The Curse for Salvation

The Curse for Salvation

Monday, 7 September 2026

Tamu, Chungu kutafuta wenza mtandaoni


Kisa cha baba mmoja toka nchini Saudia aliyetaka kuoa na akaamua kutafuta mchumba mtandaoni kinafundisha. Baba huyu toka familia tajiri na inayoheshimika aliona picha ya mrembo mmoja toka nchini Misri. Alimpenda na kuamua awe mkewe. Hivyo, alifanya mawasiliano na binti ambaye pia alionyesha kumpenda mhusika. Wawili walianza mawasiliano hadi baba akawajuza wazazi wake azma yake. Wazazi hawakumkatalia japo walionyesha shaka juu ya mke wa mtandanoni.
            Baada ya wawili hawa kukubaliana, mchumbiaji alitozwa mahali ya dola laki saba na akazitoa cash kwa alivyompenda yule binti. Bila kujua, kumbe huko nyuma ya pazia, wazazi wa Kimisri walipanga wamuozesha dada mtu ambaye alikuwa na makengeza. Siku ya siku ya jamaa kwenda kuipua jiko lake ilifika. Alisafiri kwenda Misiri. Lahaula! Jamaa alipofika hakuamini macho yake kwa alichokikuta.
            Baada ya kugundua kuwa mchumba aliyemuona mtandaoni ni tofauti na yule aliyetaka kupewa, jamaa alikataa katakata na kutaka arejeshewe pesa yake. Mgogoro mkubwa ulizuka hadi Saudia kuingilia kati. Kumaliza mgogoro, wazazi walipaswa kumtoa yule aliyeona picha yake.
            Tukiacha kisa hicho, kuna visa vingi kama hivi vimetokea kimoja kikimhusisha mzee toka Austaralia aliyetaka kuoa binti wa Kiafrika. Mzee wa watu aliingia mtandaoni na kuona picha ya binti aliyempenda na kuanza kutupa nyavu na akakubaliwa hadi kufunga safari hadi Nigeria. Bila hili wala lile, kumbe jamaa alikuwa akiwasiliana na matapeli wa kinegeria waliompokea uwanja wa ndege na kumteka na kumtaka aanze kuagiza pesa toka kwao. Jamaa alitii hadi amamlaka zilipogundua na kuingilia kumuokoa baada ya kunyonyolewa pesa kibao na mateso mengi.
            Hapa Amerika ya Kaskazini kuna visa vingi vya wanaotafuta wachumba mtandaoni hasa wanawake watu wazima au wajane matajiri. Wengi wamelizwa maelfu hata mamilioni ya dola kiasi cha serikali kuinglia kati.Kwa mfano, mamlaka za kipolisi za Kanada Royal Canadian mounted Police kitengo cha kuzuia utapeli,  mwaka 2021, lilitoa takwimu kuwa lilipokea malalamiko 1,249 ya utapeli wa kimapenzi mtandani toka kwa wahanga 925 ambao kwa pamoja walipoteza zaidi ya Dola za Kanada milioni 50. Hali ilikuwa mbaya nchini Marekani mwaka huo ambapo mamlaka ziliripoti kuwa wahanga walipoteza takriban Dola za Kimarekani 547.
            Mbali na visa hivyo, siku hizi kuna filter. Utakuja binti anachezea picha zake na kutengeneza mtu tofauti na alivyo ili kuwapata watafutao wachumba mtandaoni. Wengi wameingia uhusiano huu na kuuvunja pindipo wawaonapo wahusika.
            Tujiulize swali. Inakuwaje mtu anakosa mchumba mtaani, mkoani, hata nchini mwake hadi ategemee kumpata mtandaoni kama siyo kutafuta hasara, majuto, na matatizo? Kuna wahanga wengi wamejuta hata kuumizwa na wengine kuuliwa wakisaka vimwana mtandaoni. Tumewahi kuelezea kisa cha binti wa kikenye aliyefunga safari hadi Amerika ya Kusini akimfuata 'mtarajiwa' wa mtandaoni akaisia kutekwa, kudhalailishwa hadi wazazi wake wakaingilia na kuchangishana kumrejesha Kenya kwa machungu na majuto. Baya zaid, kwa tamaa ya kuolewa na mtu wa majuu, binti alimkataa mchumba aliyekuwa amempata kwao na wakapendana akaishia majuto.
            Kwa upande wa pili, wapo waliowapata wachumba wa mtandaoni wakawa wake au waume wema kulingana na walichokuwa wakitafuta. Wapo wamepata wanaume wa kizungu wakawaoa na kufanikiwa kwenda majuu na kuukata na wengine waliooa wanawake wa kizungu kadhali japo ikilinganishwa na walioula wa chuya, waliofanikisha walichokitaka ni wachache.
            Tujiulize. Kwanza, unajiaminisha vipi kuwa yule unayewasiliana ni yeye na si mtu bandia? Je, unamchunguzaje tabia hata mambo mengine kama afya, mila, magonjwa ya urithi na mengine kama hayo? Japo wapo waliopata na kupatikana, wachumba wa mtandaoni ni changamoto na wanahitaji watu wanaochukua risk ima tokana na ujinga, ulimbukeni, na imani kibubusa. Wahenga waliasa kuwa hisani huanzia nyumbani.
             Kwa wanaotafuta wachumba wakweli na wanaofaa, mtandaoni si mahali salama kufanya hivyo. Kufanya hivyo ni sawa na samaki kutamani kupata rafiki jangwani. Pia kuna usemi kuwa ndoa ya samaki na ndege haiwezekani tokana na makazi na maisha ya wahusika.
            Tuhitimishe kuwa, japo uamuzi na uchaguzi wa wapi pa kumpata amtakaye ni wa mtu binafsi, kuna haja ya kutahadhari mahusiano ya mtandaoni tokana na changamoto nyingi kati ya chache tulizogusia.
Chanzo: Mwananchi J'pili jana.

No comments: