Thursday, 22 October 2009

Wajue vigogo vihiyo na matapeli


Pichani ni Smuel Chitalilo (Bingwa wa kughushi), David Mathayo David, Victor Mwambalaswa, Emanuel Nchimbi, Raphael Chegeni,Makongoro Mahanga,Mary Nagu, William Lukuvi na Diodurus Kamala.
Hatukuweka shahada zao kutokana na kuwa na ugogoro-Adminstrator

Vyeti vyao vya elimu vyadaiwa vina utata
Yumo Mkuu wa Mkoa na wabunge watatu
Orodha yawasilishwa kwa Spika wa Bunge
Dk. Mary Nagu Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko.
Dk. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT)
Dk. Makongoro Mahanga, Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana.
Dr. David Mathayo David, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika.

Mawaziri sita na wabunge wanne, wametajwa kuwamo katika orodha ya watuhumiwa 19 wa walighshi vyeti vyao vya elimu.

Utafiti huru uliofanywa na Mwanaharakati, Kainerugaba Msemakweli kwa msaada wa Tume ya Vyuo Vikuu nchini (TCU), katika kipindi cha mwaka mmoja; umebaini kwamba wanasiasa hao wametumia vyeti vya kughushi na kuwasilisha katika ofisi za umma kwamba wana elimu hiyo, kitu ambacho si kweli.

Utafiti huo ulianza kufanyika Juni 25, mwaka jana hadi Oktoba 9, mwaka huu katika nchi za Marekani, India na Uingereza, ambako vigogo hao wanadaiwa kuwa walisoma na kupata shahada hizo.

Baada ya kubainika kwamba hawana sifa za elimu wanazodai kwenye wasifu wa elimu zai, ripoti hiyo imekabidhiwa kwa Ofisi ya Spika wa Bunge.

Kuwasilisha nyaraka za kughushi katika ofisi ya umma ni kinyume cha Katiba na sheria za nchi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Msemakweli aliwataja mawaziri hao kuwa ni Dk. Mary Nagu (Viwanda, Biashara na Masoko), na Dk. Diodurus Kamala (Ushirikiano wa Afrika Mashariki) kuwa miongoni mwa vigogo wanaohusika na kashfa hiyo.

Pia, kuna waziri mwingine mmoja ambaye jina linahifadhiwa kwa sababu hatukuweza kumpata kuzungumzia tuhuma zake jana.

Mbali na hao, pia Msemakweli aliwataja manaibu waziri, Dk. Makongoro Mahanga (Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana), Dk. David Mathayo David (Kilimo, Chakula na Ushirika) na Dk. Emmanuel Nchimbi (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa-JKT) kuhusika na kashfa hiyo.

Wabunge, ambao wametajwa na ripoti hiyo, ni pamoja na William Lukuvi (Ismani-CCM), ambaye pia, ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Victor Mwambalaswa (Lupa-CCM) na Dk. Raphael Chegeni (Busega-CCM).

Kuna mbunge mwingine ambaye pia alitajwa kwenye kashfa hii na kwa kuwa jana hatumpata kuzungumzia suala hilo, jina lake tumesitiri kwa sasa.

Vigogo hao wanadaiwa kuwa walighushi taaluma kwa baadhi yao kujiwasilisha kuwa wana shahada za masuala ya kimataifa na diplomasia, biashara na utawala, wengine shahada za uzamili, udaktari wa falsafa, na wengine dhahada za ualimu nakadhalika, wakati si kweli.Msemakweli alisema katika taarifa aliyowasilisha kwa ofisi ya Spika aliomba iwawajibishe vigogo hao kwa kashfa hiyo.

Alisema vigogo hao waliwaghilibu wananchi wa majimbo wanayoyawakilisha na kuwafanya wapate ubunge na kwamba, kwa kutumia shahada hizo za kujipachika, wameweza kuaminiwa na kupewa nafasi za kisiasa na kiutawala.

Alidai ana ushahidi wa kutosha juu ya madai anayoyatoa dhidi ya vigogo hao kwani ameyafanya utafiti wa uhakika na kwamba, kigogo yeyote atakayehisi kuwa ameonewa aende kwenye vyombo vya sheria na yuko tayari kwenda kuthibitisha madai yake.

Alidai Lukuvi alighushi sifa za taaluma kuwa ni msomi mwenye shahada ya masuala ya kimataifa na diplomasia wakati elimu yake ni darasa la saba na ualimu wa shule ya msingi.

“Hajawahi kuingia darasa lolote la digrii (Shahada) wala kufanya mtihani wowote wa digrii wala kusoma digrii yoyote, wakati wowote, katika maisha yake yote na mahali popote duniani,” alidai Msemakweli.

Alisema wakati anaiwakilisha Tanzania nchini Namibia katika mkutano wa wabunge wa Jumuiya ya Madola, Lukuvi aliwasilisha taarifa za kuhusu taaluma yake kwa kudanganya kuwa yeye ni msomi mwenye shahada ya uzamili katika masuala ya biashara na uongozi.

“Taarifa za kweli ni kwamba baada ya kumaliza elimu ya msingi na kuishia darasa la saba mwaka 1975 Mheshimiwa Lukuvi alienda kusomea ualimu wa shule za msingi katika Chuo Kikuu cha Ualimu, mkoani Tabora,” alisema Msemakweli.

Alisema Dk. Mahanga “…ameghushi sifa za kuwa ana shahada ya uzamivu (daktari wa falsafa) wakati hajawahi kusoma shahada hiyo wakati wowote na mahali popote duniani”.

Msemakweli alidai Mwambalaswa ameghushi sifa za taaluma kwamba ana shahada ya uzamivu ya biashara na utawala (MBA) wakati hajawahi kusoma shahada hiyo.

Alidai Dk. Nagu ameghushi sifa za taaluma na kujiwasilisha kwamba ana shahada ya udaktari wa falsafa wakati hajawahi kusomea udaktari wowote na mahali popote.

“Yeye amesoma na kuishia shahada ya pili kwa kutumia shahada hiyo ya kujipachika ameweza kuaminiwa na kupewa nafasi za kisiasa na kiutawala wakati… Katika maisha yake hajawahi kusomea udaktari wa aina yoyote,” alidai Msemakweli na kuongeza:

“Amefanya …kumdanganya Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Taarifa katika Ofisi ya Mheshimiwa Spika na ambayo Mheshimiwa Spika anazo zinaonesha kuwa Mheshimiwa Mary Nagu ni msomi mwenye digrii ya daktari wa falsafa wakati hajawahi kusoma udaktari wowote katika maisha yake yote.”

Msemakweli alidai “Dk. Nchimbi ameghushi sifa za taaluma na kujifanya kuwa ana digrii ya Uzamivu (Ph.D). Hivyo kujipachika sifa za udaktari,” alisema.

Alidai Chegeni ameghushi sifa za taaluma na kujiwasilisha kwamba ana digrii ya uzamivu (Ph.D) na hivyo kujifanya dokta wakati hajawahi kusoma digrii yoyote ya udaktari au uzamivu, wakati wowote na mahali popote duniani na vyeti alivyonavyo kuhusu elimu hiyo ni vya kughushi.

Msemakweli alidai: “Dk. Mathayo ameghushi sifa za taaluma kwamba ana stashahada ya juu katika masuala ya mahusiano ya kimataifa wakati hajawahi kusoma stashahada au diploma hiyo wakati wowote na mahali popote pale duniani.”

Kwa upande wa Dk. Kamala, Msemakweli alidai: “Ameghushi sifa za taaluma kwamba ana digrii ya uzamivu (Ph.D) wakati hajawahi kusoma digrii hiyo, wakati wowote na mahali popote duniani.”

Nipashe iliwasiliana na vigogo hao, jana kupata maelezo yao na kwanza alikuwa ni Lukuvi ambaye alikanusha vikali kuwahi kusomea au kudai kwamba, ana shahada ya biashara na kusema kuwa: “Mtu anayedai hivyo ametia chumvi.”

Alisema aliyonayo ni diploma ya sayansi ya siasa kutoka Urusi na shahada ya taaluma ya Kimataifa kutoka Marekani.

“Sijawahi kusoma biashara na wala sina Masters (shahada ya pili) ya biashara. Kama ana ushahidi athibitishe,” alisema Lukuvi.

Dk. Mahanga alisema hayuko tayari kusema lolote kwa vile mtu aliyetoa madai hayo ahamjui.

Kwa upande wake, Dk. Nagu alipoulizwa na Nipashe, alisema: “Ngoja kesho niongee na mtu huyo kwani sasa hivi niko Morogoro, nitawasiliana naye kisha tutaongea Jumanne (kesho) .”

Dk. Nchimbi alisema: “Mimi sijamsikia (huyo mtu). Wewe mwenzangu umepata kumsikia. Mimi mpaka nipate bahati ya kumsikia.”

Dk. Chegeni alipoulizwa na mwandishi wa Nipashe juu madai ya elimu yake, naye alimuuliza mwandishi kuwa: “Mtu akikuuliza mimi ni mume wa mama yako utajibu nini?” Lakini mwandishi alipomtaka ajibu swali aliloloulizwa, aliongeza: “Kama mtu huyo amesema ana haki ya kusema.”

Mwambalaswa alisema watu wanaomhusisha na kashfa hiyo kama si katika kundi la mafisadi, basi watakuwa ni watu ambao walioshindwa kufuatilia kuhusu ukweli wa elimu yake.

Alisema shahada anayodaiwa kughushi aliipata kihalali katika nchi za Uholanzi na Uingereza.

Naye Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah alipoulizwa kama barua ya Msemakweli imefika katika Ofisi ya Spika, alisema kwamba, bado hajaiona.

“Nimesikia suala hilo leo asubuhi kutoka kwa waandishi wa habari. Mimi barua sijaiona. Sina uhakika, hivyo siwezi kusema lolote,” alisema Kashilillah na kuongeza kuwa Spika amesafiri.

CHANZO: NIPASHE

No comments: