Juzi, nilipiga kanywaji hadi kakanifyatua nikafyatuka nusu Bi Mkubwa anifyatue. Si mmeona wenyewe aina mpya ya ufyatuaji wa kulinda ufyatuaji kwa kufyatuana kinamna? Mafyatu wagomapo kufyatuka na kuwafyatua wawafyatuao, jua watafyatuliwa ile mbaya. Hii ni kutoa fursa ya wafyatuaji kufyatuka na kufyatuana ili wajenge mazingira safi ya kuendelea kuwafyatua mafyatu waliogoma kufyatuka na kufyatua.
Katika kigwena kilichojiri hivi karibuni kule nonihino, nilishangaa kuona wezi wakifukuza wenzao ilhali lao moja. Sikujua kuwa fisi wanaweza kufyatuka na kufyatuana hadi mafyatu au tuseme kondoo wakajisahau na kuacha kuwafyatua wasiwamalize. Sijui tunaelewana?
Ukiwa sehemu ya wafyatuaji wawafyatuao mafyatu ukajifyatua, unafyatuliwa kabla ya kuwafyatua mafyatu mnaoshirikiana kuwafyatua mafyatu wasiofyatuka. Ukipiga kelele, unafyatuliwa. Ukipingapinga hovyo, unafyatuliwa. Ukilaani, unafyatuliwa. Ukikataa kufyatuka na kusifia, unafyatuliwa. Hata wakati mwingine ukisifu kifyatufyatu bila busara unafyatuliwa. Ni kama ile hadithi ya njomba. Nyani akikruka, nchale. Akilala, nchale. Ni nchale kwenda mbele. Ni kufyatuka na kufyatuana mtindo mmoja.
Yote katika yote, ufyatu upo wa aina nyingi. Upo ule wa kufyatuka na kupinga ufyatukaji na ule wa kufyatuka na kulinda ufyatuaji. Hata hivyo, ufyatu huu, uwe wa nia nzuri au mbaya, una gharama zake. Kama kenge akiingia kwenye kundi la mamaba, ajue. Atafyatuliwa akafyatukie mbali. Huwezi kuwa ndani na nje kwa wakati mmoja. Wala huwezi kupenda na kupenda sawia. Nani aweza kutegemea kupata kivuli kinene toka kwenye mti mwembamba? Hata ajifyatueje, fisi hawezi kuwa kondoo wala kondoo kuwa fisi. Ndoa ya samaki na ndege haiwezekani kwani waishi mazingira na maisha tofauti.
Kadhalika, ndoa ya wafyatuaji na wafyatuliwao haipo na kama ipo lazima wafyatuliwaji wajue watafyatuliwa hadi wakome wasipofyatuka. Nani kakufyatua ukafyatulika kuwa maji na moto vinaweza kukaa kiti kimoja? Wafyatuliwaji na wawafyatuao wanaweza kukaa kaya moja iwapo wafyatuliwaji watagoma kufyatuka hadi wakaruhusu wawafyatuao waendelee kuwafyatua kama ilivyo.
Kwa vile wale waliofyatuka bila kufyatua wakaishia kufyatuliwa, tutegemee nini zaidi ya kufyatuliwa zaidi kwa sababu hamtaki kufyatuka na kuwafyatua watufyatuao na hata kufyatuana kwa vile tumegoma kufyatuka na kuwafyatua. Raha ya ufyatu si kufyatuka tu bali hata kugoma kufyatuka ukafyatuliwa. Linakuijia fyatu chafu likikuhimiza uwe msafi! Jingine linafyatua njuluku za mafyatu halafu linajifyatua na kutoa ahadi za kufyatua wezi! Hamuoni mifyatu inayowafyatua mafyatu na kula kwa mikono na miguu tena bila kunawa halafu linajifyatua na kuwafyatua mafyatu kuwa linawajali? Mengine yanawafyatua mafyatu na kujihudumia yakidai yanawahudimia mafyatu ilhali yanawafyatua! Dunia hii japo gunia, imefyatuka na kugeuka ya ufyatuanaji.
Hakuna kilichonifyatua, kunisononesha, na kunitisha kama kuona Mafyatu waliopaswa kuwa sauti ya wasio na sauti kuiingizwa kwenye ufyatuaji wa wale wasio na sauti. Yamejipa sauti ya kuwafyatua wasio na sauti. Hamshangai kuona fyatu lililobukua kuishia kujifyatua na kusema na kusifia hata uchafu? Hamjaona mafyatu masomi yakisifia maamuma ilmradi yapate fursa aya kuwafyatua mafyatu wengine wasiofyatuka na kufyatua?
Kama mafyatu wapaswao kuwatetea wasio na sauti yanajifyatua na kufyatukia ulaji uchwara uwaminyao na kuwanyima sauti wasio na sauti, sijui nani atawasemea hawa Mafyatu wasio na sauti waliofyatuliwa na Mafyatu wenzao waliopaswa kuwafyatua wafyatuzi? Ukiona jambazi na ndata wamefunga ndoa, jua umefyatuliwa. Ukiona wenye macho wanafyatuliwa na vipofu, jua wenye macho yatatobolewa ili msione huu ufyatuaji wa kunuka ambapo tumbo hufyatua kichwa na kichwa kikaacha kufyatuka na kulifyatua tumbo.
Nilishangaa kuona na kusikia mafyatu wawafyatuao mafyatu wakanona kama nune wakiwasihi mafyatu wafunge mikanda kwa vile mambo yamekuwa magumu. Kama kweli mambo ni magumu hivyo, hawa mafyatu wenye matumbo na makalio makubwa wanafyatua nani na nini zaidi ya mafyatu wawafyatuao kwa kuwahimiza wafunge mikanda. Kama kufunga mikanda ni dili na heri, kwanini hawa watufyatuao kwa kutuhimiza tufunge mikanda wasianze ili kuongoza kwa mfano? Ni uongozi gani anbapo kiongozi hukaa nyuma badala ya mbele? Msitugeuze meli na ngarawa ambapo nahodha huongoza kwa kukaa nyuma. Sisi si simaki kufyatuiwa tukijiona kwa kuwekewa chambo tena chambo chenyewe ahadi na maneno matamu. Jamani, maneno hata yawe matamu na mazuri kiasi gani, hayaliwi. Mengine yanatujia na maono. Hatutaki maono. Tunataka vitendo tena vinavyoingia akilini na si vya kujifyatua na kufyatua akili.
Wakati wafyatuaji wa mafyatu wakifyatuana ilipaswa kuwa fursa kwa mafyatu kuwafyatua wakifyatuana juu ya kuwafyatua wao kwa vile hawafyatuki. Ni fursa ya fyatuaneni tuwafyatue badala ya kufyata kama mnavyolenga kutuaminisha ili muendelee kutufyatua kwa kujifanya mnafyatuana wakati lengo ni kutufyatua sisi tusiofyatuka na kuwafyatua tukabakia kufyatuana na kufyatuliwa. Kama wewe ni kondoo, ukiona fisi wanafyatuana, fyatuka haraka kabla hawajakufyatua. Ukiona adui wako anafanya makosa, usijifyatue na kumkosoa. Utampa fursa ya kukufyatua ufyatukie mbali.
Nitamatike kwa kufyatuka kuwa ukiona wafyatuaji wakifyatuka na kufyatuana, nawe fyatuka wasikufyatue kabla hawajakufyatua ukafyatukia mbali.
Loo! Sasa naanza kufyatuka!
Chanzo: Mwananchi J'tano leo.
No comments:
Post a Comment