yeye! Je, hakimu na polisi waombao na kuchukua rushwa siyo wahalifu? Waulize mshahara wao na thamani ya mali zao utajua kinachoongelewa.

Mtu anaamka maskini analala tajiri na watu wanaona, hata kama hawamwambii wanajua kinachoendelea. Je, haya ni maisha ya heshima?

Kujilisha pepo ni tabia ya wapumbavu sawa na wavuta bangi maana mvuta bangi akiishavuta hujihisi yeye ni yeye wakati si chochote wala lolote bali mhalifu wa kawaida apaswaye kuishi korokoroni. Je, ni wahalifu wangapi wanatanua mitaani ilhali wasio na kosa wanaoza magerezani? Fikiri na upige picha uone hali ikoje.

Binadamu wameukumbatia uhalibifu kiasi cha kuigeuza dunia kuwa kaburi na wao wakiwamo! Je, viumbe wa aina hii wanaweza kumcheka hayawani pweza ambaye kwa mapenzi yake na upumbavu wake hujiteketeza?

Machukizo na makufuru ni mabaya zaidi, ni kichekesho kuwa wanadai waliumbwa kwa mfano wa Mungu! Mungu gani anajiteketeza mwenyewe? Watamjuaje Mungu wakati hawajijui? Kwa nini kumsingizia Mungu au ni kwa vile hawezi kuonekana?

Leo dini kwa dini zinachukiana hata kuwagawa watu! Dini bora ni ile itumikiao utu na kuijenga jamii siyo kuinyonya na kuibomoa. Si njia zote huelekea kuliko kwema, nyingine huelekeza machinjioni na bado ni njia. Kwa hiyo siyo kila njia ni njia ya kufuata.

Kuna vilio kila kona, kila kona kuna vilio. Uchafuzi wa mazingira, uwindaji haramu, utoroshaji wa magogo, madini na ufisadi kwa ujumla. Yote hii ni ukaburi, dunia imechafuka kweli kweli. Nani ataisafisha kama siyo wewe na mimi? Watu wanatumikia leo wakiisahau na kuiharibu kesho utadhani wataishi milele!

Wanadamu wameharibikiwa, wanatumia pesa nyingi kwenye misiba wakati marehemu kabla ya kufa alilazwa kwa muda mrefu wasiende kumuona wala kumlipia gharama za matibabu. Wengine walimfilisi kwa kumfanyia matibabu ya uongo huku bila aibu wakimhadaa kuwa wamemsaidia kutibu ndwele yake wasijue wamemsaidia kubeba dhambi zake kwa sababu ya kutu yao ya kuchuma na kuvuna wasipopanda.

Kwao hawa matatizo ni mtaji, lakini wanasahau kuwa na wao wana matatizo na wakati mwingine makubwa, mengi na magumu kuliko ya huyu wanayemuongezea matatizo wakijidai wanayapunguza!

Watu wapumbavu wanachangishana pesa za kusafirisha maiti lakini siyo za kuuguza! Je, waliwahi kufikiria wangelikuwa ni wao? Ukitaka kujua ukubwa wa mguu wa tembo vaa viatu vyake. Utamchongeaje mtu jeneza la mamilioni wakati kuna umma unataka maelfu bado ubaki mzima?

Wewe huna tofauti na mdudu bungua aozeshaye ubao maana unazika vitu ukijua vitaoza. Mbona hamuwaziki na vyakula na vinywaji walivyovipenda hata watu waliowapenda ambao ni nyinyi?

Ni ukuta gani salama kati ya kuwahudumia wenye shida na kujenga nyumba ukaizungushia mikuta kama gereza?

Hapa ndipo alipo mama wa maarifa. Maarifa si kurusha madege na kuvumbua simu za bei mbaya bali kuugundua utu. Nani anafahamika duniani na kuheshimika kuliko Yesu na Mohamad? Hayupo. Je hawa walileta na kugundua nini? waliugundua utu na kuupalilia. Hakuna mvumbuzi atawazidi hawa kwa sababu waligundua kilicho bora kuliko vitu vyote.
Chanzo: Tanzania Daima Feb. 4, 2009.

No comments: