The Chant of Savant

Tuesday 14 February 2023

Chuo cha Nyerere Kisitelekezwe

Mheshimiwa Rais, Nakusalimia kwa jina la JMT. Je una tarifa kuwa Chuo cha Mwalimu Julius K. Nyerere University of Agriculture and Technology (MJKNUAT), Butiama, alipozaliwa, kukulia na kuzikwa Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere hakijawahi kupokea wanafunzi wala kutumika kwa miaka 13 tangu kuanzishwa? Je hii kama si aibu, dharau na kutojali kama Jamii na Taifa ni nini Mheshimiwa Rais japo hizi lawama si zako? Kwa mema yote aliyotenda Gwiji huyu, hii ni haki? Je mwenzako Mama Maria na familia yake wanaumia kiasi gani? Naomba uhoji yafuatayo:
Mosi, ilikuwaje wahusika wakaanzisha Chuo na kupoteza fedha na fursa za Umma bila sababu zozote za msingi kama hakihitajiki? Nini sababu za msingi zinazoingia kichwani kufanya hivi? Kama zipo, ni vizuri watanzania wenye baba yao na fedha zao wajulishwe haraka. Kama kuna hujuma au uzembe, ijulikane na wahusika washughulikiwe.
Pili, je nini mantiki ya kukipa Chuo hiki kukiita Mwalimu Nyerere kama tutazingatia hadhi, umuhimu wake kwa Taifa hata Afrika kwa ujumla halafu kikatelekezwa?
Mheshimiwa Rais, una habari, kwa wenye bongo zinazochemka, Jina la Mwalimu Nyerere ni kitega uchumi kikubwa kinachoweza kuingizia Taifa si sifa tu bali hata fedha?
Tatu, je ilikuwaje wahusika wakajenga Chuo hiki mahali alipozaliwa na kupumzishwa mpendwa wetu Baba wa Taifa wakati wakijua fika wasingekihudumia wala kukitumia? Ni matusi na uchuro kiasi gani kwa familia na Watu wake mbali na watanzania kwa ujumla? Mwalimu Nyerere si raia wa kawaida. Ni alama ya na mwanzilishi na Baba wa Taifa letu. Hivyo, tunapomdhalilisha, tunajidhalilisha wenyewe kama Taifa. Dunia inatucheka na kutuzodoa. Je hivi ndivyo tunavyomuenzi kwa kumdhalilisha ili tupate nini na kwa faida ya nani?
Baada ya kupata taarifa mbaya ya kutelekezwa kwa MJKNUAT, nilimuuliza mwanaye Madaraka Nyerere. Alinijibu kwa masikitiko kuwa hahusiki na Chuo husika. Nilishangaa sana. Sikupenda kumuuliza tena ili kuepuka kumuingiza kwenye siasa, kwani, si mwanasiasa.
Baada ya kutafakari kwa kina, niliamua kuandika waraka huu ili lau wahusika wajue baadhi yetu tunavyojisikia. Wakati nikiwaza hili na lile, nilikumbuka Chuo kingine kama hiki nchini Kenya cha Jomo Kenyatta University of Agriculture and Technology (JKUAT) chenye hadhi ya kimataifa na kinachotunzwa kweli kweli kutokana na kujengwa kumuenzi mwanzilishi wa Taifa la Kenya mbali na kubeba jina lake. Je sisi tunashindwa nini? Je tunahitaji kwenda kwa majirani kujifunza namna ya kuwaenzi waasisi wetu? Wakati nikiwaza haya, nilishangaa hata mantiki ya Tanzania Visiwani kutokuwa na Chuo kinachomuenzi Hayati Shehe Abedi Karume mwanzilishi wa sehemu hii ya Muungano aliyekuwa nguvu na nyenzo kubwa ya Muungano tunaojivunia na kuuonea fahari.
Japo Mwalimu hakuwa Mtu wa kulalamikalalamika na kulialia, naamini huko aliko analalamika na kulia japo hatumsikii. Nani hatakufa ajisahau hivi? Inakuwaje tunapata fedha za mambo mengine hata yasiyo muhimu ikilinganishwa na elimu tukashindwa kuhudumia na kutumia Chuo kama hiki? Je hatuna wanafunzi wa kutosha au ni uzembe na kuona mbali? Inakuwaje Taifa linalojinadi kuwa kilimo ndiyo uti wake wa mgongo linaachia na kufuja fursa kama hii adimu? Nashangaa hata Taasisi ya Nelson Mandela (Nelson Mandela African Institute of Science and Technology, NM-AIST) ilivyoweza kujengwa Tanzania wakati Chuo kamili cha Mwalimu Nyerere kikiendelea kuoza bila kutumika wala kuwanufaisha watu wake. Je tatizo ni kupenda na kuenzi vya wenzetu tukiviponda na kuvitelekeza vyetu? Kama tumeshindwa, kwanini tusiitishe michango lau toka kwa wapenzi wa Mwalimu watusaidie namna ya kuendesha na kunufaika na Chuo hiki pamoja na jina kubwa na muhimu kilichobeba? Inakuwaje leo tunaona wenzetu wakiwaenzi tena watu ambao hawakutusaidia kupigania uhuru kama vile mitume na watakatifu tusio nao uhusiano wala tusiowamilki wakati tukishindwa kuenzi wale wanaotuhusu zaidi? Je hapa tatizo ni nin na ni la nani?
Kabla ya kumaliza, naomba nikushauri na serikali yko inayodaiwa kuwa sikivu ili msikie na kumtendea na kututendea haki Mwalimu Nyerere na watanzania aliowapigania, kuwatumikia na kuwapenda sana.
Mosi, serikali ikubali kuwa ni jukumu lake kuhakikisha Chuo hiki kinaanza kufanya kazi mara moja si kwa heshima tu ya Mwalimu bali kwa faida ya watanzania wenye kuhitaji elimu.
Pili, ieleze inakuwaje Vyuo vingine, tena visivyo na hadhi kama ya MJKNUAT, vipate fedha za kuviendesha lakini si Chuo hiki.
Tatu, kama serikali haina nia––––japo uwezo inao–––iwatangazie watanzania ili wajitokeze wanaoweza kutafuta watu na mashirika ya kuendesha Chuo hiki.
Nne, serikali iwatake radhi watanzania na familia ya Mwalimu kwa kuwaangusha kiasi hiki.
Mwisho, baada ya kufanya yote hayo juu, itungwe sheria kulinda Chuo hiki, itamke wazi hadhi yake na priveleges zake kama alama ya Taifa ili hata tawala zitakazokuja baada yetu zibebe jukumu la kuilinda historia hii ya Taifa. Taifa lisilo na mashujaa wake ni Taifa la watu woga na wa hovyo. Taifa linalofuja tunu na turathi zake halina maana wala sababu ya kujiita Taifa. Nimalizie kwa kukuomba uingilie kati tena haraka iwezekanavyo. Shukrani na kwa heri. Mungu Ibariki Tanzania. 
Chanzo: Raia Mwema kesho.

No comments: