Thursday, 15 October 2009

Vita Dhidi ya Ufisadi Inapogeuka Maigizo

WALEVI wapendwa, sina haja ya kuwa mkweli. Kabla ya kurudi ghafla wiki iliyopita, sikuonekana kijiweni takribani wiki mbili hivi. Wajua ni aje? Kwanza, nilikuwa nimeuawa ukiachilia mbali kwenda kwa Obama kuhudhuria Kijiwe cha Umoja wa Kaya. Mungu si Mpayukaji.

Tuanze na kuuawa kwangu. Nilijipinda na kukukuruka nikayashinda mauti. Wajua kosa langu nini? Kama Spika Six, kupambana na ufisadi tena kwa kutaja majina bila ya kubahatisha wala kuzungusha. Sikujua kuwa mafisadi wana nguvu hivi!

Wajua ilikuwaje? Walitishia kuninyotoa roho. Mie sikujali. Walipoona sitishiki si wakaamua kumvaa mhariri. Nusu wamnyotoe roho. Kisa nini? Kwa nini analiruhusu Payukaji liwatilie kitumbua chao mchanga kwa kuwapayukia?

Ajabu, eti hata wale wanaonuka nongo nao walisema nawachafua! Eti kosa ni kuonya kuwa ‘vita’ dhidi ya ufisadi imetekwa na mafisadi wenyewe! Eti kosa ni kuonya tusiwaamini majemedari feki wa vita hii ambao kwa kila kigezo ni mafisadi hata uwepo wao sehemu sehemu umetokana na ufisadi.

Mambo yalikuwa mambo tena mambo mambo. Walitishia kunifikisha kwa pilato ili nisulubiwe pamoja na mhariri. Uzuri hatukukubali kufa kibudu. Mie nilipinga sijamchafua mtu bali uchoyo na ufisadi wake.

Katika hekaheka hizi mambo yalizidi kuharibika. Mhariri alijaribu kuwauliza wasomi (wanasheria). Nao bila aibu, eti walisema nina kesi just kwa kutaja majina yanayokaribia kufanana na yale ya mafisadi.

Japo tumekubali yaishe, bado kama gwiji la sheria, nakataa. Huwezi kuandika Mpuyukaji kisha Mpayukaji akaja juu. Maana, sheria inasema wazi. Lazima uthibitishe dai lako bila kubakisha chembe ya shaka.

‘By using implications you can nary prove your case beyond reasonable doubts’ kama sheria ituamuruvyo. Hayo tuyaache. Kwa vile wachumia tumbo wako katika kila sekta, napanga kurejea chuoni kufundisha jurisprudence ili kuwa na mapilato waliobobea.

Nani angeamini kuwa kupambana na ufisadi kwa vitendo kungegeuzwa kosa, tena la jinai, kiasi cha kutaka kuwanyotoa watu roho? Hivi mabunga haya yalitaka nifanye usanii kama Cheka Cheka kupambana na ufisadi kwa njia ya kuupamba huku nikiwaaminisha walevi wanichague tena wajutie ujuha wao?

Hata hivyo, kuna kosa moja kubwa hawa wajalaana walifanya. Mie si kiumbe wa kutishiwa nyau. Hivi kweli ukisema: kile kizee chenye miaka 800 kilikwiba kwa kumtumia mshirika wake wa bedroom ni kukipakazia?

Hivi ukisema EPA inaepwa kwa vile kuna mkuu wa kijiwe nako ni kumpakazia kweli? Jamani, mbona tunageuza uongo kuwa ukweli na ukweli kuwa uongo? Mbona tunabariki haramu na kulaani halali kwa kubatilisha halali na kuhalalisha haramu?

Halafu jitu linaanza eti kupiga ndogo ndogo tulipe tena ulaji litumalize. Looh! Mkifanya kosa msijesema Nabii Mpayukaji sikusema.

Hivi Mpayukaji akiangalia mateso yanayotembezwa Loliondo na lisirikali kwa kuhongwa na Mwarabu kwenye youtube akapayuka waseme anawapakazia, kusingizia au kwachafua wakati ni uroho na upofu wao?

Na haya matangazo ya Karibu Kwenye Falme za Kiarabu yameanzishwa na Mpayukaji? Waarabu walituuza kwenye utumwa, bado hatujaridhika tunawakaribisha kwa mbwembe na hoihoi kuwauza upya watu na wanyama wetu?

Kwa nini hatujifunzi kutokana na historia? Mmekumbatia wezi kwa kuwatosa watu wenu tukisema mnasema tunachochea. Mnaochochea ni ninyi mnaoendekeza njaa. Uhuru umetoweka na utumwa na ufisadi vimechukua nafasi yake.

Hivi pale Kiwila si wizi mtupu? Je, kwenye mataruma pale kuna nini zaidi ya uganga njaa na ufisadi? Kila siku mijitu inatupigia kelele eti inapambana rushwa wakati imelalia Richamando na kuepa EPA.

Acheni kutupigiza makelele. Mijitu inaiba yenyewe, wake zao, nyumba ndogo hata vitegemezi halafu inatupigia mikelele eti ina mpango wa kupambana na mafisadi wakati yenyewe ndiyo mifisadi namba moja. Mkome na mlegee, mlaaniwe na mnyong’onyee.

Leo mibaba mizima bila aibu inadanganya mchana eti ina mipango madhubuti ya kuendeleza kaya. Kwa nini saa hizi? Miaka yote mliyokuwa hapo zaidi ya kuiba mlikuwa mnafanya nini?

Kwanza lazima niwape pasenali. Mmefulia na mjue walevi washawajua kuwa nyie hamna lolote zaidi ya ufisadi. Mna uchu wa fisi. Hamuoni wala hamjitambui mkidhani na walevi wataendelea kutojitambua ili kuwatia adabu.

Anyway, hayo tuyaache. Ngoja niwamegee kidogo. Majuzi nilibahatika kukutana na Obama. Si utani. Nilikutana naye kwenye mitaa ya Washington pale Pennsylvania Avenue NW baada ya kumkosakosa kule New York kwenye makutano ya Tudor City na E Third Street. Wajua ni wapi hapa? Makao Makuu ya UN. Tuyaache.

Tulichonga sana baada ya kukasirishwa na kijiwe cha Nairobi asijue na kijiwe chetu kinaongoza hata cha Nairobi. Baada ya kupata ujiko wa kuangukia kama zali la mentali, niliwaambia wapiga upatu wangu wapige picha kwa sana ili kunipandisha chati tayari kwa walevi kunipa kula kwenye uchafuzi ujao.

Upo hapo? Atakayeendelea kufuata mkumbo ataingizwa mkenge upya mara nyingine. Na mara hii kumbuka. Ni lala salama. Tunakomba kitunituni tukijua hatuna haja tena ya kurejea kuusaka ulaji wa dezo ukuuni. Mpo wadanganyika wangu hapo?

Kwa vile nilikuwa nimeanza kuumbuka kutokana na kashfa zetu na kina Mbwa Mwitu kuzidi kufumka, naamini Obama atakuwa amenipiga tafu si kawaida. Laiti angejua nami ni kibaka kama kaka yetu wa jirani asingepoteza muda wake.

Najua kosa kubwa la Kabaki ni kumkingia kifua Dani wa Kurap Moyi. Nami nimeamua kufa na Mbwa Mwitu wangu. Napiga picha. Kama Jadwong Obama angejua ukweli kuhusiana nami si angejilaumu kuruka mkojo na kukanya kinyesi kweli?

Kaya hii kuna mtu mzima? Kama huna ukimwi una UMAKI yaani Ubutu wa Mawazo Kayani kama siyo UUKA yaani Ukosefu wa Ujasiri Kayani. Tusingekuwa wagonjwa wote nani angeridhia vita dhidi ya ufisadi kuwa maigizo na makamanda wake kuwa mafisadi wenyewe?

Hivi inawezekana nyoka akajikata kichwa chake akijua ndiyo mwisho wa maisha yake? Vita dhidi ya ufisadi tunapaswa kuanza upya kwa kasi mpya nguvu mpya na ari mpya dhidi ya kasi mpya ari mpya na nguvu mpya ya mafisadi.

Khalas kweisi.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 14, 2009.

No comments: