Wednesday, 10 September 2008

Naota naongea kama Mkuu!

HUWEZI kuamini niliota nikiwa rais tena wa nchi ya mawazo ya Tanzia.

Eti niliwaingiza mkenge Watanzia kwa kusamehe washirika wangu kwenye ulaji wa WEPA na kutimkia kwa Joji Kichaka ‘kujinoma’ na kutumbuizwa na marafiki zangu wa Boyz II Men. Mambo yalitibuliwa na shutuma za kutaka kuni-impeach ule mtindo wa Pakistan.

Nikiwa na Salama wangu tukila mikuku, mi-turkey (bukini) na mahanjumati, nilipata habari hii mbaya. Ingawa nimechukua tahadhari zote kuliepuka hili, wanoko wanazidi kunichimba.

Wanasema eti ule mdege wangu wa matanuzi ni wa bei mbaya na mkangafu! Eti uuzwe! Hawana adabu wana hizaya hawa.

Nimeliona hili kwenye ziara yangu kwa Joji Kichaka. Yeye ana Heir Fosi I. Mie nitakuwa na Heir fosi II. Mpo hapo wakosoaji? Watu wetu wapumbavu. Badala ya kujisifu wana dege la bei mbaya kuliko nchi zote barani waleta umbea na wivu wa kike!

Kuzidi kunichefua na kunichonganisha na watanzia eti wanadai na ile rada ya kulinda usalama wa taifa ni mkangafu. Waongo wakubwa. Bila rada ile hawajui nchi ingekuwa imeishavamiwa na maadui zake walioizunguka kila upande chini juu kushoto kulia nakadhalika?

Mie si akina Kikwekwe, sorry, Makapu bwana. Wao walinunua mrada huu kwa bei mbaya. Mie sinunui mwingine. Nanua betri.

Wapo wanaodai eti rada hii haiwezi kuona hata wingu inataka betri ya shilingi bilioni kumi? Eti wanadai ni kwa nini tusiweke betri za gari au hata za radio kuliko kuwaibia wachovu bure? Hata rada ingekuwa aihitaji betri lazima sisi tuhitaji hizo betri. Kwani tunakula mawe?

Mlinipa kula mkadhani ni kura. Sasa nakula nanyi mnaliwa mnaanza kupiga mikelele. Kwani nilijichagua? Kwani sikuwapa takrima? Hamuoni ninavyositasita kuwasulubu marafiki zangu katika ulaji mkuu wa EPA na Richmonduli?

Kama si wao na misheni zao mnazoita ufisadi mnadhani ningekuwa hapa nilipo nikifaidi na kufaidika? Shauri yenu. Mmeshikilia ‘yangu yangu’ kama vyura sisi tunatesa nanyi mkiteseka.

Juzi niliona umbea kwenye magazeti eti Tanzia ina mimali kibao hasa madini. Nyinyi yanawahusu nini? Nilisikia mimbea mingine ikidai nirejeshe yale machimbo ya makaa ya mawe yaliyokwanyuliwa na rafiki yangu Tunituni.

Ebo! Hivi mna akili kweli! Nyie tafuteni vitumbua. Mambo ya madini na makaa ya mawe hayawahusu. Nani ana jiko la kupikia mkaa wa mawe?

Kuna minoko inayonitaka nitangaze mali zangu na za Bi. Mkubwa. Hawa hawitakii Tanzia amani. Nani mjinga atangaze utajiri wake kabla ya NGO za Bi. Mkubwa kutiki?

Mwadhani mie juha na mvivu wa kufikiri kama nyinyi? Sitaji. Sifanyi upumbavu wa Tunituni aliyetawatajia mali zake halafu akakwapua na sasa mnamsulubu hadi mie nimpe tafu.

Wapo wanoko wanaotaka nipunguze au kuacha utalii nje ya nchi. Ama! Hivi hawa wana akili kweli? Nisipoizunguka dunia hii kama Christopher Columbus mnataka nifanye hivyo kaburini? Haachi ziara mtu hapa.

Hamjui nikikutana na washikaji wangu kama Joji Kichaka hadhi yangu na ya nchi inapanda kama alivyowahi kuwambia msemaji wangu aliyewageuka baada ya kumpa mabaki ya mapupu na jengelele.

Mna wivu wa kike nyie hata Bi. Mkubwa anawazidi anatengeneza njuruku kupitia mgongoni mwangu. Sifanyii biashara uchwara ikulu. Bi. Mkubwa ndiye anafanya hivyo.

Na anafanya waziwazi taka mistake. Ataogopa nini iwapo hamkumchagua wala hakuapa kuwatawala zaidi ya kuwala mgongoni mwangu?

Mimi si bwege kama Tunituni. Yeye aliwapigia kelele na kujisifu uongo na unafiki. Mie nakaa kimya. Hamjui simba mla nyama ni yule mkaa kimya kama mimi?

Kwanza mie ni bonge la mjanja kama yule rafiki yangu mtoto wa mjini aliyemdedisha mtu nikampa tafu hadi mauti yanamtwaa.

Mimi kipenzi cha watu hasa mafisadi. Nina mwenye upendo. Sijawahi kuua hata inzi. Nitaua wanini iwapo uchafu wa kula uko mwingi?

Hata nyinyi mnaodai naihujumu nchi kwa kuwakingia kifua mafisadi mnakosea. Inapaswa mniombe radhi. Nchi mnaihujumu wenyewe kwa kulalamika badala ya kufanya kweli.

Wapo wajinga wanaodai maisha yangu ya kifalme yanasababisha umaskini kwao. Ebo! Kwani mimi si mchungaji kuchunga kondoo nisinywe maziwa na kula nyama yao?

Umaskini wenu hausababishwi na ufalme wangu wala maisha yangu. Ni matokeo ya uvivu wenu wa kufikiri. Mzee Musa aliwahonya. Enyi Watanzia wapumbavu nani aliwaroga ambao kila kitu kiliwekwa mbele yenu?

Hamkutujua wanasiasa tunaweza kupayuka na kuahidi lolote tusifanye kitu! Sisi ni wasanii. Hatuna tofauti na mafarisayo. Tunawatwisha watu mizigo na mikenge sisi tukinema bila mzigo.

Wajinga wanauliza iko wapi safari ya Kanani. Ebo! Mmeambiwa mimi ni Musa? Mbona alikufa zamani na Haruni aliishaachana na siasa anakula pensheni yake?

Kwanza sikuwaahidi kuwapeleka Kanani. Nani awapeleke kwenye vita ya Wapalestina na magaidi wa Kimarekani? Ningepata wapi pasipoti kwa watu wote?

Kwanza niwape somo. Mlifanya kosa kubwa sana. Hamkumbuki mlinichagua kwa vile nina sura nzuri? Mzee Musa aliwaonya: hamkuwa mnatafuta Miss Tanzia.

Kwa kiranga na ujaha mlimdharau na kupuuzia wasia wake. Sasa yanawakuta mnaanza kulalama. Kwani uzuri wangu umepungua? Mnataka ningeze mkorogo tena? Mbona najiona nimechanika huku Bi. Mkubwa akikaribia kupasuka!

Ngoja nijisifu kidogo. Ninaye mke mwenye kuvutia. Ana akili sina mfano. Ameanzisha biashara kuwasaidieni wake zenu waondokane na umaskini.

Tunatembea dunia nzima pamoja akisaka misaada kuwainua wake zenu. Watu wasioitakia nchi maendeleo wanadai atakula pesa yenu. Jamani ale pesa gani iwapo mume wake anayo pesa nyingi mnayomlipa?

Mke wangu hana shida kama wale waliotutangulia. Yeye ni mzalendo wa wazalendo. Ndiyo maana, kutokana na kujua hili hata hatuna haja ya kutaja mali zetu ambazo kimsingi ni zenu. Tunaomba mzidi kutuaminini ndugu zetuni.

Wanoko wanasema nawakingia kifua mafisadi. Hawa hawajui siasa za kisasa. Hawa wanataka kuvuruga mshikamano ‘wetu’ na kuhatarisha usalama wa taifa. Hawajui ninaongoza sirikali wanayoiita serikali!

Jamini ee! Nawaletea habari njema. Yule kijana Mapepe tumemkomesha. Hana nidhamu kutwambia hatuna nidhamu na tunahujumu watoto.

Kwa ajili ya usalama wa chama na taifa, tumeamua kumjadili na kumchukulia hatua za kinidhamu kwa kutaka kuingilia na kuhatarisha ulaji wa wakubwa.

Ala! Kumbe naota?

Chanzo:Tanzania Daima Septemba 10,2008.

1 comment:

Anonymous said...

Mwanangu unatisha kama ukoma. Falsafa yako iko juu na mbali. Heri mafisadi wasikie na kuelewa wakikubali kuwa siku zao zimeisha hata kama ni mkuu.
Kazi yako imetukuka na kuvuka mipaka.Tunafarijika kuona tuna watu wenye visheni namna hii.
Lugha nyepesi kwa mambo magumu si mchezo kisanaa.
Endeleza mapambano.
Badawi
Kisauni Mombasa Kenya