Thursday, 13 May 2010

Mikakati ya Mpayukukaji kuelekea uchaguzi mkuu

BAADA ya kugundua kuwa tatizo kubwa la kaya ni kuwa na ombwe la uongozi hata utawala, nimeamua kugombea urais seriously. Kuondokana na hali hii, nikichaguliwa, nitahakikisha nafanya mabadiliko makubwa hasa uwekezaji wa kisiasa si kiuchumi. Sitarudia makosa ya Tunituni na Chekacheka kuleta uwekezaji wa kijambazi ambao ni uchukuaji na ugenishaji.

Nimeamua kufanya uwekezaji wa kisiasa badala ya kiuchumi baada ya kugundua kuwa siasa zinaathiri na kudumaza uchumi. Hivyo ukiwa na siasa safi lazima uwe na uchumi bora. uchumi bora hauwezi kupatikana bila kuwa na mifumo bora ya kijamii hasa siasa.

Nina uhakika wa kushinda mara hii kutokana na wanuka jasho kutishia kumnyima kula mpinzani wangu mkuu ambaye naye amewatolea live kuwa hataki kura zao kama wanataka kuingilia ulaji wake. Hii ni baada ya jamaa kutukuta na kutaka awaongezee mshiko wasijue mshiko ni wanene na wazito! Sasa mmeishaambiwa. Jamaa hataki kula zenu. Hapa ndugu zangu wapiga chaki wakafa kwa kukosa pumzi waliokuwa wakitumiwa kufanya kale kamchezo najua watakengeuka na kunipa mimi tafu ili niwakomboe.

Ni juzi tu niliongea na profesa Sivji ambaye amenishauri niwalipe wafa na chaki dau kubwa kuliko mawaziri wangu. Nawaahidini nitalitekeleza hili. Na amini. Mie sitoi ahadi za kipuuzi bali za kweli ambazo nisipozitekeleza mnitimue ikulu.

Sitawachoka, kuwatukana, kuwakejeli wala kuwatishia virungu. Sitawaita wanafiki na waongo pale mtakaponiambia ukweli. Chini ya utawala wangu maandamano na migomo vitaheshimika. Maana ni haki ya kikatiba na ushahidi wa kukua kwa demokrasia na uongozi bora wa sheria. Sitatawala kwa jazba wala ushikaji bali kanuni bin kanuni.

Sitawaganya kati makundi ya wazee, vijana, wanawake wala wa pwani na bara. Kadhalika nitajitahidi kutopayuka hadharani na kuwasingizia kwa vile mimi ni mkubwa. Ukubwa wangu ni wenu. Hivyo sitakuwa na ukubwa chochote zaidi ya kuwa kipenzi cha watu na tumaini lililorejea.

Naomba mniamini. Sitatumia jazba katika kujadili kero na shida zenu. Sitawasikiliza mawaziri wangu vimbelembele watakaoniletea uongo na fitina ili tusikosane bure huku wao wakinitumia na kunitia majaribuni. Nitatumia busara badala ya misuli na longo longo.

Naahidi sitaitisha mikutano ya kichama na kuiita ya umma kuwazodoa na kuwasingizia. Hapa wale wazee wangu waliozoea kutumika kama nepi wanisamehe. Mimi sihitaji kukutana na kundi lolote zaidi ya wahusika na walengwa wote yaani wananchi. Mimi si Lugard yule mwingereza mshenzi aliyeleta kanuni chafu ya gawanya utawale au divide and rule. Mie si mkoloni wala sina mawazo ya kikoloni. Nina mawazo na jazba za ukombozi. Jazba zangu si za kuwatisha na kuwaita majina ya ajabu ajabu. Ni jazba zinazohitajika kurejesha kaya yenu kwenye mstari na heshima yake.

Msianze kutoa mimacho. Sitabinafsisha ikulu yenu. Maana kufanya hivyo ni sawa na kujitia kitanzi. Kwani hili litakuwa eneo langu la kutanulia.

Nitakachofanya ni kuongea na nchi za Kanada ambako nitaomba mtu atakayefanya kazi ya waziri wa uhamiaji ili kupambana uhamiaji haramu ambao umegeuka kuwa halali kutokana na kukithiri kwa rushwa. Wale jamaa zangu mnaofichana kwenye mabohari kaa chonjo. Kale kamchezo ka kuleta jitu kihiyo na kusema ni expert katakufa siku nitakapotangaza baraza la mawaziri.

Nitakwenda Uchina ambako nitachukua mtu atakaye kuwa waziri wa viwanda na maadili. Hapa ndugu zangu mafisadi na mabingwa wa madili wangoje kitanzi tu. Waziri wa biashara na utalii atatoka Japan. Mambo ya ndani na ustawi wa raia atatoka Uswizi. Kilimo na ulinzi nitachukua Ujeruman huku fedha nikichukua toka kwa Obama.

Sayansi elimu na utafiti nitaleta mkorea kusini huku wanawake vijana watoto na wazee nikichukua toka Sweden (elimu). Mkuu wa majeshi nitachukua toka Israel huku mkuu wa polisi nikichukua Uingereza.

Michezo na burdani nitachukua Ufaransa. Afya nitarudi Ujepu ili nijue siri ya kuishi maisha marefu na watu wangu waishi maisha marefu kwa kutanua na kutesa. Nitakuwa na baraza dogo kuepuka kupoteza njuluku za umma kulipana fadhila.

Kamishina wa mamlaka ya mapato nitachukua Finland huku gavana wa benki nikichukua toka Uswizi kama kawa.

Makamu wa rais nitachukua Urusi ili awarusherushe kirusi. Jeshi la ndata litapanguliwa ili kuondokana na rushwa. Nitaajiri ndata wengi toka Ujapani kwa vile ni waadilifu sana.

Msemaji wangu nitaazima yule wa Obama huku nikiondoa body guard maana sitakuwa na maadui kwa vile sitapunyua kiduchu wala njuluku za wana kaya. Mshahara wangu utagemea taaluma yangu ya upayukaji. Mai waifu hatakuwa na NGO wala hataandamana name kila mara ili kupunguza uharibifu wa njuluku za kijiwe.

Kitu kingine nitakachofanya ni kuleta FBI, MI6 au SIS, Mosad, KGB na Interpol kuchunguza wizi wa HEPA hasa kumkamata Kagodoka na wezi wa meremeta, Deep Green Finance na majambazi wengine harak. Pia nitaleta wataalamu wa akili kumpima rafiki yangu Gus Lyatongoka ili tujue anakabiliwa na aina gani ya kichaa au utapiamlo wa kiakili.

Kitu kingine nitahakikisha kila mwakaya anakuwa na kitambulisho chenye taarifa zake zote. Vitambulisho hivi vitakuwa digitalized and computalized kuepuka kughushi kama walivyofanya wale jamaa wa shahada feki. Pia jamaa wote wanaotuhumiwa kughushi nitawafunga maisha na kukamata mali zao zote kwa vile zimetokana na utapeli.

Wale jamaa zangu wanaopewa tenda za upendeleo kama vile kujenga barabara wakajenga barabara feki kama ile ya Kilwa Road na nyinginezo wajiandae. Mbuga za wanyama nako kaa mkao wa kula. Mambo yenu yote ninayo na dawa itapatikana tu baada ya kuapishwa. Pia wale jamaa wa mishahara wanaolipa hadi maiti wajue wameishatinga kwenye runinga yangu.

Kadhalika, wale wapenda kutanua nje kufanya ziara za kipuuzi na warsha za kulipana per diem bila kufanya chochote wajue nawajua na sitawavumilia. Nitahakikisha siasa inakuwa kazi. Lazima mwenye kushiriki awe na sifa na hakuna atakayeruhusiwa kufanya siasa kama atakuwa na zaidi ya miaka 55. Sitaruhusu wazee waitwe vijana ili kuwahadaa watu wawachague. Ukiwa na kuanzia miaka 55 jua hufai kushika ofisi ya umma kwa vile umeishastaafu. Kwanini taaluma nyingine wastaafu wanasiasia wasistaafu? Dawa ni kuifanya siasa taaluma ili tuone.

Nitabadili katiba kutoa nafasi kwa wananchi kutathmini utawala. Kama wataona sitimizi matakwa yao basi waitishe snap election iwe ni kwangu rais hata wabunge. Viti vya dezo na matusi yaitwayo maalum nitafuta ili kila mtu ale jasho lake. Maana naona jamaa wameishaanza kupenyeza watoto na wake zao kufaidi viti vya ubwete ambao ni wizi kwa wanakaya wangu.

Ngoja niishie kabla sijaitwa mnafi na muongo nikarusha ngu.... malizia mwenyewe. Unadhani mie ni mtu wa kutishiwa nyau nikanywea wakati najua nina maguvu? Hivi ng’ombe na kupe nani anamhitaji mwenzie?

We nenda kachape kazi kabla hujachapwa.
Chanzo: Tanzania Daima Mei 12, 2010.

No comments: