The Chant of Savant

Wednesday 7 October 2009

Waraka wa Mpayukaji kwa wanakijiwe na walevi


BAADA ya wadau wengine kutoa nyaraka zao wakiwahimiza wafuasi wao wakiminye Chama Cha Maja-sorry, huku wakuu wakilalamika, Mzee mzima naja na waraka kwa wanakijiwe.

Kwa vile sasa dini na siasa vinachanganyikana, si vibaya kuchanganya siasa na ulevi.

Walevi fanyeni yafuatayo:
Ipigeni chini serikali au chama kinachotetea ufisadi na kuweni makini na matukio yanayodaiwa kuwakuta akina Sam Six na Mdingi Machela na vigogo wengine wa nambari nonihino.

Ogopeni serikali inayoneemesha mafisadi, isiyotekeleza ahadi yoyote isipokuwa kuwalinda na kuwaneemesha mafisadi huku ikitukana matusi ya nguoni kuwa itanunua Bajaj kwa ajili ya kuwaulieni mbali wagonjwa. Kwa nini kaya nyingine zitumie helikopta sisi tutumie Bajaj?

Wapigeni chini vihiyo wote walioghushi shahada na vyeti vyao; waliokataa kutaja mali zao huku wakijulikana walivyo wakora na vibaka.

Hakikisheni hamuwarejeshi madarakani wote waliotuhumiwa kwenye kashfa mbalimbali zinazodumaza uchumi wa taifa letu na majambazi wengine wote.

Madhumuni yawe kupambana na ufisadi baada ya serikali kuonekana kuelemewa na mzigo wa mapambano hayo.

Imani

Ondoeni imani na utawala wa kaya iliyoshikiliwa na mafisadi waliokubuhu, wakiongozwa na watu wanaotuhumiwa kuingia madarakani kwa fedha chafu pasipo kujibu tuhuma hizo.

Kitendawili. Tega. Ni kaya gani tajiri wa rasilimali, lakini wanakaya wengi ni maskini? Kwa nini?

Hiki ni kitendawili kikubwa ambacho tunapaswa kukijibu. Na kukijibu ni kuwasulubu mafisadi wawe wakubwa au wadogo wenye madaraka au la.

Kama siyo kubakwa na kutawaliwa na mafisadi, kaya hiyo ni kigogo wa utajiri barani. Mpo hapo ndugu walevi?

Kaya hiyo ina kila kitu isipokuwa uongozi wenye visheni, utashi na uadilifu. Imetamalaki mafisadi sambamba na rasilimali. Imejaza wezi na wavivu kwenye taasisi zake nyeti hasa pale kukuu.

Ingawa jamaa wa majoho wanasema: tumeumbwa kwa mfano wa Mungu, nabii Mpayukaji napinga. Mafisadi wameumbwa kwa mfano wa shetani na fisi hata mbwa.

Huoni walivyo na uroho kama fisi wakitenda madhambi ya kuua wanakaya kama shetani? Hivi akina Makombo, Tambo Hizo, Kimdunge kweli nao ni mfano wa Mungu? Kama ni mfano wa Mungu basi huyu Mungu hana maana.

Mungu ni msafi na si mlafi kama wao. Hivyo, hawa kama wana mfano mbali na fisi, ni mfano wa shimo la taka au gunia au pakacha. Hawana tofauti na dumuzi au panya wagugunao kila kitu.

Hivyo, lengo mojawapo ni kuwafunda wanakaya kuacha ukenge na woga. Wajitoe mhanga tulivamie hili genge na kulisambaratisha kabla halijauza kaya yetu.

Juzi nilikuwa kwenye mbuga za wanyama. Nilishuhudia yule Mwarabu jambazi aliyeletwa na Muhuniduni Ndongala na mzee wetu wa zamani kidogo akiendelea kufanya vitu vyake.

Baada ya kumaliza wanyama, amewageuzia kibao akina Ole akitaka wahamishwe na kuwa wakimbizi kwenye kaya yao. Hapa kweli kuna lisirikali?

Kama lipo ni ajali na ni la kijambazi. Pale kwenye shirika la mataruma kuna lisirikali zaidi ya wezi wachache wakijiuza kama vyangudoa?

Nawataka wanakaya na wapiga kura kwa ujumla, kuchagua viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kujali watu; lakini wasichague viongozi wezi, walafi, mafisadi na wakwapuaji wengine wa mali za umma.

Sitaki kuona takataka zenye uraia wa nchi mbili au zitokanazo na utajiri uchwara wa ama mama zao au baba zao na vikaragosi vingine kama hivyo.

Wala sitaki wachague takataka zitokanazo na ukubwa wa majina ya mama au baba zao. Sisi si Wahindi ambao huchagua ukoo badala ya mtu.

Hatutaki akina Kennedy, Bush, Gandhi, Bhutto wala Bandranaike weusi hapa. Wala hatuwahitaji akina Eyadema, Kabila, Karumekenge, Bongo, Khama, Mswati, Kenyatta, Mudavadi, Odinga na wengine wasio na chochote bali majina machafu yatukuzwayo ya baba zao wezi au watawala wezi wa zamani. Nop. Never. It should nary happen. On my dead body! Mkirejesha mbweha hawa, mie najitoa roho ili laana ya kumuua nabii iwaandame.

Kitu kingine, yale maeneo yaliyoathiriwa na uwekezaji uchwara hakikisheni wale wezi wote walioshirikiana na wachukuaji wawekezaji wanatimuliwa.

Hawa hawafai kuongoza hata kundi la mbwa. Wanafaa kuwa lupango. Ndugu zangu wa Mwanza, Shinyanga, Mara, Mererani, Loliondo na kwingineko shikilia nukta hii kieleweke.

Suala jingine ni kuhusu utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na jamaa yangu. Asiwaletee mashairi wala ngonjera. Kumbukeni kuwa ametimiza ahadi mbili tu.

Nazo ni kumlinda Tunituni na kumneemesha ma mkubwa. Mpo hapo washikaji wenye bongo zinazochemka? Jumlisheni mbili na mbili mtapata jibu kama siyo jipu. Mie simo.

Kwenye uchaguzi, hakikisheni hamchagui lisirikali linalotupa shinikizo ili tusibaini uchafu wake.

Namaanisha kutukandamiza na kutufanya tuwe maskini kiasi cha kunusurika na kushughulikia mambo ya kipuuzi kama wapi utabomu, kuiba, kudokoa, kudoea au kujikomba ili liende.

Hamjawaona wazee wazima na wanaume wanaojikomba kama vyangudoa? Unadhani Kimdunge alisukumwa na nini kukandia waraka wa rafiki zangu wa majoho? Na Makorongo na akina Tambo Hizo?

Lao moja. Kutumia utumbo kufikiri badala ya ubongo; kuendekeza ukuku na uumbwa ili liende. Mwenzenu siyawezi haya.

Kuna jamaa zangu wa Mbalanga mliolipukiwa na mibomu na kuambulia fidia ya madafu thelathini utadhani mlimsaliti Yesu. Nyie hakikisha hamtoi kura ya kula kwa mpuuzi yeyote toka chama cha upuuzi kilichosimamia mateso yenu. Never.

Pia hakikisheni mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na tume yenyewe, msajili wa vyama wanakuwa si wanachama wala washikaji wa chama chochote.

Hili ni muhimu sana. Maana chama fulani kwa kutumia washikaji na washirika zake hawa kimekuwa kikifanya unyani wa nyinyi kuweka wao wakachukua waaa, nanyi kuishia kuchagua balaa.

Pia ule upuuzi wa polisi au wanajeshi kusimamia uchaguzi wakati ukweli wanasimamia wizi wa masanduku ya kura unatokomezwa.

Kitu kingine, shinikizeni misikiti na makanisa, misiba, harusi na mikusanyiko mingine ya kijamii kutotumika kufanyia kampeni.

Kubwa kati ya yote ni kudurusu sera za vyama na kuwapiga chini wale waliokwishatangaza kugombea hata kabla ya kipenga cha mwisho.

Juzi nilisikia chama fulani kikisema kuwa mwenyekiti wake aachwe agombee kwa tiketi yake ili amalizie ngwe yake utadhani kaya ni mali yao!

Wale wagombea wote wenye wake wenye NGO’s pigeni chini. Maana hawa wanadaiwa kuzitumia kuiba na kupatia mtaji wa kuhonga.

Nimalizie. Msikubali kununuliwa kwa upuuzi mdogo mdogo kama bia, nyama choma, pombe, lifti wala takrima uchwara.

Mkiendeleza libeneke la kupenda takrima mauza uza katika kaya yetu hayatakoma. Mnadhani mwawala kumbe mwaliwa!

Naomba nitoe hoja.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 7, 2009.

No comments: