Saturday, 31 August 2013

Mlevi amhoji 'Festi Leidi' na `Festi Chaildi'


Baada ya kuhudhuria kuapishwa Rais Ufreedom Kinyatta, hapo mwezi wa nne, nilipata bahati ya mtende kualikwa tena kwenda kunywa chai na `Festi Leidi’ Maggie Uindependence Kinyatta na baadaye `Festi Chaldi’ Jommie.
Nilipomaliza kupata `chai nzito’ na Bi-mkubwa na `kanywaji’ na Bw-mkubwa mwenyewe, nilikaribishwa `msosi’ wa mchana na familia, uliofuatiwa na mahojiano ya kina baina yangu na Bi-mkubwa.
Huyu asiye na majivuno wala nyodo. Msosi wenyewe ulikuwa mzito kweli kweli. Nilipata mokimo, ngerima, kienyeji na githeri na ka- thubu ka-tuo na vyakula vingine vingi vya Kikikuyu.
Bi-mkubwa anajua kupika usiambiwe! Mbali na kujua kupika, Festi Leidi hana majivuno na `mashauzi’ kama wale wa `shilingi mbili’. Anakula `ung’eng’e’ utadhani alizaliwa London!
Nilianza kumchokoza kwa swali kuhusiana na aina mpya ya ulaji ambayo `ma-festi leidiz’ wengi siku hizi hutumia kuwaibia walevi.
Swali lilikuwa juu ya kuanzisha NGO ya ulaji wa `Festi Leidi’. Hakuzungusha wala kupindisha zaidi ya kusema, hana mpango wa kuanzisha Wanawake wa Kenya (WAKE).
Akasema kuwa wengi ambao hata huwezi kuwadhania walimshauri aanzishe NGO kama wake wengine wa marais, akakataa.
Nilipomuuliza ni kwanini alikataa ulaji ambao kwa sasa umegeuka `fasheni’ kwenye karibu ofisi za marais wote wa Kiafrika, akasema kwa mkato kuwa hana shida ya kufanya biashara kwa mgongo wa rais. Aliongeza kuwa kama angependa kufanya biashara au kuanzisha NGO, basi angeifanya au kuianzisha kabla ya mumewe kuingia madarakani.
Aliuliza kuwa kama si biashara inakuwaje mke wa rais aanzishe NGO baada ya mumewe kuingia madarakani?
Swali hili lilikuwa gumu kwangu hasa ikizingatiwa kuwa `Festi Leidi’ hata kwenye `kanywaji’ ketu hakanyagi.
Pia niliona aibu kuendelea na swali hili ili nisiwaumbue wale ma-`Festi Leidz’ wanaonihusu kwenye kaya ya walevi, ambao wamesemwa hata wanajifanya hawana masikio wao na waume zao.
Kwao urais ni ulaji na mali ya ukoo, mashoga na waramba viatu wao. Huenda katiba mpya itaziba mianya hii ya ufisadi wa kimfumo na kichovu.
Kabla ya kumuuliza swali jingine, ilikuwa ni kama alikuwa akisoma akili zangu. Kwani aliendelea kusema kuwa hana mpango wa kudandia safari za mumewe kila aendapo ughaibuni.
Si mshamba wala limbukeni. Yeye si mwasiasa wala hana mpango wa kuwa mwanasiasa. Hakuchaguliwa yeye bali mumewe.
Alisisitiza kuwa atamshauri na kumliwaza rais kwenye masuala ya kifamilia, lakini si kujiingiza kwenye biashara, uzururaji au kugombea vyeo vidogo vidogo kwenye chama cha mumewe.
Nilipomuuliza mbali na kumshauri mumewe na kutojihusisha na mambo ya kisiasa, atafanya nini.
Alijibu kuwa atatumia muda wake mwingi kujiendeleza kielimu ili kwenda na wakati. Akasema kwa kimombo, “power has an end and there is life after presidency. I therefore am intending to pursue more education that’ll help me after my husband’s presidency.”
Akaniambia kuwa ana Masters na sasa atahakikisha anapata PhD ili kutoa somo kwa `Festi Leidz’ vihiyo wasiotaka kujiendeleza na badala yake wakajiingiza kwenye usasi wa ngawira.
Akalaani sana wale wanaoghushi au kuendekeza shahada za kupewa na wale wanaowalinda.
Alisisitiza kuwa pamoja na kwamba si mshauri wa elimu wa mumewe, hatavumilia kuona baraza lake la mawaziri linajazwa `vihiyo’ na watu walioghushi kama kule kwenye kaya ya shamba la bibi ya wasanii na walioghushi na kuchakachua.
Kitu kingine alichonikuna huyu mama ni kwamba, hataruhusu urais wa mumewe umvurugie mpango wake wa maisha.
Nilipombana aseme anachomaanisha kwa urais wa mumewe kumvurugia maisha, akasema kuwa hatapenda kuandamana na misafara kila aendapo. Akasema atafanya hivyo ili kuokoa fedha za walipa kodi maskini wa taifa lake.
Akasisitiza kuwa yeye hana maadui wa kuhitaji misafara na ulinzi na pia yeye si rais. Aliongeza kuwa wake wa wakubwa kuandamana na misafara mirefu licha ya kuwa ufujaji na matumizi mabaya ya fedha za umma, ni aina fulani ya ulimbukeni hata ufisadi.
Akaniuliza, mbona hakuwa na misafara wala maadui kabla ya mumewe kuukwaa sasa yote haya yanatoka wapi, kama siyo ufisadi wa kimawazo.
Kusema ukweli sikupata jibu zaidi ya kuchekacheka na kufurahi jinsi huyu mama anavyoona mbali hasa baada ya kung’oka madarakani.
Nilipouliza kama atakuwa na mpango wa kupigania maendeleo ya akina mama nchini mwake, Maggie alijibu kuwa hiyo kazi ya kuleta maendeleo kwa akina mama ni kazi ya serikali hasa wizara ya wanawake na maendeleo.
Akadai kuwa kama atajiingiza kwenye kisingizio cha kutafuta maendeleo ya akina mama atakuwa anavuruga kanuni za utawala bora.
Akasema wazi kuwa kama kuna wafadhili au mtu yeyote anayetaka kuchangia maendeleo ya akina mama afanye hivyo kwa kuelekeza mchango wake kwenye wizara. Alisisitiza kuwa hakuna wizara ikulu zaidi ya zile zinazotambulika kikatiba.
Pia alilaani mawazo ya upendeleo kwa akina mama akidai kuwa nao ni wananchi wanaopaswa kupambana na kutenzwa sawa na wengine.
Maggie alitoa majibu kama hayo kuhusiana na suala la afya kwa akina mama na watoto.
Akasema kwa ufupi kuwa kama ni afya kuna wizara ya afya. Hivyo hakuna haja ya mtu yeyote kutafuta fedha kwa kisingizio cha afya au maendeleo ya akina mama.
Baada ya kuhojiana na Maggie nilifanya mahojiano na mwanae wa kwanza Jommie. Swali langu la kwanza ilikuwa ni alikuwa akijisikiaje kuwa mtoto wa Rais.
Alijibu bila kusita kuwa urais si mali yake bali ya baba yake. Hivyo, haoni jipya kwenye hali ya baba yake kuwa Rais.
Nilipomtupia swali kuwa mbona watoto wengi wa marais wengine baada ya baba zao kuukwaa ghafla hugeuka marais bandia. Alijibu kuwa hana mpango wa kujifanya Rais bandia.
Akalaani kitendo cha mtu kudandia urais wa baba yake na kujifanya rais wakati ni kupe tu. Akasisitiza kuwa kama angekuwa na mpango wa kuwa mwanasiasa asingetumia jina wala nafasi ya baba yake bali angejitengeneza mwenyewe ili kuepuka kuonekana kama kupe kwenye mgongo wa Rais.
Huu ufafanuzi wake wa kulinganisha wanaotumia madaraka ya baba zao kama kupe ulinikuna sana.
Hana mpango wa kufanya biashara wala siasa kwa mgongo wa baba yake. Unajua babu yangu alikufa mzee akiwa na miaka 16. Hivyo amejitengeneza.
Nami ningependa na nitahakikisha najitengeneza bila kujiegemeza kwenye mgongo wa baba. Madaraka ya baba ni yake. Nisingependa kuhusishwa nayo. Kwangu baba ni baba wala simchukulii kama Rais.
Nilitaka kumuhoji dada yake Nginie nikakatazwa kwa vile anatisha! 

Chanzo: Nipashe Jumamosi 31, 2013.

No comments: