Kwa kuangalia uhalisia na busara za Madaraka, inakuwaje matapeli wa kawaida tena wachovu na wachafu kujivisha ubini wa Nyerere nasi tunaangalia kana kwamba ni jambo dogo na la kawaida. Japo Nchonga ni dingi wa wote, hakuwa muasharati wa kuzaa nje ya ndoa yake. Hivyo, hata kama unampenda na kumheshimu kiasi gani, hupaswi wala huna haki ya kubeba ubini wake. Isipokuwa uwe fyatu kama mimi.
Kwanza, kama wote tutabeba ubini wake, wabaya wake watasema tunamwabudia kutokana na kutupumbaza kiakili.
Pili, tutakuwa tunawanyang’anya au kuwanyima vitegemezi vyake wa damu utambuliko na haki zao vya msingi.
Tatu, watatokea matapeli hata maadui kutaka kumtumia ili wafanya upumbavu wao.
Nne, tujikumbushe. Dingi wa kaya hakupenda kusifiwa wala kuabudiwa. Kwa wanaokumbuka, alivyowahi kusema kuwa, kidini, yeye aliuwa mwanaharamu kwa vile alikuwa mtoto wa mke wa tano.
Hata huu utakatifu anaokaribia kupewa, kama angekuwa hai, ima angehoji hata kuukataa kwa heshima kuonyesha ubinadamu na unyenyekevu wake.
Tano, hakuna mfano wowote wa mafyatu wa kuvaa ubini wa kiongozi wao. Hata wakristo, walipewa ukristo na siyo ubini wa Yesu kwa vile hakuwa na watoto. Walivaa ukristo kama upakwa mafuta. Kuna kipindi maadui wa uislam toka ulaya walianza kuwaita waislam Mohammedans. Waislamu walichachamaa kwa sababu, a) huwa hawamwabudii Mtume Muhammad bali kumheshimu. Pili, wao si watoto wa Muhammad kwa vile Muhammad mwenyewe, kabla ya kufariki, aliwahi kuwaambia wazi kuwa yeye si baba wa yeyote bali baba wa watoto wake.
Mbali na kuwa uzwazwa na utapeli, kujipachia ubini wa dingi wa kaya, ni ushahidi kuwa wanaofanya hivyo wameishiwa ubunifu. Wanaonyesha, kukopa maneno ya mwanafunzi wa Mwalimu, Benjamin Mkapa, kuwa ni wavivu wa kufikiri. Wanaonyesha wanavyotumia utumbo kufikiri badala ya ubongo. Niliwahi kuandika makala kuwakata watanzania kumuita rais Samia Suluhu Hassan hasa wale ambao wamemzidi umri waliomwitua maza. Hii ni kutokana na ukweli kuwa wanafanya hivyo kumdanganya, kumtukuza, na kutaka kumtumia mbali na kumzeesha. Kila mtu ana dingi na maza yake. Samia ana watoto wake na––––kama ilivyo kwa dingi wa kaya–––hana historia ya kuzaa kabla ya kuolewa au nje ya ndoa.
Ukiachiwa kuishiwa na kukosa ubunifu mbali na utapeli, wengi wanaojifanya kubeba ubini wa dingi wa kaya, kwanza, hawana hata dalili moja ya kufanana nae mbali na kuigiza sauti yake au kujichora kama yeye. Kiusanii, tunawaruhusu wafanye hivyo. Kiuhalisia, hapana. Haiwezekani, ukamnasifibisha simba na panya. Pia, si vizuri walevi na vichaa kufagilia makaburi ya watakatifu. Ni ujinga wa pamoja, kuwaruhusu wazinzi kufanyia uchafu wao juu ya makaburi au majina ya mafyatu wetu maarufu waliopigania uhuru wetu.
Juzi, niliona klipu ya mmoja anayejifanya kitegemezi cha dingi wa kaya akishindwa kusoma hata hotuba ya kimombo aliyoandikiwa. Nyerere alikimanya kimombo. Sasa inakuwaje anayemuingiza ni mbumbumbu na kihiyo? Ukimuigiza mtu, lazima ujitahidi ufanane naye ili kuleta maana na kuwasilisha ujumbe juu yake mbali na kuamsha kumbukumbu juu yake. Haiwezekani nune akamuigiza simba. Nune ni mdudu na simba ni mfalme na malkia wa pori. Kupe hata kwa usanii na utani, hawezi kubeba ubini wa tembo wala ng’ombe. Wawili hawa ni tofauti kabisa.
Nimalizie kwa kuwaasa mafyatu tusikubali uchokozi wa matapeli, vilaza, na vihiyo wanatafuta riziki hata kwa njia chafu kuwachafua mashujaa wetu walioleta uhuru huu tunaofaidi na kuringia. Wote wanaojiita watoto wa Mwalimu Julius Nyerere wakome na kuacha ili kuwaachia watoto na família yao wafaidi haki na utambuliko wao. Japo hili linaweza kuonekana ni jambo dogo, madhara yake ni makubwa. Hivi nimesema naitwa Fyatu Kambaage au Nyerere?