The Chant of Savant

Wednesday 7 February 2018

Kijiwe Kuwashughulikia Wanaovunja Maadili

          Baada ya mtukufu Rais John Magufuli kuwatolea uvivu malimbukeni na tabia za kilimbukeni zilizoota mizizi kayani, kijiwe kimekuja na mkakati wa kumpa tafu kuhakikisha maadili yanarudi na kuondoa madili.
          Msomi Mkata Tamaa ndiye kinara wa mjadala wa leo. Akiwa na tabu kubwa liitwalo Ethics of the Nation yaani maadili ya kitaifa, anatia timu, kuamkua na kumwaga sera “wazee, mnaongeleaje huu mkakati wa kurejesha maadili na kuondoa madili kayani kama ulivyoasisiwa na mkuu mwenyewe hivi karibuni kwa kutoa angalizo na onyo?”
          Kapende hangoji; anakwanyua mic na kuzoza “japo huwa natofautiana na mkuu kwenye masuala mengi, kwa hili ameninasa kiasi cha kunifanya nitangaze rasmi leo kuwa mie nitakuwa kamanda wake wa kupambana na ulimbukeni na uchafuzi wa maadili ya kaya yetu tukufu.”
          Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi anakula mi “hata mimi hapa nakubaliana na mgoshi mkuu kuwa hapa kwei ameona mbai. Hapa lazima timsaidie kuwakomesha hawa maimbukeni wavivu wa kufikii kama yue jamaa wa uvivu wa kufikii aiyeponzwa na bi nkubwa wake au siyo?”
          Mijjinga aliyekuwa akifunua kurasa la tabu la Msomi, analiweka pembeni na kula mic “nami hapa lazima ninene ukweli. Jamaa ameona mbali hasa usawa huu ambapo miwaya inafyeka wana kaya kama haina akili nzuri. Hata mimi nashangaa namna ambavyo kaya nzima imegeuka bubu na kipofu dhidi ya wajalaana wanaopenda kuigiza mambo ya hovyo lakini si ya maana. Haiwezekani tukageuzwa kaya ya jalala kimaadili tokana na kuwa na wanene wasio na maadili wala akili waliolea hali hii hatari kwa mustakabali wa kaya.”
          Kabla ya kuendelea Kanji anampoka mic na kuzoza “Jinga kwanza goja nitoe fano. Kama nataka pambana na limbukeni yoteni lazima naanza na ile kuba yao.” Anageuka upande wa kusini mwa kijiwe na kusema “kwanja tajama ile bango natangaza panua kalio. Veve nani napanua tako? Kama Mungu naumba veve nyembamba sasa nani tapanua kalio yako na kwanini na iveje?”
          Tokana na Kanji anavyojifanya kutojua Kiswahili kiasi cha kubukanya Kijiwe hakina mbavu. Mbwa Mwitu anaamua kuchomekea “inaonekana Kanji veve penda sana kalio. Mbona naangalia kalio tu siyo witu nyingine kama wile ile natembea kalio nje kwa kulegeza salawili zao?”
          Mipawa aliyekuwa akimalizia kipisi chake cha sigara kali anakula mic “japo tunaweza kuchukulia utani, hali ni mbaya.” Anamnyooshea mkono kijana mmoja aliyekuwa akipita huku suruali yake ikiwa mlegezo na kichwani akiwa na bonge la kiduku na kusema “kwanini tusianze na wakuda kama hawa wanaoonyesha chupi zao chafu utadhani kuna aliye a haja ya kuzitazama. Hivi siyo ushoga huu wavulana wazima kulegeza surualia na kutoboa masikio jamani? Nani anawahitaji wakati akina mama wamejaa tele ukiachia mbali kuleta laana yao?”
          Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kutia guu “mwenzenu hata mie sielewi. Maana, tulizoea rangi mbili za wanaojichubua wasijue ni upumbavu. Hii kadhia ya dada zangu kuongeza makalio, kucheza vigodoro na upuuzi mwingine mwenzenu naona kama laana. Hapa lazima tusimame kidete na kumsaidia mkuu ili atusaidie. Hakika mkuu amenikumbusha enzi za mzee Nchonga wakati ule nikiwa kinda. Hapakuwa na upuuzi huu hata kidogo.”
          Mpemba aliyekuwa kimya muda wote anaamua kula mic “yakhe mie nkubaliana nanyi. Tumepoteza maadili wallahi. Haiwezekani tuendelee na mambo kama haya hafu bado tuseme tu taifa. Taifa la nnna gani hili lisilo na maadili na utamaduni wake? Sie kule Pemba hatuna haya mambo. Kama ntu afanya hivi, twamitia popobawa antia adabu ati.”
          Msomi anarejea “nakubaliana na watoa maoni. Kaya yetu imegeuka kama nyani. Inakopi na ku-paste bila kufikiri. Wajinga na wapumbavu wengi wanapenda kupwakia kila uchafu utokao nje kwa kisingizio cha usasa. Usasa gani huu iwapo tunaowakopi hawakopi mazuri yetu? Hapa lazima nigusie jambo moja nyeti. Kuna wengi wanaosema kuwa tukipiga marufuku ukosefu wa maadili tutakosa watalii, na tuwakose. Kwani, hatuna umaskini wakati uchumi tunao lakini tunaukalia kwa uzembe na utaahira wetu. Nashauri yeyote anayethamini maadili aanze kutembea na bakora ili tuwachape waharibufu wa maadili yetu kama watu.”
          Mzee Maneno anatia neno “hili naliunga mkono mia kwa mia. Ila tutakapoanza kuwashughulikia hawa wapumbavu, tusiambiwe kuwa tunavunja haki na uhuru wa binadamu wa kujiamulia avaacho.”
          Mchunguliaji aliyekuwa akisoma gazeti anaamua kula mic japo si kawaiada yake “nakubaliana nanyi nyote. Ila napata kigugumizi namna ya kupima nani amevaa kimaadili au vinginevyo. Hivyo, nashauri tuwe na kipimo cha pamoja cha maadili kabla ya kuanza kutembezeana vichapo mchana kweupe au siyo?”
          Kijiwe kikiwa kinachangamka si kikatokea kikundi cha watalii! Mabinti wa kitasha kama wanne hivi walikuwa wamevalia vichupi tena mtepetepo mali zote zikiwa nje nje.
          Mgoshi anawangalia na kuzoza “hivi kwei huu nao ni utaii au uchafuzi wa maadii yetu? Sijui hawa nao mkuu amewaweka kundi gani. Maana tinavyoaabudia, hapa azima inshu nzima izue ukakasi na utata.
Tuonene wiki ijayo huku tukitafakari.
Chanzo Tanzania Daima: J'tano, Jan., 7, 2018.
       




No comments: