The Chant of Savant

Wednesday 12 December 2018

Picha ya leo: Moja ya Urithi wa Thamani wa Mzee Pius Msekwa


 Kwa wapenzi na watunzi wa vitabu kama mimi, mtu anapoandika kitabu huwa anatengeneza kitu ambacho kitaishi muda mrefu hata baada ya yeye kuwa ameondoka. Mmoja wa watu wanaonivutia sana walioamua kutumia fursa na uwezo wao kutengeneza urathi usiochuja si mwingine ni rafiki yangu mzee wangu na mtunzi mwenzangu mzee Pius C. Msekwa ambaye baada ya kustaafu anautumia utajiri wake wa maarifa kuelimisha jamii kupitia makala na vitabu. Hapa komredi Msekwa anaonekana akizindua kitabu chake kiitwacho Uongozi na Utawala wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye hakuwa mwalimu wake tu bali mentor wake; ambaye kadhalika mchango wake kwa taifa si haba.
Juzi juzi alipoteuliwa kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Mbeya cha Sayansi na Teknolojia, nilisoma kwenye mtandao wa Jamii Forums watu wengi wakilalamika kuwa inakuwaje Komredi Msekwa awe na vyeo viwili tofauti na falsafa ya rais John Pombe Magufuli aliyemteua. Hata hivyo, wakosoaji walisahau kitu kimoja; Komredi Msekwa si mtu mwenye njaa wala mwenye tamaa ya madaraka na mali. Nadhani, kwa tunaomfahamu unyenyekevu wake na kujitolea, alipokea wadhifa huu kwa sababu ya kumheshimu rais. Nakumbuka alipoteuliwa, alinitaarifu.  Kwa wanaomjua, Komredi Msekwa hajapewa ajira wala ulaji bali mzigo wa kusaidi taifa kutokana na utashi, utayari na uzoefu wake.  Kitu ambacho wengi hawakifahamu ni kwamba nyadhifa alizo nazo Komredi Msekwa si ajira bali heshima inayomgharimu muda wake wa kustaafu. Kama Komredi Msekwa angelikuwa mpenda madaraka si angeendelea kugombea ubunge na kupita tu. Mbali na hayo, Komredi  amejitofautisha kama mpenda jamii ambaye anapohitajika huwa hakatai. Isitoshe, tukiangalia kizazi cha sasa kilichojaa wapigaji, kwanini tusimpongeze Komredi Msekwa kwa kuwa tayari kutwishwa majukumu. Nadhani hili linajibu swali ambalo wachangiaji wengi kwenye mtandao wa Jamii Forums waliuliza: Inakuwaje rais amteue mtu mwenye umri zaidi ya miaka 80 na kumuondoa profesa Mark Mwandosya mwenye umriu wa zaidi ya miaka 60? Nani kasema ujuzi inazeeka? Isitoshe wote wawili si wasaka ajira bali viongozi waliotumikia taifa kwa uaminifu na ufanisi mkubwa na kwa muda mrefu. Hivyo basi, kwa kusherehekea na kuonyesha kufaa kwa Komredi Msekwa, nimeamua kumpamba kwenye blog hii leo lau watu waweze kutambua uwezo wake mkubwa si wa kuongoza tu bali hata kufikiri na kuweka fikra zake kwenye maandishi kwa ajili ya vizazi vijavyo.
      Kwa namna komredi Msekwa anavyojituma au tuseme anavyo-punch laptop yake kama asemavyo, sijui taifa letu lingeneemeka vipi kama viongozi wetu wote wangemuiga? Kwa kuangalia namna Komredi Msekwa alivyochangia katika uongozi wa taifa letu, nimechagua picha hii iwe picha maalumu na muhimu ya kufungia mwaka. Komredi Msekwa aka Rock, nangoja kwa hamu kusoma vitabu vyako viwili ambavyo najua uko unavimalizia. Komredi Msekwa, hongera kwa kazi pevu na tafadhali, endelea kuelimisha umma kupitia maandishi na mchango wako visivyo kifani.

No comments: