Wednesday, 19 November 2008

Huu nao ni ufisadi tena unaonuka

JUZI nilikuwa najikumbusha zama za Musa tukiwa Kanani. Nilikumbuka nikiwa Ubayani Sekondari nimetinga kwenye kaptula yangu na shati jeupe bila kusahau viatu vyeusi maarufu kama 99. Usishangae 99 ukadhani ya polisi. Viliitwa ‘nine nine’ kwa sababu viliuzwa shilingi 99.

Wakati huu fedha yetu ilikuwa fedha si fedheha ya EPA wala madafu, ukipewa mia mbili za Masai unakata muhula mzima. Ila ikumbukwe kuwa wakati ule kusoma ilikuwa dili, ‘No’ mambo ya kikubwa kwa watoto wadogo, bwimbwi, video za ngono na action uchwara, chips wala tuition za wizi.

Wakati ule hata ‘glosari na guest houses’ za karibu na mashule hakuna. Hapakuwa na kughushi vyeti wala kuiba mitihani, hapakuwa na mafisadi tunaowaona wakibembelezana kurejesha mshiko wa wizi. Nchi ilikuwa nchi na rais alikuwa rais kweli. Nchi ilikuwa ikiongozwa na viongozi siyo kutawaliwa kama punda, mbuzi kuku na kondoo na wabangaizaji.

Zama zile ukichaguliwa kuingia ‘fomu wani’ ni dili, siyo kama leo pasipo na ujiko. Usomi ulikuwa ni kama utume lazima msomi uonyeshe sifa njema.

Hatukuwa na wauza unga, hatukuwa na mambo ya kudaiana karo kama sasa. Mzee Musa alihakikisha tunazaliwa na kusoma bure ili hapo baadaye tulijenge taifa.

Ukiingia fomu faivu ndiyo usiseme. Nakumbuka zama zile unapewe ‘traveling warrant’ yako tayari kwenda zako Milambo, Mkwawa au Mazengo. Wakati ule hizi shule zilikuwa shule siyo mchezo.

Ukimaliza high yako ukapasua unatua zako Mlimani kabla haijageuka Manzese University. Zama zile Mlimani ulikuwa mlima kweli wa mawazo, hapakuwa na dada wa vimini kama sasa wala kaka wa mapanki na vihereni kama leo. Pale ilikuwa ni sehemu ya kuchemka si mchezo.

Mlimani nako huwezi kuamini, ilikuwa ni mzee Musa aliyelipa kila kitu na kukupa hata za kupata kitambi kidogo ili ukirejea Uswekeni wajue wewe ni msomi wa mbolea na haja kweli kweli.

Nikiwakumbuka wenzangu tuliokuwa nao maeneo ya Kibaha kama jamaa yangu mmoja tukisoma bure na kula bure wanavyowageuzia kibao vijana wetu, napata hata kichefuchefu cha akili kusema ukweli. Dk. Son of Kyembe nadhani anakumbuka tulivyotesa Milambo Na baadaye Mlimani kabla hajaenda Ujerumani nami Urusi.

Zama zile ukiachia digrii ya kwanza ujue una lako. Ama kichwa hakichemki au unawahi kibarua ili uwasaidie wazee, maana fedha ya kusomea ilikuwa nje nje na mzee Musa alisisitiza tusome ili tujenge nchi yetu tusije tukaibomoa kwa kutumia elimu ile ile aliyotupa bure kutokana na wazazi wetu kuwa Apeche alolo!

Wakati ule hapakuwa na ajira wala shahada za chupi (Godfather). Hapakuwa na wabunge vitaahira na vihiyo kama sasa. Nakumbuka siku zile mzee Musa alikuwa na fedha kidogo lakini aliisimamia kuhakikisha wana kaya wake wanapata kila wanachopaswa. Mzee Edwin Mtei analijua hili, nani angeingia banki kuu kujiepea kama sasa?

Angefanya hivyo, hiyo fedha angeitumia wapi? Hapakuwa na takrima wala mtu kulala maskini akaamuka tajiri asibanwe mbavu kueleza alivyo na alikopata hiyo fedha. Wakati ule hata magabacholi walikuwa Apeche alolo. Ikulu ilikuwa patakatifu pa patakatifu siyo pachafu pa pachafu kama ilivyokuja kuwa baada ya mzee kuishia.

Wakati ule, mzee Musa alikuwa mchumi sina mfano. Aliweza kutusomesha pamoja na wageni kama Yoweri Museveni na John Garang de Mabior na wengine wengi ili waende kuzikomboa nchi zao ingawa baadhi yao wamegeuka manung’ayembe na madikteta.

Si kwamba tulikuwa mazuzu, hasha, tulikuwa tukimpinga kwa hoja. Spika Six analijua vizuri sekeseke tulilopewa na Mzee Musa tulipojichanganya kwa kuigiza wenzetu wa nchi za kibepari kwa kutaka makuu yasiyo na maana. Nani angegoma hovyo hovyo ilhali haki ilikuwa ikionekana ikitendeka? Hatukuwa na wabunge wanaosinzia bungeni wala kughushi vyeti.

Zama zile tulijenga Ujamaa na Kujitegemea na siyo Uhujumaa na Utegemezi kwa wafadhili na wawekezaji uchwara na wezi.

Kumbuka. Kipindi kile dhahabu yetu ilikuwa haijaguswa wala Tanzanite ilikuwa haijagunduliwa.

Wazee wetu walichapa kazi hasa wakulima hadi wakachangishana tukasoma na kuzaliwa kwa neema na amani.

Ingawa hii ni historia, kuna ukweli kuwa huwezi kuwambia vijana wetu kuwa huna fedha tena ya kuwakopesha siyo kuwasomesha ilhali ukitoa ofa na misamaha kwa wezi wa kigabacholi na wachukuaji unaowaita wawekezaji.

Haiingii akilini. Ima uwe mwehu au wale unaowadanganya ilhali wakikuona ukiwabembeleza wezi wa EPA warejeshe chumo la wizi. Haiwezekani na haitawezekana hata kwa mtutu wa bunduki.

Zama zile tulifundishwa ukombozi, usawa na uadilifu siyo uwekezaji, unywanywa na ulamba viatu. Tulikuwa tumekomboka kweli kweli. Tulipomaliza tulikwenda jeshi la kujenga taifa na siyo kama sasa kujiunga na makundi ya kulibomoa.

Nakumbuka wakati ule tukila mikate safi na mayai ya kienyeji na siyo mazagazaga ya kisasa tena kwa fedha ya kukopa. Meza na viti vilijaa kila darasa siyo kukalia mawe na kusimama wakati wa masomo na lecture.

Vitabu vya kiada na ziada vilikuwapo na tulivisoma tena kwa mashindano. Tuliotea kuwa viongozi na siyo wazungu wa unga na wanasiasa nyemelezi. Tulilala kwa kujinafasi sana na siyo kubanana kama maharagwe kwenye magunia kwa sasa.

Tukirejea kwa Mzee Musa, hapakuwa na mabepari na matajiri uchwara watokanao na ujambazi wa kuuibia umma. Tulikuwa Kanani kabla ya kurejeshwa Misri na Gendaeka wachache waliotukamata mateka hadi leo baada ya mzee kuondoka.

Uongozi ulikuwa utumishi wa umma na siyo kuutumia umma kuchuma na kuvuna usipopanda kama ilivyokuja kuwa baadaye. Viongozi walifanana na waongozwa na watawaliwa wakijivunia kufanana na waliowaongoza. Viongozi walionyesha njia na siyo kuzungumzia juu yake.

Miiko ya uongozi ilitawala na siyo uongo na ubabaishaji. Kila kiongozi alitaja mali zake mkewe na familia yake tena bila kulazimishwa wala kuzungusha zungusha. Tuliishi kama familia na jamii ya watu na siyo mrundikano wa majambazi na vinyama vya mwitu vilivyotayari kuwauza hata wazazi wao.

Wanangu isomeni historia hii tukufu ili msinyimwe na kudhulumiwa haki zenu. Heri kuishi siku moja kama simba kuliko miaka mia kama kuku au mbwa. Heri kufa umesimama kuliko kuishi umepiga magoti.

Nanyi muwahujumuo watoto, jueni siku zote hazifanani. Jogoo wa leo ni kifaranga wa jana, ila msiwe kama jogoo kuwafundisha vifaranga kunya ndani.

Jamani mmesikia rongo rongo za jamaa wa taasisi ya kupamba na kukuza rushwa? Eti kaya inaogopa kuwafikisha kwa Pilato majambawazi wa HEPA kwa sababu inaweza kuyumba! Ebo hamuogopi umma mnaogopa mafisadi. Hovyo.

Kila la heri na tieni akilini.

Chanzo: Tanzania Daima Novemba 19, 2008.

1 comment:

Anonymous said...

Enzi zile pia, pale mlimani ulikuwa hukuti mwanachuo zaidi ya kuwa na vihereni hakuna ambaye alikuwa na rasta, au sio?