Yoo-hoo, Africa Is Yowling

Yoo-hoo, Africa Is Yowling

Wednesday 3 July 2024

Mkimbinafsisha Bi Mkubwa Wangu Naua Mjue


Mtukufu Dk. Rahis, msikivu, mwenye maono, ndoto, uthubutu, ukimya, nk., naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, rahis, du! A’udhu billahi min ash-shaytaan-ir-rajeem. Nimemsahau Mtume! Naona yule anshangaa. Kwani nazusha? Wanagapi, sijui chawa, sijui kunguni, wakianza kuchonga wanafanyahivyo kwa maangamizi yao na mafyatu wao?
Nasikia kila mara rahis akisifiwa kuwa na ‘maono’ tena yasiyooneka. Kupitia maono, amegawa, sorry, binafsisha bahari, bandari, barabara, mbuga za waanimo, n.k. kama ni kweli. Hii inantisha kwelikweli. Naomba leo nifyatue kitu. Hivi huyu Bi Mkubwa ni Mungu, muungu, malaika, hata ntume? Hakosei? Je hizi sifa za kweli au kupakana mafuta kwa ngongo wa chupa au uchawa na ukunguni wa kutumia matumbo kufikiri badala ya vichwa ili kujaza matumbo?
Nasikia Bi Mkubwa ametenda ‘maajabu.’ Je ni maajabu kweli katenda au ni ajabu kusema katenda? Kamwaga njuluku. Mafyatu wanazipata? Kamwaga kiasi gani na kwa yupi?  Nasikia. Kamwaga pikipiki. Tunahoji ni za nini na hiyo njuluku ameitoa wapi au kuipataje na anategemea kupata nini na kwanini sasa tunapoelekea kwenye uchakachuaji wa uchaguzi? Ananunua nini? Ajabu, wakati rahis akitoa pikipiki kwa kila nkoa bwerere, akina maza wenzake wajawazito wanajifungulia nje ya zahanati! Mwe! Kwani hajui adha ya ujauzito na machungu ya kujifungua? Hayo tuyaache.
         Je rahis ni tajiri kiasi gani na nini chanzo cha ukwasi, ‘huruma na upendo’ hivi, ni vya nini, na anategemea kupata nini? Mafyatu tukienda hospitali tunaandikiwa dawa tukanunue! Maji ya mgao! Je hizi njuluku za pikipiki zingesaidia wajawazito, mafyatu, hata upatikanaji wa maji kiasi gani? Je hii njuluku ingeondosha michango ya hovyo na tozos kiasi gani? Je mikoa yetu inahitaji pikipiki wakati pesa inayopata tokana na bajeti ni kiduchu? Kwanini hatangazwi mmojawapo wa mabilionea wa kaya? Inakuwaje anakwenda ughaibuni kukopa na kubomu wakati ana ukwasi kiasi hichi? Kaya yake inashindwa hata kuendesha mangwalangwala ya mwendo kinyonga, sorry, kasi?
Tunapaswa kuwa wakweli. Pia, naye awe mkweli kwake na kwa mafyatu. Hizi pikipiki ni za nini kama hakuna namna ya kuhongana, sorry, kuchanganyana, kuelekea kwenye uchakachuaji mwakani? Kwanini sasa na si jana wala juzi? Je huyu bilionea wa sirini analipwa nshahara kiasi gani? Tukiuliza haya, mengine, na mengineyo tunakosea?
Turejee kwenye uwekezaji ambao wapingaji wanauita uchukuaji kama siyo uchakachuaji na uhujumu uchumi uliohalalishiwa na kufanywa na wanene tena kwa mlango wa nyuma. Bandari, tumewekeza. Juzi tuliona magawio la madafu 153.9 bilioni sawa na dolari za Kijoji Kichaka milioni 80! Kiduchu hichi kwa mwaka! Je waliingiza kiasi gani tujue kama kweli ni gawio au zenguo? Tunapaswa tujiulize na kuwauliza wamepata nini na wanatupa nini na nini tulipaswa kupata kisheria na kimakadirio. 
        Tusifanye magawio kuwa hisani bila kujiridhisha kuwa tunachopata ndiyo sitahili yetu badala ya kujiruhusu kupigwa na kufyatuliwa kijiiinga tu.  Fine. Je kwa namna bandari inavyotema njuluku kweli tulichopewa ni stahiki au chenga la mato? Mwaka 2016, bandari iliripoti mapato ya shilingi trilioni 13.37 (Mwananchi, Julai 6, 2016). Je kwa gawio hili walipata kiasi gani? Je walifikia, kutofikia, au kuvuka malengo? Je hiki ndicho tulichoahidiwa na kutegemea baada ya kugawiwa, sorry, kuuzwa, sorry, kubinafsishwa bandari kwa watasha wa Do Buy?
        Barabara tunawekeza baada ya kuunguza njuluku ndefu za mafyatu kuzitengeneza ili kuwanufaisha wachache? Nafyatua maswali yote haya na mengine kuepuka kuuziwa goat kwenye gunia tunajiona.
        Bahari, tumebinafsisha. Natamani na visiwa vibinafsishwe uone wazenj watakavyocharuka na kudai uhuru. Natamani hata makaburi yabinafsishwe. Bado milima na mito. Tukimaliza yote haya, tunabinafisha na machawa. Sijui nani atakuwa tayari kuwanunua wamkondeshe kama mafyatu. Tukimaliza vyote kweli kesho hamtabinafsisha hata hewa? Je Bi. Wakubwa zetu watanusurika? Wallahi, ikifikia kubinafisishana na mkamgusa Bi. Mkubwa wangu––––tate nane tate nane––––nakufa na fyatu. Hata hivo, kabla ya kumfyatua fyatu, nitamwambie Bwa. Hafith amwambie Bi Nkubwa wake ajibinafsishe kwa wamanga aone inavyouma na kuumiza. Nimesemeje? We koma!
Najua Ngolongolo akina Yero weshabinafsishwa na kuhongwa, sorry, kujengewa vibanda kule Msomea. Ukisikia maono ya maza na wamanga ndiyo haya. Si juzi niliowaona wakiwa wameishakubuhu kukata vikalio utadhani walizaliwa Tangamano. Huo nao uwekezaji au siyo. Soon, nitawaona wamanga wamepiga migolole ya kiyero wakipambana na lion. Nao ni uwekezaji au siyo.
Nimalizie. Hata kama mnatuaminisha hata kutufyatua kuwa uwekezaji ni muhimu kama kweli ni uwekezaji kama siyo uchukuaji, basi wekezeni kwa busara, tushirikishe, msituhamishe na kutuchuuza kama ilivyo sasa. Pia, wajibikeni na kueleza mnavyotumia njuluku zetu na zenu kama mnazo kama kwenye skandali ya pikipiki. Hivi Bi Nkubwa wangu bado yu salama kwa sera hizi? Hivi niko wapi? Kama naota!
Chanzo: Mwananchi leo.

No comments: