The Chant of Savant

Tuesday 21 November 2023

Nilipoteua na kutengua kidhabi aliyetaka kunitumia

 


Katika chata letu kuna siri kali. M/kiti ni rahisi, kila kitu. Ni muungu unaopaswa kuabudiwa na kusifiwa hata unaboronga au kukosea. Ukiwa M/kiti, unaweza kumteua umtakaye akuhusu au asikuhusu, awe mshikaji, mshirika, mkeo, mkweo, shemeji, au mumeo na usivunje sharia. Katika kufaidi na kutumia umungu mtu na utukufu wangu, juzi nikamteua na kutengua kidhabi limbukeni, mjivuni, msanii, na msakatonge kuwa katibu wa danganya toto na rongorongo wa chata. Anaitwa Dau Alberyt Bushite aliyeibuliwa na mtangulizi wangu toka jalalani. Baadae walikosana akapotea hadi juzi niliopofumfua nisijue la kufa halisikii daw ana la kuvunda halisikii ubani. Najuta. Nilifanya kosa kumfufua, kumteaua, kumuacha akaniudhi, kunitumia, kunichafua, na kunigeuza kituko na ngazi ya kupandia. Baada ya kugundua hila zake, nikamtumbulia mbali kulaleki.
            Kweli, mwanaharamu ni mwanaharamu. Ukimuweka kwenye chupa, atatoa kidole. Bushite, kwa upofu wake, alidhani nilimteua ili kufyatua mafyatu wenzake wa kanda yake. Hivyo, nisingeweza kumfyatua. Kumteua tu, aliona fursa kutaka kufanya alichomfanyia aliyemuumba. Alianza kutoa matamko ya nguvu kana kwamba ndiye M/kiti. Alipayuka na kujidai hata kuingilia mamlaka ya wenzake wanaomzidi vyeo akiwapigia simu, kuwaanika hadharani akitoa maagizo ya ajabuajabu bila aibu. Alituchonganisha kwelikweli. Siri kali haiendeshwi majukwaani na kwa rukono. Hata hivyo, simshangai tokana na tamaa ya mamlaka na ukihiyo wake. Badala ya kutangaza chata, alijitangaza akidhani hajulikani janja yake. Badala ya kueneza itakadi ya chata, alijieneza na itikadi zake za kitapeli uchwara akidhani siku moja atakuwa rahisi wa mafyatu ning’atukapo. Thubutu!
            Badala ya kujenga chata, alilibomoa kwa kujijenga binafsi tena kwa knibomoa na kufanya nionekane mbaya na asiyefaa. Alifanya mambo yaliyonitia aibu sina hamu! Alijizuga kunitukuza wakati ukweli alijitukuza na kujikweza. Alijifanya rafiki na kipenzi changu kumbe adui mkubwa nyambaff!
 Juzi nilimsikia akiwataka mafyatu wamuombee awe msemaji wa wanyonge. Je mimi siyo msemaji wao au nawatesa? Hichi kifyatu kinachofyatufyatuka nilipokiteua, nilidhani kingenifaa. Kumbe kilitaka kunitumia kujitengenezea ulaji japo mafyatu sijui kama ni mazwazwa wakipe hata ujumbe wa nyumba kumi. Juzi mkwe wangu alipigiwa simu na kidhabu huyu na kunilalamikia. Ndugu yangu mwingine alihoji ilikuwaje nikateua kituko hiki kinachoniaibisha na chata langu! Aliuliza kwa uchungu kama ni washauri walionishauri, niwafyatue kabla huyu kidhabi hajanifyatua kwa kufanya mafyatu wanifyatue kwenye uchakachuaji ujao.
            Wasaidizi wangu wengi walilalamika kuwa fyatu huyu kihiyo mhalifu alikuwa akiwaingilia kwenye nafasi zao asijue kazi yangu kubwa ni kuteua na kutengua kwa mujibu wa katiba yetu fyatu ya mafyatu. Badala ya kufuata kanuni za uongozi, alizivunja zote. Kugundua aliniona zwazwa akizidisha kabobo, nilimtengulia mbali. Kumbe mtangulizi wangu aliyemtupa jalalani alikomtoa hakukosea. Nimeaibika, kuhuzunika, kushangaa, na kujifunza sana. Sijui ni kukata tamaa au uzembe, maana hata mafyatu wanamuamini wasijue janja ya nyani na wanaingizwa chaka na mkenge mchana kweupe! Je kuna kitu hatukuelewa uzuri au tulipitiwa? Inakuwaje fyatu, tena asiye na chochote, kujifanya anaweza kutatua mataizo yote wakati hana uwezo?
            Kwa kutumia jina langu, alijijengea imani, umaarufu, na sifa asizo nazo. Kwa makusudi, alijua hatatui bali kukuza matatizo ili baadaye ayatumie kutufyatua sisi tuliomfyatua na kumpa nafasi ambayo alitaka kutumia kutufyatua. Ametufanya tuonekana wote mazwazwa naye bonge la mjanja. Alianza kuwachonganisha watendaji wangu katika kila idara akiwapigia simu hovyohovyo wengi ambao kimadaraka, wako juu yake kwa kusingizia chata letu. Juzi hata mshirika wangu kanishauri niachane na kijitapeli hiki kichumiatumbo kinachoota kuna siku kitakuwa M/kiti na rahisi wa mafyatu.
            Kwa ujuha, kidhabi huyu alidhani nilimteua kama kijibwa cha kuwatisha wanene. Siri kali haiendeshwi hivyo. Ni M/kiti mshamba anayeweza kutengeneza vijimbwa na vichawa kuwatisha wasaidizi wake. Kama unajiamini kama mimi unateua na kutengulia mbali bila kuangalia sura ya nyani. Si una dola. Siku hizi ni rahisi kwa rahisi kuteua na kutengua. Kumejaa machawa na mafyatu wanaojipendekeza wakijiruhusu kubadilishwa kama nepi mradi wapate tonge.
            Du! Hamjanielewa walengwa?
Chanzo: Mwananchi kesho.
 

No comments: