Kuna hiki kisa cha binadamu, kuku, na mbwa. Mbwa alimfyatua kuku wa mwenyewe. Acha kuku, mbwa, na wenyewe walaumiwe na kulaumiana kwa kuku kufyatuliwa na mbwa! Mwenye mbwa alimlaumu kuku na aliyemfuga kwa kujiruhusu na kuruhusu aliwe. Kisa hiki cha kufikirika na kufikirisha. Kina maswali na mafunzo mengi. Kwanini alaumiwe mbwa na si yule aliyemfuga kuku au mbwa? Kwani, kazi ya kuku ni nini kama siyo kuliwa? Kwanini kuku alijiachia na kukubali kufyatuliwa? Kwanini ana nyama inayoliwa na siyo isiyoliwa? Je, walitaka mbwa ale nini na kuku aliwe na nani? Mbwa, akila kuku, ni kosa ila binadamu hapana! Kuku, japo kazi yake ni kuliwa na kutaga mayai yaliwayo pia, akiliwa, analaumiwa! Ebo! Kuku lake ni kuliwa bila kujali kaliwa na binadamu, kicheche au mbwa. Kuku ni kuku lazima ataliwa tu.
Uzuri ni kwamba mbwa hakujilaumu na hatajakaa ajilaumu kwa kumfyatua kuku. Kuna mafyatu wanakosea. Wanapaswa kuomba radhi hata kutubia kuwalaumu kuku na mbwa kulana. Kwani, wanakosea kwa kudhani wanawazodoa kuku na mbwa wakati ukweli ni kwamba wanajizodoa na kujiambia wenyewe kama siyo mafyatu wenzao.
Kinachoendelea kayani na lawama hizi ni ile hali ya kuwatupia lawama kuku na mbwa wakati wahusika ni nyinyi. Hata kesi yake ipelekwe mahakama kuu, kuku hatashinda kesi wala kuwa na haki zaidi ya kufugwa na kuliwa. Kwanini mnataka kumpaka kitimoto lipstick mkidhani atarembeka? Kitimoto ni kitimoto. Mnamsumbua kitimoto bure kama mnamsumbuavyo mbwa kwa kula kuku na kuku kuliwa na mbwa. Nani anamjali kuku? Nani anamuombolezea kuku? Kweli, kuku ana haki au ni kwa vile kaliwa na mbwa? Kuliwa ni kuliwa. Kuku aliwaye na mbwa hata simba hana tofauti na yule aliwaye na mafyatu. Anafyatuliwa tu. Hivi, kweli hawa wanaomtetea kuku wanamtetea au kutetea mlo wao? Kigombacho ni pale fyatu anapowala mafyatu wenzake halafu akawalaumu kwa kujiruhusu kufyatuliwa naye bila wala yeye kujilaumu au kukubali kulaumiwa.
Juzi, nilisika maboksi na mashehena yakitika ka debe tupu. Huu uliitwa muujiza na wanaojifanya wana dini wakati ni duni. Ajabu ya maajabu, hawaongelei wala kuhoji. Inakuwaje mafyatu wanaongelea amani na kuitenga haki wakati hawa ni mapacha? Kunani hapa? Eti walitetea mafyatu wale kuku kwa amani wakati wakijiganya hawajui wala kuona haki ya kuku! Hivi mwenye mbwa anapokuwa mbwa mwenyewe mtasema nini? Je, kwanini kumdhalilisha mbwa ambaye yuko radhi kumfia bwana wake ambaye hawezi hata kumlilia? Mheshimu mbwa tafadhali. Kwani, ni kiumbe mwaminifu na anayelinda hata wahalifu wamfugao.
Jikumbushe yafuatayo ndipo unene. Mbwa hulinda mali zenye thamani kubwa lakini hufa maskini. Sindano hushona nguo nyingi lakini daima iko uchi. Kijiko huungua kuchota chakula na mchuzi. Nini hufuata baada ya mwenye kushiba kushiba kama siyo kukiosha na kukikausha? Hatushangai uongo unapogeuka uogozi na uongozi kuwa uongo? Najua. Wengi mlikuwa wakati wa Ticha Mchonga. Muelewe. Mambo yamebadilika na kuharibika au siyo? Kubalini. Wakati ule, mliona nuru. Leo, mtaona kiza totoro mtake msitake. Si shehe Ruksa aliwaonya kuwa kila zama ina kitabu chake?
Tafuta hicho kitabu ukisome uelewe. Najua wengi ni wasomi tena wenye PhD ziwe za kweli au za kuzawadiwa, kununua, na kuhongwa. Wangapi wayajua mateso ya kuzisomea na kuzipata baada ya kuhangaishwa na maprofesa wenye wivu kuwa utakuwa kama wao? Kumbuka. Unasimamiwa wakati mwingine jitu ambalo kiakili haliwezi hata kugusa sole ya kiatu chako. Jiumbushe. Ni committee chairs wa PhD unaowakumbuka ambao hata kufikiri namna ya kufikiri hawajui? Si ajabu mjinga kumfundisha msomi au mwenye macho kuongozwa njia na kipofu. Ndo mambo ya siku hizi. Tusizinguane wala kuhadaana na kugeuzana mazwazwa wakati tuna akili. Tusijitoe ufahamu na kufanya ukuku wa kumtetea kuku au umbwa wa kumla kuku wa wenyewe.
Naona yule anashangaa! Unashangaa nini mwenye macho kuongozwa na kipofu mwanangu? Amka uchangamke. Usilaumu wasiolaumiwa. Jilaumu mwenyewe. Ikizidi ikapungua, lalamika lakini si kulaumu. Kwani, ni kosa la jinai tena kubwa kuliko uhaini na ugaidi. Wakubwa huwa hawakosei. Wakikosea, hawakosei wala kukosolewa.
Wenye mbwa, huwa hawaaibishwi. Unalaumu kwanini mbwa kala kuku! Ebo! Mbwa akila kuku ni kosa la kuku siyo mbwa wala mwenye mbwa. Kama ukitaka kuwaingiza wamilki, mbwa akila kuku, kosa ni la mwenye kuku ambaye hakumfunga wala kumtahadharisha na mbwa. Kazi ya mbwa, kama kicheche na mafyatu, ni kula kuku. Na kazi ya kuku ni kutoliwa na mbwa japo ataliwa na wengine bila kujali ni nani na kwanini. Naomba utie akilini. Hii dunia ni ya mbwa si ya kuku.
Acha nisiwachoshe kabla hawajanichoka, kunichosha, kuniteka, na kunitesa kabla ya kuniua. Wajue. Wakiniteka, nawateka tutekane kama ilivyo kwa sasa ambapo mtekaji na mtekwaji wote ni mateka wa utekaji. Hivi, leo, nimekunywa gongo kiasi gani?
Chanzo: Mwananchi Jtano leo.
No comments:
Post a Comment