The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Sunday, 8 March 2026

talaka yenu inawafundisha nini watoto wenu?


Si mara ya kwanza wala ya mwisho kujadili talaka. Leo, tutadurusu talaka na madhara kwa watoto wa watalaka. Japo talaka ni jambo la kuhuzunisha, kwa watoto wa watalaka wenye busara na wanaojua na kuchukia madhara ya talaka, linaweza kuwa funzo kubwa katika maisha yao. Hata hivyo, inategemea na wahusika. Wapo wanaoweza kuchukia talaka na kuhakikisha watakapokuwa na kufunga ndoa, hawatapenda kupitia waliyopitia. Pia, wapo, hatujui tuwaiteje wanaoweza kuona talaka kama jambo la kawaida.
Tutatoa mfano wa rafiki yetu toka Jimboni Darfur, Sudan. Huyu bwana ana mke mmoja. Kanada, ndoa za mitala  haziruhusiwi. Ajabu, huwa halali kitanda chumba wala kitanda kimoja na mkewe. Siku moja walitutembelea kama familia ya kulala kwetu. Ilipofika wakati wa kulala, tuliwaandalia chumba mke na mume Pia, kuwaandalia watoto wao vyumba viwili tofauti. Bila hili wala lile, wanandoa walituita kona. Walisema vyumba vitatu tulivyowatengea vilikua vingi. Walihitaji viwili tu. Tulishangaa. 
Tuliuliza kwanini wakati walikuwa wana watoto jinsia tofauti ambao tusingewalaza chumba kimoja. Walijibu kuwa watoto wa kike wangelala na mama yao, na wa kiume wangelala chumba kimoja na baba yao. Hatukuwapinga. Ila tuliwashangaa.
Zamu yetu ilipofika kuwatembelea, walitupangia vyumba viwili badala ya vitatu. Walitushangaa tulipouliza ni kwanini? Marafiki hawa walisema kuwa, kawaida, hawalali mke na mume pamoja. Tulishangaa hakuna mfano.
Hata hivyo, katika kuwadurusu kujua ni kwanini hawalali chumba wala kitanda kimoja, mume alijibu kuwa walikuta wazazi wao wakiwa na utaratibu huo. Katika kuzidi kuwadurusu, tulishangaa kugundua kuwa wazazi tajwa walikuwa na wake wengi. Hivyo, kwa kuzingatia kuwa waliishi kwenye vijumba vidogo vilivyojengwa sehemu moja ndani ya boma moja. Baba alikuwa na kijumba chake ambapo kila aliyemhitaji huenda kwa zamu kupata chakula cha usiku.
Tulizidi kushangaa ni kwanini wawili hawa waliamua kulala mbalimbali wakati ndoa yao ilikuwa ya mke mmoja. Jibu tulilopewa ni “tulikuta hali hii.”
Je, tukirejea kwenye talaka, hii inafundisha nini? 
Funzo la kwanza ni kwamba watoto, mara nyingi, huathiriwa na matendo na tabia za wazazi.
Pili, tuligundua kuwa kuna mambo watoto hufuata bila kuyapinga wala kuyadurusu na kujua maana na sababu zake.
Hivyo, basi, linapokuja suala la talaka, yawezekana kabisa watoto wa wataliki wakaona ni jambo la kawaida kiasi cha kutoona madhara yake kwao.
Kama tulivyogusia hapo juu, pia wapo wanaoweza kuichukia talaka wakaitahadhari katika maisha yao ya utu uzima. Maana, hata katika kisa cha marafiki zetu hapo juu, tuliambiwa kuwa wapo Wadarfur wanaolala kitanda kimoja na wake zao hasa wawapo kwenye nchi kama Kanada zisizoruhusu mitala. Tuliwabana na kuwauliza ni kwanini hawa hawafuati mila. Majibu yalikuwa tofauti. Walisema hii ni kutokana na usomi au kuiigiza ukristo na uzungu.
Je, ukiachia mafunzo tuliyotaja hapo juu, wewe unajifunza nini? Unawahukumuje hawa wanaofuata mila bila kuhoji? Je, wewe unayo mila gani uliyorithi kwa wazazi wako ambayo yaweza kuwa hasi na bado ukaifuata au ukaikataa?
Tukiachia mbali madhara ya kimahusiano, talaka yaweza kuwa chanzo cha ukosefu wa amani na raha kwa watoto. Kwani, huishi kwenye mvutano wa nani wawe naye baina ya wazazi wawili walioachana. Tunaye rafiki yetu ambaye ni tajiri wa kupigiwa mfano. Huyu baba alitalikiwa na mkewe. Wanao watoto wanne wa kike wawili na wa kiume wawili watu wazima. Kati yao, ni mmoja tu ameolewa. Katika maongezi naye mara nyingi, huwa anasema kuwa Watoto wake watatu ambao hawajaoa wala kuolewa huwa hawapendi kujadili suala la ndoa na yeye.
Pia, Watoto wake huwa wanaepuka kutaja majina ya baba au mama yao wala mambo yao kulingana wako nan ani. Jambo hili, haliwaathiri Watoto tu bali hata baba yao. Kwani, siku zote ana wasiwasi kuwa talaka yao imewaathiri vibaya watoto wao. Hayo ni machache tunayoambiwa. Kwa mujibu wa wataalamu wa mahusiano, ndoa, na saikolojia, yapo mengi hata ya kiakili na kiafya kwa ujumla kama msongo wa mawazo, chuki zisizo na sababu, hasira, upweke, na mengine mengi.
Ni vizuri kujua. Talaka ni hatari.
Chanzo: Mwananchi Jpilil leo.

No comments: