Kudos to President Magufuli

Wednesday, 2 May 2018

Siku Tundu Lissu aliponiita mbwa mwitu-sijui ni hasira au kuchanganyikiwa sijui

Ujumbe huu chini ni wa Tundu Lissu kama ulivyotokea kwenye jamii forums. Lissu ananishutumu kuwa mbwa mwitu kwa sababu tu niliandika makala kumshauri asirejee nyumbani. Sina ugomvi na Lissu na uamuzi wake wa kurudi nyumbani. Aende hata kesho. Hata hivyo, angepima akili yake kabla ya kufanya hivyo.Wandugu wapendwa salaam,

Naomba nizungumzie kidogo nia na malengo halisi ya Josephat Nyamwaya na wenzake.

Alianza mtu aitwaye Nkwazi Mhango yapata wiki moja iliyopita. Jana akafuatia Nyamwaya na leo ni zamu ya anayeitwa Martin Maranja Masese.

Wote wanaelekea kunipenda sana. Wote hawataki niuawe na 'watu wasiojulikana' pindi nitakaporejea nyumbani. Ijapokuwa hawasemi wazi wazi, wote hawapendi nirudi nyumbani kwa sababu nikirudi nitauawa.

Nyamwaya ametoa mfano wa marehemu Masinde Muliro wa Kenya. Maranja Masese ametoa mfano wa marehemu Ninoy Aquino wa Filipino.

Nyamwaya ameshauri nisirudi kupitia Dar es Salaam au Nairobi, bali nipitie Malawi halafu nije kwa barabara hadi Tanzania.

Je, hao wauaji wanaonisubiri Dar Es Salaam au Nairobi hawawezi kunisubiri Malawi au mpakani Kyela, au mahali pengine popote katika barabara ndefu ya kutoka Malawi hadi Dar?

Kwa kufuata hoja za wapendwa wangu hawa, je, niendelee kukaa nje ya Tanzania hadi lini itakapokuwa salama kurudi?

Je, nisubirie mpaka Jiwe atakapoamua kuondoka madarakani? Na nani ana uhakika ataondoka lini, maana kuna vijineno vya kutaka aongezewe muda.

Mimi ni mbunge wa kuchaguliwa na wananchi. Je, niachie ubunge wangu kwa kuhofia usalama wangu?

Mimi pia ni kiongozi wa juu wa CHADEMA. Je, niachane na siasa ili nisiuawe?

Maswali yote haya hayana majibu katika hoja za hawa watatu wanaonipenda sana.

Kuna kingine hawakisemi, angalau wazi wazi. Ukiangalia hoja zao kwa umakini, wanachosema ni kwamba watakaoniua ni Serikali ya Magufuli kwa kutumia pengine Idara ya Usalama wa Taifa au polisi au Jeshi kama ilivyokuwa kwa Masinde Muliro na Ninoy Aquino.

Kama wanawajua hawa wauaji watarajiwa kwa nini hawapigi kelele kwa Serikali ya Magufuli ili iachane na mipango hiyo ya uovu?

Serikali ina wajibu wa kulinda maisha ya raia wake kama mimi. Kwa nini watu hawa hawataki kuishinikiza serikali itekeleze wajibu wake kwa kulinda maisha yangu?

Kwa sababu zote hizi, nafikiri wanachotaka hawa wanaojifanya kunipenda ni kwamba nisimnyime Magufuli na watu wake usingizi kwa kurudi kwangu.

Wanachotaka kimsingi ni kwamba niachane na siasa za upinzani kwa kukaa uhamishoni. Nikifanya kama wanavyotaka basi Magufuli atapata afueni kubwa.

Ndicho wanachotaka hawa wanaoleta vijihoja vya namna hii. Kukubaliana nao ni kumpa Magufuli na watu wake ushindi mkubwa lakini wa chee.

Kukubaliana nao ni kukubali kuwa maumivu na mateso yote niliyopitia na ambayo wamepitia watu wengine wengi yalikuwa ni ya bure.

Ni kweli Tanzania ya Magufuli imekuwa nchi ya hatari sana kuishi, hasa ukiwa mpinzani wa CCM. Lakini dawa sio kukimbia nchi, bali ni kukabiliana na hatari hizo na wanaozisababisha.

Akina Nkwazi Mhango na Joe Nyamwaya na Martin Maranja Masese wanataka Magufuli atawale anavyotaka bila bughudha ya akina mimi.

Wanajifanya kunipenda na kunitakia mema lakini, kwa hoja zao, wanampenda Magufuli na watu wake zaidi.

Tuwe makini sana na watu wa aina hii. Ni mbwa mwitu waliojivika ngozi za kondoo.
Chanzo: Jamii forums

No comments: