The Chant of Savant

Wednesday 7 February 2018

Tanzania iondoe sheria nyingi za kikoloni na kifisadi



            Hukumu ya kesi ya watu waliokamatwa wakitaka kutorosha vipande vya dhahabu vyenye thamani ya shilingi 989.7 milioni ilinitisha na kunikumbusha jambo ambalo nilishaliona muda mrefu bila kupata fursa ya kulidurusu.  Kwa mjuibu wa vyombo vya habari ni kwamba watuhumiwa wawili waliokamatwa wazi wazi na mali hizi za taifa, walihukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni sita. Niliposoma hukumu hii nilishangaa. Kwa vile nafahamu sheria, nilijua lilipo tatizo. Kwa wasiojua sheria wanaweza kuanza kumtupia lawama hakimu ambaye kimsingi, hufungwa mikono na sheria. Wengi wanaweza kudhani kuna chochote kitu kimetembezwa wasijue tatizo halipo mahakamani bali bungeni na kwenye mfumo wetu mzima tuliourithi toka kwa wakoloni. Hizi ni sheria au shari?
            Kimsingi, sheria nyingi za nchi zilizokuwa makoloni bado zina makandokando mengi ya kikoloni zikiwamo sheria kiasi cha kuhitaji kuondolewa ukoloni au sumu yake au to be decolonised. Si sheria, tu, hata ukiangalia namna nchi za kiafrika zinavyotawaliwa kwa sasa miaka zaidi ya 50 ya kuwa huru, utakubaliana name kuwa uhuru zinaodai kuwa nao si chochote wala lolote bali ukoloni unaosimamiwa na waswahili wenyewe dhidi ya wenzao.  Hili ni jambo linalopaswa kupigiwa kelele na kutokomezwa ili kuzipa fursa nchi husika kujikomboa na kuendelea. Matokeo mojawapo ya ukoloni mweusi ni kuwa na watawala walioko juu ya sheria huku wakiyatumia vibaya kufilisi nchi husika ukiachia mbali baadhi yao kubadili katiba na kuendelea kuwa madarakani kinyume cha sheria ili kulinda uovu na uoza wao na magenge ya ndugu, marafiki na waramba makalio yaliyowazunguka yakiziibia na kuzifuja nchi husika. Ni bahati mbaya kuwa hata watawala wa mwanzo wa nchi za kiafrika, hawakuondoa ukoloni huu wa kimfumo na kitaasisi zaidi ya kuurithi na kuurudufu kwa manufaa yao binafsi na mabwana zao yaani wakoloni weupe. Kiongozi mwenye dhana na dhima madhubuti ya kukomboa taifa lake hawezi kukubali kuwekwa juu ya katiba. Kwani binadamu ni nini hadi awe juu ya sheria asiitumie vibaya kuwakandamiza watu wake ukiachia mbali kuwaibia? Nadhani ni Mungu pekee anayepaswa kuwa juu ya sheria ila si binadamu.
            Tukirejea kwenye hukumu husika, pamoja na kwamba mahakama imeamuru dhahabu iliyokamatwa kutaifishwa, bado hukumu hii laini itatumika kama motisha tosha kwa wahalifu ambao hawajakamatwa kujaribu kutorosha mali zetu hasa wakijua kuwa wakifanikiwa kufanya hivyo, watatajirika. Na kama wakikamatwa, watatoa faini na kurejea kwenye biashara kama kawaida.
            Kwanza inashangaza kwanini wahujumu hawa hawakushitakiwa kwa sheria ya kuhujumu uchumi? Utaaambiwa kuwa mali na fedha walizokamatwa nazo hazifikii kiwango kilichotajwa katika sheria. Nadhani hujuma ni hujuma bila kujali ni kiasi gani kinahujumiwa. Nadhani, kinachopaswa kuangaliwa hapa si thamani ya mali wala fedha bali nia ya kutenda kosa (men rea).Hapa napo kuna utata wa kisheria kulingana na thamani ya mali husika na mambo mengine ya kisheria. Nadhani kwa wanaojua maana ya kuhujumu, wangeshauri watunga sheria zetu wasiangalia kiasi cha fedha au thamani ya mali husika bali nia ya kitendo.
            Pili, kwa mazingira ya taifa letu na mifumo mibovu, bila kubadili sheria na kuipa meno zaidi, tutaendelea kuibiwa kila mara. Kwanini hatujifunzi kutokana na uzoefu kuwa sheria nyingi zinazotungwa ima zinatungwa na mafisadi walioingia kwenye vyombo vya kutunga sheria kutokana kuhonga, kununua au kuiba kura? Hapa napo kuna tatizo la kimfumo na kitaasisi ambapo chaguzi zetu si huru na za haki hasa kwenye nchi ambazo zimetekwa na vyama vikongwe au watawala maimla na wezi.
            Tatu, Tanzania inapaswa kujifunza toka Uchina ambako makosa ya uhujumu, wizi wa mali za umma na ufisadi hubeba adhabu ya kifo au vifungo virefu. Ni bahati mbaya sana kuwa taifa letu limeendelea kujitangaza kama linalopambana na ufisadi kwa dhati bila ya kuangalia namna ya kuodokana na kadhia ya kutungwa sheria za kifisadi zinazowapa motisha wahalifu kuibia taifa letu na watu wake. Huwezi kuwa na sheria legelege ukapambana na uhujumu uchumi hata kama utakuwa na vyombo madhubuti vya usalama na upelelezi vya kudhibiti kadhia hii.
            Nne, je mbali na kurekebisha sheria nini kifanyike? Nadhani kuna haja ya serikali kuleta mswaada bungeni unaomlazimisha kila mtanzania kuwa anatoa taarifa za mali yake na namna alivyozichuma.  Hili lifanyike kila mwaka ili kuepuka watu kutoa taarifa mara moja wakaendelea kuuhujumu na kuuibia umma watakavyo kama ilivyo sasa ambapo sheria za maadili zimeishia kuwa makabrasha ya sheria yasiyofanyiwa kazi. Nadhani ni Afrika tu na nchi nyingine za kijambazi ambapo mtu anaweza kulala maskini na kuamka tajiri asichukuliwe hatua. Tusipoondokana na ukale na ukoloni huu wa kimfumo tutaendelea kuwa maskini wakati nchi yetu imejaliwa raslimali zenye thamani lukuki. Tutaendelea kuishi kwa kujidhalilisha kwa kutegemea kuombaomba, mikopo na misaada bila sababu zozote za msingi.
            Tumalizie kwa kuzita mamlaka kuchukua hatua dhidi ya mfumo, taasisi na sheria za kikoloni zenye kusaidia wezi kuja nchini kutuibia na kuondoka wakituacha tukiwa maskini iwe ni kwa kupitia magendo, utoroshaji au uwekezaji kwa kisingizio cha biashara.
Chanzo: Tanzania Daima: J'tano, Jan., 7, 2018.

No comments: