The Chant of Savant

Wednesday 22 February 2023

PhD za Mchongo ni Aibu na Jinai

Pamoja kuwa na PhD, kwa sasa, ni kawaida kwa waliofuata taratibu na kuzisotea, kuzipata na kufaa kuzitumia. Hata hivyo, siku za hivi karibuni–––tokana na tamaa,ujinga, ukosefu wa maadili, na usasi wa sifa, PhD zinaanza kupoteza maana. Badala ya kuwa ishara kuwa mhusika amefikia kilele kitaaluma kwenye eneo lake, zinaanza kudhalilika kama nyanja nyingine kama dini ambapo si vigumu kukuta matapeli na wezi wa kawaida wakijiita mitume, manabii na vyeo vingine vitukufu wakati ni utapeli na upumbavu wa kawaida. Hii maana yake, tunaanza kujigeuza taifa la wahalifu na vilaza kwa tunavyokubali hii jinai na uoza.

            Kutokana na kadhia hii, leo nitajadili aina za PhD. Nitaanza na daraja la kwanza ambalo mwenye PhD huitwa Daktari hata kama siyo wa hospitali. Mtunukiwa huisomea si chini ya miaka minne hadi nane–––kwa Amerika ya Kaskazini ambako kuipata si kazi kidogo. Ili kusomea na kupata shahada hii lazima mhusika awe na shahada mbili yaani ya kwanza (Bachelor) na ya pili (Master’s) japo kuna kesi chache ambapo mtu anaweza kuisomea akiwa na shahada ya kwanza kulingana na masharti ya chuo kinachoitoa.

            Aina ya pili ya PhD inayoaanza kukubaliwa ni ile ‘inayosomewa’ na wakubwa, mfano, baadhi ya mawaziri wetu ambao unashangaza wanavyoweza kujikunja kusomea shahada hii na kuendelea na mikikimikiki ya kazi za umma. Hata hivyo, tokana na nafasi zao na kukiuka kwa tamaa na ukiukaji wa maadili, uwezekano wa kutembeza fedha na kupendelewa ni mkubwa. Mfano, ni Rais wa nchi moja jirani ‘aliyepata’ PhD akiwa Naibu wa Rais aliyesifika kutumia muda mwingi akifanya kampeni. Rafiki yangu mmoja, Profesa wa sheria alisema kuwa shahada hizi ni feki na zinatolewa kisiasa sawa na PhD iliyowahi kutolewa kwa mke wa imla wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe, Grace aliyopewa miezi michache baada ya kujisajili. Baada ya Mugabe kuangushwa, PhD ya Grace iligundulika ilikuwa feki. Kundi hili lina wanasiasa wengi ambao hata huwezi kuwadhania kama huyu Rais wa nchi jirani. Nchini tunao wengi tena wanaojisifu walisomea darasani wakati ukifuatilia utakuta kuna namna. Ukitaka kujua nani alihenyekea na kukidhi vigezo vya kusomea na kupata PhD halali, angalia Tasnifu yake iko wapi.

            Wengi wa vilaza hawa huzificha tasnifu zao kwa vile zinawafichua na ni aibu na feki. Wengine wanaweza kuandikiwa na wajuzi na kuwalipa fedha. Hii inanikumbusha kashfa ambayo ilipita bila kuripotiwa sana nchini. Jamaa mmoja ninayemfahamu vizuri kuwa hakuwa na hata shahada ya kwanza aliweza kuwadanganya watanzania kuwa yeye ni Daktari hadi akachaguliwa meya wa Jiji la Dar. Alipokufa, ukaandikwa wasfu wake. Hakuna hata mstari mmoja ulioonyesha alikuwa na shahada hata moja!

            Aina ya tatu ni PhD ya heshima (Honoris Causa). Hii hupewa watu maarufu kama vile marais, au watu waliotumikia mataifa yao vizuri. Mfano mzuri ni rafiki yangu na mwandishi mwenzangu Mhe. Pius Msekwa, Spika mstaafu na mwandishi nguli wa makala na vitabu. Wengine ni marais Baba wa taifa, mzee Mwinyi, Hayati Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete, Amani Abeid Karume na sasa Samia Suluhu Hassan. Mbali na Kikwete, wengi hawakuruhusu waitwe Madaktari kwa sababu wanajua kuwa Honoris Causa haikupi hadhi ya kujiita Daktari–––japo kwa wasiojua vizuri maana yake wanaweza kujiita au kukubali kuitwa Madaktari. Shahada hizi hutolewa na vyuo vinavyotambulika kimataifa.

            Aina ya nne ya PhD ambayo kimsingi ni uchafu ni hizi za kupewa na vyuo vya kitapeli vya mifukoni au degree au diploma mills au viwanda vya kufyatua shahada ambavyo huwatoza fedha vilaza wanaoingizwa mkenge. Hi jinai ambayo–––kama wahusika wangejua–––wasingelipa fedha yao au kukubali kuchafuliwa kupewa ujinga huu. Waulize wengi wanaokuja na tambo kuwa wamepewa PhD hizi wakwambie ni vyuo gani vimetunuku. Wakivitaja vichunguze hadhi zake. Utakuta ni vya kitapeli. Kimsingi, kinachoitwa PhD hapa ni upuuzi na utapeli. Waulize hawa wanaokuja wakijtapa wametunukiwa Udaktari, inakuwaje watoe fedha wakati Udaktari husomewa au kutunukiwa na vyuo vyenye stahaki kama heshima. Hii imenikumbusha jamaa mmoja aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana kitaifa ambaye baadaye aliteuliwa kuwa balozi katika nchi moja kubwa ya Amerika ya Kusini akijiita Daktari. Baada ya kupata wa kuhonga na kumpitisha kwenye chuo kimoja mkoa jirani na Pwani, alionekana akitabasamu kwa ‘kuhitimu’ shahada hii ya uzamivu wakati miaka yote alikuwa akijiita daktari.  Kwenye kitabu changu cha Africa Reunite or Perish, uk.162 kinataja wazi watu kama Bingu wa Mutharika na mtangulizi wake Bakili Muluzi walivyotapeliwa na kupewa shahada feki za heshima.

            Mwisho, naishauri serikali na watanzania wakatae, wachukie, waiadhiri na kupambana nayo. Nasema kutokana na uzoefu wa kuisomea shahada hii. Tungeni sheria ya kumtaka kila anayepewa au kudai ana PhD aisajili serikalini baada ya kuhakikiwa kuwa ni halali. Hapa Kanada huwezi kufanya kitu kama hiki bila kuchukuliwa hatua za kisheria. Hata chuoni kama unaiosomea unakaribia kuipata, huwezi kujiita Daktari hadi ufanye mahafali na kutunukiwa rasmi. Kwa ufupi, kuna Madaktari wengi feki ambao wanapaswa kuwa gerezani.

Chanzo: Raia Mwema leo.

No comments: