The Chant of Savant

Tuesday 2 April 2024

Toka Wanyonge Hadi Machawa


Mafyatu tumejengewa dhana na utamaduni mchafu na hovyo. Tumepewa majina ya hovyo sababu tu hovyo. Tunaonekana hivyo. Tume/ligeuzwa wanyonge wao wababe, tukaamini, tukaupokea, kukuubali, kutukuza, kusifia, kuridhika, na kushangilia. Ukiwa mnyonge uhitaji kutetewa badala ya kujitetea. Huwezi kupigania na kuinyakua haki kwa vile umenyongonyea. Tusikubali kunyonyong'onyezwa hata kunyongwa na kunyongeka.
Ukiwa chawa unahitaji uchafu ili uishi. Chawa ni mdudu  hana haki wala haistahiki. Leo, nitafyatua awamu mbili mtawalia, faivu na sikisi. Faivu ilituita na kutufanya wanyonge. Hatukuuliza wanyonge katika nini na kwanini! tuliridhika kuambiwa na kusikia tulichotaka kusikia. Ghafla bin vu, kaya ya mafyatu ikageuka ya wanyonge! Walichipuka wanyonge, wanyongeaji, wanyonyaji hata wanyongaji. Kkkkk! Inasikitisha japo nacheka. Wapo walionyonga na walionyongwa tukaanza, taratibu, kuzoea. Tuliambukizwa tukaugua ugonjwa wa nyongea na unyonge. Badala ya kufyatuka tukafyatua, tulivyatuliwa jumla.
            Kama haikutosha, tuliupokea na kuukubali unyonge tukaanza kujikomba, kusifia waliotunyong’onyesha mbali na kuunga mkono unyonge wetu. Tulinyong’onyeshwa tukanyong’onyea kwelikweli tukashindwa kufyatuka na kufyatua. Katika unyonge wetu tulinyonywa tukanyonyeka tukaendelea kunyong’onyea. Walizuka wanyonyaji wateule wakaendesha kaya kigeshi. Wapo waliogeuka miungu tusijue nao wanavyatuliwa hata wakiwafyatua wenzao au kuwanyonya, kuwanyonga, na kuwanyong’onyeza.  Huwezi kuendesha kaya kinyonge, kinyonyaji, na wanyonywaji ukajisifu umefanikiwa.
Haiwi huwa! Kwa mkono wake, Al-Ma’buwd, ghafla bin vu, akafyatua ikaingia awamu mazeri doktari. Iliutosa unyonge japo iliuendeleza kidizaika. Ilikuja dhana ya machawa. Ghafla, tukaondoka unyongeni tukaelekea uchawani tulioupwakia kama ushahidi kuntu wa uchafu na unyonge wetu na wao. Baada ya kunyong’onyezwa, na kunyong’onyea, tunanyonywa. Kazi ya chawa na machawa nini? Sitaki nirudie unyonywaji uliopewa majina matamu kama vile tonzo, kikokotezo, nk. Pamoja na kunyonywa, hatukufyatuka na kufyatua wanaotunyonya au kutuchawisha. Tumeukubali uchawa, dharau, udhalili, na udhalilishaji. Japo tunajua nani anamnyonya nani, hakuna anayelalamika zaidi ya kujipendekeza kwa kupwakia kila uchafu kifalsafa.
            Kimsingi na kifyatu, anayewaita au kuwageuza wenzake wanyonge au machawa, naye mnyonge au chawa. Ni mnyonyaji na mchafu kama chawa. Chawa na uchawa ni alama za uchafu na unyonyaji asivyopaswa kutumia fyatu aliyefyatuliwa na Mungu. Hapa, lazima kuwe na ima mtindio wa ubongo, ugonjwa wa akili, ukichaa, hata utaahira wa pamoja au collective mental malade kwa kifipa. Kufuga chawa, lazima uwe mchafu. Kuwa chawa, lazima uwe umeishiwa ubunifu, ufyatu hata ungurumbili. Waanimo (hayawani) wanatuzidi! Kumbe wanyama ni mafyatu wa kweli? Digidigi, faru, nyati, swala, n.k hugaragara ima matopeni au mavumbini kuwaondoa chawa wasiwanyonye. Nyani huwafukua na kuwatafuna, maana wanachukia kunyonywa. Nyani, pamoja na unyani wao, hawajidai wala kuridhika na kufuga chawa. Inakuwaje mafyatu, tena wanene, waridhike na kufuga machawa? Inakuwaje mafyatu waliojaliwa bongo zinazochemka, mikono, na nguvu wakubali au kugeuzwa au kujigeuza machawa ndiyo waishi? Pamoja na ufyatu na uprofesa emeritus wangu, hii anomaly (sina kimakonde chake) imenishinda kuitanzua na kuipatia jawabu mujarabu.
            Ni hiari na jukumu la wanyonywao kuwaulia mbali chawa. Ni jukumu la wanene kujenga mifumo safi na si uchawa wala uchafu. Tunawafundisha nini vitegemezi vyetu japo vyao vimeridhika na uchawa tokana na kuwa chawa wanaonufaika na uchawa? Je tutafuga chawa hadi lini na iwe nini kwa faida gani au kumkomoa nani? Je falsafa za maana zimeisha hadi tuishiwe na kuanzisha na kuendekeza falsafa za kichawachawa? Chawa wanatucheka. Wanatuona hamnazo kwa vile hatujui udhalili wao. Mnadhani chawa wana furaha na heshima? Kawaulize wenyewe.
            Leo tuna uchawa. Tunajivunia. Nani ajuaye kama kesho hatutageuzwa funza, kunguni, panya, na viroboto? Nani ajuaye kama hatutageuzwa jamii ya mbu mueneza malaria au inzi msambaza kipindupindu? Namna hii tutapona? Je tufanye nini? Jibu ni rahisi. Tusijirahisi, kurahisishwa, na kugeuzwa wadudu tena  wabaya. Tuukatae uchawa, ududu, na udhalili kulhali. Kazi yangu ni kufyatuka na kufyatua. Kazi kwenu mafyatu kunielewa na mkafyatuka na kufyatua kwelikweli.
            Anayewaita wenzake chawa anashindwa nini kuwaua? Anayekubali kuitwa na kuwa chawa atashindwa kusiginwa na yule amuitae na kumuona ni chawa? Chawa na uchawa, hata wafuga chawa, wote ni wachafu. Hawahitajiki katika jamii ya mafyatu. Lazima tuwafyatue tunapopata fursa.
            Juzi nilitembelea kaya ya mafyatu tuliowaita manyang’au. Bila hili wala lile jamaa mmoja akaniita chawa! Kama siyo kuogopa karau, ningemdedisha ajue mie fyatu si chawa wala kunguni. Chawa huchukia mwanga na kupenda giza. Hula na kuishi gizani. Anapenda vya gizani. Huyu, hakika, ni mpenzi wa mgao wa umeme alale na ale uzuri. Mafyatu hamuyajui haya! Nshawaambieni. Fumbo nimefumbua. Kazi kwenu kuendelea kuwa au kuliwa na machawa au kufyatuka na kutaka lugha ya uchawa ikome haraka. Nashauri. Tuuchukie na kuukataa unyonge kwa sauti na herufi kubwa. Du! Nahisi kuna chawa ananinyonya! Anawasha ja upupu. Ngoja nimuulie mbali. Are you there?
Chanzo Mwananchi Jne iliyopita.

No comments: